top of page

Mwandishi;

Mhariri:

Imeboreshwa

23 Agosti 2026, 12:48:25

Kuumwa na nyoka: Huduma ya kwanza
Kuumwa na nyoka: Huduma ya kwanza
Kuumwa na nyoka: Huduma ya kwanza
Kuumwa na nyoka: Huduma ya kwanza

Kuumwa na nyoka: Huduma ya kwanza

Kuumwa na nyoka ni dharura ya kitabibu, hasa ikiwa kuna uwezekano kwamba nyoka alikuwa na sumu. Sumu ya nyoka inaweza kuathiri mfumo wa fahamu na kusababisha kupooza kwa misuli ya kupumua, kuharibu tishu, kusababisha kutokwa damu, kushindwa kwa figo au madhara mengine makubwa. Kwa hiyo, lengo kuu la huduma ya kwanza ni kumzuia aliyeumwa asisogee, kuzuia madhara zaidi na kumfikisha hospitali haraka iwezekanavyo.


Si kila kuumwa na nyoka husababisha sumu, lakini mtu aliyeng'atwa na nyoka anayeshukiwa kuwa na sumu hapaswi kusubiri dalili zianze kabla ya kwenda hospitali. Matibabu maalumu ya sumu ya nyoka ni dawa ya kuzuia sumu (antivenom), ambayo hutolewa na wataalamu wa afya inapokuwa na dalili zinazoonyesha kuathirika kwa sumu.


Dalili zinazoweza kutokea baada ya kuumwa na nyoka

Dalili hutofautiana kulingana na aina ya nyoka, kiasi cha sumu kilichoingia mwilini, sehemu iliyoumwa na hali ya mtu. Mtu anaweza kuwa na:

  • Maumivu kwenye sehemu iliyoumwa

  • Alama za meno au michubuko kwenye ngozi

  • Uvimbe unaoweza kuongezeka

  • Kutokwa damu kwenye eneo la kuumwa au sehemu nyingine za mwili

  • Malengelenge au kuharibika kwa tishu

  • Kichefuchefu au kutapika

  • Kizunguzungu, udhaifu au kuchanganyikiwa

  • Kuona kwa shida au kuona mara mbili

  • Kushindwa kufungua macho vizuri au kope kulegea

  • Ugumu wa kuongea au kumeza

  • Udhaifu wa misuli unaoweza kuendelea hadi kushindwa kupumua

  • Mkojo kuwa na rangi isiyo ya kawaida au kupungua kwa kiasi cha mkojo

  • Kupoteza fahamu katika hali kali


Muhimu: kutokuwepo kwa uvimbe mkubwa au maumivu makali mwanzoni hakumaanishi kwamba hakuna sumu. Baadhi ya sumu huathiri zaidi mfumo wa fahamu au damu kuliko kusababisha uharibifu mkubwa wa ngozi.


Huduma ya kwanza kwa mtu aliyeumwa na nyoka

1. Ondoa mtu kwenye eneo lenye nyoka

Kwanza, mtoe mtu kwenye eneo ambalo anaweza kuumwa tena. Usijaribu kumkamata, kumfukuza au kumuua nyoka.


Usijiweke kwenye hatari kwa kutaka kumtambua nyoka kwa karibu. Ikiwa nyoka ameondoka, acha aende.

Ikiwa unaweza kumpiga picha nyoka akiwa mbali na kwa usalama kabisa, picha hiyo inaweza kusaidia wataalamu kumtambua, lakini usichelewesha safari ya kwenda hospitali kwa ajili ya kutafuta picha au kumshika nyoka.


2. Mtulize aliyeumwa

Mwambie mtu aliyeng'atwa atue na asitembee. Hii ni muhimu kwa sababu harakati za mwili zinaweza kuongeza mzunguko wa damu na kusaidia sumu kusambaa kwa kasi zaidi. Kwa hiyo, mtu aliyeng'atwa anapaswa kubebwa au kusafirishwa badala ya kutembea mwenyewe kwenda hospitali.


Mtu anayemsaidia pia anapaswa kuwa mtulivu. Hofu inaweza kumfanya aliyeumwa kutembea au kufanya harakati zisizo za lazima.


3. Ondoa vitu vinavyobana mwili

Ondoa vitu vinavyoweza kubana sehemu iliyoathirika ikiwa uvimbe utaanza, kwa mfano:

  • Pete

  • Bangili

  • Saa

  • Viatu

  • Mikufu ya mguu

  • Nguo zinazobana eneo lililoumwa

Usivute nguo ambayo imegandia kwenye jeraha. Lengo ni kuondoa vitu vinavyobana bila kuongeza jeraha.


