top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Dkt. Benjamin S, MD

Dkt. Lugonda, MD

13 Agosti 2026, 16:13:38

Vidonge vya majira (Vidonge vya uzazi wa mpango)

Vidonge vya majira vipo vya aina nyingi kama vile vya mchanganyiko wa homoni estrojeni na projesteroni ambazo huitwa kitaalamu vidonge mseto au yenye kichochezi cha projesterone tu na hufahamika pia kama majira ya projestoni pekee(POP).

Vidonge vyenye vichocheo viwili (Majira mseto mseto)

Kazi gani hufanywa dawa hizi; njia hii ya majira huzuia ujauzito kwa asilimia 99 kama zikitumiwa vyema kila siku kwa wakati uleule. Dawa hizi pia hupunguza dalili wanazopata wanawake wanapoingia kipindi kukoma kuona siku zao za mzunguko wa hedhi- yaani dalili za kuingia za kuingia komahedhi (wanapokuwa zaidi ya miaka 45) na pia huwa na faida ya kufanya mzunguko wa hedhi usibadilike badilike

Vidonge hivi hufanya kazi kwa:

  • Kuzuia yai kupevuka (uovuleshaji)

  • Kubadilisha ute wa mlango wa kizazi kuwa mzito ili kuzuia mbegu kupita

  • Kuweka ukuta wa wa ndani ya mfuko wa uzazi kuwa mwembamba ili kuzuia upandikizaji wa kijusi


Faida zake:

  • Kufanya mzunguko wa hedhi kuwa wa kawaida

  • Kupunguza dalili za kuingia komahedhi na maumivu ya hedhi

  • Kupunguza dalili kwa wanawake wanaoingia kipindi cha kukoma hedhi (premenopause)


Tahadhari:

  • Haifai kwa wanawake wanaovuta sigara na walio na umri zaidi ya 35(huongeze hatari zaidi ya kuganda kwa damu)

  • Kama una historia ya kipandauso (migraine) wasiliana na daktari kabla ya kutumia


Soma zaidi kuhusu vidonge hivi kwenye makala ya vidonge vya uzazi wa mpango vyenye vichocheo viwili

Vidonge vya projestini tu(POP)

Aina ya dawa hizi huwa salama kwa wanawake wanaovuta sigara, wenye kisukari, magonjwa ya moyo na pia kwa wanawake walio hatarini kupata migando ya damu. Dawa hizi pia hazipunguzi maziwa ya mama wakati ananyonyesha


Kama unashida kukumbuka kunywa dawa hii kwa wakati uleule basi unaweza kuchagua njia zingine maana hii haitafaa kwako.


Vidonge hivi havina estrojeni, hivyo ni salama kwa wanawake:

  • Wanaovuta sigara

  • Wenye kisukari

  • Wenye magonjwa ya moyo

  • Walio hatarini kupata damu kuganda

  • Wanaonyonyesha – havipunguzi maziwa


Hasara ndogo:

Vinahitaji kutumiwa wakati uleule kila siku, hata kuchelewa kwa dakika 3–12 (kutegemea aina) hupunguza ufanisi wake.


Soma zaidi kuhusu vidonge vya projestin kwenye makala ya vidonge vya projestin kwenye uzazi wa mpango.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, vidonge vya uzazi wa mpango vinaanza kufanya kazi baada ya muda gani?

Vidonge vya mchanganyiko huanza kufanya kazi ndani ya siku 7 ukianza siku ya kwanza ya hedhi. POP (projestin pekee) hufanya kazi ndani ya siku 2 endapo umeanza mwanzoni mwa hedhi. Ukianza siku nyingine, daktari atashauri kutumia kinga ya ziada kwa muda mfupi.

2. Je, vidonge vinaweza kurejesha hedhi iliyopotea kwa miezi miwili?

Inawezekana kama sababu ya kupotea kwa hedhi inahusiana na homoni, lakini si kila wakati. Kumbuka: Kupotea kwa hedhi kuna sababu nyingi (mfadhaiko(msongo wa mawazo), uzito, homoni, Sindromu ya Vifukomaji vingi kwenye ovari-PCOS n.k).


Ni muhimu kuonana na daktari ili kujua sababu halisi na kupata matibabu yanayofaa.

