top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Helen L, M.D

Alhamisi, 21 Januari 2021

Acha mazoea ya kula chakula taka

Acha mazoea ya kula chakula taka

Chakula taka, ni aina ya chakula kisicho na thamani kubwa mwilini mwako. Sifa yake kubwa ni kuwa na nishati kwa wingi zinazotokana na mafuta au sukari, huku kikikosa au kuwa na kiwango kidogo sana cha protini, vitamin, madini, nyuzinyuzi na virutubisho vingine muhimu kwa mwili wako. Acha uteja wa kula chakula taka, kula vyakula vinavyoshauriwa kiafya.


Kwanini usile vyakula taka


Vyakula taka ni maarufu sana duniani kwa sababu havina bei, ni rahisi kuandaa haraka na ni vitamu mbali na kuvutia machoni. Vyakula hivi pia huhitaji viungo vya bei rahisi kama vile mafuta ya wanyama na sukari, badala ya vyakula vyenye umuhimu kama matunda, mboga za majani, nyama na nafaka zisizokobolewa.


Licha ya kuwa vitamu na kuvutia macho, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa watumiaji wa vyakula hivi hupata uteja wa kula vyakula hivyo endapo watatumia kwa muda mefu. Majaribio ya kisayansi yanaonyesha kuwa vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi huathiri ubongo sawa na dawa ya kulevya iitwayo cocaine.


Mtumiaji wa vyakula hivi kwa muda mrefu hukosa uwezo wa kujizuia kula na hutamani mara kwa mara kuvila ili afurahishe moyo wake. Tafiti zingine zinaonyesha kuwa, kemikali zilizowekwa kwenye baadhi ya vinywaji na vyakula vya kusindikwa mfano soda, hupelekea walaji wengi kuwa teja wa vyakula hivyo.


Nchi nyingi za bara la Amerika na Ulaya zimeacha matumizi ya vyakula hivi baada ya kupata madhara makubwa ya kiafya. Wanachi wengi asili ya bara la Afrika kwa sasa wanadhani kula vyakula hivi ni kuendana na wakati au ishara ya kuwa na uwezo wa kipesa, kinyume na ukweli kwamba ni vyakula taka.


Kutokana na taarifa za Shirika la afya duniani (WHO), inakadiriwa kuwa asilimia 12 ya watu duniani walikuwa na unene wa kupindukia (ugonjwa wa obeziti), na watu zaidi ya milioni 4.7 walikufa mapema kabla ya wakati kwa sababu ya ugonjwa wa obeziti (mwaka 2017), na huku kila mwaka watu milioni 2.8 hufa kwa sababu ya ugonjwa wa obeziti. Idadi hii ya vifo ni mara tano ya vifo vinavyosababishwa na UKIMWI na mara nne ya vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani. Idani ya watu wanaopata ugonjwa wa obeziti inategemea kuongezeka zaidi na kuua watu wengi zaidi duniani kwa siku zijazo.


Baadhi ya mifano wa vyaakula taka ni;

  • Vyakula vyenye mafuta mengi na sukari mfano keki, pipi, donati na chipsi

  • Vinywaji vyenye sukari nyingi mfano Soda, juisi za kusindikwa, vinywaji vya kuongeza nguvu

  • n.k


Kwanini usile vyakula taka?


Kula vyakula taka huongeza hatari ya kupata magonjwa sungu kama vile kisukari aina ya pili, obeziti, magonjwa mbalimbali ya moyo, saratani na ini kujaa mafuta.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

19 Julai 2023 20:41:55

Rejea za mada hii:

1.Ashley N Gearhardt etal. The addiction potential of hyperpalatable foods. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/21999688/. Imechukuliwa 20.01.2021

2.Junk food. https://www.imedpub.com/scholarly/junk-food-journals-articles-ppts-list.php#. Imechukuliwa 20.01.2021

3.Margaret J Morris etal. Why is obesity such a problem in the 21st century? The intersection of palatable food, cues and reward pathways, stress, and cognition. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/25496905/. Imechukuliwa 20.01.2021

4.C Rob Markus, etal. Eating dependence and weight gain; no human evidence for a 'sugar-addiction' model of overweight. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/28330706/. Imechukuliwa 20.01.2021

5.Alexandra G Di Feliceantonio, etal. Supra-Additive Effects of Combining Fat and Carbohydrate on Food Reward. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/29909968/. Imechukuliwa 20.01.2021

6.Adrian Carter , etal. The Neurobiology of "Food Addiction" and Its Implications for Obesity Treatment and Policy. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/27296500/. Imechukuliwa 20.01.2021

7.D W Tang, etal. Food and drug cues activate similar brain regions: a meta-analysis of functional MRI studies. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22450260/. Imechukuliwa 20.01.2021

8. Nicole M. Avena, etal. Sugar and Fat Bingeing Have Notable Differences in Addictive-like Behavior. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2714381/. Imechukuliwa 20.01.2021

9. WHO. Obesity and overweight. https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/obesity-and-overweight#. Imechukuliwa 20.01.2021

10.WHO. Obesity. https://www.who.int/news-room/facts-in-pictures/detail/6-facts-on-obesity#. Imechukuliwa 20.01.2021

bottom of page