4. Zuia kiungo kilichoumwa kisisonge

Ikiwa kuumwa ni kwenye mkono au mguu, tuliza kiungo na ukizuie kusogea kadiri inavyowezekana.

Unaweza kutumia kifaa kigumu kama ubao au kitu kingine kinachofaa kama splint ili kusaidia kiungo kisipinde wakati wa usafirishaji. Kifaa hicho kisifungwe kwa kubana sana.


Kwa mfano, ikiwa ameumwa mguuni, mguu unaweza kutulizwa ili goti na kifundo cha mguu visiendelee kujikunja. Ikiwa ameumwa mkononi, mkono unaweza kutulizwa karibu na mwili kwa njia ambayo inapunguza harakati. WHO inapendekeza kumzuia mtu mzima au mtoto kusogea kabisa na kutuliza kiungo kilichoumwa wakati wa kumpeleka kituo cha afya.


Muhimu kuhusu kufunga bandeji ya kubana

Usifunge tourniquet(toniketi) au kamba inayobana mshipa wa damu kuzunguka mkono au mguu. Njia hii inaweza kusababisha madhara makubwa kwenye tishu.


Bandeji ya pressure immobilization inayotumika kwa baadhi ya kuumwa na nyoka ni mbinu maalumu ambayo haifai kutumika kwa kila aina ya nyoka. Miongozo inaeleza kuwa inaweza kufaa hasa kwa kuumwa na nyoka wenye sumu inayoshambulia mfumo wa fahamu lakini isiyosababisha uvimbe mkubwa wa eneo lililoumwa; kwa kuumwa kunakosababisha uharibifu mkubwa wa tishu, inaweza kuwa isiyofaa.


Kwa hiyo, kwa mazingira ya kawaida ya huduma ya kwanza, kipaumbele ni kutuliza mtu na kiungo na kumpeleka hospitali haraka, badala ya kujaribu mbinu maalumu ya kubana bila mafunzo.


5. Mpeleke hospitali haraka

Usisubiri kuona kama dalili zitaanza. Mtu aliyeng'atwa na nyoka anayeshukiwa kuwa na sumu anapaswa kufikishwa katika kituo cha afya haraka iwezekanavyo, ikiwezekana kituo kinachoweza kutoa huduma za dharura na dawa maalumu ya kuzuia sumu ya nyoka.


Ikiwa kuna gari au huduma ya dharura, mtu aliyeng'atwa asitembee mwenyewe. Ikiwezekana, asafirishwe akiwa amelala au amekaa kwa usalama huku kiungo kilichoumwa kikiwa kimetulia.


6. Mfuatilie kupumua na fahamu

Baadhi ya sumu za nyoka zinaweza kusababisha kupooza kwa misuli ya kupumua. Hali hii inaweza kuanza na udhaifu, kope kulegea, kuona mara mbili, kushindwa kuongea au kumeza, na baadaye kupumua kwa shida.

Mfuatilie aliyeumwa wakati wote wa safari. Ikiwa anatapika au amepoteza fahamu lakini bado anapumua, mgeuze kwa uangalifu katika pozi la kupona, ikiwezekana akiwa amelalia ubavu wa kushoto, ili kupunguza hatari ya kutapaliwa na matapishi.


Ikiwa amepoteza fahamu na hapumui kawaida, anahitaji CPR mara moja na msaada wa dharura.


Je, kidonda kisafishwe?

Ikiwa usafiri wa kwenda hospitali unapatikana mara moja, usipoteze muda kufanya taratibu nyingi kwenye kidonda.


WHO inaeleza kwamba kidonda kinaweza kusafishwa ili kupunguza hatari ya maambukizi, lakini jambo muhimu zaidi ni kumfikisha mgonjwa katika kituo cha afya haraka na bila kuchelewesha. Usikate, kuchoma au kuchokonoa kidonda kwa ajili ya kutoa sumu.


Mambo ambayo hupaswi kufanya kwa mtu aliyeumwa na nyoka

Usifanye yafuatayo:

  • Usikate kidonda ili kutoa sumu

  • Usinyonye sumu kwa mdomo

  • Usitumie kifaa cha kunyonya sumu

  • Usifunge toniketi au kamba inayozuia kabisa mzunguko wa damu

  • Usichome au kuchoma eneo lililoumwa

  • Usipake kemikali, dawa za kienyeji au mitishamba kwenye kidonda

  • Usitumie “jiwe la nyoka” au njia nyingine zisizothibitishwa

  • Usimlazimishe aliyeumwa kutembea

  • Usipoteze muda kumkamata au kumuua nyoka

  • Usimpe pombe au tiba za kienyeji

  • Usisubiri dalili kali kabla ya kwenda hospitali


Njia kama kukata kidonda, kunyonya sumu, kutumia toniketi, kuchoma au kutumia kemikali zinaweza kuongeza madhara na kuchelewesha matibabu sahihi.


Dalili hatari zinazohitaji msaada wa haraka sana

Piga huduma za dharura na mpeleke mtu hospitali haraka zaidi ikiwa ana:

  • Kupumua kwa shida au kushindwa kupumua

  • Kushindwa kumeza mate

  • Sauti kubadilika

  • Kope kulegea au kushindwa kufungua macho

  • Kuona mara mbili

  • Udhaifu unaoongezeka wa misuli

  • Kutokwa damu kusiko kawaida

  • Damu kwenye mkojo au mkojo kupungua sana

  • Uvimbe unaoenea haraka

  • Maumivu makali au uharibifu mkubwa wa tishu

  • Kuzimia au kuchanganyikiwa

  • Kutapika mara kwa mara

  • Dalili za mshtuko kama ngozi kuwa baridi, udhaifu mkubwa na mapigo ya moyo kwenda haraka.


Matibabu ya hospitalini

Matibabu hutegemea aina ya nyoka, dalili na kiwango cha sumu kilichoingia mwilini. Antivenom ndiyo tiba maalumu inayoweza kuzuia au kubadilisha madhara mengi makubwa yanayosababishwa na sumu ya nyoka. Hutolewa na wataalamu wa afya inapohitajika; si kila mtu aliyeumwa na nyoka anahitaji antivenom.


Hospitali pia inaweza kutoa huduma ya kusaidia kupumua, kudhibiti kutokwa damu, kutibu mshtuko, kutibu uharibifu wa tishu, kudhibiti maumivu na kutoa huduma nyingine kulingana na madhara yaliyotokea.


Kwa baadhi ya mazingira, mtaalamu anaweza kufuatilia mgonjwa kwa muda kwa sababu dalili za sumu zinaweza kujitokeza au kuongezeka baada ya kuumwa. Kwa hiyo, kutokuwa na dalili mara moja hakumaanishi mtu yuko salama kabisa.


Hitimisho

Mtu aliyeng'atwa na nyoka mtoe kwenye hatari, mtulize, mzuie kutembea, ondoa vitu vinavyobana, tuliza kiungo kilichoumwa na mpeleke hospitali haraka bila kukata, kunyonya au kubana mshipa wa damu.


Ikiwa ana shida ya kupumua, udhaifu unaoongezeka, kutokwa damu, uvimbe mkubwa, kupoteza fahamu au dalili nyingine kali, hali hiyo ni dharura inayohitaji msaada wa haraka. Antivenom na huduma nyingine za hospitali ndizo njia muhimu za kutibu madhara ya sumu ya nyoka.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu huduma ya kwanza kwa mtu aliyeumwa(aliyeng'atwa) na nyoka

1. Je, mtu anaweza kuumwa na nyoka mwenye sumu bila kuona alama za meno?

Ndiyo, muonekano wa kidonda pekee hauwezi kutumika kuthibitisha kwamba sumu imeingia au haijaingia mwilini. Alama zinaweza kuwa ndogo, na wakati mwingine mtu anaweza kutokuwa na kidonda kinachoonekana kwa urahisi.


Pia, aina tofauti za sumu zinaweza kusababisha madhara tofauti. Baadhi husababisha zaidi uharibifu wa tishu na uvimbe, wakati nyingine zinaweza kuathiri mfumo wa fahamu na kusababisha udhaifu au kupooza bila kuanza na uharibifu mkubwa wa ngozi.


Ndiyo maana mtu aliyeng'atwa na nyoka anayeshukiwa kuwa na sumu hapaswi kuamua mwenyewe kwamba “sijapata sumu kwa sababu kidonda ni kidogo.” Tathmini ya kitabibu ndiyo njia salama ya kuamua kama kuna dalili za sumu na kama matibabu maalumu yanahitajika.

