top of page

Mwandishi:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

21 Julai 2026, 08:01:40

Uvimbe wa umio

Uvimbe wa umio

Uvimbe wa umio ni ukuaji usio wa kawaida wa seli ndani ya umio, ambao ni mrija unaosafirisha chakula kutoka kooni kwenda tumboni. Uvimbe huu unaweza kuwa usio wa saratani au wa saratani. Aina inayojulikana zaidi ni saratani ya umio, ambayo inaweza kuathiri uwezo wa mtu kumeza chakula kadri inavyokua.


Dalili kuu za uvimbe wa umio ni ugumu wa kumeza chakula (disfagia), hasa chakula kigumu mwanzoni na baadaye hata vinywaji, maumivu wakati wa kumeza (odinofagia), hisia ya chakula kukwama kifuani au kooni, kupungua uzito bila sababu, kukosa hamu ya kula, maumivu ya kifua, sauti kuwa ya kukwaruza na kukohoa sugu. Dalili huweza kuanza taratibu na mara nyingi huonekana zaidi uvimbe unapokuwa mkubwa.


Chanzo cha uvimbe wa umio hutegemea aina yake. Saratani ya umio huhusishwa na sababu kama matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi, ugonjwa wa kucheua tindikali (GERD) wa muda mrefu unaoweza kusababisha umio la Barrett, unene kupita kiasi na baadhi ya mabadiliko ya seli za umio. Uchunguzi hufanyika kwa kutumia endoskopi(kamera ya maalumu) ya njia ya juu ya chakula ambapo daktari huangalia umio na kuchukua sampuli ya tishu (bayopsi) kwa uchunguzi wa maabara. Vipimo vingine kama CT scan, PET scan au ultrasound ya kuangalia ndani ya umio vinaweza kusaidia kujua ukubwa na kuenea kwa uvimbe.


Matibabu hutegemea aina ya uvimbe, ukubwa wake na hatua ya ugonjwa. Njia zinazoweza kutumika ni pamoja na upasuaji wa kuondoa sehemu ya umio yenye uvimbe, tiba ya mionzi, dawa za kuua saratani (chemotherapy), tiba lengwa (targeted therapy) au tiba ya kinga ya mwili (immunotherapy) kwa baadhi ya wagonjwa. Uvimbe usio wa saratani unaweza kufuatiliwa au kuondolewa endapo unasababisha dalili.


Kumbuka: Uvimbe wa umio ni tofauti na akalazia (Akalasia). Katika akalazia, tatizo si uvimbe bali ni kushindwa kwa misuli ya mwisho wa umio kulegea vizuri, hivyo chakula hukwama kwa sababu ya tatizo la mwendo wa umio. Hata hivyo, hali zote mbili zinaweza kusababisha dalili inayofanana ya ugumu wa kumeza.


Tazama pia: Akalazia (Akalasia), Disfagia, Maumivu wakati wa kumeza (Odinofagia), Kipimo cha kumeza bariamu, manometri ya umio, Ugonjwa wa kucheua tindikali (GERD), Umio.

Imeandikwa:

21 Julai 2026, 08:01:40

bottom of page