top of page

Tovuti salama za afya

Updated: Sep 19, 2021


Kuna ongezeko kubwa la utafutaji mada za afya mtandaoni ulimwenguni kote kutokana maendeleo makubwa ya tekinolojia. Inakadiliwa asilimia 80 ya watu wazima Amerika sawa na watu milioni 93, wamewahi kutafuta angalau mada moja ya afya mtandaoni katika mwezi November hadi December 2002 (Pew Internet na American Life Project).


Tovuti ya datareportal imeripoti kuwa kuna jumla ya watumiaji milioni 15.5 Tanzania wameingia mtandaoni kutafuta mada mbalimbali ikiwa pamoja na mada ya afya. Idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia 3 kutoka kwenye taarifa za mwaka 2020.


Kwanini Makala hii imeandikwa?


Kuna zadi ya tovuti 70,000 za afya duniani na zinaongezekaa kila kukicha. Katika tovuti zote hizo na zile zinazoongezeka, ni jukumu la mtumiaji kufahamu vyanzo vilivyo salama na vile visivyo salama kutumika kama mshauri wa afya.


Makala hii imekusudia kumwelekeza mtumiaji wa mada za afya mtandaoni namna gani anaweza kupata taarifa za kuaminika katika vyanzo vilivyopo kwa lugha mbalimbali ikiwa pamoja na Kiswahili. Mada hii imetengenezwa kwa vichwa vya habari vifuatavyo;

  • Je ni wapi utapata mada za afya za uhakika mtandaoni?

  • Nini cha kujiuliza kabla ya kuamini tovuti ya afya?

  • App za kiafya na usalama wake

  • Taarifa za afya za mitandao ya kijamii

  • Taarifa kutoka kwa daktari wako

Je ni wapi utapata mada za afya za uhakika mtandaoni?


Taarifa za kuaminika zinaweza patikana kwenye tovuti kubwa za kiafya duniani kama vile national institute of health website (NIH), tovuti ya wizara ya afya, tovuti ya TFDA , WHO, CDC au tovuti zinazotumia rejea kutoka kwenye tovuti hizo.


Hata hivyo, tovuti ambazo zimefadhiliwa na serikali pia zinaweza kuwa na taarifa za kuaminika.

Vyanzo vingine vya kuaminika ni kutoka kwenye taasisi kubwa za afya zinazotoa huduma za afya, kufanya tafiti za kiafya ikiwa kama kliniki, hospitali, vyuo vikuu n.k


Vyama vikubwa pia ya vya wataalamu wa afya hutoa taarifa za kuaminika. Vyama hivi ni vile ambavyo vimetengenezwa na kuendesha na wataalamu wa afya



Nini cha kujiuliza kabla ya kuamini tovuti ya afya?


Unapotafuta habari ya afya mtandaoni, utakutana na maelfu ya tovuti zinazozungumzia mada hiyo huku baadhi yake unazifahamu na zingine huzifahamu kabisa. Ili kufahamu kama kuna usalama kwenye tovuti unayosoma unapaswa kujiuliza na kupata majibu ya kujiridhisha kwenye maswali yafuatayo;


a. Nani mtunzaji wa mada hizo, na je zinapatikana kirahisi?


Uundaji na uendeshaji wa tovuti hutumia gharama nyingi, unapaswa kupata taarifa za mtunzaji wa tovuti na mfadhiri wa hiyo tovuti kirahisi katika tovuti unayotembelea. Kufahamu taarifa hizi zitakupa mwangaza wa madhumuni ya tovuti hiyo. Wakatim mwingine unaweza tumia jina la kiungo cha kwenye tovuti (URL) ili kutambua madhumuni ya tovuti kwa mfano tovuti zinazoishia na neno;

  • .tz ni tovuti inayoashiria nchi ya Tanzania, tovuti hii mara nyingi huwa ya serikali

  • .edu inatumika kwa taasisi za elimu ya juu, vyuo vya kati na shule

  • .org huashiria shirika lisilo la kiserikali na lisilo la kifaida mfano vyama vya wataalamu wa afya, wanasayansi, wanasheria n.k

  • .com hutambulisha tovuti za kibiashara mfano makampuni ya dawa na wakati mwingine hospitali na kliniki


b.Ni nani mwandishi wa mada na nani amehariri?


