top of page

Mwandishi:

Dkt Benjamin L ,MD

Mhariri:

Dkt. Adolf S, MD na Dkt. Mangwella S, MD

Jumamosi, 18 Septemba 2021

Tovuti salama kwa ushauri wa afya

Tovuti salama kwa ushauri wa afya

Kuna zadi ya tovuti 70,000 za afya duniani zinaongezekaa kila kukicha, ni jukumu la mtumiaji kufahamu namna ya kutambua na kutumia vyanzo salama ili kuepuka madhara. Baadhi ya sifa ya chanzo salama ni kuonyesha madhumuni ya tovuti, mada zimeandikwa na kuhaririwa na mtaalamu wa afya na kutoshawishi mtumiaji kununua au kutafuta huduma kutoka kwenye chanzo tu.


Utambuzi wa tovuti salama za afya


Kuna ongezeko kubwa la utafutaji mada za afya mtandaoni ulimwenguni kote kutokana maendeleo makubwa ya tekinolojia. Inakadiliwa asilimia 80 ya watu wazima Amerika sawa na watu milioni 93, wamewahi kutafuta angalau mada moja ya afya mtandaoni katika mwezi November hadi December 2002 (Pew Internet na American Life Project).


Tovuti ya datareportal imeripoti kuwa kuna jumla ya watumiaji milioni 15.5 Tanzania wameingia mtandaoni kutafuta mada mbalimbali ikiwa pamoja na mada ya afya. Idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia 3 kutoka kwenye taarifa za mwaka 2020.


Kwanini Makala hii imeandikwa?


Kuna zadi ya tovuti 70,000 za afya duniani na zinaongezekaa kila kukicha. Katika tovuti zote hizo na zile zinazoongezeka, ni jukumu la mtumiaji kufahamu vyanzo vilivyo salama na vile visivyo salama kutumika kama mshauri wa afya.


Makala hii imekusudia kumwelekeza mtumiaji wa mada za afya mtandaoni namna gani anaweza kupata taarifa za kuaminika katika vyanzo vilivyopo kwa lugha mbalimbali ikiwa pamoja na Kiswahili. Mada hii imetengenezwa kwa vichwa vya habari vifuatavyo;


  • Je ni wapi utapata mada za afya za uhakika mtandaoni? Na nini nini cha kujiuliza kabla ya kuamini tovuti ya afya?

  • App za kiafya na usalama wake

  • Taarifa za afya za mitandao ya kijamii

  • Taarifa kutoka kwa daktari wako


Je ni wapi utapata mada za afya za uhakika mtandaoni? Na nini nini cha kujiuliza kabla ya kuamini tovuti ya afya?


Je ni wapi utapata mada za afya za uhakika mtandaoni?


Taarifa za kuaminika zinaweza patikana kwenye tovuti kubwa za kiafya duniani kama vile national institute of health website (NIH), tovuti ya wizara ya afya, tovuti ya TFDA , WHO, CDC au tovuti zinazotumia rejea kutoka kwenye tovuti hizo.


Hata hivyo, tovuti ambazo zimefadhiliwa na serikali pia zinaweza kuwa na taarifa za kuaminika.

Vyanzo vingine vya kuaminika ni kutoka kwenye taasisi kubwa za afya zinazotoa huduma za afya, kufanya tafiti za kiafya ikiwa kama kliniki, hospitali, vyuo vikuu n.k


Vyama vikubwa pia ya vya wataalamu wa afya hutoa taarifa za kuaminika. Vyama hivi ni vile ambavyo vimetengenezwa na kuendesha na wataalamu wa afya



Nini cha kujiuliza kabla ya kuamini tovuti ya afya?


Unapotafuta habari ya afya mtandaoni, utakutana na maelfu ya tovuti zinazozungumzia mada hiyo huku baadhi yake unazifahamu na zingine huzifahamu kabisa. Ili kufahamu kama kuna usalama kwenye tovuti unayosoma unapaswa kujiuliza na kupata majibu ya kujiridhisha kwenye maswali yafuatayo;


a. Nani mtunzaji wa mada hizo, na je zinapatikana kirahisi?

Uundaji na uendeshaji wa tovuti hutumia gharama nyingi, unapaswa kupata taarifa za mtunzaji wa tovuti na mfadhiri wa hiyo tovuti kirahisi katika tovuti unayotembelea. Kufahamu taarifa hizi zitakupa mwangaza wa madhumuni ya tovuti hiyo. Wakatim mwingine unaweza tumia jina la kiungo cha kwenye tovuti (URL) ili kutambua madhumuni ya tovuti kwa mfano tovuti zinazoishia na neno;


  • .tz ni tovuti inayoashiria nchi ya Tanzania, tovuti hii mara nyingi huwa ya serikali

  • .edu inatumika kwa taasisi za elimu ya juu, vyuo vya kati na shule

  • .org huashiria shirika lisilo la kiserikali na lisilo la kifaida mfano vyama vya wataalamu wa afya, wanasayansi, wanasheria n.k

  • .com hutambulisha tovuti za kibiashara mfano makampuni ya dawa na wakati mwingine hospitali na kliniki


b.Ni nani mwandishi wa mada na nani amehariri?

Mwandishi, mchangiaji na mhariri wa habari mara nyingi hutajwa kwenye tovuti zinazoaminika, hata hivyo si mara zote kwenye baadhi ya tovuti. Kama mwandishi ameandikwa, unaweza kujiuliza je ni mtaalamu wa afya au kwenye mada hiyo aliyoandika? Je ni mfanyakazi kwenye taasisi hiyo na kama ndio, je taasisi ina madhumuni gani? Na nini mahusiano yake na mchangiaji?


c. Je mada za afya zilizoandikwa zimehaririwa na mtaalamu wa afya?

Tovuti zinazoaminika tu zitakuambia taarifa zimeandikwa na nani na nani aliyehariri Makala hiyo.


Tovuti ya kuaminika itakuwa na mawasiliano ya simu au barua pepe chini ya tovuti kwenye kila kurasa, au kurasa ya mawasiliano au ya kuwahusu.


Kama tovuti imeweka shuhuda za watumiaji, kuwa makini na shuhuda hizo kwani si kila mtu mwenye tatizo Fulani huweza tibika kama mtu mwingine mwenye tatizo hilohilo kutokana na utofauti wa mwili na muitikio kwenye dawa. Pia kuna baadhi ya watoa shuhuda huaidiwa kupata faida fulani wanapotoa shuhuda za ukweli kwenye tovuti fulani. Tovuti nyingi zinazoaminika huwa haziweki shuhuda za watumiaji wala idadi ya watembeleaji wa tovuti hiyo.


d. Nini kilichoandikwa mwishoni mwa mada?

Unaposoma mada na kufika mwishoni, hutakiwi kukutana na maneno yanayokushawishi uwasiliane na mwandishi wa mada ili upate huduma au kununua bidhaa kutoka kwao. Kama taarifa hizi zipo, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba tovuti hiyo malengo yake ni kukuvutia upate huduma kutoka kwao.


Maneno ya kwanza kabisa unayopaswa kukutana nayo mwishoni mwa mada ni kukushauri uonane na daktari wako kwa ushauri na huduma zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma mada hiyo. Unapaswa kuwa na uchaguzi wa nani na wapi upate huduma baada ya kusoma mada.


e. Taarifa zimeandikwa lini?

Tovuti za kuaminika zitaonyesha mada husika imeandikwa lini mwanzoni mwa mada na mwishoni mwa itaonyesha mada imeboreshwa lini. Kuonyeshwa kwa taarifa hizi husaidia kutambua usasa wa taarifa hizo. Kila siku tafiti mbalimbali za afya zinafanyika na mara zinapopatikana zinapaswa kutumika boresha taarifa za zamani. Hutakiwi kufanya uamuzi kuhusu afya yako kwa taarifa zilizopitwa na wakati, bali kwa kutumia taarifa za hivi karibuni zaidi.


Mada mbalimbali katika tovuti zinaweza kuboreshwa kwa wakati tofauti, baadhi ya tovuti zinaboresha taarifa zao mara kwa mara na zingine baada ya muda mrefu kupita.


Taarifa za zamani si kwamba hazina umuhimu, hata hivyo fanya maamuzi kwa kutumia taarifa za hivi karibuni zaidi kutokana na tafiti.


f. Madhumuni ya tovuti ni nini?

Kwanini tovuti iliundwa?

Kufahamu kwanini tovuti iliundwa itasaidia kufahamu madhumuni ya tovuti hiyo na kuhukumu. Je tovuti ipo kwa ajili ya kutaarifu au kuelezea? Au je ni kwa nia ya kuuza biadhaa fulani mwishoni mwa Mada?

