top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Dkt. Sospeter B, MD

Dkt. Adolf S, MD

1 Januari 2026, 09:56:41

Hedhi baada ya uzazi wa mpango

Hedhi baada ya uzazi wa mpango

Baada ya kuacha kutumia njia za uzazi wa mpango zenye vichochezi, mzunguko wa hedhi unaweza kuchukua muda kurejea katika hali ya kawaida. Kwa wanawake wengi, hedhi hurejea ndani ya siku 90, lakini kwa baadhi ya njia—hasa sindano ya Depo-Provera—inaweza kuchukua hadi miezi 18–22.


Kuchelewa huku hakumaanishi tatizo mara moja; mara nyingi mwili unahitaji muda kurejesha uzalishaji wa homoni za asili na kurudia mzunguko wa kawaida. Hata hivyo, hedhi isiporejea ndani ya siku 90 (isipokuwa kwa watumiaji wa Depo-Provera), unapaswa kuona daktari.


Kwa nini hedhi huchelewa Baada ya kuacha vichochezi?

Hii hutokea kwa sababu mwili unahitaji muda kufufua mfumo wa asili wa homoni unaodhibiti uovuleshaji na mzunguko wa hedhi. Kiasi na muda wa kurejea kwa hedhi hutegemea:

  • Aina ya uzazi wa mpango uliotumika

  • Muda wa matumizi

  • Msongo wa mawazo

  • Mabadiliko ya uzito

  • Lishe na mazoezi

  • Afya ya jumla ya homoni


Kila njia inavyoathiri kurejea kwa hedhi


1. Vidonge vya Majira (mchanganyiko na Projestine tu)
  • Asilimia 97% ya wanawake hupata hedhi ndani ya siku 90 baada ya kuacha vidonge.

  • Inawezekana kupata hedhi isiyoeleweka mwanzoni (spotting, kuchelewa au kuja mapema).

  • Hedhi isiporejea baada ya siku 90 wasiliana na daktari kuchunguza visababishi vingine kama matatizo ya tezi, Sindromu ya ovari yeney vifukomaji vingi, uzito kupita kiasi, au ujauzito.


2. Kipandikizi (Implant – Nexplanon)
  • Kipandikizi kinaweza kusababisha kukosa hedhi (amenorea) baada ya mwaka wa kwanza wa matumizi.

  • Baada ya kuondolewa, hedhi hurejea haraka kwa wengi ndani ya siku chache hadi wiki chache.

  • Mzunguko wa kawaida hurudi ndani ya siku 90.


3. Kitanzi chenye kichocheo (Hormonal IUD)
  • Hupunguza hedhi au kuisimamisha kabisa.

  • Baada ya kuondoa, mwili hurudi katika hali ya kawaida haraka.

  • Hedhi inatarajiwa kurejea ndani ya siku 30–90.


4. Bangiri yenye kichochezi (Bangira ya ukeni – bangiri-Nuva)
  • Hedhi hutarajiwa kurejea ndani ya siku 2–3 baada ya kutoa bangiri.

  • Mzunguko hurudi katika hali ya kawaida ndani ya siku 90.


5. Sindano ya Depo-Provera
  • Njia hii husababisha kuchelewa zaidi kwa hedhi kurejea kuliko zote.

  • Hedhi hurejea ndani ya miezi 18–22 baada ya sindano ya mwisho.

  • Baadhi ya wanawake hurejea mapema (miezi 6–12), lakini kuchelewa hadi miaka miwili bado huwa ndani ya kiwango kinachokubalika kitaalamu.


Lini unapaswa kumwona Daktari?

Wasiliana na daktari iwapo:

  • Hedhi haijarejea ndani ya siku 90 baada ya kuacha vidonge, bangiri au kitanzi chenye kichocheo.

  • Hedhi haijarejea ndani ya miezi 22 baada ya Depo-Provera.

  • Unapata maumivu makali, kutokwa damu nyingi, au mabadiliko yasiyo ya kawaida.

  • Una dalili za ujauzito.

  • Unashukiwa kuwa na matatizo ya homoni kama Sindromu ya ovari yeney vifukomaji vingi au thairoid(tezi shingo).


