top of page

Imeandikwa na daktari wa ULY CLINIC

 

Tatizo la kujing’ata ulimi

 

Ulimi ni msuli muhimu sana kwa binadamu, huonekana kuwa na msaada mkubwa katika suala la kula chakula kwa kuchanganya chakula pamoja na mate na kukisogeza chakula karibu na meno pia kukipeleka nyuma ya koo kwa ajili ya kukurahisishia ukimeze. Bila ulimi ingekuwa ngumu sana kula chakula. Mbali na kazi hiyo ulimu huwa muhimu kutengeneza matamshi na upumuaji.

Kujingata ulimi huweza kutokea sana wakati wa kula, huambatana na maumivu makali sana na kuleta vidonda. Kila mtu katika maisha yake anapofikia umri wa miaka 30 anaweza kuwa ameshajingata ulimi, idadi hutegemea na visababishi. Makala hii imezungumzia kujingata ulimi kwa ujumla. Soma makala ingine kuhusu kujingata ulimi wakati umelala kwa kubonyeza hapa.

 

Visababishi

 

Visababishi vinafofahamika kuleta tatizo la kujingata ulimi ni pamoja na;

 • Ajali ya gari, baiskeli n.k

 • Kuanguka

 • Majeraha kutokana na michezo mbalimbali

 • Kupigana

 • Degedege na kifafa

 • Tabia ya mtu kung’ata ulimi kama vile ilivyo tabia ya kung’ata kucha

 • Mijongeo isiyo hiari ya misuli ya kinywa wakati umelala

 • Kutafuta harakaharaka

 • Kutafuta kinywa wakati umelala

 

Utambuzi wa tatizo

 

Endapo umejingata ulimi na kufika hospitali, daktari atakuchunguza kwa kutazama ulimi wako, umbo la kidonda na mipaka yake. Endapo umejing’ata ulimi wakati wa usiku daktari atataka kujua zaidi visababishi kwa kuuliza maswali(soma kwenye makala ya kujing’ata ulimi wakati umelala)

 

Matibabu

 

Mara nyingi kujing’ata ulimi huwa hakuhitaji matibabu isipokuwa dawa za kutuliza maumivu endapo mgonjwa ana amaumivu makali. Hata hivyo kuna hali zinaweza kusbabisha uhitaji kupata matibabu ya haraka endapo mgonjwa ana mambo yafuatayo;

 • Kutokwa na damu nyingi

 • Mpasuko mkubwa kwenye ulimi

 • Mapigo ya moyo kwenda haraka kutokana na kupoteza damu

 • Kupumua kwa shida

 • Ngozi ya mwili kupauka

 • Dalili za maambukizi kwenye ulimi

Daktari atakupatia tiba kwa kukupa dawa au kufanya upasuaji mdogo wa kushona mpasuko kwenye ulimi. Utapewa dawa za maumivu pamoja au pasipo dawa za antibayotiki.

 •  

 

Kujikinga

 

 • Funga mkanda unapokuwa unatumia usafiri wa gari

 • Vaa vifaa muhimu vya kukinga kinywa kuumia endapo unajihusisha kwenye michezo ya kupigana na mengine ya hatari inayoweza kusabaisha ujing’ate ulimi mfano helmeti n.k

 • Weka mazingira yako yasiwe ya kuteleza kuzuia kuanguka, ondoa vihatarishi kwa watoto wasianguke

 • Kuwa makini wakati wa kutafuna, tafuta taratibu na wafundishe wanao pia

 • Kwa wanaojing’ata ulimi wkati wa kulala, hakikisha unaonana na daktari wako kujua kisababishi na upate matibabu kulingana na kisababishi

 

Madhara ya kujing’ata ulimi

 

Madhara yanayoweza kutokea huwani;

 • Vidonda kwenye ulimi

 • Maambukizi kwenye ulimi

 • Maumbile ya ulimi kuharibika

 • Kuziba kwa njia ya hewa

 • Ulimi kushindwa kufanya kazi vema

Mara baada ya kujingata ulimi, ni vyakula gani unashauriwa kula ili kupona haraka?

 

Kwa kawaida, ulimi hupona ndani ya siku hadi wiki chacheharaka mara baada ya kujing’ata. Unashauriwa kutumia vyakula laini ili kufanya upone haraka. Hata hivyo vyakula vifuatavyo havishauri kutumika kwa sababu huchelewesha uponyaji;

 

 • Matunda na Vyakula vyenye tindikali kwa wingi kama limau, chungwa n.k

 • Nyanya na mazao yatokanayo na nyanya

 • Vyakula vyenye chumvi nyingi na viungo

 • Kutumia tumbaku au sigara

 • Pombe

 

ULY CLINIC inakushauri siku zote wasiliana na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba inayoendana na tatizo lako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile.

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubonyeza Pata Tiba au piga namba za simu chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa mara ya mwisho 18.07.2020

 

Rejea za mada hii,

 

 1. Tongue bite. https://www.medicalnewstoday.com/articles/bit-tongue#diagnosis. Imechukuliwa 18.07.2020

 2. Kifafa. ULY CLINIC. https://www.ulyclinic.com/dalili-za-ugonjwa/Dalili-za-kifafa. Imechukuliwa 18.07.2020

 3. Willey online library. https://onlinelibrary.wiley.com/doi/abs/10.1111/j.1600-0722.2004.00114.x. Imechukuliwa 18.07.2020

 4. Epilepsy and behavior. Tongue bitting during in epileptic seizure. https://linkinghub.elsevier.com/retrieve/pii/S1525505012004507. Imechukuliwa 18.07.2020

 5. RDH. Tongue chewing. https://www.rdhmag.com/pathology/oral-pathology/article/16406588/tongue-chewing. Imechukuliwa 18.07.2020

 6. WHO. Epilepsy. https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/epilepsy. Imechukuliwa 18.07.2020

bottom of page