top of page

Imeandikwa na Daktari wa ULY CLINIC

Jumanne, 28 Aprili 2020

Parathairoidi

Parathairoidi

Tezi za parathairoidi ni tezi nne ndogo zilizopo nyuma ya tezi ya thairoidi inayopatikana mbele ya koromeo maeneo ya shingo.Kati ya tezi hizi nne, mbili zipo kulia na mbili kushoto ya tezi ya thairoidi, nyuma ya kila bawa la tezi ya thairoidi. Jina parathairoidi limetokana na kukaa kwa tezi hizi sambamba na tezi ya thairoidi. Tezi hii hotoa homoni ya parathairoidi.

Kazi ya homoni ya parathairoidi

• Kazi kubwa ya homoni ya parathairoidi ni kurekebisha kiwango cha madini kalisiamu kwenye damu kwa kuhakikisha kinabaki kwenye kiwango cha kawaida kwa kupandisha kiwango hicho pindi kinapo shuka chini ya kiwango cha kawaida.

• Kazi nyngine ni kurekebisha kiwango cha madini ya magneziamu (Magnesium) na fosfeti(phosphate) kwenye damu.

Namna homoni ya parathairoidi inavyofanya kazi mwilini

Kuongeza kasi ya kufyonzwa kwa kalisiamu na magnesium kwenye figo ili madini hayo yasipotee kwenye mkojo hivyo kubaki kwenye damu.

Kuongeza kasi ya ufyonzaji wa kalisiamu na magnesium kutoka kwenye mfumo wa mmeng'enyo chakula kwenda kwenye damu.

Kuchochea figo kutengeneza vitamin D ambayo itaenda kusaidia kalisiamu kufyonzwa kutoka kwenye mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.

Kuruhusu kalisiamu kumomonyoka kutoka kwenye mifupa kwenda kwenye damu. Asilimia 99 ya kalisiamu huifadhiwa kwenye mifupa.

Namna mwili unavyorekebisha uzalishaji wa homoni ya parathairoidi

Ikiwa kiwango cha kalisiamu kwenye damu kitapanda kufikia kiwango cha kawaida na kuelekea kuzidi, ubongo hutambua na kutuma taarifa kwa tezi ya parathairoidi kupunguza au kuacha kutoa homoni ya parathairoidi.

Kwa upande mwingine kiwango cha kalisiamu kikushuka zaidi ya kiwango cha kawaida ubongo hutambua na kutuma taarifa kwa tezi ya parathairoidi kutoa tena homoni hiyo. Mfumo huu huitwa mfumo wa taarifa hasi

Lakini pia kiwango cha madini ya kalisiamu kwenye kwenye damu kikizidi kawaida basi, homoni ya calcitonin huzalishwa kutoka kwenye tezi ya thairoidi na hufanya kazi ya kushusha kiwango cha homoni hii.

Umuhimu wa kalisiamu mwilini

• Kuwezesha misuli kufanya kazi.
• Kuwezesha taarifa mbalimbali kusafiri kwenye mfumo wa fahamu.
• Kuwezesha damu kuganda ili isivuje mtu anapo umia.

Dosari za tezi ya parathairoidi

Dosari za tezi ya parathairoidi zinaweza kusababisha jambo moja kati ya mawiwili:-

1. Homoni ya parathairoidi kutolewa nyingi kuzidi kiwango cha kawaida, au
2. Homoni ya parathairoidi kutolewa chini ya kiwango cha kawaida.

Homoni ya parathairoidi kutolewa nyingi kuzidi kiwango cha kawaida.

Mara nyingi dosari hii husababishwa na uvimbe kwenye tezi ya parathairoidi.

Dalili za homoni ya parathairoidi kutolewa nyingi kupita kiwango cha kawaida ni;

• Kukojoa sana kupita kiasi
• Kuhisi kiu sana kupita kiasi
• Mawe kujitengeneza kwenye figo
• Kichefuchefu
• Kutopapata choo
• Mwili mzima kuchoka

Homoni ya parathairoidi kutolewa chini ya kiwango cha kawaida;

Tatizo hili huweza kusababishwa na jeraha kwenye tezi ya parathairoidi wakati wa upasuaji, miale ya mionzi mikali au kasoro za kuzaliwa.

Dalili za homoni ya parathairoidi kutolewa chini ya kiwango cha kawaida ni;

• Misuli kukakamaa
• Kuchoka
• Kupata ganzi sehemu mbalimbali za mwili
• Kupata degedege
• Kupata ukungu machoni

Wasiliana na daktari wako endapo umeona kuwa una dalili yoyote ile katika maelezo haya kwa ushauri na tiba

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba zaidi kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii au kubonyeza hapa.

Imeboreshwa,

13 Julai 2021 18:34:19

Rejea za mada hii;

1.Ross and Wilson Anatomy and Physiology in healthy and illness 12th Edition ISBN 978-0-7020-5325-2 ukurasa wa 223 na 233.

2.Principles of anatomy and physiology twelfth edition ISBN 978-0-470-08471-7 by Gerard J. Tortora and Bryan Derrickson ukurasa wa 662

3.Madscape: https://emedicine.medscape.com/article/874690-overview imechukuliwa 27/04/2020.
bottom of page