Vipimo

Daktari anaweza kupendekeza vipimo vifuatavyo kutegemea na hali yako:


1. Kipimo cha Ujauzito (β-hCG)

Kipimo cha kwanza na cha muhimu, hata kama una uhakika hujapata ujauzito.


2. Vipimo vya Homoni

Hutumika kutathmini sababu nyingine zinazoweza kuchelewesha hedhi, kama vile:

  • FSH na LH: kutathmini kazi ya ovari na uovuleshaji

  • Prolactin: kiwango kikubwa hupunguza uovuleshaji

  • TSH: matatizo ya tezi yanaweza kuchelewesha hedhi

  • Projesteron: kuangalia kama Uovuleshaji unatokea

  • Androjen (Testosteroni, DHEAS): kusaidia kuchunguza Sindromu ya ovari yeney vifukomaji vingi


3. Ultrasound ya via vya nyonga

Huangalia umbo la ovari (mfano matatizo kama sindromu ya ovari yenye vifuko maji vingi-PCOS), hali ya mji wa mimba, na ukuta wa kizazi (endometrium).


4. Hesabu kamili ya damu- FBP

Kwa wagonjwa wanaopata kutokwa damu kusiko kawaida au uchovu, kusaidia kutathmini upungufu wa damu.


5. Vipimo vya maambukizi kama magonjwa ya zinaa– inapobidi

Hufanyika ikiwa kuna maumivu, uchafu usio wa kawaida, au kutokwa damu baada ya tendo la ndoa.


Matibabu ya hospitali


Jedwali: Matibabu ya hospitali kwa hedhi inayochelewa baada ya kuacha uzazi wa mpango

Kisababishi Kinachowezekana

Matibabu ya Hospitali Yanayopendekezwa

Maelezo ya Ziada / Lengo la Matibabu

Ujauzito

• Huduma za kliniki ya ujauzito (ANC) kulingana na matokeo ya ultrasound na vipimo


• Ushauri wa uzazi salama

Hedhi kuchelewa ni dalili kuu ya ujauzito, hivyo matibabu hufuata mwongozo wa huduma za wajawazito.


Kiwango kikubwa cha Prolaktin

• Dawa aina ya dopamine agonists (Cabergoline, Bromocriptine)

Hupunguza prolaktin ili kuruhusu uovuleshaji kurudi kwa kawaida.

Matatizo ya tezi (uzalishaji mwingi au duni wa homoni za tezi shingo)

• Thyroxine (kwa uzalishaji duni wa homoni za tezi shingo)


• Dawa za kutibu kiwango cha juu za homoni za thairoidi (kama Carbimazole)

Kuimarisha kazi ya tezi hurudisha mzunguko wa hedhi kawaida.


PCOS (Sindromu ya ovari yeneye vifukomaji vingi)

• Metformin


• Kupunguza uzito



• Dawa za kusawazisha homoni (kwa tathmini ya daktari)

Husaidia kurejesha uovuleshaji na kupunguza athari za insulini zilizopinduka.


Upungufu wa damu au lishe duni

• Vidonge vya madini chuma


• Folic asidi



• Ushauri wa lishe

Hutibu uchovu na kurekebisha usawa wa homoni unaohitajika kwa mzunguko wa hedhi.


Msongo sugu au usingizi hafifu

• Ushauri


• Usimamizi wa msongo (Tiba ushauri na kupumzika)

Msongo huathiri homoni za uzazi, hivyo kutibu chanzo hurejesha hedhi.


Mzunguko kuchelewa baada ya Depo-Provera

• Kawaida hakuna dawa—hutibiwa kwa kuangaliwa tu bila dawa


• Dawa za kurekebisha mzunguko (projesteron) hutolewa tu kama kuna sababu maalum

Depo-Provera huchukua muda mrefu, hivyo matibabu ni ushauri na ufuatiliaji.


Endometrium kuwa nyembamba sana baada ya vichochezi

• Progesterone therapy (kwa muda mfupi)

Husaidia mwili kuanza mzunguko wa kawaida na kuzuia kutokwa damu isiyoeleweka.

