top of page

Imeandikwa na Daktari wa ULY CLINIC

Jumatatu, 11 Mei 2020

Pineal

Tezi ya Pineal

Pineal ni tezi iliyopo sehemu ya ndani ya ubongo. Jina lake limetokana na umbo la tezi hiyo kufanana na pinecone. Tezi hii huzalisha homoni ya melatonin.

Kazi za homoni ya melatonin

Utendaji wa homoni hii bado haujulikani vizuri lakini miongoni mwa kazi zake muhimu ni hizi mbili:-

• Kusimamia mzunguko wa kulala na kumka
• Huchelewesha ukuaji na ukomavu wa viungo vya uzazi kabla ya kubalehe.

Soma maelezo ya ziada kuhusu kazi hizi hapa chini;

Kusimamia mzunguko wa kulala na kumka

• Homoni hii hutolewa kwa kiwango kikubwa nyakati za usiku kuliko mchana,

• Majiribio yaliyofanyika kwa watu waliopewa vidonge vyenye homoni ya melatonin iliwafanya walale nyakati za mchana.

• Hii ilionekana kuwa melatonin inaweza kutumika kuwafanya watu wanaofanya kazi usiku kuwa na mazoea ya kulala mchana.

Kuchelewesha ukuaji na ukomavu wa viungo vya uzazi kabla ya kubalehe

• Ushahidi mojawapo juu ya hili ni tafiti zinazo onyesha kwamba kiwango cha homoni hii ni kikubwa kwenye damu ya watoto kuliko kwa watu wazima na pia tezi ya pineal hupungua ukubwa taratibu kadri umri unvyo ongezeka baada ya mtu kubalehe.

• Baadhi ya majaribio yaliofanyika kwa wanyama ambao huzaliana kwa msimu ambayo walipewa melatonin, ilizuia kuzaliana kwa wanyama hao.

• Pia majaribio yaliofanyika kwa wanyama yanaonesha kua melatonin inasabisha korodani au ovari za wanyama hao kupungua ukubwa.

Ingawa bado kazi za homoni hii katika mwili wa binaadamu hazija julikana vizuri. Hivyo inaweza kuwa na kazi zaidi ya hizo na tafati Zaidi zinaendelea kufanyika.

Dosari za tezi ya peneal

Dosari za tezi ya peneal zinaweza kusababisha mwili kutofanya kazi vizuri nakusababisha:-

• Kukosa usingizi
• Matatizo ya akili kama vile kuchanganyikiwa na ukichaa
• Matatizo katika mfumo wa uzazi na utasa
• Wanawake kuwa na mzunguko usio wa kawaida.

Uvimbe kwenye tezi hii huweka shinikizo kwenye sehemu nyingine za ubongo na kupelekea:-

• Degedege
• Kupoteza kumbukumbu
• Kichwa kuuma
• Kichefuchefu na kutapika
• Matatizo ya macho na hata ya milango mingine ya fahamu.

Wasiliana na daktari wako endapo umeona kuwa una dalili yoyote ile katika maelezo haya kwa ushauri na tiba

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba zaidi kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii au kubonyeza hapa.

Imeboreshwa,

13 Julai 2021 18:23:19

Rejea za mada hii;

1.Principles of anatomy and physiology twelfth edition ISBN 978-0-470-08471-7 by Gerard J. Tortora and Bryan Derrickson ukurasa wa 673.

2.Ross and Wilson Anatomy and Physiology in healthy and illness 12th Edition ISBN 978-0-7020-5325-2 ukurasa wa 228.

3.Healthline.com: https://www.healthline.com/health/pineal-gland-function#complications imechuliwa 01/05/2020.

4.The human memory: https://human-memory.net/pineal-gland/ imechuliwa 01/05/2020.
bottom of page