3. Je, vidonge vinaongeza uzito?

Si lazima. Baadhi ya wanawake hutunza maji mwilini au kuwa na hamu ya kula, lakini hii hutofautiana sana. Mabadiliko mengi huwa madogo na hupotea ndani ya miezi michache.

4. Nikisahau kidonge kimoja nifanye nini?

Kwa vidonge vya mchanganyiko: kunywa mara tu utakapoikumbuka.Kwa POP: ukichelewa zaidi ya kipindi kinachoruhusiwa, ufanisi hupungua – muone daktari ili kupata mwongozo salama.

5. Je, vidonge vinaweza kusababisha uchafu wa ukeni?

Mabadiliko madogo kwenye ute wa uke yanaweza kutokea, lakini harufu mbaya, maumivu au kuwashwa si kawaida. Ukiona mabadiliko yasiyo ya kawaida, muone mtaalamu wa afya.

6. Je, naweza kupata mimba nikiwa natumia vidonge?

Ufanisi wake ni karibu 99% ikiwa unatumiwa vizuri. Lakini ukisahau vidonge mara kwa mara, hatari ya ujauzito huongezeka.

7. Je, vidonge vinazuia magonjwa ya zinaa?

Hapana. Vidonge vinazuia mimba pekee. Kwa kinga dhidi ya magonjwa ya zinaa, kondomu bado inahitajika.

8. Je, vidonge vinaweza kusababisha hedhi kuwa nzito au hafifu?

Ndiyo. Vidonge vya mchanganyiko mara nyingi hupunguza uzito wa hedhi. POP mara nyingine husababisha kutokwa kidogo au hedhi kusimama – ni kawaida na si hatari.

9. Je, vidonge vinaweza kusababisha maumivu ya kichwa au kichefuchefu?

Ndiyo, kwa baadhi ya watu, lakini mara nyingi hutoweka ndani ya wiki kadhaa. Dalili zikizidi, muone daktari kwa ushauri salama.

10. Je, nitachelewa kurudi kwenye uwezo wa kupata mimba nikiacha vidonge?

Kwa kawaida uwezo wa kushika mimba hurudi haraka sana (wiki chache hadi miezi michache), kutegemea mwili wako. Kwa POP, kurudi huwa haraka zaidi.

11. Nilikuwa nataka kujua kuhusu vidonge vya uzazi wa mpango. unatakiwa kunywa baada ya kufanya tendo la ndoa au kabla ya kufanya tendo la ndoa?

Jibu hutegemea aina ya vidonge vya uzazi wa mpango unavyotumia, kwa sababu si vidonge vyote hutumiwa kwa njia moja. Vidonge vya uzazi wa mpango vya kawaida vya siku 28 hutumiwa kila siku kwa wakati unaokaribiana, bila kujali umefanya tendo la ndoa au la. Hufanya kazi kwa kuzuia ovulesheni (kutolewa kwa yai), kufanya ute wa mlango wa kizazi kuwa mzito ili kuzuia mbegu za kiume kupita, na kubadilisha mazingira ya mji wa mimba ili kupunguza uwezekano wa ujauzito. Kwa hiyo, vidonge hivi havimezwi kabla au baada ya kila tendo la ndoa, bali humezwa kila siku kulingana na maelekezo ya daktari au yaliyopo kwenye kifurushi cha dawa.


Kwa upande mwingine, vidonge vya kuzuia mimba vya dharura, kama vile Postinor-2- P2 (levonorgestrel) au dawa nyingine zinazofanana, hutumiwa baada ya kufanya tendo la ndoa bila kinga au pale njia ya uzazi wa mpango imeshindwa kufanya kazi, kwa mfano kondomu kupasuka. Dawa hizi zinapaswa kutumiwa haraka iwezekanavyo baada ya tendo la ndoa, kwani ufanisi wake hupungua kadri muda unavyopita. Hazipaswi kutumiwa kama njia ya kawaida ya uzazi wa mpango kwa sababu zina kiwango kikubwa cha homoni na hazina ufanisi sawa na njia za uzazi wa mpango zinazotumiwa mara kwa mara.


Ikiwa huna uhakika ni aina gani ya vidonge unavyotumia, usivimeze bila kufahamu matumizi yake. Muulize mtoa huduma wa afya au mfamasia akueleze jinsi vinavyotumika. Kutumia vidonge kwa usahihi ndiyo njia bora ya kuongeza ufanisi wake katika kuzuia ujauzito na kupunguza hatari ya kupata ujauzito usiopangwa.

12. Ukiwa hujatumia vidonge vya uzazi wa mpango kwa muda, ukafanya tendo la ndoa bila kuwa umetumia vidonge hivyo, kisha baada ya tendo ndipo ukaanza kuvitumia, je unaweza kupata mimba?

Ndio, unaweza kupata mimba. Vidonge vya uzazi wa mpango havitoi kinga ya dharura kwa tendo la ndoa ambalo tayari limefanyika. Ikiwa hukuwa unavitumia kwa usahihi kabla ya kufanya tendo la ndoa na shahawa ziliingia ukeni, kuanza kutumia vidonge baada ya tendo hakutazuia uwezekano wa yai kurutubishwa.


Kwa wanawake wanaoanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango kwa mara ya kwanza au baada ya kuviacha kwa muda, vidonge vya kawaida vya uzazi wa mpango huhitaji muda kabla ya kutoa kinga kamili. Mara nyingi, inashauriwa kutumia kondomu au kujizuia kufanya ngono kwa siku 7 za kwanza za matumizi (isipokuwa kama umeanza vidonge ndani ya siku 5 za kwanza za hedhi, kulingana na aina ya vidonge na mwongozo wa matumizi).


Ikiwa tendo la ndoa lisilo na kinga limetokea ndani ya saa 120 (siku 5) zilizopita na hutaki kupata ujauzito, unaweza kuhitaji kutumia vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango, kwa kuwa vidonge vya kawaida vya uzazi wa mpango haviwezi kulinda dhidi ya tendo ambalo tayari limefanyika. Kama hedhi itachelewa kwa zaidi ya wiki moja kuliko ulivyotarajia, fanya kipimo cha ujauzito na wasiliana na mtoa huduma za afya kwa ushauri zaidi.

13. Ukiwa umeacha kutumia vidonge vya uzazi wa mpango kwa muda, ukafanya tendo la ndoa bila kutumia kinga na mwanaume akamwaga shahawa ndani, unaweza kupata mimba?

Ndiyo, unaweza kupata mimba. Baada ya kuacha kutumia vidonge vya uzazi wa mpango, uwezo wa kupata ujauzito unaweza kurudi haraka kwa wanawake wengi. Kwa baadhi ya wanawake, ovulesheni (kutolewa kwa yai) inaweza kurejea ndani ya wiki chache baada ya kuacha vidonge, hata kabla ya kupata hedhi ya kwanza.


Iwapo ulifanya tendo la ndoa bila kutumia njia yoyote ya uzazi wa mpango na shahawa ziliingia ukeni, kuna uwezekano wa kupata ujauzito, hasa kama tendo hilo lilitokea siku ambazo yai linaweza kutolewa. Hata kama ulikuwa hujapata hedhi baada ya kuacha vidonge, bado inawezekana yai likawa limetolewa na kurutubishwa.


Ikiwa tendo la ndoa limetokea ndani ya saa 120 (siku 5) zilizopita na hukupanga kupata ujauzito, unaweza kuzingatia kutumia vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango mapema iwezekanavyo, kwa kuwa hufanya kazi vizuri zaidi zinapotumika haraka baada ya tendo la ndoa. Ikiwa umeshapita muda huo au unashuku unaweza kuwa mjamzito, subiri hadi hedhi ikichelewa kisha fanya kipimo cha ujauzito. Pia, kama hutaki kupata ujauzito kwa sasa, ni muhimu kuanza kutumia tena njia ya uzazi wa mpango inayokufaa kwa ushauri wa mtoa huduma za afya.

14. Ikiwa umesahau kumeza majira na umeshiriki tendo, unaweza kumeza baada ya kufanya tendo?

Ndiyo, kama unamaanisha umesahau kutumia kidonge cha uzazi wa mpango cha kila siku(majira), unaweza kukimeza baada ya kukumbuka, lakini hatua inayofuata hutegemea aina ya kidonge na umechelewa kwa muda gani. Kwa baadhi ya vidonge, kuchelewa kwa muda mfupi hakupunguzi sana kinga, wakati kwa vingine kuchelewa kunaweza kupunguza ufanisi wa kuzuia mimba.


Kama tayari umefanya tendo bila kinga baada ya kusahau kidonge, usitegemee tu kumeza kidonge hicho kama kinga ya dharura. Kidonge cha kawaida cha uzazi wa mpango si sawa na kidonge cha dharura. Ikiwa kuna uwezekano wa ujauzito, uzazi wa mpango wa dharura unaweza kuhitajika, na hufanya kazi vizuri zaidi unapotumiwa mapema baada ya tendo.


Kwa hiyo, kama tendo limetokea hivi karibuni, ni muhimu kujua jina la kidonge unachotumia, ni kidonge gani umesahau, umechelewa kwa saa ngapi au umeacha siku ngapi, na tendo lilifanyika lini. Taarifa hizo huamua kama unahitaji kidonge cha dharura na kama unapaswa kutumia kondomu kwa muda fulani wakati ukiendelea na vidonge vyako vya kawaida.

15. Natumia vidonge vya uzazi wa mpango sipati hedhi, shida ni nini?

Kama unatumia vidonge vya uzazi wa mpango na huupati hedhi, mara nyingi ni madhara(maudhi) ya matumizi ya vidonge hivyo. Vidonge vya uzazi wa mpango vina homoni zinazoweza kufanya ukuta wa ndani ya kizazi(endometriamu) kuwa mwembamba, hivyo damu ya hedhi inaweza kuwa kidogo sana au kutotokea kabisa.


Hata hivyo, kuna mambo muhimu ya kuzingatia:

  • Kama unatumia vidonge kwa usahihi na hujawahi kuruka dozi, kutokupata hedhi kunaweza kuwa athari ya kawaida ya vidonge.

  • Kama umesahau vidonge, umechelewa kutumia vidonge mara kwa mara, au umetapika/kuharisha sana baada ya kutumia kidonge, uwezekano wa ujauzito unaweza kuongezeka.

  • Kama umefanya ngono bila kinga na una wasiwasi, fanya kipimo cha ujauzito.

  • Usiachane na vidonge kwa sababu tu hujapata hedhi, ikiwa unavitumia kwa ajili ya kuzuia mimba na huna sababu nyingine ya kuacha.


Ikiwa vipimo vya ujauzito ni hasi lakini hujapata hedhi kwa muda mrefu, au una maumivu makali ya tumbo, kutokwa damu isiyo ya kawaida, kizunguzungu kikali au kuzimia, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na mtoa huduma wa afya.



Imeandikwa:

3 Novemba 2021, 15:31:24

ULY clinic inakushauri siku zote ufuate ushauri wa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia mawasiliano yetu.

Rejea za mada hii:

  1. American College of Obstetricians and Gynecologists. Amenorrhea: absence of periods. Washington, DC: ACOG; 2024.

  2. Klein DA, Poth MA. Amenorrhea: an approach to diagnosis and management. Am Fam Physician. 2013;87(11):781-788.

  3. Practice Committee of the American Society for Reproductive Medicine. Current evaluation of amenorrhea: a committee opinion. Fertil Steril. 2024;122(2):248-263.

  4. Munro AK, Critchley HOD, Fraser IS. The FIGO classification of causes of abnormal uterine bleeding in the reproductive years. Int J Gynaecol Obstet. 2018;143(3):393-408.

  5. Goodman NF, Cobin RH, Futterweit W, Glueck JS, Legro RS, Carmina E. American Association of Clinical Endocrinologists, American College of Endocrinology, and Androgen Excess and PCOS Society disease state clinical review: guide to best practices in the evaluation and treatment of polycystic ovary syndrome. Endocr Pract. 2015;21(11):1291-1300.

  6. World Health Organization. Family planning: a global handbook for providers. 3rd ed. Baltimore: Johns Hopkins Center for Communication Programs; 2022.

  7. Faculty of Sexual and Reproductive Healthcare. UK Medical Eligibility Criteria for Contraceptive Use. London: Faculty of Sexual and Reproductive Healthcare; 2019. Amended 2024.

  8. Jameson JL, Fauci AS, Kasper DL, Hauser SL, Longo DL, Loscalzo J, editors. Harrison's Principles of Internal Medicine. 21st ed. New York: McGraw Hill; 2022.

bottom of page