top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Sospeter M, MD

Jumapili, 13 Juni 2021

Saratani ya ependimoma

Saratani ya ependimoma

Ependimoma ni aina ya saratani inayoweza kutokea kwenye seli za ependimo zinazopatikana ndani ya mfumo wa kati wa fahamu yaani ubongo au uti wa mgongo. Seli za ependimo zinapatikana ndani ya mfumo wa kati wa fahamu kwenye kuta na mifereji inayotengene na kusafirisha maji ya uti wa mgongo. Saratani ya ependimoma ni nadra sana kutokea, tafiti nyingi sasa zinafanyika kutambua matibabu pekee.


Licha ya kuweza kutokea katika umri wowote ule, saratani hii hutokea sana kwa watoto wadogo na huwapelekea kupata maumivu ya kichwa na degedege.


Endapo saratani itatokea kwa watu wazima, mara itakuwa kwenye seli zilizo kwenye uti wa mgongo badala ya ubongo, kuathiriwa kwa uti wa mgongo hupelekea kuonekana kwa dalili ya kupooza kwa sehemu zinazohudumiwa na mshipa wa fahamu ulioathirika.


Matibabu ya awali ya saratani ya ependimoma ni upasuaji, ingawa endapo saratani ni kubwa na haiwezi kuondolewa na upasuaji tu, matibabu ya mionzi au dawa za saratani hutumika.


Je saratani ya ependimoma hutokeaje?


Saratani huhusiana na mabadiliko kwenye jeni zinazotengeneza seli mbalimbali, mabadiliko kwenye seli za ependimo hupelekea kutokea kwa saratani ya ependimoma, hata hivyo haifahamiki ni nini mpaka sasa kinachosababisha mabadiliko kwenye jeni ya seli hizo na kupelekea saratani, tafiti zinaendelea fanyika kutambua ni nini kisababishi na vihatarishi.


Je saratani ya ependimoma husambaa sehemu nyingine ya mwili?


Inaonekana kuwa ni nadra saratani ya ependimoma kusambaa sehemu nyingine za mwili nje ya mfumo wa kati wa fahamu. Hata hivyo saratani hii inaweza kusambaa ndani ya mfumo wa fahamu ambako majimaji ya uti wa mgongo yanazalishwa, zunguka na yanapofyonzwa yaani saratani kwenye ubongo inaweza kusambaa kwenye sehemu zingine za uti wa mgongo na kinyume chake.


Endapo itasambaa nje ya mfumo wa fahamu, maeneo ambayo saratani hii inaweza kuonekana ni kwenye tezi limfu, ogani za ndani ya kifua, mapafu, kuta za mapafu, dayaframu, ini, mifupa na ogani nyuma ya ukuta wa peritoniamu.


Dalili


Dalili za saratani ya ependimoma hutegemea mahali saratani ilipo, kwenye ubongo au uti wa mgongo


Dalili za saratani ya ependimoma kwenye ubongo

  • Maumivu ya kichwa

  • Kichefuchefu

  • Kutapika

  • Kizunguzungu


Dalili za saratani ya ependimoma kwenye uti wa mgongo

  • Maumivu ya mgongo

  • Kufa ganzi kwenye mikono, kiwiliwili au miguu

  • Matatizo ya uono pamoja na mfumo wa mkojo


Utambuzi wa saratani ya ependimoma


Utambuzi wa pekee wa saratani ya ependimoma ni kipimo cha bayopsi, kipimo hiki hufanyika kwa baada ya kukata kinyama na kupimwa na mpatholojia kuangalia sifa za chembe za saratani endapo zimeanzia kwenye chembe za ependimo. Utambuzi mwingine wa kushuku unaweza kufanyika kwa kufanya;


  • Uchunguzi wa mfumo wa fahamu

  • Vipimo picha

  • Vipimo vya maji yaliyonyonywa kwenye uti wa mgongo


Uchunguzi wa mfumo wa fahamu

Wakati daktari anachunguza mishipa ya fahamu, utaulizwa maswali kadhaa kuhusu dalili zingine za madhara ya saratani katika mfumo huo. Uchunguzi wa mfumo wa fahamu utaangalia, uono, usikivu, usawia wa kusimama wima, uratibu utembeaji, nguvu ya misuli na rifleksi. Uchunguzi huu wa awali utatoa majibu wa sehemu gani ya mfumo wa fahamu imeathiriwa na saratani.