Magonjwa ya uterasi au ovari (mfano polipsi, sisti-Vivimbe maji)

• Upasuaji mdogo


• Dawa kulingana na ugunduzi

Hhutegemea tatizo lililopo baada ya ultrasound.


Kutokwa damu isiyo ya kawaida kwa muda mrefu

• Dawa za kusimamisha damu (Tranexamic acid)


• NSAIDs (kupunguza maumivu na damu)

Hutumika iwapo kutokwa damu ni nyingi au kuna maumivu makali.



Matibabu ya nyumbani

Haya siyo matibabu ya kubadili homoni moja kwa moja, bali kusaidia mwili kurudi katika mfumo wa kawaida wa homoni baada ya kuacha vichochezi. Hayabadilishi ushauri wa daktari ikiwa tatizo linaendelea.


1. Punguza msongo wa mawazo
  • Tumia mbinu kama:

    • Kupumua kwa kina

    • Kutembea kwa dakika 30

    • Yoga ya viwango vya chini

  • Msongo hupunguza homoni ya GnRH, na kuchelewesha ovulation.


2. Kula mlo kamili

Angalia lishe ifuatayo:

  • Mboga za kijani (spinach, mchicha, kale) – kusaidia usawa wa homoni

  • Vyanzo vya protini (mayai, maharage, samaki)

  • Mafuta yenye afya (avocado, mbegu, korosho)

  • Epuka sukari nyingi na vyakula vya kusindikwa


3. Dhibiti uzito
  • Uzito kupita kiasi au kuwa chini sana unaweza kuchelewesha mzunguko.

  • Lengo liwe kupunguza au kuongeza kiwango cha 0.5–1 kg kwa wiki kwa usalama.


4. Mazoezi ya wastani
  • Mazoezi makali kupita kiasi hupunguza ovulation.

  • Fanya mazoezi ya wastani: kutembea, kuogelea, au aerobics nyepesi.


5. Kunywa maji ya Kutosha

Maji husaidia mfumo wa homoni na hewa (metabolism) kufanya kazi vizuri.


6. Epuka kuacha na kurejea uzazi wa mpango mara kwa mara

Kubadilika-badilika mara kwa mara huchanganya mfumo wa homoni na kuchelewesha mzunguko kurejea.


7. Tumia virutubisho kama unashauriwa na daktari

Vinavyoweza kusaidia katika baadhi ya hali:

  • Vitamin D

  • Omega-3

  • Folate

  • Iron (endapo una upungufu wa damu)Usitumie virutubisho bila ushauri wa daktari.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara

1. Ninatokwa damu kidogo na natumia uzazi wa mpango, shida ni nini?

Hili huitwa matone ya damu. Mara nyingi hutokana na mwili kuzoea kiwango cha homoni, kupitwa na muda wa kutumia dawa, msongo wa mawazo, au kushuka kwa kiwango cha homoni mwishoni mwa mzunguko wa dozi. Lakini kama damu inatoka kila mara au baada ya tendo la ndoa, daktari anaweza kuchunguza uambukizi au mabadiliko ya njia ya uzazi wa mpango.

2. Je, naweza kupata ujauzito kabla hata ya kurudia kuiona hedhi?

Ndiyo. Uovuleshaji unaweza kurudi kabla ya hedhi, hivyo uwezekano wa kupata ujauzito upo hata kama bado hujaona hedhi.

3. Je, kuchelewa kwa hedhi baada ya kuacha uzazi wa mpango kunamaanisha nina tatizo la uzazi?

Hapana. Mara nyingi mwili unahitaji muda tu kujirekebisha. Tatizo huzingatiwa pale tu inachukua muda mrefu zaidi ya kiwango cha kawaida (kwa Depo miezi 22).

4. Je, athari za uzazi wa mpango zinaweza kubaki muda mrefu mwilini?

Kwa vidonge, kipandikizi na kitanzi—hapana. Homoni hutoka mwilini ndani ya siku 1–2. Kwa Depo-Provera athari huchukua muda mrefu zaidi kwa sababu homoni hukaa kwenye tishu za mafuta.

