Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Mangwella S, MD
Dkt. Adolf S, MD
Jumatatu, 20 Septemba 2021
Sindromu ya antifosfolipid
Sindromu ya antifosfolipid hutokana na mfumo wa kinga ya mwili kujishambulia wenyewe kwa bahati mbaya. Wanawake wengi wenye sindromu hii hupoteza ujauzito kwa kujirudia bila sababu maalumu. Kuna matibabu ya kupunguza dalili na madhara licha ya kutokuwa na tiba ponyaji.
Kwa kawaida mfumo wa kinga ya mwili hutambua vitu vingeni (bakteria, virusi n.k) vilivyo ingia mwilini kisha kuzalisha protini (antibody) zinazofanya kazi ya kuamsha mfumo wa kinga ya mwili kufanya mashambulizi ya kuviondoa. Kwa bahati mbaya mfumo huu wa kinga unaweza kutambua baadhi ya protini zilizojishikiza kwenye mbalimbali kuwa ni vitu vigeni na kutengeneza antibodi tayari kwa mashambulizi.
Kwa ugonjwa wa sindromu ya antifosfolipidi, mfumo wa kinga ya mwili hutengeneza antibodi dhidi ya protini zilizojishikiza kwenye damu na mishipa ya damu zenye jina la fosfolipid na wakati mwingine kardiolipin. Antibodi hizi hufanya mashambulizi dhidi ya mishipa ya damu na damu kiasi cha kupelekea ishara na dalili mbalimbali zinazofahamika kama sindromu ya antifosfolipid
Shambulio dhidi ya fosfolipid na kardiolipin hupelekea ishara na dalili ya kuganda kwa damu kwenye miguu, figo, mapafu na ubongo. Kwa mjamzito, sindromu hii huweza pelekea kupoteza ujauzito.
Hakuna matibabu ya kuponya tatizo hili, ila kuna dawa za kuzuia hatari ya kuganda kwa damu.
Epidemiolojia ya tatizo
Hali ya watu wenye afya kuwa na antibodi dhidi ya kardiolipin umeripotiwa kuwa kati ya asilimia 1 hadi 5.6 na kati ya 1.0 mpaka 3.6 kwa antibody za LAC. Hali ya kuwa na antibodi dhidi ya fosfolipid huongezeka pia kwa jinsi mtu anavyoongezeka umri.
Asilimia 40 ya wagonjwa wenye Lupus iliyosambaa huwa na antibodi dhidi ya fosfolipid hata hivyo ni chini ya asilimia 40 ya wagonjwa wanaweza kupata tatizo la damu kuganda.
Antibodi dhidi ya fosfolipid huchangia kwa kiasi kikubwa kupata matatizo yanayotokana na damu kuganda. Kwa mtu mwenye antibodi hizi pamoja na vihatarishi vingine kama uvutaji wa sigara, kutumia dawa za uzazi wa mpango, kufanyiwa upasuaji, kutulia muda mrefu bila kijongesha mwili na kurithi jeni za magonjwa ya kuganda damu huongeza hatari zaidi ya kuganda damu.
Dalili
Ishara na dalili za sindromu ya antifosfolipid ni;
Kuganda kwa damu kwenye mishipa
Kuvimba kwa mguu, Maumivu ya mguu na wekundu kwenye mguu
Mimba kujirudia kutoka bila sababu
Maumivu makali ya kifua kutokana na embolizimu ya palmonari
Mtoto kufia tumboni
Shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito
Kujifungua kabla ya wakati
Shinikizo la juu la damu linaloelekea kifafa cha mimba (preeclampsia)
Kiharusi
Kiharusi cha mpito
Ngozi kupata madoa yenye rangi ya zambarau
Kupungua kwa kiwango cha chembe sahani za damu (livedo reticularis)
Kuharibiwa kwa chembe nyekundu za damu
Dalili kali
Maumivu sugu ya kichwa
Kipanda uso
Degedege
Daimenshia
Kubadilika kwa mapigo ya moyo
Dalili za kuferi kufanya kazi kwa milango ya moyo
Kutokwa damu puani, fizi
Kuvia damu ndani ya ngozi
Wakati gani wa kuwasiliana na daktari
Wasiliana na daktari endapo unapatwa na dalili zifuatazo;
Kutokwa damu puani na kwenye fizi bila sababu
Kuwa na hedhi yenye damu nyingi
Kutapika damu au matapishi ya kahawia
Kujisaidia kinyesi kinachonata kama rami au chenye damu
Maumivu makali ya tumbo yasiyo na sababu
Kiharusi (kupooza kwa mikono au miguu na misuli ya usoni, kushindwa kuongea au kuona vema na maumivu makali ya kichwa)
Kuishiwa pumzi ghafla, maumivu ya kifua na kutoa makohozi yenye michirizi ya damu
Kuvimba kwa mguu au mkono kunakoambatana na maumivu na wekudu wa ngozi
Namna ugonjwa unavyotokea
Haifahamiki vema kisababishi cha tatizo hili, hata hivyo kuna nadharia tatu za kisanyasi zinazodhaniwa kuchangia hili;
Usafirishaji wa antibodi za mashambulizi binafsi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati yupo tumboni na akiwa amezaliwa. Usafirishaji huu bado haueleweki hata hivyo.
