top of page

Mwandishi:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

9 Agosti 2026, 14:45:41

Sepsisi

Sepsisi

Sepsisi ni hali hatari ya kitabibu inayotokea pale mwili unapokuwa na mwitikio usiodhibitiwa dhidi ya maambukizi, na mwitikio huo kusababisha kuharibika kwa utendaji wa kiungo kimoja au zaidi cha mwili. Sepsisi ni dharura ya kitabibu inayohitaji matibabu ya haraka kwani inaweza kuhatarisha maisha.


Sepsisi inaweza kusababishwa na maambukizi yanayoanzia sehemu mbalimbali za mwili, kama vile mapafu, mfumo wa mkojo, tumbo, ngozi au ubongo. Ingawa bakteria ndio chanzo cha kawaida, sepsisi inaweza pia kusababishwa na virusi, fangasi au vimelea wengine.


Dalili za sepsisi zinaweza kujumuisha homa au kushuka kwa joto la mwili, mapigo ya moyo kwenda kasi, kupumua haraka, kuchanganyikiwa, usingizi kupita kiasi, shinikizo la damu kushuka na kupungua kwa mkojo. Isipotibiwa mapema, sepsisi inaweza kuendelea na kusababisha mshtuko wa sepsisi, kushindwa kufanya kazi kwa viungo muhimu na kifo.


Kumbuka: Sepsisi si sawa na bakteremia (uwepo wa bakteria kwenye damu). Mtu anaweza kuwa na bacteremia bila kupata sepsisi, na pia anaweza kupata sepsisi hata kama bakteria hawajapatikana kwenye damu.


Tazama pia: Bakteremia, Mshituko wa sepsisi, Maambukizi, UTI, Kushindwa kwa ogani.

Imeandikwa:

21 Julai 2026, 05:38:47

bottom of page