Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Helen L, M.D
Jumamosi, 16 Januari 2021
Kuwashwa njia ya haja kubwa
Mabaki ya uchafu kwenye njia ya haja kubwa, huchangia kwa kiasi kikubwa kuwashwa tundu la haja kubwa na maambukizi kwenye mfumo wa mkojo. Jikinge kwa kujifunza namna sahihi ya kujisafisha, anza sasa.
Namna ya kutunza njia ya haja kubwa
Kusafisha njia ya haja kubwa kisahihi kwa kutumia maji safi kila siku husaidia sana kuepusha matatizo mbalimbali ya kiafya unayoweza kuyapata, mfano maambukizi ya UTI kwa wanawake, kuwashwa sehemu za siri na maambukizi kwenye maeneo ya njia ya haja kubwa. Hata hivyo nguo zako za ndani pia hazitachafuka endapo utajisafisha vema.
Namna ya kusafisha njia ya haja kubwa
Unapokuwa unasafisha njia ya haja kubwa andaa maji safi kisha fuata hatua zifuatazo;
Kaa mkao wa kuchuchumaa
Shika chombo cha maji katika mkono wako wa kulia
Pitisha mkono wa kushoto kwa nyuma ili kuifikia njia ya haja kubwa kisha uache hapo
Fanya kama unasukuma haja kubwa (usitumie nguvu) ili njia ya haja kubwa ifunguke na kuta ya ndani ya zichungulie nje kidogo, kisha shikilia hapo hapo na endelee na hatua inayofuata. (kumbuka endapo kinyesi kitatoka inamaana bado kuna kinyesi kwenye njia hiyo, hivyo unahitaji kujisaidia ili kiishe ndipo ujisafishe)
Mimina maji safi kwenye mkono wa kushoto ulio karibu na njia ya haja kubwa, kisha safisha. Wakati unasafisha hakikisha mkono wako wa kushoto unaelekea nyuma badala ya mbele kuzuia kusambaza majimaji na kinyesi kwenye njia ya mkojo au ukeni (hii itazuia kupata maambukizi ya UTI). Safisha kama unanawisha mikono au vidole, pitisha vidole katikati na pembeni ya tundu la haja kubwa kwa kutumia maji mengi
Endapo uchafu umeisha, jikaushe kwa tishu kwa kukanda badala ya kufuta
Nawa na sabuni mikono yako kisha vaa nguo zako.
Vitu ambavyo hutakiwi fanya
Kutumia sabuni zinazokausha ngozi, sabuni hizi huondoa mafuta asilia na kufanya ngozi ikauke, hali hii huweza amsha kuwashwa
Kutumia tishu kavu au karatasi au majani wakati wa kujisafisha. Badala yake tumia maji safi ili kuzuia kupata majeraha yanayopelekea kuwashwa na maambukizi kwenye njia haja kubwa.
Kutumia vimiminika vya kutakasa au kusafishia.
Tabia njema za kufuata kwa afya ya njia ya haja kubwa;
Usizuie hamu ya kwenda haja kubwa inapotokea
Usikenye wakati unajisaidia(usitumie nguvu kutoa haja kubwa)
Usikae chooni kwa dakika nyingi
Endapo unaendelea kuwashwa ni nini ufanye?
Endapo una unawashwa kwenye njia ya haja kubwa fanya mambo yafuatayo kuipunguza;
Kalia maji ya uvuguvugu kwa dakika 10 hadi 20 mara tatu au zaidi kwa siku
Unaweza changanya detol kwenye maji ya uvuguvugu kabla ya kukalia endapo una mipasuko au maambukizi kwenye njia ya haja kubwa
Kama njia ya haja kubwa inawasha sana, kanda kwa kutumia barafu iliyotiwa kwenye mfuko wa plastiki. Kanda kwa dakika 10 kisha pumzika kwa dakika 20, na baada ya hapo unaweza kurudia zoezi hilo tena mpaka maumivu yatakapopungua. Usikande kwa zaidi ya dakika 30 mfululizo kwa kuwa utakata mawasiliano ya mishipa ya damu na kusababisha tishu za njia ya haja kubwa kufa kwa baridi.
Tumia dawa za kuondoa kuwashwa endapo itahitajika, wasiliana na daktari wako kwa ushauri wa dawa gani zinazokufaa wewe.
Kumbuka
Endapo tatizo la kuwashwa linaendelea licha ya kufuata Eushauri, inawezekana kuwa limesababishwa na maambukizi kwenye njia ya haja kubwa, bawasili n.k. Wasiliana na daktari wako mara moja kama tatizo lako halijaisha ndani ya masaa 72.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 20:41:55
Rejea za mada hii: