top of page

Imeandikwa na Daktari wa ULY clinic

Ijumaa, 27 Machi 2020

Pituitari

Tezi ya Pituitari

Pituitari ni tezi ya endokrini yenye umbo dogo kama njegere na uzito wa gramu 0.5. Tezi hii hulala kwenye kitanda kiitwacho sela tusika kilichotengenezwa na fuvu la kichwa ambacho hupatikana chini kidogo ya ubongo na tezi ya hypothalamasi.

Tezi ya pituitari hufahamika kuwa ni tezi kuu kwenye mwili wa binadamu kwa sababu hutoa homoni nyingi kuliko tezi zingine, hata hivyo utendaji kazi wa tezi hii hudhibitiwa na tezi ya Haipothalamasi.

Homoni zinazotolewazo tezi hii hufanya kazi mbalimbali mwilini ikiwa pamoja na kuchochea au kuhimiza tezi zingine za endokrini kutoa homoni.

Pituitari huwa na sehemu kuu mbili, kimsingi baadhi ya vitabu husema kuwa ina sehemu tatu, sehemu ya tatu ni sehemu ya katikati ya sehemu kuu mbili. Sehemu hizo ni

• Sehemu ya mbele ambayo inaitwa adenohaipofisisi
• Sehemu ya nyuma inayoitwa nyurohaipofisis na
• Sehemu ya katikati

Sehemu ya mbele ya pituitari imeungwanishwa na mshipa wa damu unaotokea kwenye ubongo, sehemu ya nyuma ya tezi hii, huchukuliwa kuwa sehemu mojawapo ya ubongo na hufanya kazi chini ya maagizo ya ubongo.

Homoni zinazotolewa kwenye adenohaipofisisi

Sehemu hii ya mbele ya tezi ya pituitari huzalisha homoni sita ambazo ni;

• Homoni ya ukuaji (GH), -hufanya kazi kuu ya kuchochea ukuaji ndani ya mwilini

• Homoni ya kuchochea tezi ya Thairoidi -TSH- Homoni hii huchochea tezi ya thairoidi kutoa homoni ya
thairoidi

• Homoni ya Adrenokotikotropiki -ACTH- kwa jina jingine huitwa kotikotropini, homoni hii huchochea tezi
ya adreno kutoa homoni jamii ya steroidi, homoni kuu ikiwa ni homoni ya kotiso.

• Homoni ya kuchochea Foliko na homoni ya lutenaizing- hufahamika kama homoni za
gonadotrofini ambazo hufanya kazi kubwa za kuamuru ovari na korodani kuzalisha homoni za jinsia kama
homoni ya testosteroni na estrogeni

• Homoni ya Prolaktini – homoni hii hufanya kazi ya kuchochea chuchu kutoa maziwa.

Homoni zinazotolewa na nyurohaipofisisi

Homoni zinazotolewa na nyurohaipofisisi huzalishwa kutoka kwenye haipothalamasi na kuhifadhiwa sehemu hii ya nyuma ya tezi ya pituitari. Uzalishaji wa homoni hii hudhibitiwa na tezi ya haipothalamasi

Homoni hizo ni kama zifuatavyo;

• Homoni ya vasopresini kwa jina jingine homoni ya antiduretiki- kazi yake ni kudhibiti chumvi na shinikizo
la damu mwilini

• Homoni ya oksitosini- huamsha uchungu kwa kujongesha misuli ya kizazi wakati wa kujifungua na pia
kushinikiza misuli ya chuchu ikamue na kutoa maziwa baada ya kujifungua

Sehemu ya katikati ya pituitari

Sehemu ya katikati ya pituitari hutoa homoni ya melanosaiti (Homoni hii inakazi ya kuipa ngozi rangi yake) na homoni ya endofini ambayo ni dawa asili ya maumivu inayozalishwa na mwili wenyewe.

Magonjwa ya tezi ya pituitari

Baadhi ya magonjwa yanayoweza kutokea kwenye tezi ya pituitari yamegawanyika kwenye makundi matatu kama yalivyoorodheshwa hapo chini;

• Magonjwa yanayposababisha tezi kuzalisha homoni kwa wingi- kama ugonjwa wa
gingantizimu/akromegali, sindromu ya Cushing's na prolaktinoma

• Magonjwa yanayotokana na tezi kuzalisha homoni ndogo kama vile upungufu wa homoni ya ukujai
kwenye utuuzima, kisukari cha inspidazi na haipopituitarizimu

• Magonjwa yanayobadilisha umbo la tezi kama vile sindrome ya sella tupu na adenoma

Soma zaidi kuhusu magonjwa haya kwenye mada zilizo kwenye tovuti hii

Wasiliana na daktari wako endapo umeona kuwa una dalili yoyote ile katika maelezo haya kwa ushauri na tiba

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba zaidi kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii au kubonyeza hapa.

Imeboreshwa,

13 Julai 2021 19:00:07

Rejea za mada hii;

1.Kenneth S. S. (2005): Human Anatomy: USA: McGraw –Hill Companies. p. 105-108. ISBN 998-0-19-842878-0.

2.Moore, Keith, Agur, Anne (2007). Essential Clinical Anatomy, 3rd Edition. Lippincott William & Wilkins p. 73. ISBN 9788537215802

3.Seeley, R. R., Stephens, T. D., & Tate, P. (2003). Anatomy and Physiology. USA: McGraw Hill Companies.p. 154. ISBN 9781643468916.

4.Waugh, A., & Grant, A. (2006). Ross and Willson Anatomy and physiology in Health and illness. Churchill Livingstone Elservier: Elsevier Limited China. p. 144-152. ISBN 978-0-19-422278-0.

4.Seeley, R. R., Stephens, T. D., & Tate, P. (2003). Anatomy and Physiology. USA: McGraw Hill Companies

5.Waugh, A., & Grant, A. (2006). Ross and Willson Anatomy and physiology in Health and illness. Churchill Livingstone Elservier: Elsevier Limited China.
bottom of page