Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Helen L, M.D
Jumatano, 20 Januari 2021

Jifunze tabia tano za kiafya
Pata kifungua kinywa cha kiafya, kula matunda na mboga za majani angalau mara tatu kwa siku, kula chakula kutoka kwenye nafaka zisizokobolewa, tumia chakula kilichopikwa kwa mafuta ya kiafya na fanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku. Tabia hizi zitaufanya mwili wako uwe imara na afya njema.
Pata kifungua kinywa chenye afya
Pata kifungua kinywa cha kiafya kila siku asubuhi, ingawa hutakiwi kula sana, chakula chako kiwe kitu ambacho kinaweza kufanya uanze siku yako vema.
Ni nini chakula asubuhi
Tafiti zinaonyesha kuwa watu wanaopata kifungua kinywa chenye afya asubuhi, huweza kukabiliana vema na tatizo la uzito mkubwa, hivyo kuwa na afya njema kuliko wale ambao hawapati kifungua kinywa asubuhi.
Ni nini unatakiwa kula asubuhi?
Kula mbegu za nafaka zisizokobolewa mfano mtama wa kuchemsha, mkate usiokobolewa n.k
Kula matunda bila kuongezea sukari
Kunywa maziwa mgando na au karanga, mayai. Kutumia vyakula hivi hukufanya ujihisi umeshiba na hivyo kukufanya ule kidogo wakati wa mchana
Kunywa juisi isiyochujwa, kutiwa maji wala sukari kutoka kwenye matunda aina tatu hadi tano. Unaweza ongeza maziwa mgando kwenye juisi hiyo
Tembea na chakula ambacho unaweza kukibeba na kwenda nacho kazini. Vyakula vya kutembea navyo ni kama matunda mbalimbali, juisi isiyotiwa maji wala kuchujwa n.k
Mafuta ya kiafya
Mafuta ya kiafya ni yale ambayo yana kiwango kidogo cha kolestrol(lehamu). Mwili hautakiwi kukosa kabisa kolestrol kutoka kwenye mafuta kwa sababu kolestrol ni muhimu mwilini na huhusika kutengeneza homoni na kazi zingine mwilini. Mafuta mazuri ya kutumia ni yale yaliyotokana na mimea baadhi yake ni;
Mafuta ya alizeti
Mafuta ya ufuta
Mafuta ya karanga
Mafuta ya ubuyu
Mafuta ya mzeituni
Matuta kutoka kwenye mboga za majani
Hata hivyo, licha ya kuwamafuta haya ni mazuri kiafya, hakikisha unatumia kwa kiwango kidogo kinachoshauriwa kiafya.
Tumia vyakula kutoka kwenye nafaka zisizokobolewa
Vyakula kutoka kwenye nafaka zisizokobolewa huwa pamoja na;
Mahidi
Mtama
Uwele
Ngano
Nafaka hizi zinaweza kutengeneza vyakula mbalimbali ambavyo vinaliwa na binadamu. Umuhimu wa kutumia nafaka zisizokobolewa ni mkubwa kwa sababu nafaka zisizokobolewa huwa na virutubisho, madini na nyuzinyuzi kwa wingi vinavyochangia kukupa afya njema na kukukinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwa pamoja na saratani
Tumia matunda na mboga za majani
Umuhimu wa matunda na mboga za majani umezidi kufahamika duniani kote na hata nchi za afrika ambazo zina matunda mbalimbali kwa wingi. Mtunda huwa na virutubisho, madini pamoja na nyuzinyuzi nyingi ambazo zina umuhimu mkubwa mwilini. Matumizi ya matunda na mboga za majani huweza kukukinga dhidi ya saratani za utumbo, magonjwa ya mifupa, ngozi, macho na mengine mengi.
Inashauriwa kutumia matunda pamoja na mbegu zake ili kupata kila kirutubisho kilichomo kwneye tunda. Endapo unaandaa juisi ya matunda, tuma angalau matunda ya aina tatu na kuendelea na usipende kuongeza sukari, kuchuja au kutia maji ili kuepuka kupoteza virutubisho na nyuzinuzi zilizomo kwenye matunda hayo.
Fanya mazoezi
Kwa sababu unakula, ukifanya mazoezi unafanya mwili utumie chakula ulichokula na hivyo kukuzuia mwili kuongezeka uzito usiotakiwa.
Mazoezi gani ya kufanya?
Unaweza kufanya zoezi lolote lile ambalo linakutoa jasho mfano;
Kupalilia bustani au kulima shamba
Kutembea haraka haraka kwa muda wa dakika 10 hadi 15
Kufanya mazoezi ya viungo vya mwili kwa muda wa dakika 30
Kuendesha baiskeli
Kupanda mlima
Kuogelea kwa muda angalau wa nusu saa n.k
Mazoezi mazuri ni yapi?
Mazoezi mazuri ni yale unayoweza kuyafanya kirahisi na utayafanya bila kukata tamaa, chagua mazoezi ambayo ukiyafanya yanakufurahisha na kukupa moyo kuendelea kuyafanya.
Soma zaidi kuhusu mazoezi kwa kubofya hapa
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
19 Julai 2023, 20:41:55
Rejea za mada hii: