Huduma za matibabu mtandaoni ni nini na zina mipaka gani?
Huduma za matibabu mtandaoni (Telemedicine) ni huduma inayokuwezesha kupata ushauri wa kitabibu kutoka kwa daktari bila kufika hospitalini, kwa kutumia mtandao. Kupitia huduma hii, daktari hukusanya historia ya ugonjwa wako, huchambua dalili zako na, pale inapowezekana, hutoa ushauri, mwongozo wa matibabu au kupendekeza vipimo vinavyohitajika.
​
Huduma hizi zimeundwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa usalama na kwa kuzingatia miongozo ya kitaalamu. Hata hivyo, si kila tatizo la kiafya linaweza kutathminiwa au kutibiwa kwa njia ya mtandao. Baadhi ya magonjwa yanahitaji uchunguzi wa mwili, vipimo vya haraka au matibabu ya ana kwa ana hospitalini.
​
Huduma za matibabu mtandaoni zinafaa kwa matatizo gani?
Huduma hizi zinafaa zaidi kwa wagonjwa ambao wanaweza kutathminiwa kwa kutumia historia ya ugonjwa, majibu ya maswali ya daktari na, inapohitajika, picha, video au mawasiliano ya video (video call).
Baadhi ya huduma zinazoweza kutolewa ni pamoja na:
-
Ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa daktari.
-
Tathmini ya tatizo lako kulingana na historia ya ugonjwa na dalili ulizonazo.
-
Kupendekezewa vipimo vinavyohitajika.
-
Kutafsiri na kufafanua majibu ya vipimo vya maabara au mionzi.
-
Kuandikiwa dawa pale ambapo daktari ameona zinafaa baada ya tathmini ya kina.
-
Kupewa cheti cha dawa (prescription) kinachoweza kutumika kununua dawa katika vituo vinavyokubalika.
-
Kuelekezwa jinsi ya kutumia dawa ulizoandikiwa.
-
Ushauri wa kitabibu kuhusu magonjwa sugu na ufuatiliaji wake.
-
Ushauri kuhusu lishe, mtindo wa maisha na kinga ya magonjwa.
-
Uchambuzi wa picha au video ulizotuma ikiwa zinaweza kusaidia kufanya tathmini ya tatizo lako.
-
Ushauri kupitia video call pale ambapo daktari ataona kuna umuhimu wa kufanya tathmini ya karibu zaidi.
Kila mgonjwa hutathminiwa mmoja mmoja. Hivyo, aina ya huduma utakayopata hutegemea tatizo lako na taarifa utakazompa daktari.
​
Ni lini unaweza kuhitaji kuonana na daktari ana kwa ana?
Baadhi ya matatizo hayawezi kutolewa uamuzi wa kitabibu kwa kutumia historia ya ugonjwa pekee. Katika hali hizo, daktari anaweza kukushauri kwenda hospitali au kituo cha afya kilicho karibu nawe ili kufanyiwa uchunguzi wa mwili, vipimo au matibabu yanayohitajika.
Unaweza kuhitaji huduma ya ana kwa ana ikiwa:
-
Unahitaji uchunguzi wa mwili ambao hauwezi kufanyika kwa njia ya mtandao.
-
Unahitaji vipimo vya maabara au mionzi kabla ya kupewa matibabu.
-
Tatizo lako linahitaji vifaa maalumu vya uchunguzi.
-
Dalili zako zinaashiria ugonjwa unaohitaji matibabu ya haraka hospitalini.
-
Unahitaji kufanyiwa upasuaji au utaratibu mwingine wa kitabibu.
-
Daktari ataona kuwa usalama wako unahitaji tathmini ya ana kwa ana.
Lengo letu ni kuhakikisha unapata huduma salama na sahihi, hata kama hiyo itamaanisha kukuelekeza kwenye kituo kingine cha afya.
​
Ni hali zipi zinazohitaji kwenda hospitali mara moja?
