Kamusi Tiba ya ULY CLINIC
Thairotoksikosisi
Ni hali ambapo mwili unakuwa na kiwango kikubwa cha homoni za tezi ya shingo kwenye damu, hali inayofanya shughuli za mwili kwenda kwa kasi kuliko kawaida. Homoni hizi hutengenezwa na tezi ya shingo na husaidia kudhibiti matumizi ya nishati, joto la mwili na kasi ya kazi za viungo mbalimbali.
Mesothelioma
Ni aina ya saratani inayotokea kwenye mesotheliamu, yaani utando mwembamba unaofunika baadhi ya viungo vya ndani ya mwili. Aina inayojulikana zaidi ni mesothelioma ya pleura, inayotokea kwenye utando unaozunguka mapafu. Aina nyingine zinaweza kutokea kwenye utando unaozunguka tumbo au viungo vya uzazi.
Bronkolaitisi
Ni hali ya kuvimba kwa mirija midogo ya hewa ndani ya mapafu, inayojulikana kama bronkioli. Kuvimba huku husababisha mirija hiyo kuwa nyembamba na kufanya hewa kuingia na kutoka kwenye mapafu kwa shida. Bronkolaitisi huonekana zaidi kwa watoto wadogo, hasa walio chini ya miaka 2, na mara nyingi husababishwa na maambukizi ya virusi.

Kidole Rungu
Ni hali ambapo ncha za vidole huongezeka ukubwa na kuwa pana na za mviringo, huku kucha zikiwa zimejikunja zaidi na kuwa na mwonekano wa mviringo. Si ugonjwa wenyewe bali ni ishara inayoweza kuhusishwa na magonjwa mbalimbali, hasa magonjwa sugu ya mapafu kama saratani ya mapafu, maambukizi sugu ya mapafu na baadhi ya magonjwa ya tishu za mapafu.
