top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Jumapili, 4 Julai 2021

Polisaithemia

Polisaithemia

Kuwa na damu nyingi hufahamika kwa jina jingine la polisaithimia (polycythemia) ni tatizo linalotokea endapo kiwango cha himoglobin ni kingi kuliko kawaida ya umri au jinsia ya mtu. Kwa mwanaume mtu mzima kiwango kikizidi gramu 16.5 kwa desilita moja ya damu (16.5g/dL) au kuzidi 16g/dL kwa mwanamke mtu mzima hufaa kuitwa tatizo la polisaithemia au damu nyingi. Kiwango cha damu cha kwaida kwa watoto kimeandikwa sehemu nyingine katika tovuti hii.


Katika makala hii utasoma kuhusu kuhusu polisithemia ya awali kwa jina jingine la polisaithemia vera na polisaithemia ya sekondari.


Dalili


Dalili za kuwa na damu nyingi kupita kawaida mwilini ni;


 • Muwasho

 • Maumivu ya kichwa

 • Kizunguzungu

 • Kupata majeraha kirahisi au kutokwa na damu kirahisi

 • Kutokwa na jasho zaidi ya kawaida

 • Maumivu na kuvimba kwa maungio

 • Kupungua uzito bila sababu

 • Njano kwenye macho na ngozi

 • Kuchoka

 • Maumivu ya tumbo

 • Alama za zambarau au nyekundu kwenye ngozi

 • Wakati gani wa kutafuta msaada wa dataktari haraka mwenye damu nyingi?

 • Endapo unatatizo la damu nyingi na unapata dalili zifuatazo, unapaswa kuonana na daktari haraka kwa uchunguzi na tiba;

 • Kutokwa na damu muda mrefu

 • Kuvimba endelevu kwa maungio

 • Kupumua kwa shida

 • Kuishiwa pumzi

 • Dalili za kiharusi kama kushindwa kuongea au kuwa dhaifu sehemu moja ya mwili


Visababishi


Visababishi vya polisithemia vinaweza kuwa vya awali au sekondari. Visababishi vya awali vinahusisanishwa na mabadiliko kwenye jeni JAK2 ya mifupa inayopelekea uzalishaji endelevu wa damu na huweza kurithiwa. Bado haijulikani kwanini mabadiliko haya yanatokea na pia ugonjwa unaotokana na mabadiliko hayo huitwa polisaithimia vera.


Visababishi vya sekondari hutokana na sababu zinazopunguza kiwango cha oksijeni kwenye tishu, kwa jina la haipoksia ya tishu au matumizi ya homon erythropoietin. Sababu mbalimbali zinaweza pelekea polisaithimia ya sekondari ni;


 • Magonjwa ya mapafu na moyo

 • Saratani ya figo, ini, na mfuko wa kizazi na polisaithimia vera

 • Uvutaji sigara

 • Upungufu wa maji mwilini

 • Msongo

 • Matumizi ya homon erythropoietin bila sababu ya msingi


Tatizo la kurithi la polisaithimia vera

Tatizo hubebwa kwenye jeni na mtoto anaweza kuzaliwa nalo. Hata hivyo kuna visababishi vingine ambavyo mtu anaweza kupata ugonjwa wa polisaithimia vema isiyo ya kurithi.


Saratani ya polisaithimia vera

Husababisha uboho wa mifupa kuzalisha chembe nyekundu za damu kwa wingi.


Kuishi mbali na usawa wa bahari.

Maeneo ya nyanda za juu na milimani huwa na kiwango kidogo cha oksijeni, mwili hutambua hilo na hivyo kuanza kuzalisha himoglobin (damu) kwa wingi ili kuweza kubeba oksijeni ya kutosha kwa ajili ya mwili wako. Hii inadhihirisha kuwa mwili wa binadamu una namna ya kujirekebisha kutegemea mazingira.


Uvutaji wa tumbaku au sigara

Uvutaji wa sigara husababisha chembe nyekundu za damu kubeba kabondayoksaidi kwa muda mrefu na hivyo mwili hutambua kama kuna upunfugu wa damu na kuamrisha ongezeko la uzalishaji wa damu.


Msongo

Msongo wa mwili pia husababisha kupungua kwa kiwango cha plasma, sehemu ya maji maji ya damu. upungufu wa majimaji kwenye damu husababisha mzunguko wa damu unaosafirisha oksijeni na virutubisho mwilini kuwa mdogo na hivyo figo huongeza uzalishaji wa homon erythropoietin ili kukabiliana nao. Hutokea kwa vijana wa umri wa kati wenye nguvu na shauku kuu na maisha.


