top of page

Mwandishi:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

9 Agosti 2026, 17:44:56

Traiglaiseraidi

Traiglaiseraidi

Traiglaiseraidi watu wengine wakitamka pia kama triglaiseraidi ni aina ya mafuta yanayopatikana kwenye damu na mwilini. Mwili huyatumia kama chanzo cha nishati, na kiasi cha ziada cha nishati kutoka kwenye chakula kinaweza kubadilishwa kuwa traiglaiseraidi na kuhifadhiwa kwenye tishu za mafuta.


Kwa mtu mzima, kiwango cha traiglaiseraidi kwenye damu hupimwa kwa mg/dL au mmol/L na hutafsiriwa kwa ujumla kama ifuatavyo:

  • Chini ya 150 mg/dL (chini ya 1.7 mmol/L): Kawaida

  • 150–199 mg/dL (1.7–2.2 mmol/L): Juu kidogo

  • 200–499 mg/dL (2.3–5.6 mmol/L): Juu

  • 500 mg/dL (5.6 mmol/L) au zaidi: Juu sana


Kiwango cha traiglaiseraidi kinaweza kuongezeka kutokana na uzito kupita kiasi, ulaji mwingi wa sukari na wanga uliosindikwa, unywaji wa pombe, kutofanya mazoezi, kisukari kisichodhibitiwa, baadhi ya magonjwa na baadhi ya dawa. Pia kuna watu ambao huwa na viwango vya juu kutokana na sababu za kurithi.


Traiglaiseraidi nyingi mara nyingi hazisababishi dalili, hivyo kipimo cha damu ndicho njia kuu ya kugundua hali hii. Hata hivyo, kiwango cha juu sana, hasa 500 mg/dL au zaidi, huongeza hatari ya uvimbekinga wa kongosho, hali inayoweza kusababisha maumivu makali ya tumbo.


Matibabu hutegemea kiwango cha traiglaiseraidi na chanzo chake. Anaweza kushauriwa mgonjwa kupunguza uzito, kufanya mazoezi, kupunguza vyakula vyenye sukari nyingi na wanga uliosindikwa, kuepuka au kupunguza pombe na kudhibiti kisukari. Baadhi ya wagonjwa huhitaji dawa kulingana na kiwango cha traiglaiseraidi na hatari yao ya kupata ugonjwa wa moyo.


Kumbuka: Traiglaiseraidi inapaswa kutathminiwa pamoja na lehemu(kolestro) nyepesi, lehemu(kolestro) nzito na jumla ya kolestroli yotekwenye damu, kwa sababu mabadiliko katika aina hizi za mafuta yanaweza kutokea pamoja na kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa.

Imeandikwa:

9 Agosti 2026, 17:44:55

bottom of page