top of page
Mawe kwenye tezi tonsil-ulyclinic

Imeandikwa na daktari wa ULY CLINIC

 

 

Mawe kwenye tezi ya tonsil

 

Mawe kwenye tezi ya tonsils  kwa jina jingine mawe ya tonsil au tonsilithi ni mawe yanayofanyika kutokana na muunganiko wa uchafu wa chakula, vimelea vya bakteria na mrenda wa mfumo wa chakula. Uchafu huu ukizama kwenye vijishimo vya tezi za tonsil husababisha kufanyika kwa mawe. Mawe huweza kufanyika kwenye tezi endapo mtu hazingatii usafi wa kinywa chake, haswa kusafisha kinywa kwa kupiga mswaki na kusukutua kinywa mara baada ya kula chakula.

Watu wengi hupatwa tatizo hili katika maisha yao lakin si kubwa na wala si rahisi kutambua. Umeshawahi kukohoa na ukatema kitu cha njano kinachonuka kama kinyesi? Hiki kitu kinachonuka ni moja ya mawe yanayotoka kwenye tezi za tonsil. Baadhi ya watu hupata mawe makubwa na magumu zaidi yenye maumbo tofauti.

Dalili za mawe kwenye tezi ya tonsils huwa ni;

  • Kuvimba kwenye maeneo ya tezi ya tonsil

  • Koo kuwa chungu na Kuhisi kuziba kwa koo

  • Kutoa harufu mbaya ya pumzi

  • Kushindwa kupumua vema

  • Kupata maumivu wakati wa kula kunywa au kumeza

  • Maumivu ya masikio

  • Kukauka kwa koo

  • Kutoa vitu vya njano vigumu unapokohoa

  • Kuhisi kuna kitu kwenye koo lako

  • Hisia za mawe kusuguana kwenye tezi tonsil unapozigusa

 

Vipimo

 

Mara nyingi vipimo huwa havihitajiki, daktari atakapokuangalia kinywa chako ataona uvimbe au kuona mawe yakichugnulia kwenye tezi zako.

 

Matibabu

Endapo mawe kwenye tezi za tonsil si makubwa, matibabu maalumu hayahitajiki, kwa jinsi utakavyokuwa unakazana kusafisha kunywa chako na kusukutua mara baada ya kula, mawe hayo yatapotea.

 

Matibabu ya  mawe makubwa huhusisha

 

  • Matumizi ya dawa za kuua vimelea vya bakteria. Zipo daw amaalumu zinazotumika katika matibabu haya

  • Upasuaji wa kuondoa mawe kwenye tezi hizi au upasuaji w akuondoa kabisa tezi za tonsil huweza kufanyika

 

Matibabu ya nyumbani

 

Unapogundua kuwa una mawe kwenye tezi ya tonsil, na endapo mawe hayo si makubwa sana, unaweza kufanya mambo fulani ili kujitibu ukiwa nyumbani kwako.

 

Matumizi ya dawa maalumu za kutibu maambukizi na kuondoa inflamesheni hutakiwa kutumika pia ili kuondoa chanzo. Fanya mambo yafuatayo kujitibu mwenyewe ukiwa nyumbani endapo tatizo sio kubwa;

  • Tumia  maji ya limao kusukutua kinywa, maji haya huwa na uwezo wa kuyeyusha mawe hayo kwa kuwa huwa na tindikali nyingi, mbadala wake unaweza kutumia vinega. SUkutua kinywa chako mara tatu kwa siku na angalau kila unapomaliza kula chakula.

  • Tumia vitunguu swaumu vilivyosagwa au tafuna na kisha vipake kwenye tezi hizo, vitunguu swaumu huweza kufanya kazi kama dawa za antibakteria kwa kuua na  kuzuia shambulio la bakteria kwenye tezi. Ongea na daktari kabla ya kufanya hivi

  • Tumia kijiti kilichofungwa pamba kwenye ncha yake ili kutoa  mawe kwenye tezi. Fanya hivi tu endapo unaweza ona mawe na unaweza yafikia kirahisi. Usitumie nguvu nyingi  nguvu kuepuka kujiumiza na kutokwa na damu nyingi.

  • Sukutua kinywa kwa kutumia maji ya uvuguvugu yenye chumvi, changanya chumvi kijiko kimoja cha chai kwenye maji kikombe kimoja kidogo cha chai kila unapotoa mawe

  • Jikoholeshe ili kuondoa mawe ambayo ni madogo 

  • Tafuna karoti  pamoja na vitunguu ili kuweka ulinzi kwenye kinywa na kusaidia kutoa mawe kwenye tezi tonsil

 

Kumbuka. Usitumie mswaki kujisafisha kwa nguvu, utapasua tezi hizi na kusabaisha kutokwa na damu nyingi. Endapo umejaribu kufanya mambo yote hapo juu bila mafanikio hakikisha unaonana na daktari wako.

 

Madhara

 

Mawe yanapoendelea kuongezeka kwenye tezi tonsil huweza kupelekea kuvimba kwa tezi hizo na kisha kusababisha upumuaji wa shida pamoja na kushidnwa kumeza chakula kiurahisi.

 

Kujikinga

Unaweza kujikinga na mawe kwenye tezi hii kwa kuzingatia  usafi wa kinywa chako. Safisha kinywa na kusukutua kila mara unapomaliza kula au endapo una tatizo hili la kujirudia, njia pekee ni upasuaji wa kuondoa tezi hizo.

 

Tumia maji ya uvuguvugu yenye chumvi kijiko kimoja cha chai kwa kikombe kimoja cha chai kusukutua kinywa chako baada ya kupiga mswaki. Usilale bila ksuafisha kinywa vema.

Kusoma zaidi kuhusu ugonjwa wa tonsil/tonsesi aumaambukizi kwenye tezi koo bonyeza hapa

 

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kwa ushauri na tiba, utatakiwa kupata matibabu maalumu kulingana na mahitaji ya mwili wako.

 

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na matibabu kwa kubonyeza pata tiba au kupiga namba za simu chini ya tovuti hii.

 

Rejea za mada hii,

bottom of page