Vipimo picha

Vipimo picha humsaidia daktari kufahamu ukubwa wa saratani, sehemu ilipo kwenye mfumo wa fahamu na kupanga aina ya matibabu. Mara nyingi kipimo cha MRI ni kizuri zaidi kuangalia tishu za ubongo na uti wa mgongo. Kipimo kingine cha CT scan kinaweza kutumika endapo MRI hakipatikani, ingawa inashauriwa kutumia MRI kwa majibu mazuri zaidi.


Vipimo vya maji yaliyonyonywa kwenye uti wa mgongo

Mtaalamu wa afya atatumia sindano maalumu ili kunyonya majimaji yaliyo ndani ya uti wa mgongo, kisha kuyapeleka maabara kwa vipimo mbalimbali za kutambua uwepo wa chembe za saratani ndani ya mfumo wa majimaji ya uti wa mgongo.


Magonjwa mengine yanayoweza kufanana na saratani ya ependimoma kwenye vipimo vya MRIni yapi?


Magonjwa yafuatayo yanaweza kufanana na saratani ya ependimoma;


  • Medulloblastoma

  • Subependimoma

  • Glioblastoma

  • Papilloma ya Koroidi pleksasi

  • Koroidi pleksasi iliyosambaa

  • Neurosistoma ya mfumo wa kati wa fahamu

  • Teratoid isiyo kawaida/uvimbe wa rhabdoid


Matibabu


Kuna aina mbalimbali za matibabu yanayoweza kuchaguliwa na yameelezewa hapo chini ni;


  • Upasuaji wa kutoa saratani ya ependimoma

  • Tiba mionzi

  • Upasuaji mionzi

  • Tiba dawa za saratani

  • Tiba dawa za asili

  • Tiba za majaribio


Upasuaji wa kutoa saratani ya ependimoma

Madaktari wa ubongo na mishipa ya fahamu (daktari wa mfumo wa fahamu) watafanya kazi ya kutoa saratani kwa kuitaka kwa kiasi jinsi itakavyowezekana. Madhumuni ya upasuaji ni kutoa saratani yote, lakini baadhi ya nyakati haiwezekani kwa sababu ya sehemu saratani ilipo endapo itatolewa yote inaweza leta madhara mengine katika mfumo wa fahamu.


  • Endapo saratani yote imefanikiwa kutolewa wakati wa upasuaji, matibabu mengine hayatahitajika. Endapo pia imeshindikana kutoa saratani yote, daktari wa mfumo wa fahamu anaweza kupendekeza upasuaji mwingine ufanyike ili kujaribu toa sehemu ya saratani iliyobaki. Matibabu ya nyongeza endapo saratani imebaki na haiwezekani kutolewa ni tiba mionzi.


Tiba mionzi

Tiba mionzi ni tiba inayotumia mionzi yenye nguvu kali ya kuua chembe hai. Mionzi hii huelekezwa kwenye chembe za saratani tu ili kuepuka uharibifu wa chembe zingine zisizo saratani. Wakati wa kupigwa mionzi, utalazwa kwenye kitanda cha mionzi kisha mionzi hiyo itaelekezwa kwenye sehemu saratani ilipo. Tiba mionzi hutumika baada ya upasuaji endapo saratani haikutolewa yote.

Upasuaji mionzi

Upasuaji mionzi hutumia mionzi mingi inayoelekezwa kwenye sehemu moyo zilipo chembe ya saratani ili kuziua. Utofauti wa upasuaji mionzi na tiba mionzi ni wingi wa mionzi na sio kwamba inahusisha kupasua mwili. Tiba hii hutumika endapo tiba ya upasuaji na tiba mionzi imetumika na kufeli kunya kazi vema.


Tiba dawa za saratani

Dawa za kuua saratani hazina ufanisi mkubwa mara nyingi kwa wagonjwa wa saratani ya ependimoma. Madhumuni ya matibabu ya dawa za saratani kwenye saratani hii ni kwa majaribio tu na haswa pale saratani inapojirudia tena kufuatia tiba ya upasuaji na mionzi.


