Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Benjamin L, MD
Dkt. Salome A, MD
Alhamisi, 12 Mei 2022

Herpes sehemu za siri
Ni moja ya ugonjwa wa zinaa unaotokea sana na unasababishwa na maambukizi ya kirusi Herpes (HSV) hasa aina ya pili yaani HSV2. Ugonjwa huu huenezwa awali kwa njia ya kujamiiana.
Baada ya maambukizi kirusi hujificha mwilini na kutoleta dalili za ugonjwa kwa muda mrefu. Baadhi ya nyakati virusi hawa huamka na kuleta dalili kisha kujificha, hali hii huendelea kwa muda mrefu.
Dalili za maambukizi ya kirusi Herpes wa sehemu za siri
Baadhi ya watu wanaweza wasionyeshe dalili yoyote ile, na endapo mtu ataonyesha dalili huweza kuwa kati ya zifuatazo;
Maumivu sehemu za siri
Muwasho sehemu za siri au hisia za kuungua na kuchomachoma
Malengelenge sehemu za siri yanayoweza kutokea sehemu yoyote ya uume au uke
Vidonda sehemu za siri baada ya kupasuka kwa lenge
Makovu sehemu za siri
Magamba shemu za siri
Maumivu ya mgongo makalio na miguu kama ugonjwa umejirudia
Dalili zingine zinazoweza kuambatana ni
Homa
Maumivu ya mwili
Kuvimba kwa mitoki
Uenezaji
Ugonjwa wa herpes sehemu za siri huenezwa awali kwa kufanya ngono, na mtu mwenye maambukizi hata kama haonyeshi dalili yoyote. Ngono inaweza kuwa ya ume kwa uke, ume kwa njia ya haja kubwa, ume kwa mdomo au mdomo kwa uke.
Maambukizi hutokea endapo mgusano utatokea kati ya majimaji ya vidonda au malengelenge ya sehemu za siri, ngozi ya sehemu za siri au njia ya haja kubwa hata kama haionyeshi kuwa na vidonda.
Maambukizi yanaweza kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine endapo utashika kidonda au sehemu iliyoathiriwa na kirusi kisha kujishika kwenye maeneo mengine ya;
Macho
Njia ya haja kubwa
Midomo
Tundu la mkojo
Ngozi ya korodani
Shina la uume
Mashavu ya uke
Njia zingine
Njia nyingine ya uenezaji wa ugonjwa huu ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua
Madhara ya ugonjwa wa herpes sehemu za siri
Hatari yakupata UKIMWI.
Ugonjwa huu huongeza hatari ya kupata UKIMWI mara tatu zaidi na magonjwa menfine ya zinaa. Mgonjwa mwenye maambukizi ya pamoja ya UKIMWI pamoja na Herpes sehemu za siri, hueneza kwa kasi magonjwa hayo kwa wengine.
Kupata maambukizi makali
Kwa mtu mwenye kinga ya mwili ya chini ikiwa pamoja na mtu aliye kwenye hatua za mwisho za UKIMWI, hupata maambukizi makali ya ugonjwa huu yanayoweza kusambaa kwenye uti wa mgongo pamoja na ubongo hivyo kuleta homa ya uti wa mgongo, na homa a ubongo.
Magonjwa ya mfumo wa neva na vifo
Kwa watoto ambao wamezaliwa na herpes, hupata madhara ya muda mrefu kwenye mfumo wa fahamu na baadhi yao hufariki katika kipindi cha uchanga.
Magonjwa ya mfumo wa mkojo
Kuziba kwa njia ya mkojo kutokana na kuota kidonda kwenye mrija wa mkojo
Matatizo kwenye nji ya haja kubwa
Michomo kwenye njia ya haja kubwa haswa kwa wanaume wanaoshiriki ngono ya jinsia moja( au kwa wale waliohamisha maambukizi kwa kujishika kwenye njia ya haja kubwa)
Matibabu
Mpaka sasa hakuna tiba ya kutokomeza ugonjwa huu mara baada ya kupata maambukizi hata kama hujapata dalili baada ya kuambukizwa. Zipo tiba za kupunguza dalili tu na makali ya ugonjwa kwa kutumia dawa za kudhibiti uzalianaji wa kirusi ambazo utaandikiwa na daktari wako. Matumizi ya dawa hizo huweza kuzuia kueneza maambukizi kwa wengine.
Kinga
Njia zifuatazo zinaweza kutumika kama kinga;
Kutumia kondomu kama njia ya kuzuia kupata na kueneza maambukizi kwa wengine kila mara unaposhiriki ngono
Endapo una dalili za ugonjwa huu unashauriwa kutoshiriki ngono mpaka pale utakapopona
Kuepuka kushiriki ngono na mpenzi ambaye ana maambukizi au vidonda sehemu za siri