top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Helen L, M.D

Alhamisi, 4 Februari 2021

Baadhi ya dawa zilizoisha muda wa matumizi zinaweza kutumika kwa tahadhari

Baadhi ya dawa zilizoisha muda wa matumizi zinaweza kutumika kwa tahadhari

Tafiti nyingi zinaonyesha, kiini cha dawa hupungua tangu siku dawa inatengenezwa na asilimia 90 ya kiini cha dawa nyingi, hubakia kwenye dawa hadi miaka mitano tangu siku ya kuisha muda wa matumizi. Endapo unahitaji matokeo ya asilimia 100 kutoka kwenye dawa, tumia dawa ambayo haijaisha muda wake wa matumizi.


Kwanini dawa inawekewa muda wa kuisha matumizi?


Sheria ya kuandika muda wa dawa kutumika ilitungwa na malaka ya dawa Amerika (FDA) miaka ya 1970, ikitaka kila dawa iwekewe tarehe ya kutengenezwa na tarehe ya kuisha muda wake wa matumizi.


Hata hivyo, makampuni mengi hutengeneza dawa na kuweka tarehe ya mwisho wa matumizi kama matakwa ya sheria hiyo, bila kufanya tafiti za kufahamu muda halisi wa kiini cha dawa hizo kuisha kabisa au kutofaa kwa matumizi. Hii inasababisha kuharibiwa kwa dawa nyingi kabla ya wakati na kuongeza mzigo wa gharama kwa wanunuaji na watumiaji wa dawa hizo, licha ya kuwa bado zinaweza kutumika kwa kuwa zina kiini cha dawa kinachotosha kutibu. Kwa mujibu wa FDA, dawa ambazo zinapaswa kutumika kwa binadamu kwa ajili ya matibabu ya magonjwa na hali mbalimbali, zinatakiwa kuwa na asilimia 90 hadi 110 ya kiini cha dawa ili kuleta ufanisi zaidi. Hata hivyo tafiti nyingi zinaonyesha kuwa, dawa zilizoisha muda wake wa matumizi, huwa bado zina kiini cha dawa kwa asilimia 90 au zaidi miaka mitano tangu kuisha kwa muda wa matumizi (‘expire date’)


Ifahamike kwamba si dawa zote zilizoisha muda wake wa matumizi ni sumu au hazina uwezo wa kutibu, bali dawa nyingi zilizoisha muda wa matumizi huwa na kiwango kizuri cha kiini cha dawa mpaka miaka 10 toka dawa imeisha muda wake wa matumizi.


Mipango ya kuongeza muda wa dawa kutumika baada ya kuisha muda wake wa matumizi

Baadhi ya tafiti na mashirika mbalimbali yanashauri kuongezwa kwa muda wa matumizi ya dawa hata baada ya kuisha muda wake wa kutumika, ili kukabiliana na tatizo la kifedha linalowakumba watu wengi kwa kukosa uwezo wa kununua dawa. Programu maalumu ya kuongeza muda wa matumizi ya dawa baada ya kuisha muda wake wa matumizi ilianzishwa mwaka 1986 na Idara ya ulinzi ya Amerika kwa kushirikiana na mamlaka ya chakula na dawa Amerika(FDA), kwa jina la ‘Shelf Life Extension Program’ (SLEP). SLEP inataka makampuni na viwanda vinavyotengeneza dawa kufanya tafiti zaidi kwenye dawa zilizoisha muda wake kuangalia kiwango cha uwepo wa kiini cha dawa na endapo dawa hizo ziongezewe muda wa matumizi au la. Katika programu hii, mamlaka ya chakula na dawa Amerika (FDA) inafanya baadhi ya tafiti na majaribio kwenye dawa zilizoisha muda wake, dawa zinazoonekana kwenye tafiti hizo kuwa na kiini kwa asilimia 90 au zaidi hata baada ya kuisha muda wa matumizi, huruhusiwa kuongezewa muda wa matumizi chini ya uangalizi wa mamlaka hiyo.


Mifano ya dawa zinazoweza kuishi baada ya muda wa matumizi kuisha

Dawa zinazoweza kuishi muda mrefu hata baada ya kuisha muda wa matumizi ni;


  • Dawa za vidonge

  • Dawa za tembe


Baadhi ya dawa ambazo haziishi muda mrefu ni;

  • Nitroglycerin

  • Insulin

  • Dawa za kimiminika jamii ya ‘antibiotics’


Madhara ya kutumia dawa zilizoisha muda wake


Muundo wa kampsundi ya baadhi ya dawa hubadilika baada ya kuisha muda wake, kampaundi mpya inayozalishwa huwa na uwezo mdogo wa kutibu na pia huweza kuwa sumu au kusababisha madhara mengine mwilini


Baadhi ya vimelea endapo watatibiwa na dawa iliyoisha muda wake hutengeneza usugu dhidi ya dawa na hivyo huweza kusababisha kufeli kwa dawa hiyo kutibu vimelea hao


Ushauri wa kuzingatia


Endapo unahitaji ufanisi wa dawa kwa asilimia 100, ni vema ukatumia dawa ambayo haijaisha muda wake wa matumizi.


Mashirika ya dawa yapewe muda wa kufanyia tafiti uwezo wa dawa kutibu maradhi mbalimbali hata baada ya dawa hizo kuisha muda wake. Hii itasaidia kuongeza muda wa matumizi ya dawa na kupunguza gharama kwa watumiaji wanaonunua dawa hizo.


Ili kufanya dawa iishi muda mrefu, hifadhi dawa kwenye sehemu ya ubaridi kwenye jokofu ili kusaidia iishi kwa muda mrefu.


Makampuni na viwanda vinavyotengeneza dawa, zinunue dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi ili kuzihuisha tena kwa ajili ya kutumika, badala ya kuziharibu. Hii itapunguza kuharibiwa kwa dawa pamoja na gharama kwa watumiaji na kutunza mazingira.


Onyo

Usitumie dawa ambayo imekweisha muda wake wamatumizi, wasiliana na mfamasia au daktari wako kabla ya kutumia dawa yoyote ile.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

19 Julai 2023 20:41:55

Rejea za mada hii:

1.Why do medicines have expiry dates. https://www.nhs.uk/common-health-questions/medicines/why-do-medicines-have-expiry-dates/#. Imechukuliwa 04.02.2021

2.https://www.health.harvard.edu/staying-healthy/drug-expiration-dates-do-they-mean-anything. Imechukuliwa 04.02.2021

3.Dan Gikonyo, et al. Drug expiry debate: the myth and the reality. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC7040264/#R2. Imechukuliwa 04.02.2021

4.Robbe C Lyon, et al. Stability profiles of drug products extended beyond labeled expiration dates. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/16721796/. Imechukuliwa 04.02.2021

5.Lee Cantrell, PharmD, et al. Stability of Active Ingredients in Long-Expired Prescription Medications. https://jamanetwork.com/journals/jamainternalmedicine/fullarticle/1377417. Imechukuliwa 04.02.2021

6.US food and drug administration. Expiration Dating Extension. https://www.fda.gov/emergency-preparedness-and-response/mcm-legal-regulatory-and-policy-framework/expiration-dating-extension. Imechukuliwa 04.02.2021

bottom of page