Kuridhi antibodi za fosfolipidi kunakohusiana na allele zifuatazo HLA-DR4, DR7, DRw53 na C4
Kwa kuwa kuna aina nyingi za molekyuli za fosfolipidi zinazopatikana ndani ya chembe za binadamu na vimelea na virusi. Wakati wa mfumo wa kinga wa mwili kufanya mashambulizi dhidi ya vimelea na virusi na magonjwa (mfano, VVU, kirusi Epstein-Barr [EBV], cytomegalovirus [CMV], adenoviruses), bakteria (mfano, bakteria endocarditis, tuberculosis, Mycoplasma pneumonia) na ugonjwa kama kaswende, leptospirosis, Lyme na malaria, uharibifu wa ukuta wa chembe za vimelea hawa huzalisha fosfolipidi zinazoamsha uzalishaji wa antibodi dhidi ya fosfolipid hizo.
Hitimisho;
Hata hivyo kwa ujumla sindromu ya antifosfolipid hutokana na shambulio binafasi la mfumo wa kinga ya mwili. Mwili huzalisha kwa bahati mbaya antibodi zinazaoshambulia protini zilizojishikiza katika kuta ya chembe ya damu na mishipa ya damu.
Vihatarishi
Vihatarishi vya kupata sindromu ya antifosfolipid ni;
Kuugua kaswende, UKIMWI, Hepatitis C, ugonjwa wa Lyme, maambukizi ta cytomegalovirus (CMV), parvovirus B19, Eschelician coli
Kuwa mwanamke
Kuwa na historia kwenye familia ya tatizo hili
Kuwa na madhaifu ya mfumo wa kinga ya mwili kama lupas au sindromu ya Sjogren's
Matumizi ya dawa kama hydralazine quinidine, phenytoin, amoxicillin na dawa za uzazi wa mpango
Viamsha dalili
Unaweza kuwa na antibodi zinazoambatana na sindromu ya antifosfolipid bila kuonyesha ishara au dalili yoyote. Hata hivyo kwa mtu mwenye antibodi endapo atakuwa na vihatarishi vifuatavyo anaweza kuonyesha dalili;
Kupata ujauzito
Kutojongesha mwili kwa muda mrefu mfano kusafiri kwa muda mrefu
Kufanyiwa upasuaji
Kuvuta sigara
Kutumia vidonge vya uzazi wa mpango
Matumizi ya estrogen baada ya koma hedhi
Kuwa na kiwango kikubwa cha kolestro na traiglaiseridi
Kuwa na uwiano mkubwa kupita kiasi wa uzito kwa urefu(obeziti)
Madhara
Madhara ya sindromu ya antifosfolipid hutegemea ni ogani gani ya mwili iliyodhuriwa na tatizo. Baadhi yake huwa pamoja na;
Kuferi kwa figo
Kiharusi
Madhaifu ya moyo
Madhaifu ya mapafu
Madhara kwa mjamzito
Kiharusi
Kupata shinikizo la juu la damu linaloelekea kifafa cha mimba
Kifafa cha mimba
Kuganda kwa damu
Kujifungua mtoto mfu
Kujirudia haribika kwa mimba
Mtoto kudumalia tumboni
Kujifungua kabla ya wakati
Utambuzi
Utaulizwa na daktari maswali mbalimbali kuhusu dalili ulizonazo pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa kuangalia ishara za ugonjwa kwenye mwili kisha kuagizwa fanya vipimo kama vile;
Kipimo cha hali ya ugandaji wa damu
Lupus anticoagulant
Anticardiolipin antibodi
Anti-β2-glycoprotein
Uchunguzi maalumu kwa mjamzito
