Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Charles W, M.D
Jumatano, 17 Februari 2021

Kushusha homa kwa vichanga na watu wazima
Mtoto chini ya umri wa miezi mitatu, endapo ana joto la mwili nyuzi za selisias 38 au zaidi, wasiliana na daktari wako mara moja kwa ushauri na tiba. Kwa watoto zaidi ya umri wa miezi mitatu na watu wazima, pumzisha mwili, kunywa maji ya kutosha. Tumia panadol au ibuprofen kutuliza homa endapo kuna ulazima, na endapo homa imedumu zaidi ya siku tatu onana na daktari wako mara moja.
Mambo ya kufanya unapopata homa
Homa ni dalili inayotokea kwa watu wengi ambayo hutokea kama ongezeko la joto la mwili. Baadhi ya watu hutumia neno homa kumaanisha hali ya mwili kuumwa hata endapo joto la mwili halijaongezeka. Makala hii imeelezea namna ya kukabiliana na homa ukiwa nyumbani kwa watoto na watu wazima.
Kwanini homa hutokea?
Homa ni ishara ya uhai wa kinga ya mwili kupambana na maradhi au shida fulani iliyo kwenye mwili. Mwili unapopata maambukizi au majeraha hutoa chembe za ulinzi na kemikali ili kukabiliana nayo, matokeo kuingia kwa kemikali na chembe za ulinzi kwenye mzunguko wa damu hupelekea kutokea kuongezeka kwa joto la mwili. Kutokana na maelezo haya, kutokea kwa homa ni jambo zuri kwani huashiria uhai wa mfumo wa kinga ya mwili wako.
Tumia maelezo yaliyoandikwa hapa chini kama mwongozo wa kuthibiti homa kwa watu ambao hawana magonjwa sugu.
Unatakiwa kuwa na kipimajoto ili kuweza kutambua joto la mwili wako/mwanao kwa kupima kwenye kinywa au njia ya haja kubwa. Endapo utatumia joto la kwapani ni vema ukasoma makala ingine ya joto la mwili na utofauti wake katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Watoto chini ya umri wa miaka miwili
Umri wa Miezi 0-3,nyuzi joto zinazofika 38 C au zaidi
Nini cha kufanya?
• Mpigie daktari wako mara moja kwa matibabu hata kama mwanao hana dalili zingine za ugonjwa
Umri wa Miezi 3-6,nyuzi joto 38.9 C au zaidi
Nini cha kufanya
Mhimize mtoto apumzike na kunywa maji ya kutosha.Matumizi ya dawa hayahitajiki wakati huu. Endapo mtoto anaonyesha dalili za kuwa thaifu, kutepetwa au kulialia kusiko kawaida, wasiliana na daktari wako.
Umri wa Miezi 3-6,nyuzi jotokuanzia 38.9 C au zaidi
Nini cha kufanya?
Mpigie daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba.
Umri wa Miezi 6 hadi miaka 2,nyuzi joto zaidi ya 38.9 C
Nini cha kufanya?
Mpatie mwanao parasetamo. Endapo mwanao ana umri wa miezi 6 na zaidi, unaweza kumpatia dawa ya ibuprofen pia lakini unabidi kuchagua mojawapo sio kumpatia zote. Zingatia dozi inayoshauriwa kwa mtoto, haishauriwi kuwapa watoto aspirin katika umri huu. Endapo homa haipungui licha ya kutumia dawa au kudumu zaidi ya masaa 24, mpigie daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba
Umri wa Miaka 2 mpaka 17,nyuzi joto zinazofikia 38.9C
Nini cha kufanya?
Mhimize mtoto kupumzika na kumpa vinywaji vya maji au maji ya kutosha. Mtoto hahitajiki kutumia dawa za homa. Endapo mwanao ataonekana kuwa dhaifu, kulia lia au kuishiwa nguvu, wasiliana na daktari wako mara moja.
Umri wa miaka 2 mpaka 17,nyuzi joto zaidi ya 38.9 C
Nini cha kufanya?
Endapo mtoto hajihisi vema, mpatie Panadol au ibuprofen lakini si zote kwa pamoja. Soma maelekezo vema ya kiasi cha kumpa kulingana na uzito wake. Usimpe mtoto dawa zingine zenye kiini cha dawa ya ibuprofen ay Panadol kuepuka kupata dozi kubwa zaidi. Hakikishaunawasiliana na daktari endapo homa haishuki kwa dawa zaidi ya masaa 24
Umri wa miaka 18 na zaidi, nyuzi joto zinazofikia 38.9 C
Nini cha kufanya?
Huhitaji kutumia dawa, cha kufanya pumzika na kunywa maji ya kutosha. Endapo homa inaambatana na dalili ya maumivu ya kichwa, kukakamaa kwa shingo, kuishiwa pumzi na dalili zingine zisizo za kawaida wasiliana na daktari wako mara moja kwa ushauri na tiba.
Umri wa miaka 18 au zaidi, nyuzi joto zaidi ya 38.9 C
Nini cha kufanya?
Endapo unajihisi vibaya, tumia parasetamo au ibuprofen. Soma maelekezo kwa umakini ili kufahamu kiasi sahihi cha kutumia. Usitumie dawa zingine zenye kiini cha acetaminophen pamoja na ibuprofen ili kuzuia kupata kiwango kikubwa kuliko kawaida cha dawa hizi. Hakikisha unawasiliana na daktari wako kwa uchunguzi na tiba endapo joto la mwili wako halipungui licha ya kutumia dawa zaidi ya siku tatu.
Kumbuka
Mwongozo huu ni ule unaotumia joto la mwili lililopimwa kwenye kinywa au njia ya haja kubwa
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
19 Julai 2023, 20:41:21
Rejea za mada hii:
1. Bennett JE, et al. Temperature regulation and the pathogenesis of fever. In: Mandell, Douglas, and Bennett's Principles and Practice of Infectious Diseases. 9th ed. Elsevier; 2020. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 17.02.2021
2. Kliegman RM, et al. Fever. In: Nelson Textbook of Pediatrics. 21st ed. Elsevier; 2020. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 17.02.2021
3. Schmitt BD. Fever. In: Pediatric Telephone Protocols: Office Version. 16th ed. American Academy of Pediatrics; 2018.
4. Ward MA. Fever in infants and children: Pathophysiology and management. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 17.02.2021
5. Fever. Merck Manual Professional Version. https://www.merckmanuals.com/home/infections/biology-of-infectious-disease/fever-in-adults. Imechukuliwa 17.02.2021
6. Dinarello CA, et al. Pathophysiology and treatment of fever in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 17.02.2021