2. Kwa nini mtu aliyeng'atwa na nyoka hatakiwi kutembea kwenda hospitali?

Harakati za mwili zinaweza kuongeza mzunguko wa damu na hivyo zinaweza kuchangia kusambaa kwa sumu kwa kasi zaidi. Kwa sababu hii, Miongozo inapendekeza kumzuia aliyeumwa kusogea na kumpeleka kituo cha afya akiwa ametulia.


Hili ni muhimu zaidi kwa mtu aliyeng'atwa mguuni. Kumruhusu atembee umbali mrefu kwenda hospitali kunaweza kuongeza harakati za misuli ya mguu na pia kunaweza kuongeza uchovu na hatari ya kuanguka.


Kwa hiyo, kama usafiri unapatikana, ni bora kumbeba au kumpeleka kwa njia inayomfanya asitumie kiungo kilichoumwa. Ikiwa kuna huduma ya dharura, iombe mapema badala ya kumlazimisha kutembea.

3. Kwa nini si vizuri kumfunga mtu mkanda(kamba au mpira) baada ya kuumwa na nyoka?

Mpira au mikanda inayobana sana inaweza kuzuia damu kufika kwenye sehemu ya mwili iliyo chini yake. Ikikaa kwa muda mrefu, inaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa tishu na kuongeza hatari ya kupoteza kiungo.


Pia, kuondoa mpira uliyobana sana kunaweza kuwa na madhara katika mazingira fulani kwa sababu ya mabadiliko ya ghafla katika mtiririko wa damu na kuachiliwa kwa vitu vilivyokusanyika kwenye tishu. Ndiyo maana miongozo inapendekeza kutotumia toniketi ya ateri kwa huduma ya kwanza ya kuumwa na nyoka.


Kuna mbinu maalumu inayoitwa pressure immobilization ambayo inaweza kutumika kwa baadhi ya kuumwa na nyoka wenye sumu ya mfumo wa fahamu, lakini si mbinu ya jumla kwa kila nyoka na haifai kwa kuumwa kunakosababisha uharibifu mkubwa wa tishu. Inapaswa kufanywa kwa kuzingatia mwongozo unaofaa wa eneo husika.

4. Kwa nini mtu hatakiwi kukata kidonda ili kutoa sumu?

Kukata kidonda hakutoi kiasi cha maana cha sumu ambacho tayari kimeingia kwenye tishu au mfumo wa damu. Badala yake, kunaweza kuongeza damu inayotoka, kuharibu mishipa ya damu na tishu na kuongeza hatari ya maambukizi.


Pia, jeraha lililokatwa linaweza kufanya hali iwe ngumu zaidi kwa mtaalamu wa afya kulitathmini na kulihudumia. Hakuna faida ya kuendelea kukata kidonda wakati jambo muhimu ni kuzuia harakati na kumfikisha mgonjwa hospitali.


Kwa hiyo, usiikate ngozi, usichome kidonda na usijaribu kukamua sumu. Muda unaotumika kufanya hivyo ni bora utumike kumpeleka mtu kwenye huduma ya afya.

5. Kwa nini baadhi ya watu hupata kupooza baada ya kuumwa na nyoka?

Baadhi ya sumu za nyoka huathiri mfumo wa fahamu na kuzuia mawasiliano ya kawaida kati ya mishipa ya fahamu na misuli. Hii inaweza kuanza kwa udhaifu wa misuli, kope kulegea, kuona mara mbili au kushindwa kuongea na kumeza.


Ikiwa madhara yataendelea, misuli inayosaidia kupumua inaweza kudhoofika. Mtu anaweza hivyo kuhitaji msaada wa kupumua na huduma ya haraka ya hospitali.


Ndiyo maana mtu aliyeumwa na nyoka hapaswi kuachwa peke yake akidai kwamba “bado anaonekana mzima.” Mfuatilie hali yake wakati wa kusafirishwa na ukiwaona dalili za kupumua kuwa mbaya, tafuta msaada wa dharura mara moja.

6. Kwa nini mtoto aliyeumwa na nyoka anaweza kuwa katika hatari zaidi kuliko mtu mzima?

Kiasi kilekile cha sumu kinaweza kuwa na athari kubwa zaidi kwa mtu mwenye uzito mdogo wa mwili. Watoto kwa kawaida wana uzito mdogo kuliko watu wazima, hivyo baadhi ya madhara ya sumu yanaweza kuwa makubwa zaidi na kuendelea kwa kasi.


Mtoto pia anaweza kushindwa kueleza vizuri dalili anazohisi au kutambua umuhimu wa kutulia. Anaweza kuogopa na kuanza kukimbia au kulia sana, jambo linaloongeza harakati za mwili.


