top of page

Dalili na viashiria bonyeza herufi ya kwanza kusoma zaidi

​

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [#]

Mwandishi:

Dkt. Sospeter B, MD

Mhariri:

Dkt. Salome A, MD

11 Juni 2021 11:34:48

Tiba ya kukojoa kitandani

Tiba ya kukojoa kitandani

Tafiti zinaonyesha kuwa kati ya watoto 100 waliotumia dawa za kuacha kukojoa, ni watoto 19 tu waliweza kuacha kukojoa katika kipindi cha siku 14 mfululizo walizofuatiliwa. Tafiti nyingine ilifanyika kwa watoto 100 pia, kundi hili halikutumia dawa bali lilitumia njia asili ya kubadili mazoea, matokeo yake ni kati ya watoto 100 waliofanyiwa tafiti, watoto 69 waliacha kukojoa kitandani. Hii ni dhahili kuwa njia ya kubadili mazoea ni bora zaidi kuliko dawa na ukiunganisha njia kubadili mazoea na dawa, matokeo huwa makubwa zaidi.


Tiba asili ya kuacha kukojoa kitandani ni ipi?


Tiba asili ya kuacha kukojoa kitandani inahusisha;


  • Kuzawadia

  • Kukojoa kabla ya kulala na mida Fulani wakati wa usiku

  • Kutumia king’ora cha mkojo

  • Dhibiti kiwango cha maji kabla ya kulala

  • Kufunza kibofu kutunza mkojo mwingi

  • Njia za kubadili mazoea ni zipi?


Kuzawadia


Njia hii hufanyika kwa kumpa zawadi mtoto endapo amefikia malengo fulani mliyokubaliana, mfano endapo mtoto ataenda chooni kabla ya kwenda kulala, au kukusaidia kutandika kitanda endapo amekojoa kitandani. Utaangalia ni zawadi gani utampatia mtoto mfano unaweza mpatia stika nzuri ambayo mtoto ataweka kwenye kalenda siku ambayo hajakojoa kitandani, kisha endapo amefikia malengo labda ya kuwa na zawadi ya stika 4 au 5 kwa wiki, atapatiwa zawadi nyingine ndogo. Njia hii ni nzuri kwa watoto wadogo tu.


Kukojoa kabla ya kulala na mida Fulani wakati wa usiku


Mtu mzima na Watoto wengi hupelekwa au huenda chooni muda kabla ya kulala, wazazi pia wanaweza kuwafunza watoto wao kuamka mara kadhaa wakati wa usiku ili kukojoa. Kufanya hivi kwa kujirudia rudia muda ule ule, kutamfunza mtoto kuwa na tabia ya kuamka muda huo kwenda chooni kukojoa mwenyewe.


Kutumia king’ora cha mkojo


Kuna aina tofauti za ving’ora vya kuamsha mtoto au mtu mzima kabla ya kujikojolea ambavyo huwekwa kwenye nguo ya ndani. King’ora cha mkojo hupiga kelele tone la kwanza linapotoka na hivyo mtu(mtoto) huacha kukojoa na kuamka.


Kwa siku za mwanzo, inaweza kuwa usumbufu kwa mama au mtoto kwa kuwa usingizi huwa unakatishwa na sauti za mara kwa mara za king'ora, hata hivyo baada ya muda kupita utazoea hali hiyo na mtoto au mtu mzima atakuwa na uwezo wa kuamka bila hata kutumia king’ora hiko. Vingor’a hivi vinapatikana sehemu nyingi na pia unaweza kununua kwa kuagiza mtandaoni.


Dhibiti kiwango cha maji kabla ya kulala


Baadhi ya wazazi huzuia watoto kukojoa kitandani kwa kuwazuia wasinywe maji mengi au kutotumia kabisa kimiminika chochote wakati karibu na kulala. Jambo hili ni jema, hata hivyo endapo mtoto ana kiu ya maji, mpatie maji ya kunywa. Zuia mtoto asitumie vinywaji vyenye sukari au kafeini kwa kuwa huongeza uzalishaji wa mkojo. Kwa ufanisi zaidi, usimpatie mtoto maji ya kunywa masaa mawili kabla ya kulala.


Kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo


Mafunzo ya kibofu kutunza mkojo na kuongeza uwezo wake wa kukaa na mkojo hulenga kuongeza kiwango cha mkojo kinachotunzwa na kibofu na hivyo kutunza mkojo mwingi wakati wa usiku. Hii hufanyika mchana kwa kumfunza mtoto(mtu mzima) kutokojoa pale anapopata hamu ya kwenda kukojoa, unaweza anza kuzuia mkojo dakika 10 kisha kuruhusu akojoe na kuongeza muda jinsi siku au wiki zinavyokwenda, wasiliana na daktari kufahamu namna gani ya kufunza kibofu na endapo inafaa kwako.


Zoezi hili hupunguza tatizo la kukojoa kitandani. Njia hii ni nzuri endapo itaunganishwa na njia zingine.


Matibabu mengine ni yapi?


Kufahamu kuhusu dawa za kukojoa kitandani, ingia kwenye makala ya dawa au kwa kubofya hapa.


1.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasilianane na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY clinic kwa kupiga namba za simu  au kubonyeza sehemu imeandikwa "Pata tiba" chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

21 Julai 2023 16:18:21

Rejea za mada hii;

1. Caldwell PH, et al. Simple behavioural interventions for nocturnal enuresis in children https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/23881652. Imechukuliwa 11.06.2021

2. Glazener CM, et al. Alarm interventions for nocturnal enuresis in children.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/15846643. Imechukuliwa 11.06.2021

3. Huang T, et al. Complementary and miscellaneous interventions for nocturnal enuresis in children. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/22161390. Imechukuliwa 11.06.2021

4. National Institute for Health and Care Excellence (NICE). Nocturnal Enuresis: The Management of Bedwetting in Children and Young People. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmedhealth/PMH0016295/. Imechukuliwa 11.06.2021

5.Patrina HY Caldwell, et al. Simple behavioural interventions for nocturnal enuresis in children.https://www.cochranelibrary.com/cdsr/doi/10.1002/14651858.CD003637.pub3/full#. Imechukuliwa 11.06.2021

bottom of page