5. Je, kurudi kwa uzito au kupungua kunaathiri hedhi baada ya kuacha vichochezi?

Ndiyo. Uzito kupita kiasi au kupungua kupita kiasi huathiri homoni za uzazi na kuchelewesha mzunguko kurudi kawaida.

6. Je, kunyonyesha kunaathiri hedhi kuanza tena baada ya kuacha uzazi wa mpango?

Ndiyo. Homoni ya prolactin inayoongezeka wakati wa kunyonyesha hupunguza ovulation, hivyo hata ukiacha vichocheo, hedhi inaweza kuchelewa.

7. Je, ni salama kurudi kwenye njia ile ile baada ya kupata matatizo ya mzunguko?

Inategemea kisababishi. Ikiwa shida ni ya muda (mfano mwili kuzoea homoni), unaweza kurudi. Lakini kama ulikuwa na madhara kama shinikizo la juu, migraines au kutokwa damu isiyoisha, daktari atapendekeza mbadala.

8. Ninaweza kufanya nini kuharakisha kurejea kwa hedhi?

  • Punguza msongo

  • Kula lishe yenye afya

  • Fanya mazoezi ya wastani

  • Lala vizuri

  • Epuka uzito kupita kiasiHata hivyo hakuna dawa salama ya “kuamsha hedhi” bila uchunguzi wa daktari.

9. Je, sindromu ya ovari yenye vifukomaji vingi inaweza kujitokeza ghafla baada ya kuacha uzazi wa mpango?

Uzazi wa mpango hausababishi sindromu ya ovari yeney vifukomaji vingi, bali unaweza kuficha dalili zake. Baada ya kuacha, dalili kama kuchelewa hedhi, chunusi au nywele nyingi zinaweza kuonekana kwa sababu mfumo wa homoni unarudi katika hali yake ya awali.

10. Nimeacha uzazi wa mpango lakini hedhi inakuja mara mbili kwa mwezi, je ni kawaida?

Ndiyo, muda mfupi baada ya kuacha vichochezi unaweza kupata mizunguko mifupi au ya mara mbili kwa mwezi. Hii hutokana na homoni kurudi katika viwango vya asili. Ikiwa hali inaendelea zaidi ya miezi 3, fanya uchunguzi.

11. Je, nikitokwa na damu ya matone kila siku au karibu kila siku baada ya kuacha uzazi wa mpango, ninaweza kushika ujauzito?

Ndiyo, inawezekana kushika ujauzito. Damu ya matone haimaanishi kuwa uovuleshaji haujatokea. Wanawake wengine huanza uovuleshaji bila kupata hedhi ya kawaida kwanza. Ikiwa hutumii njia ya uzazi wa mpango na una mahusiano ya ndoa, uwezekano wa ujauzito upo—ndiyo maana kipimo cha ujauzito ni muhimu hata kama damu ndogo inatoka.

12. Kwa nini baadhi ya wanawake hupata hedhi ya maumivu zaidi baada ya kuacha uzazi wa mpango?

Wakati wa matumizi ya vichochezi, utando wa ndani wa mfuko wa uzazi (endometriam) huwa mwembamba. Baada ya kuacha, mwili unapojenga upya ukuta huo, misuli ya mfuko wa uzazi hukaza zaidi, hali inayoweza kusababisha maumivu makali ya hedhi kwa miezi ya mwanzo.

13. Je, ni kawaida kupata mabadiliko ya hisia baada ya kuacha uzazi wa mpango?

Ndiyo. Kubadilika kwa viwango vya estrojen na projesteroni kunaweza kuathiri kemikali za ubongo kama serotonin, hivyo kusababisha:

  • Hasira isiyoelezeka

  • Huzuni ya muda

  • WasiwasiHali hii mara nyingi hupungua ndani ya miezi 2–3.

14. Je, kuchelewa kwa hedhi baada ya kuacha uzazi wa mpango kunaweza kuathiri uwezo wa kushika mimba baadaye?

Hapana. Kuchelewa kwa hedhi hakiharibu uwezo wa uzazi. Mara mzunguko unapokuwa wa kawaida na uovuleshaji unarudi, uwezo wa kushika mimba huwa sawa na wa mwanamke ambaye hakuwahi kutumia uzazi wa mpango.

