top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Lugonda B, MD

Jumamosi, 7 Agosti 2021

Ganzi na maumivu ya mikono wakati wa ujauzito

Ganzi na maumivu ya mikono wakati wa ujauzito

Ganzi na hisia za maumivu ya mikono wakati wa ujauzito husababishwa na mgandamizo kwenye mshipa wa fahamu unaopita shimo la kapo. Kukanda kwa maji baridi kisha moto, kufanya zoezi la kukunja ngumi na kunyoosha vidole au kukunja na kunyoosha maungio ya kiganja ni tiba asili ya maumivu hayo.


Nini husababisha ganzi na hisia za kuchomachoma wakati wa ujauzito?


Hisia za ganzi, maumivu au kuchomachoma mikononi hutokana na sindomu ya kapo ambayo hutokea kwa asilimia 60 ya wajawazito, ikimaanisha kati ya wajawazito 100, wajawazito 60 watapata maumivu hayo.


Sindromu ya kapo hutokea kama mshipa wa median unaopita kwenye shimo la kapo umegandamizwa kiasi cha kushindwa kupitisha vema taarifa za mfumo wa fahamu kutoka kwenye ubongo kwenda kwenye vidole vya mikono na hivyo kupelekea ishara ya maumivu au ganzi kwenye vidole au kiganja cha mkono.


Nini husababisha sindromu ya kapo wakati wa ujauzito?


Sindromu ya kapo wakati wa ujauzito hutokana na ongezeko la mgandamizo kwenye mshipa wa fahamu wa median kutokana na ongezeko la maji kwenye tishu wakati wa ujauzito. Shimo la kapo limetengenezwa kwa mifupa pamoja na ligament za kapo. Shimo la kapo hupitisha mishipa ya damu na mishipa ya fahamu inayopeleka taarifa za mfumo wa fahamu kwenye kiganja na vidole vya mikono.


Ongezeko la maji kwenye tishu hutokea wakati wa ujauzito, baadhi ya maji hukusanyika kwenye shimo la kapo kiasi cha kupelekea ongezeko la shinikizo kwenye mshipa wa median na hivyo kupelekea kuonekana kwa dalili za ganzi au maumivu ya mkono na vidole vya mikono.


Dalili za sindromu ya kapo

Dalili za sindromu ya kapo wakati wa ujauzito hutofautiana baina ya wajawazito


  • Ganzi kwenye vidole (kidole gumba, kidole index, kidole cha kati na sehemu ya pembeni ya nusu ya kidole pete)

  • Maumivu au ganzi ya kiganja au mkono

  • Kuvimba na kwa kidole gumba na kidole cha 2 na 3

  • Kushindwa kushika kitu na kufanya kazi zinazohitaji vidole kujituma


Mambo ya kufanya ili kupunguza ganzi na maumivu ya kiganja cha mkono wakati wa ujauzito


Pumzisha mikono yako

Jaribu kutofanya kazi ambazo si lazima kuzifanya zinazohusisha kutumikisha kiganja cha mkono na maungio kati ya mkono na kiganja. Tumia mto kupumzisha mikono yako wakati umekaa kwa jinsi utakavyoweza.


Kanda kwa barafu

Tumia barafu ndogo iliyo kwenye kifungashio cha nailoni kugandamiza ligament kapo kwa muda wa dakika 10 ili kuongeza ubaridi kwenye maungio ya kiganja. Mbadala wake pia unaweza kumwagia maji ya ubaridi kwenye maungio ya kiganja cha mkono. Kufanya hivi husaidia kuondoa ganzi na maumivu kutokana na sindromu ya kapo. Ili kupata matokeo mazuri zaidi, baada ya kukanda kwa kutumia barafu, kanda kwa kutumia kutumia chupa ya maji ya moto iliyofunikwa na taulo ili kuepuka kuungua. Unapaswa kutumia chupa maalumu ili isipasuke na kukuunguza mkono wako.


Kama unatumia barafu na maji ya moto, fanya hivyo kwa kukanda kwa dakika moja kwa barafu, kisha dakika moja kwa maji ya moto kwa muda wa dakika 6 hadi saba kisha pumzika. Rudia kitendo hiki mara sita kwa siku.


Weka mikono yako juu

Unapopumzisha mikono yako, iweke juu zaidi ya usawa wa moyo, hii inamaanisha, mfano ukiwa umekaa, tumia mito miwili kuweka mikono juu zaidi ya usawa wa moyo ulipo. Kufanya hivi kutasaidia kuondoa maji kwenye tishu zinazozunguka shimo la kapo.


Fanya mazoezi

Ingawa kupumzika ni jambo la msingi, unapaswa kufanya mazoezi ya maungio kati ya mkono na kiganja cha mkono. Kufanya mazozi kama yanayonekana kwenye picha na yaliyoorodheshwa hapa chini husaidia sana kupunguza maumivu ya shimo la kapo.


Wakati gani wa kuwasiliana na daktari unapokuwa na ganzi au maumivu ya mikono wakati wa ujauzito?


Wasiliana na daktari haraka endapo umefanya juhudi zote zilizoorodheshwa hapo juu bila kupata unafuu wowote. Baada ya kujifungua ni matarajio kwamba dalili za sindromu ya kapo zitaisha ndani ya wiki moja hadi mbili, endapo hazijaisha unapaswa kuonana na daktari kwa uchunguzi na tiba.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

6 Oktoba 2021 15:44:38

Rejea za mada hii:

1. Presazzi A, et al. Carpal tunnel: Normal anatomy, anatomical variants and ultrasound technique (https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3558235/). Imechukuliwa 07.08.2021

2. NHS. Carpal tunnel syndrome during pregnancy maternity information. https://www.uhs.nhs.uk/Media/UHS-website-2019/Patientinformation/Pregnancyandbirth/Carpal-tunnel-syndrome-during-pregnancy-maternity-information.pdf. Imechukuliwa 07.08.2021

3. National Institute of Neurological Disorders and Stroke. Carpal Tunnel Syndrome Fact Sheet (https://www.ninds.nih.gov/Disorders/Patient-Caregiver-Education/Fact-Sheets/Carpal-Tunnel-Syndrome-Fact-Sheet). Imechukuliwa 07.08.2021

4. Arthritis Foundation. Carpal Tunnel Syndrome (https://www.arthritis.org/about-arthritis/types/carpal-tunnel-syndrome/). Imechukuliwa 07.08.2021

5. American Society for Surgery of the Hand. Carpal Tunnel. Syndrome (http://www.assh.org/handcare/Anatomy/Details-Page/articleId/27950). Imechukuliwa 07.08.2021

6. American Association of Neurological Surgeons. . Accessed 10/2/201.Carpal Tunnel Syndrome (https://www.aans.org/Patients/Neurosurgical-Conditions-and-Treatments/Carpal-Tunnel-Syndrome). Imechukuliwa 07.08.2021

7. American Academy of Orthopaedic Surgeons, OrthoInfo. . Accessed 10/2/2019. Carpal Tunnel Syndrome (https://orthoinfo.aaos.org/en/diseases--conditions/carpal-tunnel-syndrome)

bottom of page