Mwandishi, mchangiaji na mhariri wa habari mara nyingi hutajwa kwenye tovuti zinazoaminika, hata hivyo si mara zote kwenye baadhi ya tovuti. Kama mwandishi ameandikwa, unaweza kujiuliza je ni mtaalamu wa afya au kwenye mada hiyo aliyoandika? Je ni mfanyakazi kwenye taasisi hiyo na kama ndio, je taasisi ina madhumuni gani? Na nini mahusiano yake na mchangiaji?


c. Je mada za afya zilizoandikwa zimehaririwa na mtaalamu wa afya?


Tovuti zinazoaminika tu zitakuambia taarifa zimeandikwa na nani na nani aliyehariri Makala hiyo.


Tovuti ya kuaminika itakuwa na mawasiliano ya simu au barua pepe chini ya tovuti kwenye kila kurasa, au kurasa ya mawasiliano au ya kuwahusu.


Kama tovuti imeweka shuhuda za watumiaji, kuwa makini na shuhuda hizo kwani si kila mtu mwenye tatizo Fulani huweza tibika kama mtu mwingine mwenye tatizo hilohilo kutokana na utofauti wa mwili na muitikio kwenye dawa. Pia kuna baadhi ya watoa shuhuda huaidiwa kupata faida fulani wanapotoa shuhuda za ukweli kwenye tovuti fulani. Tovuti nyingi zinazoaminika huwa haziweki shuhuda za watumiaji wala idadi ya watembeleaji wa tovuti hiyo.


d. Nini kilichoandikwa mwishoni mwa mada?


Unaposoma mada na kufika mwishoni, hutakiwi kukutana na maneno yanayokushawishi uwasiliane na mwandishi wa mada ili upate huduma au kununua bidhaa kutoka kwao. Kama taarifa hizi zipo, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba tovuti hiyo malengo yake ni kukuvutia upate huduma kutoka kwao.

Maneno ya kwanza kabisa unayopaswa kukutana nayo mwishoni mwa mada ni kukushauri uonane na daktari wako kwa ushauri na huduma zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma mada hiyo. Unapaswa kuwa na uchaguzi wa nani na wapi upate huduma baada ya kusoma mada.


e. Taarifa zimeandikwa lini?


Tovuti za kuaminika zitaonyesha mada husika imeandikwa lini mwanzoni mwa mada na mwishoni mwa itaonyesha mada imeboreshwa lini. Kuonyeshwa kwa taarifa hizi husaidia kutambua usasa wa taarifa hizo. Kila siku tafiti mbalimbali za afya zinafanyika na mara zinapopatikana zinapaswa kutumika boresha taarifa za zamani. Hutakiwi kufanya uamuzi kuhusu afya yako kwa taarifa zilizopitwa na wakati, bali kwa kutumia taarifa za hivi karibuni zaidi.


Mada mbalimbali katika tovuti zinaweza kuboreshwa kwa wakati tofauti, baadhi ya tovuti zinaboresha taarifa zao mara kwa mara na zingine baada ya muda mrefu kupita.


Taarifa za zamani si kwamba hazina umuhimu, hata hivyo fanya maamuzi kwa kutumia taarifa za hivi karibuni zaidi kutokana na tafiti.


f. Madhumuni ya tovuti ni nini?


Kwanini tovuti iliundwa?


Kufahamu kwanini tovuti iliundwa itasaidia kufahamu madhumuni ya tovuti hiyo na kuhukumu. Je tovuti ipo kwa ajili ya kutaarifu au kuelezea? Au je ni kwa nia ya kuuza biadhaa fulani mwishoni mwa Mada?

Unashauriwa kusoma mada za tovuti zilizoandikwa kwa kufuata ushahidi wa tafiti mbalimbali za kiafya zilizofanyika na sio maoni ya mtu binafsi. Utafahamu hivyo kama mada imeweka rejea kutoka kwenye tovuti zinazoaminika kama ilivyoelezewa hapo juu.


g. Je taarifa zako zinatunzwa kwa usiri au wanazitumia vipi?


Soma kuhusu vigezo na mashariti ya tovuti hiyo na sera ya matumizi ya tovuti hiyo. Kiungo cha kuingia kwenye taarifa hizi mara nyingi hupatikana chini ya tovuti sehemu zilizoandikwa ‘sera ya matumizi’ au ‘sheria na mashariti’. Kama tovuti haina kurasa hizi, basi uhakika wa taarifa zako kutumika kwa nia njema ni mdogo.