15. Je, damu nyingi baada ya kuacha uzazi wa mpango ni hatari?

Damu nyingi inaweza kuwa sehemu ya mwili kujirekebisha, lakini ikiwa:

  • Unabadilisha pedi kila saa

  • Unapata kizunguzungu au uchovu mkali

  • Damu inadumu zaidi ya siku 7–10unapaswa kumuona daktari haraka ili kuchunguza upungufu wa damu au matatizo ya mfuko wa uzazi.

16. Je, ninaweza kuanza kutumia uzazi wa mpango mwingine kabla hedhi haijarudi?

Ndiyo, inawezekana. Hata hivyo, daktari anaweza kupendekeza kusubiri mzunguko mmoja wa asili ili kutathmini hali ya homoni zako, hasa kama ulipata matatizo makubwa kwa njia uliyotumia awali.

17. Je, kuna vyakula vinavyoweza kusaidia kurudisha hedhi haraka?

Hakuna chakula kinacholazimisha hedhi kuja, lakini vyakula vyenye:

  • Chuma

  • Omega-3

  • Vitamin B na D husaidia mwili kujenga mazingira bora ya homoni na uovuleshaji.

18. Je, kukosa hedhi baada ya kuacha uzazi wa mpango kunaweza kuwa dalili ya sindromu yenye vifukomaji vingi hata kama sikuwa na dalili kabla?

Ndiyo. Uzazi wa mpango unaweza kuficha dalili za sindromu ya ovari yenye vifukomaji vingi. Baada ya kuacha, dalili kama kuchelewa kwa hedhi, chunusi au nywele nyingi zinaweza kujitokeza, si kwa sababu uzazi wa mpango umeleta sindormu hii, bali kwa sababu homoni zinarudi katika hali yake halisi.

19. Je, ni lini hasa nianze kuhesabu siku za rutuba baada ya kuacha uzazi wa mpango?

Unaweza kuanza:

  • Kufuatilia ute wa mlango wa kizazi

  • Kupima joto la mwili asubuhi

  • Kufuatilia dalili za uovuleshaji. Hata kabla ya hedhi ya kwanza, dalili hizi zinaweza kuonyesha kuwa uovuleshaji umeanza.

20. Je, ni kosa kuacha na kurejea uzazi wa mpango mara kwa mara?

Ndiyo, si salama kwa mfumo wa homoni. Kubadilisha mara kwa mara huongeza:

  • Damu isiyoeleweka

  • Mizunguko isiyotabirika

  • Athari za kihisiaNi bora kuchagua njia inayokufaa kwa muda mrefu kwa ushauri wa daktari.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

21 Septemba 2021, 14:33:21

Rejea za mada hii:

Girum, et al. “Return of fertility after discontinuation of contraception: a systematic review and meta-analysis.” Contraception and reproductive medicine vol. 3 9. 23 Jul. 2018, doi:10.1186/s40834-018-0064-y.

Pardhaisong T, et al.. Return of fertility after discontinuation of depot medroxyprogesterone acetate and intra-uterine devices in northern Thailand. Lancet. 1980;l:509–512. doi: 10.1016/S0140-6736(80)92765-8.

Kaplan B, et al. Use of various contraceptive methods and time of conception in a communitybased population. Eur J Obstet Gynecol Reprod Biol. 2005;123:72–76. doi: 10.1016/j.ejogrb.2005.06.033.

Shearman RP. Amenorrhea after treatment with oral contraceptives. Lancet. 1966;2:1110–1111. doi: 10.1016/S0140-6736(66)92197-0.

Robert E. Roe, M.D, et al. DOI:https://doi.org/10.1016/0002-9378(72)90176-7https://www.ajog.org/article/0002-9378(72)90176-7/fulltext. Imechukuliwa 20/09/2021

Halbert DR, et al. Amenorrhea following oral contraceptives. Obstet Gynecol. 1969;34:161–167.

Barnhart, K. T. Return to fertility following discontinuation of oral contraceptives.
https://www.sciencedirect.com/science/article/abs/pii/S0015028209000491.

bottom of page