top of page

Mwandishi;

Mhariri:

Jaza jina na cheo cha mwandishi

Jumanne, 23 Machi 2021

Kiharusi-Huduma ya kwanza
Kiharusi-Huduma ya kwanza
Kiharusi-Huduma ya kwanza
Kiharusi-Huduma ya kwanza

Kiharusi-Huduma ya kwanza

Ubongo wa binadamu unahitaji kupata hewa safiya oksijeni pamoja na sukari ya glucose muda wote ili uweze kufaya kazi yake vema, vitu hivi viwili hupelekwa kwenye ubongo kupitia damu. Kiharusi kinaweza kutokea endapo damu haiwezi fika vema eneo fulani la ubongo, hii husababisha kukosa oksijen na sukari hivyo kufa na kupelekea kuonekana kwa dalili za kiharusi. Endapo mtu amepata kiharusi, kitu cha pekee unachoweza kufanya ni kumsaidia kuweza kuzuia eneo kubwa la ubongo kuathirika kwa kukosa damu.


Kiharusi kwa jina jingine huitwa mshituko wa ubongo.


Aina za kiharusi


Kuna aina mbili za kiharusi, aina ya kwanza ni kiharusi kinachotokana na kuziba kwa mshipa fulani wa damu unaolisha sehemu fulani ya ubongo, kuziba huku husababishwa na damu iliyoganda inayosafiri ndani ya mishipa ya damu, na aina ya pili ni kiharusi kutokana na kuvia damu ndani ya ubongo. Kiharusi cha kuziba kwa mishipa ya damu hufahamika kitiba kama kiharusi cha ischemia wakati kile cha kupasuka kwa mishipa ya damu hufahamika kama kiharusi cha hemorrhagia. Kiharusi kinachotokea sana kwa zaidi ya asilimia 80 kwa binadamu ni kiharusi cha ischemia


Dalili za kiharusi


 • Kuanguka kwa uso upande mmoja

 • Kupooza upande mmoja wa mwili

 • Kuongea kama mlevi

 • Kupoteza uono ghafla

 • Kizunguzungu

 • Kupungua kiwango cha kuweza kujitambua

 • Kupata kifafa

 • Kuona vitu vinazunguka(mgonjwa)

 • Kushindwa kutembea


Namna ya kutambua mtu mwenye kiharusi


Unaweza kumtambua mhanga wa kiharusi kwa kufanya mambo yafuatayo pia


 • Je uso wa mgonjwa umeanguka au kuonyesha haupo sawa upande wa kushoto na kulia? Fanya hivyo kwa kumwambia atabasamu

 • Je anaweza inua mikono yote miwili bila mmoja kuanguka?

 • Je ana mabadiliko kwenye kutamka maneno au anaongea kama mlevi?


Kama kuna dalili hizo, piga simu haraka ili wataalamu wa afya wa huduma ya dharura waje kumsaidia


Namna ya kumpa huduma ya kwanza mhanga wa kiharusi


Kama unahisi mgonjwa wako ana kiharusi, fanya mambo yafuatayo haraka


 • Piga simu za huduma ya dharura haraka iwezekanavyo, usimwache mgonjwa alale au kupumzika kabla ya kupiga simu

 • Muweke mhanga kwenye pozi la pumziko

 • Endapo amepoteza fahamu na mapigo ya moyo hayasikiki, mfanyie CPR(jifunze namna ya kufanya CPR kwenye Makala zingine za ULY CLINIC)

 • Andika muda wa dalili za kiharusi kuonekana na dalili zilizotokea ili kumfahamisha kiongozi wa huduma za dharura atakapofika

 • Mpe tumaini mgonjwa na pima viashiria uhai mpaka timu ya dharura itakapofika

 • Usimpe mhanga chochote cha kula au kunywa kwani utaongeza hatari ya kupaliwa na hivyo kumsababishia matatizo zaidi

 • Usimpatie mgonjwa aspirini au dawa zingine za kuyeyuesha damu kwani hii itapalekea damu kuvia zaidi kwenye ubongo endapo kiharusi ni kutokana na kuvia kwa damu

 • Legeza mavazi au vitu vinavyobana mhanga

 • Kama anahisi baridi mfunike na blanketi

 • Angalia kama nnjia ya hewa haina kitu, kama vile chakula au matapishi yanayoweza kuzuia upumuaji wake. Kama vipo unaweza kutoa kwa kufuata utaratibu ilioandikwa sehemu nyingine katika tovuti hii ya ULY CLINIC


Kwanini kukumbuka muda dalili zilipotokea?


Matibabu ya kiharusi hutegemea muda tangu ilipotokea, endapo muda ni chini ya masaa 4 na nusu, mgonjwa anaweza faidika kupata matibabu kwa dawa endapo kiharusi chake kinasababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu. Hata yule mwenye kiharusi kutokana na kupasuka kwa mshipa wa damu anaweza kupata huduma ya dharura ya upasuaji. Kupata huduma za dharura za dawa au upasuaji huzuia sehemu kubwa ya ubongo kuathirika na hivyo kuondoa au kupunguza athari inayoweza kutokea kutokana na kiharusi.

ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba'  chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

1 Oktoba 2021 08:12:15

Rejea za mada:

 1. Penn medicine. If Someone is Having a Stroke: 3 Things To Do and 3 Things Not To Do. https://www.pennmedicine.org/updates/blogs/neuroscience-blog/2019/april/if-someone-is-having-a-stroke-3-things-to-do-and-3-things-not-to-do. Imechukuliwa 23.03.2021

 2. Elite medica centre. FIRST AID FOR STROKE. https://elitelv.com/doctors-corner/first-aid-for-stroke/. Imechukuliwa 23.03.2021

 3. “Stroke Facts.” Centers for Disease Control and Prevention, Centers for Disease Control and Prevention. www.cdc.gov/stroke/facts.htm. Imechukuliwa 23.03.2021

 4. Stroke: First Aid.” Mayo Clinic, Mayo Foundation for Medical Education and Research. www.mayoclinic.org/first-aid/first-aid-stroke/basics/art-20056602. Imechukuliwa 23.03.2021

 5. “About Stroke.” www.stroke.org, www.stroke.org/en/about-stroke. Imechukuliwa 23.03.2021

 6. René Handschu , et al. First aid in acute stroke. Introducing a concept of first action to laypersons. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC1705488/. Imechukuliwa 23.03.2021

 7. Jen Heng Pek, et al. Guidelines for Bystander First Aid 2016. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5523093/. Imechukuliwa 23.03.2021

 8. Pathophysiology and Treatment of Stroke. https://www.mdpi.com/1422-0067/21/20/7609/pdf. Imechukuliwa 23.03.2021

bottom of page