Kwa tovuti zinazotumia cookies, taarifa za mtumiaji mara nyingi zinakuwa si siri, licha ya matumizi ya cookies kuongeza urahisi wa kukuletewa taarifa zinazoendana na kile unachopenda kuperuzi kwenye mitandao hata kama hutaki kuona tena. Unaweza kusitisha cookies kupitia setting ya kiperuzio chako.


h. Namna ya kulinda taarifa zako


Kama tovuti inataka kuchukua taarifa zako mfano barua pepe, jina, taarifa za kibenki n.k unapaswa kuwa makini na kiunganishi cha kuingia kwenye tovuti hiyo. Tovuti Salama inapaswa kuwa na alama ‘S’ baada ya kiungo chake cha “http” mwanzoni kabisa mwa kiungo yaani (https://) na mara zote hukutaka kutengeneza jina la mtumiaji na nywila mpya tofauti na ile unayoitumia.


Tahadhari muhimu za kuchukua ukiwa unafungua viungo (linki) vya tovuti mbalimbali;

· Tumia ufahamu wako unapoperuzi mtandao, usifungue viungo vyoyote tu hata vile usivyotarajia au kubofya kiungo chochote kinachodai kuwa ukibofya kitakupeleka kwenye tovuti ya kuaminika.

  • Tumia nywila yenye nguvu zaidi (strong password) kwa kuchanganya namba, alfabeti za herufi kubwa na ndogo na alama mbalimbali mfano *, $, @ n.k ili kuongeza ugumu wa kudukuliwa nywila yako wadukuzi wa mtandaoni. Badilisha nywila yako kila baada ya miezi kadhaa (angalau miezi mitatu hati minne)

  • Tumia uthibitisho wa upili kama ukiweza. Hii inamaanisha kutumia zaidi ya kifaa kimoja kudhibitisha mtumiaji, mfano unapokuwa unaingia kwenye barua pepe yako, unapaswa kutumiwa taarifa kwenye simu ili uthibitishe kama ni wewe unayetaka kuingia. Unaweza kutumia meseji, kupigiwa simu au kubofya namba fulani kwenye simu yako kila mara unapoingia kenye kifaa kipya kielektroniki

  • Usiweke taarifa zako za siri kwenye wireless ambayo inatumika na jamii pamoja na zile ambazo hazijafungwa kwa nywila

  • Kuwa makini ni taarifa gani unazozituma kwenye tovuti za mitandao ya kijamii. Hii inajumuisha barua pepe, makazi, namba ya simu n.k kumbuka na fanya taarifa zako kuwa za siri.


i. Je tovuti inadai kukupa suluhisho la haraka?


Kuwa makini na tovuti au kampuni zinazodai kutoa tiba ponyaji kwa maradhi kadhaa hata ambayo hayatibiki. Jiulize maswali kuhusu kwamba kinachosemwa kuwa kinaponya au kilichowekewa mvuto kama ni kweli kinafahamika kufanya hivyo. Tafuta tovuti nyingine yenye taarifa kama hizo ili kujithibitishia kama ni ukweli kabla ya kuchukua hatua yoyote hata kama mada ya tovuti hiyo imeandikwa kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika.



Rejea za mada hii;


  1. Lila J. Finney Rutten, PhD, MPH, et al. Online Health Information Seeking Among US Adults: Measuring Progress Toward a Healthy People 2020 Objective. https://journals.sagepub.com/doi/10.1177/0033354919874074. Imechukuliwa 18/09/2021

  2. Dickerson, Suzanne et al. “Patient Internet use for health information at three urban primary care clinics.” Journal of the American Medical Informatics Association : JAMIA vol. 11,6 (2004): 499-504. doi:10.1197/jamia.M1460

  3. NIH. Online health information is it reliable?.https://www.nia.nih.gov/health/online-health-information-it-reliable. Imechukuliwa 17/08/2021

  4. Internet users in Tanzania. https://datareportal.com/reports/digital-2021-tanzania#. Imechukuliwa 17/08/2021

  5. Boon-itt, S. Quality of health websites and their influence on perceived usefulness, trust and intention to use: an analysis from Thailand. J Innov Entrep 8, 4 (2019). https://doi.org/10.1186/s13731-018-0100-9.

  6. Pew Internet and American Life Project. Internet Health Resources, Health Searches and Email Have Become More Commonplace, But There Is Room for Improvement in Searches and Overall Internet Access. 2003. http://pewInternet.org/. Imechukuliwa 18/09/2021

  7. Sbaffi, L., & Rowley, J. (2017). Trust and credibility in web-based health information: a review and agenda for future research. Journal of Medical Internet Research, 19(6), 454–471.

93 views0 comments

Recent Posts

See All

Commentaires


bottom of page