Tatizo sugu la kuziba kwa mfumo wa upumuaji (COPD)

Ni mkusanyiko wa magonjwa ya imphizima, Bronchaitiz na bronnkiektasis. Ugonjwa huu hupelekea michomo kwenye njia za hewa inayozuia hewa ya oksijeni kusafiri vema na kuingia kwenye damu. hii hupelekea mwili kuhisi kiwang cha himoglobin hakitoshi na hivyo kuongeza uzalishaji wa damu.


Magonjwa ya moyo

Magonjwa ya moyo na mapafu yanayozuia uwezo wa mapafu kupumua au moyo kusukuma damu kwenda kwenye chembe hai, husababisha mwili hutambua upungufu wa oksijeni na hivyo kuongeza uzalishaji wa damu. mfano wa magonjwa ni fuferi kwa moyo.


Matumizi ya dawa erythropoietin

Kutumia homoni erythropoietin kama dawa bila kuwa na sababu maalumu hupelekea mwili kuzalisha damu kwa wingi. Kwa kawaida watu wenye upungufu wa damu kutokana na magonjwa ya figo au mapafu hupewa erythropoietin inayoamrisha mifupa kuzalisha au kupunguza uzalishaji wa damu. Endapo mtu atatumia bila kuwa na upungufu wa damu, hupelekea damu kuwa nyingi kuliko kawaida.


Magonjwa na saratani zinazozalisha homoni erythropoietin

Saratani ya figo, ini, kizazi na adenokasinoma huzalisha homon erythropoietin kwa wingi inayopelekea ongezeko la uzalishwaji wa chembe nyekundu za damu kupita kiasi.

Baadhi ya nyakati, magonjwa ya figo kama haidroneflosis na vifuko maji kwenye figo, huweza pelekea uzalishaji wa homon erythropoietin kwa wingi na hatimaye kusababisha tatizo la damu nyingi.

Uchunguzi na vipimo tambuzi


Mara nyingi wingi wa damu mwilini hutambuliwa kwa bahati mbaya pale daktari anapoagiza vipimo vya damu kuchunguza visababishi vya dalili ulizonazo. Hata hivyo kabla ya kuagiza vipimo, daktari atakuuliza historia ya tatizo lako kwa maswali mbalimbali ya kitaalamu kisha kukufanyia uchunguzi wa mwili wako na baadaye ataagiza kufanyika kwa vipimo mbalimbali kutokana na kisabababishi alichokishuku au anavyotaka kuvitoa kuwa si sababu.


Kipimo pekee cha kutambua kisababishi cha damu nyingi ni kipimo cha mabadiliko kwenye jeni JAK2

Endapo vipimo vingine vitaagizwa huwa pamoja na;


 • Kipimo cha picha halisi ya damu (FBP)

 • Kipimo cha kiwango cha homon erythropoietin

 • Kipimo cha ufanyaji kazi wa figo (RFT)

 • Kipimo cha ufanyaji kazi wa ini (LFT)

 • Vipimo vya ufanyaji kazi wa mapafu

 • Vipimo vya picha sauti ya Ini, figo)

 • Vipimo vya picha mionzi ya Ini, Mapafu au figo

 • Kipimo cha MRI au CT scan ya Mapafu, Ini, figo au moyo


Kumbuka vipimo vitategemea kisababishi ambacho kimeshukiwa kutokana na historia na dalili za tatizo lako zilizoonwa na daktari.


Matibabu


Matibabu ya damu nyingi hutegemea kisababishi, kuna matibabu ya dawa, upasuaji na kubadili mazingira au mfumo wa maisha;


Kubadili mazingira

Endapo kisababishi ni kuishi kwenye maeneo ya nyanda za juu, utahitaji kubadili mazingira, yaani kwenda kuishi maeneo ya usawa wa bahari au kukushauri uwe unapunguza damu kwa kutoa damu.

Kama unafanya kazi kwenye hewa ya ukaa (kabonmonoksaidi) unapaswa kuhama mazingira hayo au kutafuta kazi nyingine ili kuepuka tatizo hii


Matibabu dawa

Kuna dawa zinazotumika kuzuia uzalishaji wa damu nyingi jamii ya chemotherapi baadhi yake ni;


 • Chlorambucil

 • Radiophosphorus

 • Pipobroman

 • Anagrelide


Hata hivyo matumizi yake yanaambatana na madhara mengi hivyo wataalamu wengi huwa hawachagui matibabu hayo


Dawa mpya za kupunguza uzalishaji wa damu

Dawa mpya zinazoonekana kuwa na madhara kiasi nab ado zipo kwenye tafiti ni;


 • IFN-α

 • Ruxolutinib


Dawa za kupunguza madhara ya damu nyingi

Matibabu ya dawa za kupunguza uwezekano wa kupata madhara ya damu kuganda kama dawa za hydroxyurea, aspirin au dipyridamole huwasaidia sana wagonjwa.