Unashauriwa kusoma mada za tovuti zilizoandikwa kwa kufuata ushahidi wa tafiti mbalimbali za kiafya zilizofanyika na sio maoni ya mtu binafsi. Utafahamu hivyo kama mada imeweka rejea kutoka kwenye tovuti zinazoaminika kama ilivyoelezewa hapo juu.


g. Je taarifa zako zinatunzwa kwa usiri au wanazitumia vipi?

Soma kuhusu vigezo na mashariti ya tovuti hiyo na sera ya matumizi ya tovuti hiyo. Kiungo cha kuingia kwenye taarifa hizi mara nyingi hupatikana chini ya tovuti sehemu zilizoandikwa ‘sera ya matumizi’ au ‘sheria na mashariti’. Kama tovuti haina kurasa hizi, basi uhakika wa taarifa zako kutumika kwa nia njema ni mdogo.


Kwa tovuti zinazotumia cookies, taarifa za mtumiaji mara nyingi zinakuwa si siri, licha ya matumizi ya cookies kuongeza urahisi wa kukuletewa taarifa zinazoendana na kile unachopenda kuperuzi kwenye mitandao hata kama hutaki kuona tena. Unaweza kusitisha cookies kupitia setting ya kiperuzio chako.


h. Namna ya kulinda taarifa zako

Kama tovuti inataka kuchukua taarifa zako mfano barua pepe, jina, taarifa za kibenki n.k unapaswa kuwa makini na kiunganishi cha kuingia kwenye tovuti hiyo. Tovuti Salama inapaswa kuwa na alama ‘S’ baada ya kiungo chake cha “http” mwanzoni kabisa mwa kiungo yaani (https://) na mara zote hukutaka kutengeneza jina la mtumiaji na nywila mpya tofauti na ile unayoitumia.


Tahadhari muhimu za kuchukua ukiwa unafungua viungo (linki) vya tovuti mbalimbali;

  • Tumia ufahamu wako unapoperuzi mtandao, usifungue viungo vyoyote tu hata vile usivyotarajia au kubofya kiungo chochote kinachodai kuwa ukibofya kitakupeleka kwenye tovuti ya kuaminika.

  • Tumia nywila yenye nguvu zaidi (strong password) kwa kuchanganya namba, alfabeti za herufi kubwa na ndogo na alama mbalimbali mfano *, $, @ n.k ili kuongeza ugumu wa kudukuliwa nywila yako wadukuzi wa mtandaoni. Badilisha nywila yako kila baada ya miezi kadhaa (angalau miezi mitatu hati minne)

  • Tumia uthibitisho wa upili kama ukiweza. Hii inamaanisha kutumia zaidi ya kifaa kimoja kudhibitisha mtumiaji, mfano unapokuwa unaingia kwenye barua pepe yako, unapaswa kutumiwa taarifa kwenye simu ili uthibitishe kama ni wewe unayetaka kuingia. Unaweza kutumia meseji, kupigiwa simu au kubofya namba fulani kwenye simu yako kila mara unapoingia kenye kifaa kipya kielektroniki

  • Usiweke taarifa zako za siri kwenye wireless ambayo inatumika na jamii pamoja na zile ambazo hazijafungwa kwa nywila


Kuwa makini ni taarifa gani unazozituma kwenye tovuti za mitandao ya kijamii. Hii inajumuisha barua pepe, makazi, namba ya simu n.k kumbuka na fanya taarifa zako kuwa za siri.


i. Je tovuti inadai kukupa suluhisho la haraka?

Kuwa makini na tovuti au kampuni zinazodai kutoa tiba ponyaji kwa maradhi kadhaa hata ambayo hayatibiki. Jiulize maswali kuhusu kwamba kinachosemwa kuwa kinaponya au kilichowekewa mvuto kama ni kweli kinafahamika kufanya hivyo. Tafuta tovuti nyingine yenye taarifa kama hizo ili kujithibitishia kama ni ukweli kabla ya kuchukua hatua yoyote hata kama mada ya tovuti hiyo imeandikwa kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika.


