Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Jumatano, 18 Agosti 2021
Epuka kula chumvi nyingi
Kula vyakula vya kusindikwa au kuongeza chumvi wakati wa kula ni chanzo kikuu cha kula chumvi nyingi. Epuka kula zaidi ya gramu 2.3 za chumvi kila siku kwa kuacha chumvi ya nyongeza na kuchagua chakula chenye chumvi kidogo.
Chumvi ni nini?
Chumvi ni madini ya sodium yaliyoungana na chloride, gramu moja ya chumvi huwa na asilimia 40 ya sodium na asilimia 60 ya chloride.
Mwili unahitaji kiasi gani cha chumvi kila siku?
Ili mwili uweze kufanya kazi vema unahitaji kula kila siku kati ya gramu 1.5 hadi 2.3 kama inavyoshauriwa na mashirika mbalimbali ya kiafya. Gramu 2 za chumvi huwa sawa na robo kijiko cha chai. Wagonjwa wa shinikizo la damu pia wanapaswa kupata chumvi kwenye chakula ili waweze kupata afya njema, kiasi wanachoshauriwa ni gramu 1.5 kwa siku. Kiasi cha chumvi kinachopaswa kutumika kwa siku kulingana na umri kimeainishwa hapa chini;
Umri wa mwaka 1–3 Gramu 1.5
Umri wa miaka 4–8 Gramu 1.9
Umri wa miaka 9–13 Gramu 2.2
Umri wa miaka 14–18 Gramu 2.3
Hasara za nyingi mwilini
Licha ya kuwa na umuhimu pamoja na faida lukuki mwilini, kula chumvi nyingi husababisha madhara ya moja kwa moja kwenye ubongo, mishipa ya damu, mishipa ya fahamu, moyo na figo. Tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa m’mbwa na panya na uchunguzi uliofanyika kwa biandamu unathibitisha kuwa madhara hayo hutokea pasipo kuchangiwa na shinikizo la damu. Madhara mengine ya chakula chenye chumvi nyingi ni;
Kukakamaa kwa mishipa ya damu
Kuamka kwa magonjwa ya shambulio binafsi la kinga ya mwili
Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu
Saratani
Namna ya kutambua kiasi cha chumvi kwenye vyakula vya kusindikwa
Ili kutambua kiasi cha chumvi kwenye vyakula vya kusindikwa, soma maelezo ya vilivyomo ndani ya chakula hicho. Maelezo yanayokuwepo na maana yake halisi yameorodheshwa hapa chini;
Majina yanayoonekana kwenye lebo ya chakula na maana yake iliyofichika
Salt/Sodium
Free- ina chumvi chini ya miligramu 5 kwa kila zao
Very Low Sodium
Ina miligramu 35 ya sodium au pungufu
Low Sodium
Ina miligramu 140 ya sodium au pungufu
Reduced Sodium
Ina upungufu wa asilimia angalau 25 ya chumvi ukilinganisha na vyakula vingine vya kusindikwa
Light in Sodium au Lightly Salted
Imepunguzwa chumvi kwa asilimia 50 kulinganisha na vyakula vingine vya kusindikwa
No-Salt-Added au Unsalted
Chakula hakijaongezewa chumvi wakati wa maandalizi na huwa hakina chumvi.
Namna ya kuepuka kula chakula chenye chumvi nyingi
Soma kila lebo ya chakula cha kusindikwa, hakikisha kama unatumia chakula chenye chumvi, hautumii zaidiya gramu 2.3 kwa siku( hii ni jumla ya chakula hicho cha kusindikwa na vyakula vingine)
Andaa chakula chako mwenyewe ambacho kinafahamika kina kiasi gani cha chumvi
Ongeza ladha ya chakula bila kuongeza chumvi
Tumia nyama isiyosindikwa badala ya mazao yake kama soseji n.k
Kama unatumia mboga za majani za kusindikwa, tumia ambazo hazijawekewa chumvi
Osha kwa maji vyakula vilivyosindikwa kwa chumvi kabla ya kula au kupika
Nunua vyakula vya kusindikwa visivyo na chumvi
Punguza kiasi cha mlo unaokula ili kuepuka kula chumvi nyingi
Kama unakula mgahawani, pendelea vyakula vyenye chumvi kidogo sana.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
6 Oktoba 2021 15:42:53
Rejea za mada hii:
1. William B. Farquhar, PhD, et al. Dietary Sodium and Health: More Than Just Blood Pressure. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5098396/. Imechukuliwa 18.8.2021
2. Feng J He, et al. Importance of salt in determining blood pressure in children: meta-analysis of controlled trials. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/17000923/. Imechukuliwa 18.8.2021
3. Róbert Agócs,et al. Is too much salt harmful? Yes. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC7384997/. Imechukuliwa 18.8.2021
4. Izzat Alawwa, et al. Dietary salt consumption and the knowledge, attitudes and behavior of healthy adults: a cross-sectional study from Jordan. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5990954/. Imechukuliwa 18.8.2021
4. Ralf Willebrand, et al. The role of salt for immune cell function and disease. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6002217/. Imechukuliwa 18.8.2021
5. The Role of Potassium and Sodium in Your Diet. https://www.cdc.gov/salt/potassium.htm. Imechukuliwa 18.8.2021
6. Dietary Guidelines. https://health.gov/sites/default/files/2019-09/2015-2020_Dietary_Guidelines.pdf. Imechukuliwa 18.8.2021
7. Guideline: Sodium Intake for Adults and Children. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK133309/. Imechukuliwa 18.8.2021
8. How much sodium should I eat per day?. https://www.heart.org/en/healthy-living/healthy-eating/eat-smart/sodium/how-much-sodium-should-i-eat-per-day. Imechukuliwa 18.8.2021