Michomo kwenye kidole tumbo (Maambukizi kwenye kidole tumbo)
Imeandikwana madaktari wa uly clinic
​
Kidole tumbo ni kiungo kimojawapo kilicho jishikiza kwenye utumbo sehemu ya utumbo mwembamba unapoishia na utumbo mnene unapoanzia, hujichomoza na huwa na umbo kama la kidole hukaa sehemu ya chini kulia ya tumbo. Kitaalamu Kidole tumbo huonekana kuwa hakina kazi maalumu mwilini.
Michomo kwenye kidole tumbo husababishwa na maambukizi, michomo hii husababisha maumivu ya tumbo la chini upande wa kulia wa tumbo. Hata hivyo kwa watu wengi maumivu huanzia kwenye maeneo ya kitovu na badae huenda upande huo wakulia wa tumbo. Michomo inapozidi kusambaa, maumivu huongezeka zaidi na dalili kuwa dhahiri.
Ingawa kila mtu anaweza kupata michomo kwenye kidole tumbo, mara kadhaa hutokea kwa watu walio na umri kati ya miaka 10 na 30. Matibabu yanaayo tumika ni upasuaji wa kuondoa kidole tumbo au matibabu ya dawa.
Dalili
Dalili za michomo kwenye kidole tumbo huwa pamoja na;
-
Maumivu ya ghafla yanayoanza upande wa kulia chini ya tumbo
-
Maumivu ya ghafla yanayoanzia kwenye kitovu na baadae kuhamia upande wa kulia chini ya tumbo
-
Maumivu yanayo ongezeka unapo kohoa, tembea au kufanya mijongeo ya kujikunja
-
Kichefuchefu na kutapika
-
Kupoteza hamu ya kula
-
Homa kiasi, huweza kuongezeka jinsi ugonjwa unavyoendelea kusambaa
-
Choo kigumu au kuharisha
-
Kuhisi umeshiba-tumbo kujaa gesi
Sehemu ya maumivu ya michomo kwenye kidole tumbo huweza kutofautiana mahali yalipo kwa kutegemea kidole tumbo kimekaa sehemu gani ya mwili. Kwa mama mjamzito maumivu yanaweza kuanza sehemu ya juu ya tumbo upande wa kulia kwa sababu kidole tumbo husukumwa sehemu hiyo.
Kisababishi
Kitu chochote kitakacho sababisha kuziba kwa kidole tumbo hupelekea kutokea kwa maambukizi kwenye kidole tumbo na hatimae michomo. Bakteria hukua haraka na kusababisha michomo, kuvimba na kujaa kwa usaha kwenye kidole tumbo. Kama usipo pata matibabu sahihi kidole tumbo huweza kupasuka.
Madhara
Madhara ya michomo kwenye kidole tumbo huweza kuwa makubwa kama vile
-
Kupasuka kwa kidole tumbo- Kupasuka kwa kidole tumbo husababisha kusambaa kwa maambukizi tumbo zima, tatizo hilo huitwa peritonitis. Hali hii Hutishia maisha na hu hitaji upasuaji wa haraka wa kuondoa kidole tumbo na kusafisha tumbo.
-
Kifuko cha usaha kutengenezwa tumboni- Kama kidole tumbo kikipasuka, kijifuko cha usaha kinaweza kutengenezwa kwenye maeneo ya kidole tumbo kilipo. Kwa watu wengi, daktari wa upasuaji atatoa usaha kwa kutumia mrija maalumu linalopitishwa kupitia tumbo mpaka kwenye kifuko cha usaha. Mrija huu huweza kuachwa kwa wiki mbili na utapewa dawa za kupambana na bacteria ili kusafisha mweili na maambukizi
-
Maambukizi yanapoisha, utapata upasuaji wa kuondoa kidole tumbo. Kwa baadhi ya wagonjwa usaha hutolewa na kidole tumbo huondolewa mara moja bila kusubiri muda kupita.
Vipimo na ugunduzi
Daktari atachukua historia ya ugonjwa wako na kisha atafanya uchunguzi wa tumbo lako.
Daktari atapima kwa kutumia mikono yake kwenye tumbo lako na kuweka mgandamizo kiasi kuangalia ukubwa wa tatizo la kidole tumbo na sehemu maumivu yalipo. Kwa kufanya hivi anaweza kutambua ni nini kinachosababisha maumivu ya tumbo lako.
Kipimo cha damu-Kitaangalia kuongezeka kwa chembe nyeupe za damu ambapo humamaanisha maambukizi.
Kipimo cha mkojo- Kitamsaidia daktari kutofautisha maambukizi ya njia ya mkojo au uwepo wa mawe kwenye njia ya mkojo, dalili za matatizo haya huweza kufanana na dalili za michomo kwenye kidole tumbo.
Vipimo vya mionzi- X- ray ya tumbo, kipimo cha mionzi sauti (ultrasound) ama kipimo cha CT scan huweza kufanyika kwa lengo la kuchunguza kidole tumbo kama ni kisababishi cha maumivu au la. Kipimo kimoja wapo tu kinaweza kufanyika, uchaguziwa kipimo hutegemea aina ya kipimo kilichopo lakini kipimo cha CT-Scan huwa kizuri zaidi kwenye utambuki kikifuatiwa na Utrosound.
Matibabu
Matibabu ya michomo kwenye kidole tumbo yana husisha upasuaji wa kuondoa kidole tumbo na dawa za kupambana na bakteria ili kusafisha ama kuzuia maambukizi yasisambae kwenye damu. Daktari atachana tumbo kidogo upande wa kulia kwa ajili ya kuondoa kidole tumbo. Kama kidole tumbo kimepasuka tiba huhusisha mchano mkubwa katikati ya tumbo kuanzia juu ya kitovu.
Mshono utakuwa wa sentimeta 5 hadi kumi tu. Kama upasuaji wa kifaa kamera utafanyika basi utakuwa na kovu kidogo sana kama la sentimeta 1 hadi 2. Upasuaji huu wa kifaa cha kamera kinacho chungulia ndani ya tumbo huwa ni mzuri kwani utakaa mda mfupi hospitali na utapona haraka bila kuwa na makovu makubwa tumboni.
​
​
Toleo la 3
Imeboreshwa 8/12/2018