Dawa za kutibu magonjwa sugu

Matibabu ya damu nyingi kutokana na magonjwa sugu ya moyo na mapafu huhusisha dawa zinazotibu tatizo husika. Mgonjwa unashauriwa kutimia vema dawa zako ili kuepuka tatizo la damu nyingi.


Kubadili mtindo wa maisha

Endapo una tatizo la damu nyingi unapaswa kubadili mtindo wa maisha kwa kuacha kuvuta sigara, kupunguza uzito na kufanya mazoezi pamoja na kula mlo wa kiafya unaoshauriwa kwa mgonjwa mwenye damu nyingi.


Matibabu ya upasuaji

Hufanyika kwa watu wenye tatizo la maumivu ya mara kwa mara ya bandama kutokana na kuziba kwa mishipa ya damu ya bandama.


Madhara


Kuwa na damu nyingi huongeza hatari ya kupata madhara yafuaatayo;

 • Damu kuganda inayoweza kupalekea kupata kiharusi, mshituko wa moyo, embolizimu ya palmonari na kifo

 • Mawe kwenye figo

 • Gauti

 • Saratani ya damu

 • Mayelofibrosis


Endapo tatizo ni saratani ya ini au figo, utapatiwa dawa za saratani ili kuzibiti uzalishaji wa chembe nyekundu za damu.


Magonjwa yanayofanana na polisaithimia vera


Magonjwa mengine yanayoweza kufanana na polisithemia vera


 • Thrombosaithemia ya awali

 • Leukemia sugu ya mayeloginaz

 • Agnogenic myeloid metaplasia

 • Mayelofaibrosis ya awali


Namna ya kujikinga


Ili kujikinga na uzalishaji wa damu nyingi kupita kiasi, inakubidi ufanya mambo yafuatayo;


 • Pata matibabu ya magonjwa ya mapafu na moyo

 • Acha kuvuta sigara

 • Jiepushe kukaa muda mrefu kwenye maeneo yenye gesi ya cabonmonoksaidi kama machimboni, kwenye miji yenye magari mengi yanayotumia mafuta ya petrol au dizeli, gereji au kufanya kazi za kurekebisha eksozi ya gari.

 • Ishi maeneo karibu na usawa wa bahari

 • Fanya uchunguzi wa vinasaba vya polisaithimia vera kabla ya kuamua kupata mtoto.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

26 Oktoba 2021 18:22:46

Rejea za mada hii:

1. Ayalew Tefferi, et al. Polycythemia vera treatment algorithm 2018. https://www.nature.com/articles/s41408-017-0042-7. Imechukuliwa 02.07.2021

2. Xiao Lu, et al. Polycythemia Vera. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK557660/. Imechukuliwa 02.07.2021

3. Anemia in chronic kidney disease. niddk.nih.gov/health-information/kidney-disease/chronic-kidney-disease-ckd/anemia. Imechukuliwa 02.07.2021

4. Barbui T, et al. Diagnostic impact of the 2016 revised WHO criteria for polycythemia vera. DOI: 10.1002/ajh.24684. Imechukuliwa 02.07.2021

5. Lung.org. Chronic obstructive pulmonary disease (COPD). lung.org/lung-health-and-diseases/lung-disease-lookup/copd/. Imechukuliwa 02.07.2021

6. Complete blood count (CBC). labtestsonline.org/tests/complete-blood-count-cbc

7. Hematocrit. labtestsonline.org/tests/hematocrit. Imechukuliwa 02.07.2021

8. Hemoglobin. labtestsonline.org/tests/hemoglobin. Imechukuliwa 02.07.2021

9. Hypothyroidism (underactive thyroid). niddk.nih.gov/health-information/endocrine-diseases/hypothyroidism. Imechukuliwa 02.07.2021

10. Mayo Clinic Staff. High hemoglobin count.
mayoclinic.org/symptoms/high-hemoglobin-count/basics/causes/sym-20050862. Imechukuliwa 02.07.2021

11. Polycythemia vera in children. stanfordchildrens.org/en/topic/default?id=polycythemia-90-P02398. Imechukuliwa 02.07.2021

12. Maana ya Marrow. http://www.elimuyetu.co.tz/subjects/arts/eng-swa/m.html. Imechukuliwa 02.07.2021

13. Arber, D. A. et al. The2016 revision to the World Health Organization classification of myeloid neoplasms and acute leukemia. Blood 127, 2391–2405 (2016)

14. Marchioli, R. et al. Cardiovascular events and intensity of treatment in polycythemia vera. N. Engl. J. Med. 368, 22–33 (2013).

15. Landolfi, R. et al. Leukocytosis as a major thrombotic risk factor in patients with polycythemia vera. Blood 109, 2446–2452 (2007).

16. Chievitz, E. & Thiede, T. Complications and causes of death in polycythaemia vera. Acta Med. Scand. 172, 513–523 (1962).

bottom of page