Kwa hiyo, mtoto aliyeng'atwa na nyoka anahitaji kuondolewa kwenye hatari, kutulizwa, kutosogezwa na kupelekwa kwenye huduma ya afya haraka. Usisubiri kuona uvimbe mkubwa kabla ya kuchukua hatua.

7. Kwa nini mtu aliyeng'atwa na nyoka anaweza kutapika, na anapaswa kuwekwa vipi?

Kutapika kunaweza kutokea kutokana na athari za sumu, hofu, maumivu au mabadiliko mengine yanayotokea mwilini. Tatizo kubwa ni kwamba mtu mwenye udhaifu au kupoteza fahamu anaweza kuvuta matapishi kwenda kwenye njia ya hewa.


Miongozo inapendekeza kwamba mtu anayehitaji kulala wakati wa kusafirishwa, hasa ikiwa kuna hatari ya kutapika, awe katika pozi la kupona akiwa amelalia ubavu, ili kusaidia kulinda njia ya hewa.


Ikiwa mtu amepoteza fahamu na hapumui kawaida, hali hiyo inabadilika kuwa dharura ya kupumua na CPR inapaswa kuanzishwa. Katika hali kama hiyo, usicheleweshe msaada wa kuokoa maisha kwa kuendelea kuangalia kidonda cha nyoka.

8. Je, ni muhimu kumtambua nyoka aliyemng'ata mtu?

Kumtambua nyoka kunaweza kusaidia wataalamu kuelewa aina ya sumu inayoweza kuhusika na aina ya antivenom inayofaa katika maeneo ambako utambuzi wa nyoka unatumika katika maamuzi ya matibabu.


Hata hivyo, usalama ni muhimu kuliko kumtambua nyoka. Usimfuate, usimshike, usimkamate wala usimkaribie ili kupata picha. Nyoka anaweza kumng'ata mtu mwingine hata kama anaonekana amekufa au ametulia.


Ikiwa picha inaweza kupigwa kutoka umbali salama bila kuchelewesha safari ya kwenda hospitali, inaweza kuchukuliwa. Vinginevyo, mwambie mtaalamu maelezo yoyote unayoyakumbuka bila kuhatarisha maisha ya mtu mwingine.

9. Kwa nini antivenom haipewi kila mtu aliyeng'atwa na nyoka?

Antivenom ni tiba maalumu inayolenga sumu za nyoka, lakini si kila kuumwa husababisha kuingia kwa sumu yenye madhara. Pia, antivenom inapaswa kuchaguliwa kulingana na aina ya sumu inayohusika na upatikanaji wa bidhaa inayofaa katika eneo hilo.


Kutoa antivenom bila sababu ya kitabibu kunaweza kumweka mtu kwenye hatari za matibabu, kwa hiyo uamuzi wa kuitumia hufanywa na wataalamu baada ya kumchunguza mgonjwa na kutathmini dalili za envenoming.


Hii ndiyo sababu hospitali inaweza kumchunguza na kumfuatilia mtu aliyeng'atwa hata kama anaonekana vizuri, badala ya kumpa antivenom moja kwa moja. Matibabu mengine ya kusaidia kupumua, kudhibiti damu au kutibu madhara ya tishu yanaweza pia kuhitajika kulingana na aina ya sumu.

10. Mtu akifika hospitali bila dalili, bado anaweza kuhitaji kuchunguzwa?

Ndiyo. Kutokuwa na dalili kali mara moja hakumaanishi kwamba madhara hayawezi kutokea baadaye. Aina tofauti za sumu zina muda tofauti wa kuanza kuonyesha madhara, na baadhi ya madhara yanaweza kuendelea kuongezeka baada ya kuumwa.


Katika hospitali, mtaalamu anaweza kufuatilia hali ya kupumua, mzunguko wa damu, mfumo wa fahamu, uvimbe, kutokwa damu na dalili nyingine kulingana na aina ya kuumwa. Vipimo vinaweza kufanywa inapohitajika ili kutathmini madhara ya sumu.


Kwa hiyo, usimrudishe mtu nyumbani kwa sababu tu maumivu yamepungua au hakuna uvimbe mkubwa. Kipaumbele baada ya kuumwa na nyoka anayeshukiwa kuwa na sumu ni kufika kwenye huduma ya afya mapema na kufuata ufuatiliaji utakaoelekezwa na wataalamu.


ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba'  chini ya tovuti hii

Imeandikwa;

23 Agosti 2026, 12:27:30

Rejea za mada:

bottom of page