Huduma za matibabu mtandaoni hazipaswi kuchelewesha huduma za dharura.
Nenda hospitali au piga huduma za dharura mara moja ikiwa una:
-
Kupumua kwa shida au kushindwa kupumua.
-
Maumivu makali ya kifua.
-
Kupoteza fahamu au kuchanganyikiwa ghafla.
-
Kutokwa na damu nyingi isiyokoma.
-
Degedege.
-
Dalili za kiharusi kama kupooza upande mmoja wa mwili au kushindwa kuzungumza.
-
Jeraha kubwa au ajali.
-
Maumivu makali ya tumbo yanayoendelea kuongezeka.
-
Dalili nyingine zozote ambazo zinaonekana kuhatarisha maisha.
Katika hali hizi, usisubiri huduma ya mtandaoni.
​
Je, picha na video zinaweza kusaidia kufanya uchunguzi?
Ndiyo. Kwa baadhi ya matatizo, picha au video zinaweza kuongeza taarifa muhimu zinazomsaidia daktari kufanya tathmini.
Kwa mfano, picha zinaweza kusaidia kutathmini baadhi ya:
-
Magonjwa ya ngozi.
-
Vidonda.
-
Uvimbe unaoonekana kwa nje.
-
Mabadiliko yanayoonekana kwenye macho, mdomo au sehemu nyingine za mwili.
Hata hivyo, picha au video pekee hazitoshi kuthibitisha ugonjwa. Daktari anaweza bado kuhitaji historia ya kina, vipimo au uchunguzi wa ana kwa ana kabla ya kutoa hitimisho.
​
Je, video call hutumika lini?
Kwa baadhi ya wagonjwa, daktari anaweza kupendekeza video call ili kupata maelezo zaidi au kuona dalili ambazo haziwezi kutathminiwa vizuri kupitia ujumbe wa maandishi.
Video call si lazima kwa kila mgonjwa. Hutumika pale ambapo daktari anaona inaweza kuboresha tathmini ya tatizo lako.
​
Je, ninaweza kupewa dawa bila vipimo?
Baadhi ya magonjwa yanaweza kutathminiwa na kutibiwa kwa kutumia historia ya ugonjwa na dalili pekee, kulingana na miongozo ya kitabibu.
Hata hivyo, kwa magonjwa mengi, daktari anaweza kukuandikia vipimo kwanza ili kuhakikisha dawa utakazopewa zinafaa na ni salama. Hivyo, kupewa dawa hutegemea tathmini ya daktari na si ombi la mgonjwa.
​
Mambo ambayo hayajumuishwi katika huduma hizi
Huduma hii haijumuishi:
-
Kuuziwa au kupewa dawa.
-
Kufanyiwa vipimo vya maabara au mionzi.
-
Kufanyiwa upasuaji au taratibu nyingine za kitabibu.
-
Kutembelewa nyumbani na daktari au mhudumu wa afya.
-
Huduma za dharura zinazohitaji matibabu ya haraka hospitalini.
-
Dhamana ya kupata dawa, vipimo au rufaa bila tathmini ya kitabibu.
-
Utoaji wa vyeti vya ugonjwa, vyeti vya kazi au nyaraka nyingine bila vigezo vya kitabibu kutimizwa.
​
Ahadi yetu kwako
ULY Clinic tunazingatia usalama wa mgonjwa kuliko jambo lolote. Ikiwa tatizo lako linaweza kushughulikiwa kwa njia ya mtandaoni, tutakupa huduma kwa kuzingatia miongozo ya kitaalamu. Ikiwa tutagundua kuwa unahitaji uchunguzi wa ana kwa ana au huduma za dharura, tutakushauri kufika hospitali au kituo cha afya kilicho karibu nawe.
Lengo letu si kutoa huduma kwa lazima kupitia mtandao, bali kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma iliyo salama, sahihi na yenye manufaa kwa afya yake.
​