Hali ya ugandaji damu
Kuchunguzwa dalili za shinikizo la damu
Kupimwa tumbo kwa kipimo cha picha ya mawimbi sauti ili kuangalia mjongeo wa damu ndani ya kondo na maendeleo ya ukuaji wa mtoto
Uchunguzi na ufuatiliaji wa mapigo ya moyo ya mtoto
Kipimo cha Doppler kuangalia mjongeo wa damu kati ya kitovu cha mtoto na kondo la nyuma
Matibabu
Licha ya kuwa na dawa za kupunguza ugandishaji wa damu, tatizo hili la kuganda kwa damu linaweza kutokea. Mama mjamzito anapaswa kufuata ushauri wa daktari wake na kuhudhuria kliniki ili kuendelea kufanyiwa uchunguzi na tiba
Msingi wa matibabu
Kutumia dawa za kuyeyusha damu kama warfarin na heparin au aspirin kama una tatizo la damu kuganda. Utafanyiwa uchunguzi wa karibu wakati unatumia dawa jamii hii ili kudhibiti madhara yanayoweza tokea kutokana na matumizi ya dawa. Kama una ujauzito, dozi ya dawa itatakuw ainabadilishwa kutokana na mwitikio wa mwili wako.
Maudhi ya dawa
Ni mara chache sana kwa maudhi ya dawa hizi kutokea kama utapewa dawa na kuchunguzwa mwitikio wa mwili wako. Kama yakitokea hususisha hisia za kuvimbiwa, hisia za kuumwa na kichefuchefu. Maudhi makali ni ambayo utapaswa kuripoti hutokana na kutokwa na damu au kuvia kwa damu ndani ya mwili ambapo italeta dalili za;
Kinyesi chenye rangi nyeusi na kinachonata kama rami
Kukojoa damu
Kuvia damu kirahisi au kupata majeraha kirahisi
Kutokwa damu puani kwa muda mrefu (zaidi ya dakika 10)
Kutapika damu
Kukohoa damu
Matibabu ya nyumbani
Mbali na matibabu ya dawa za kuzuia dalili mbalimbali haswa tiba ya dawa za kuyeyusha damu, unaweza fanya mambo yafuatayo ili kuzuia kuvia damu ndani ya mwili;
Kuepuka shughuli au michezo inayopelekea kupata majeraha kirahisi ( mfnao, mpira, ngumi na michezo inayoleta shinikizo kwenye mwili wako)
Kutumia mswaki laini na dawa ya meno yenye waksi
Kutumia mashine ya kunyolea badala ya kiwembe
Kuwa makini unapotumia vitu vyenye ncha kali kama kisu, mkasi, sindano
Vyakula na dawa za virutubishi nyongeza
Baadhi ya dawa za virutubisho nyongeza na vyakula vinaweza kuwa na mwingiliano na dawa za kuyeyusha damu. Unashauriwa kuwasiliana na daktari kwa ushauri wa kuacha au kuendelea tumia vitu vifuatavyo ili kuepuka mwingiliano;
Vidonge vya Vitamin K
Parachichi
Bruzeli
Maharagwe ya garbanzo
Kabeji
Mboga za kijani
Kitunguu swaumu
Ginkgo
Mazao ya chai
Pombe
Juisi ya klaniberi
Dawa za mitishamba
Vidonge vya Multivitamin
Mambo ya ziada kuzingatia
Kula mlo kamili wenye matunda na mboga za majani kwa wingi wakati huo dhibiti kiasi cha mafuta unayotumia
Kufanya mazoezi yenye mpangilio
Kuwa na uzito wa kiafya na kupunguza uzito kama uwiano wako wa uzito kwa uefu ni zaidi ya 30