top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

Alhamisi, 12 Agosti 2021

Kupata ujauzito baada ya kutoa mimba

Kupata ujauzito baada ya kutoa mimba

Unaweza kupata ujauzito ndani ya siku 14 baada ya kutoa mimba, hata hivyo kama una mzunguko mfupi wa hedhi unaweza kupata mapema zaidi. Tumia kondomu kuzuia mimba isiyotarajiwa.


Ujauzito baada ya kutoa mimba


Kutoa mimba mara nyingi hakudhuru uwezo wako wa kupata ujauzito mwingine mapema. Unaweza kupata ujauzito ndani ya wiki chache tu baada ya kutoa mimba, na hata hivyo inategemea pia mzunguko wako wa hedhi ni wa siku ngapi na ulibeba ujauzito kwa muda gani kabla ya kuutoa.


Muda gani wa kufanya kipimo cha ujauzito kwa njia ya mkojo baada ya kutoa mimba?


Muda wa kufanya kipimo cha mkojo baada ya kutoa mimba ni baada ya wiki 2 toka siku ya kutoa mimba. Endapo utafanya kipimo mapema zaidi majibu hayo yataonyesha una ujauzito na hili linaweza kuwa si kweli kama hujashiriki ngono na ujauzito ulishatoka. Kiwango cha homon ya ujauzito (HCG) kwenye damu hupungua kila siku kwenye damu na mkojo baada ya kutoa mimba na huwa hakisomeki kwenye mkojo baada ya wiki 2 na kwenye damu baada ya wiki 6


Baada ya muda gani unaweza kupata ujauzito baada ya kuutoa?


Mara baada ya kutoa mimba mzunguko mpya wa hedhi huanza mara moja na hivyo kufanya yai jingine litolewe siku ya 14 kama mzunguko wako ni wa siku 28 au mapema zadi hadi siku nane kama mzunguko wako ni mfupi zaidi. Kama utashiriki ngono isiyo salama siku chache kabla au siku moja baada ya ovulesheni, unaweza kupata ujauzito mwingine.


Mambo yanayodhuru ovulesheni


Kutolewa kwa yai (ovulesheni) baada ya kutoa ujauzito hutegemea umri wa ujauzito wakati wa kutoa mimba. Ujauzito wa mfupi unapotolewa, kiwango cha homon ya ujauzito kwenye damu hurejea kawaida haraka zaidi ya yule ambaye ameetoa kwenye ujauzito wenye wiki nyingi zaidi. Hii inapelekea hatari kubwa ya kupata ujauzito mwingine kama mimba ilitolewa ikiwa na wiki chache zaidi.


Dalili za kupata ujauzito baada ya kutoa mimba


Dalili za kupata ujauzito mwingine baada ya kutoa mimba ni;


  • Maumivu ya titi

  • Hisia kali kwenye harufu au ladha ya chakula

  • Kichefuchefu

  • Kutapika

  • Uchovu

  • Kutoona hedhi


Namna gani ya kuzuia kupata ujauzito mwingine baada ya kutoa mimba


Ili kujikinga kupata ujauzito mwingine, uashauriwa kutumia njia mojawapo ya uzazi wa mpango mfano kondomu au vidonge ili kuzuia uwezekano wa kupata mimba nyingine isiyotarajiwa.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

6 Oktoba 2021 16:05:47

Rejea za mada hii:

1. Butler Tobah Y. (2017). Could an abortion increase the risk of problems in a subsequent pregnancy?
mayoclinic.org/healthy-lifestyle/getting-pregnant/expert-answers/abortion/faq-20058551. Imechukuliwa 12.08.2021

2. Pregnancy: Ovulation, conception and getting pregnant. my.clevelandclinic.org/health/articles/11585-pregnancy-ovulation-conception--getting-pregnant. Imechukuliwa 12.08.2021

3. Steier JA, et al. Human chorionic gonadotropin in maternal plasma after induced abortion, spontaneous abortion, and removed ectopic pregnancy. ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/6462569. Imechukuliwa 12.08.2021

bottom of page