Tiba dawa za asili

Kuna dawa nyingi za asili zinazosemekana kutibu saratani, hakuna tafiti za kutosha kuhusu ufanisi wake licha ya kuruhusiwa kutumika na mashirika ya dawa ulimwenguni kutumika kwa binadamu. Dawa nyingi zimetengenezwa kutoka kwenye viini vya mbegu za zabibu, tufaa, tipisi, apricot n.k zzinazosemekana kuwa na virutubisho pamoja na viua sumu kama vitamin B17. Hata hivyo ikumbukwe kuwa dawa nyingi pia za saratani zimetengeneza kutoka kwenye mimea kama vile vinblastine, vincristine, vindesine), etoposide, teniposide, paclitaxel, docetaxel, camptotecin na irinotecan. Unaweza pata maelezo kwenye mitandao mbalimbali inayoaminika kuhusu dawa hizo.


Tiba za majaribio

Tiba majaribio ya kutumia dawa mpya za saratani, dawa za imunotherapi hupatikana pia katika nchi zinazofanya tafiti za kugundua aina nyingine za matibabu. Matibabu huamuliwa na mtaalamu wa afya wa mgonjwa kutegemea umri, saratani iliyobaki baad aya upasuaji, aina ya saratani na sehemu saratani ilipo.


Nini matokeo ya saratani ya ependimoma?


Asilimia 83.9 ya wagonjwa wanaweza kuishi miaka 5 baada ya kutambuliwa na kupata matibabu. Vitu vinavyoweza kuchangia uwezekano huu wa kuishi huko ni aina na hatua ya saratani, umri na afya ya mtu wakati ametambulika na mwitikio wa mwili kwenye matibabu. Kutambua matokeo ya saratani wasiliana na daktari wako kwa mazungumzo.


Matokeo huwa mabaya endapo saratani imetokea kwenye sehemu ambayo ni vigumu kufanya upasuaji wa kutoa saratani yote. Vitu vifuatavyo vinaonyesha kuwa saratani itakuwa na matokeo mabaya;


  • Saratani kuwepo kwenye ventriko ya 4

  • Kutotolewa saratani yote kwa upasuaji

  • Umri


Kwa ujumla endapo saratani imetokea kwa watoto chini ya umri wa miaka 3 na saratani ikawa kwenye ventriko ya 4, wastani wa watoto wanaoweza kuishi baada ya miaka mitano ni asilimia 50 hadi 75

Endapo saratani itajirudia baada ya upasuaji, wastani wa kuishi baada ya miaka mitano ni asilimia 10.


Wapi unaweza pata msaada?


Kujiunga ili kufanya survey ya saratani ya ependimoma tumia linki zinazofuata


https://www.cancer.gov/rare-brain-spine-tumor/refer-participate/clinical-studies/risk-study

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

26 Oktoba 2021, 21:04:36

Rejea za mada hii:

1. Winn HR, ed. Ependymomas. In: Youmans and Winn Neurological Surgery. 7th ed. Philadelphia, Pa.: Elsevier; 2017. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 13.06.2021

2. Uptodate. Kieran MW. Ependymoma. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 13.06.2021

3. National Cancer Institute. Childhood ependymoma treatment (PDQ). https://www.cancer.gov/types/brain/patient/child-ependymoma-treatment-pdq. Imechukuliwa 13.06.2021

4. Ependymoma Diagnosis and Treatment. https://www.cancer.gov/rare-brain-spine-tumor/tumors/ependymoma. Imechukuliwa 13.06.2021

5. Smith A, et al. From the Radiologic Pathology Archives: Intraventricular Neoplasms: Radiologic-Pathologic Correlation. http://radiographics.rsna.org/content/33/1/21.full. Imechukuliwa 13.06.2021

6. Ahmed Alzahrani, et al. Extraneural Metastasis of an Ependymoma: A rare occurrence. https://journals.sagepub.com/doi/10.15274/NRJ-2014-10017. Imechukuliwa 13.06.2021

7. Radiopedia. Ependymoma. https://radiopaedia.org/articles/ependymoma. Imechukuliwa 13.06.2021

8. Avni G. Desai, et al. Medicinal Plants and Cancer Chemoprevention. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4160808/#. Imechukuliwa 13.06.2021

bottom of page