Kamusi Tiba ya ULY CLINIC
Kipimo cha kuotesha majimaji ya mrija wa mkojo
Pia huitwa kipimo cha kuotesha vimelea kwenye majimaji ya mrija wa mkojo, ni kipimo cha maabara kinachotumika kutafuta na kutambua bakteria wanaoweza kusababisha maambukizi kwenye mrija wa mkojo. Sampuli ya majimaji kutoka kwenye mrija wa mkojo hukusanywa kwa kutumia kijiti cha sampuliĀ au njia nyingine inayofaa, kisha hupelekwa maabara kwa ajili ya kuotesha na kutambua bakteria.
Kipimo cha kuotesha majimaji ya perikadiamu
pia huitwa kipimo cha kuotesha vimelea kwenye majimaji ya perikadiamu, ni kipimo cha maabara kinachotumika kutambua bakteria au vimelea wengine wanaoweza kusababisha maambukizi kwenye mfuko unaozunguka moyo (perikadiamu). Sampuli ya majimaji ya perikadiamu huchukuliwa kwa utaratibu unaoitwa perikadiosentesisi, kisha hupelekwa maabara kwa ajili ya kuotesha na kutambua vimelea.
Kipimo cha kuotesha majimaji ya peritoniamu
Pia huitwa kipimo cha kuotesha vimelea kwenye majimaji ya peitoniamu, ni kipimo cha maabara kinachotumika kutambua bakteria au vimelea wengine wanaoweza kusababisha maambukizi ndani ya tundu la tumbo. Sampuli ya majimaji ya peitoniamu huchukuliwa kwa utaratibu unaoitwa parasentesisi, hasa kwa mtu mwenye majimaji mengi tumboni (ascites) au anayeshukiwa kuwa na maambukizi ndani ya tundu la tumbo.
Kipimo cha kuotesha majimaji ya pua
Pia huitwa kipimo cha kuotesha vimelea kwenye majimaji ya pua, ni kipimo cha maabara kinachotumika kutambua bakteria wanaoweza kuwepo au kusababisha maambukizi katika eneo la pua. Sampuli huchukuliwa kutoka ndani ya pua kwa kutumia kijiti cha sampuli, kisha hupelekwa maabara kwa ajili ya kuotesha na kutambua bakteria wanaopatikana.