Taarifa za kwenye application za afya (app za afya)


Application za afya au app za afya ni programu maalumu unazoweza kupakua mtandaoni na kuhifadhi kwenye simu yako kwa ajili ya matumizi. Mtu yeyote anaweza kuanzisha application ya afya kwa sababu yake binafsi na kuiweka mtandaoni ili itumike na watu. Application hizi zinaweza kuwa na taarifa za kupotosha au zisizo za kweli kama hazijaaandikwa na wataalamu wa afya. Hakikisha unafahamu, madhumuni ya application hiyo na usitoe taarifa zako bila kujihakikishia usalama.


Tovuti, blogi na mitandao ya kijamii


Unapaswa kufahamu kuwa kuna utofauti mkubwa kati ya tovuti, blogi na mitandao ya kijamii.

Blogi na mitandao ya kijamii huandika wazo la mtu mmoja tu alilofikiria, wakati huo tovuti huandikwa kwa kutumia taarifa zilizothibitishwa na hutokana na mkusanyiko wa taarifa kutoka kwenye tafiti na majaribio mbalimbali ya kisayansi. Taarifa za tovuti pia zinazoaminika huwa na rejea za mada hiyo mwishoni mwa mada na husema taarifa hizo zimechukuliwa lini na kichwa cha mada cha chanzo hiko. Unaweza ingia kwenye rejea hizo na kujisomea ukweli kama kilichoandikwa kimetoka kwenye rejea zilizoorodheshwa.


Mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, na Instagram, ni mitandao ya watu na marafiki mbalimbali wenye elimu na wasio na elimu. Unaweza ungana na watu unaowafahamu au wale usio wafahamu. Uonapo habari za afya kwenye mitandao hii, jiulize kama ni habari sahihi au zisizo sahihi na kumbuka mara nyingi taarifa zinazotolewa kwenye mitandao hii si za kuaminika. Usiamini kila post hata kama imetoka kwa rafiki yako kama haina ushahidi kutoka kwenye tafiti. Unapaswa kutafuta chanzo cha taarifa hiyo yaani ni kwenye tovuti gani taarifa hiyo imetengenezwa na kama tovuti ina rejea za kuaminika kuhusu post hiyo iliyotolewa.


Jiamini na ongea na daktari wako siku zote


Tumia ufahamu wako kufikiria na kufanya uamuzi sahihi wakati wote kwa kuongea na daktari kabla ya kuchukua hatua baada ya kusoma mada ya afya mtandaoni. Licha ya kuwa kuna tovuti zilizojaribu kuelezea kila kitu, si wakati wote vilivyoelezewa vinaweza kuendana na hali yako ya kiafya kwa ujumla.


Unapaswa kutumia taarifa za mtandaoni kutoka kwenye tovuti za kuaminika ili kukupa mwangaza tu kabla ya kuwasiliana na daktari kwa uchunguzi, ushauri zaidi na tiba na si kuzitumia kujitibu. Usiogope gharama kuwasiliana na daktari kwani afya yako ni gharama.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

7 Oktoba 2021 04:53:41

Rejea za mada hii:

Lila J. Finney Rutten, PhD, MPH, et al. Online Health Information Seeking Among US Adults: Measuring Progress Toward a Healthy People 2020 Objective. https://journals.sagepub.com/doi/10.1177/0033354919874074. Imechukuliwa 18/09/2021

Dickerson, Suzanne et al. “Patient Internet use for health information at three urban primary care clinics.” Journal of the American Medical Informatics Association : JAMIA vol. 11,6 (2004): 499-504. doi:10.1197/jamia.M1460

NIH. Online health information is it reliable?.https://www.nia.nih.gov/health/online-health-information-it-reliable. Imechukuliwa 17/08/2021

Internet users in Tanzania. https://datareportal.com/reports/digital-2021-tanzania#. Imechukuliwa 17/08/2021

Boon-itt, S. Quality of health websites and their influence on perceived usefulness, trust and intention to use: an analysis from Thailand. J Innov Entrep 8, 4 (2019). https://doi.org/10.1186/s13731-018-0100-9.

Pew Internet and American Life Project. Internet Health Resources, Health Searches and Email Have Become More Commonplace, But There Is Room for Improvement in Searches and Overall Internet Access. 2003. Available at: http://pewInternet.org/. Imechukuliwa 18/09/2021

Sbaffi, L., & Rowley, J. (2017). Trust and credibility in web-based health information: a review and agenda for future research. Journal of Medical Internet Research, 19(6), 454–471.

bottom of page