top of page

Mwandishi:

Dkt. Sospeter B, M.D

Mhariri:

Dkt. Salome A, M.D

Jumapili, 23 Julai 2023

Matibabu kamili ya gono

Matibabu kamili ya gono

Matibabu kamili ya gono kwa nchi nyingi duaniani ikiwa pamoja na Tanzania huhusisha matibabu ya magonjwa yote yanayosababisha kutokwa usaha sehemu za siri. Kama hautapona kwenye matibabu hayo yenye awamu tofauti, utatakiwa kufanya vipimo zaidi kutambua vimelea wasababishi na dawa yake.


Kutoa usaha sehemu za siri

Watu wengi wamekuwa wakidhania kuwa kutoa usaha sehemu za siri husababishwa na gono tu, hivyo wamekuwa wakititafutia dawa za kutibu gono mtandaoni na kuanza kuzitumia pasipo kupata ushauri wa daktari. Wengi waliofanya hivi na kutopona wamekuwa wakitafuta huduma za matibabu kwa wataalamu ili kupata suluhisho.


Usaha sehemu za siri husababishwa na nini?

Kutokwa usaha sehemu za siri huweza kusababishwa na magonjwa mbalimbali ya zinaa yanayosabishwa na vimelea kama vile

  • Neisseria gonorrhoeae

  • Chlamydia trachomatis

  • Mycoplasma genitalium

  • Trichomonas vaginalis


Vimelea wote waliotajwa hapo juu husikia aina fulani ya dawa, kama unavyoona kimelea N. gonorrhoeae husababisha usaa na ugonjwa wake huitwa gono, hata hivyo C. trachomatis naye husababisha usaha na ugonjwa wake huitwa klamidia n.k


Wanaume wengi wenye maambukizi haya huwa na dalili ya kuwashwa kwenye kilele cha mrija utoao mkojo nje na dalili ya maumivu wakati wa kukojoa au la pamoja na au pasipo kutoa ute unaoweza kuwa kidogo mweupe au njano, au mwingi na mweupe au mwingi wenye rangi ya usaha.


Je unaweza kutofautisha usaha wa Gono na vimelea wengine?

Kutofautisha usaha unaosababishwa na gonorrhoea, chlamydia au vimelea wengine kwa dalili ni jambo lisilowezekana. Hii ndio maana matibabu ya kutokwa usaha sehemu za siri huchukuliwa kama magonjwa ya zinaa na huhusisha mchanganiko wa dawa zenye uwezo wa kuua vimelea hao wote.


Je nikitibiwa mwenyewe tu inatosha kutibu gono?

Kujitibu mwenyewe dalili ya kutokwa usaha sehemu za siri haitoshi, ni sawa na kuwa na ofisi chafu nawewe ukawa umevaa nguo safi na hutaki ipate vumbi, unapoingia katika ofisi hiyo kwa namna yoyote utachafuka kwa vumbi lililopo ofisini. Vivyo hivyo, unapopata gono au unapokuwa na dalili ya kutokwa usaha sehemu za siri inawezekana wewe kuwa umeambukizwa au umeambukiza wengine. Watu wote waliokuambukiza au uliowaambukiza wanaweza wasionyeshe dalili yoyote. Ili kuvunja mnyororo wa maambukizi unatakiwa usishiriki nao ngono au nawao wapate matibabu kamili. Endapo tendo hili halitafanyika, utapona lakini tatizo litajirudia ndani ya wiki chache. Kama hutaonyesha dalili haimaanishi kwamba hujapata maambukizi, maambukizi yanaweza kuendelea kimya kimya na baadae utaonyesha athari za ugonjwa.


Acha kujitibu mwenyewe

Wataalamu wa afya wana ufahamu mzui kuhusu ugonjwa huu, wanaweza kukutibu na kukuepusha na madhara yanayoweza kujitokeza. Epuka ushauri kutoka kwa watu wasio na utaalamu kwa kuwa wanaweza kukuchelewesha kupata suluhisho na kukujengea usugu kwenye dawa. Kutoka usaha kukidumu kwa muda mrefu husinyaza na kutia makovu katika njia ya mkojo na kiwanda cha manii kiasi cha kusababisha ugumba na maumivu endelevu katika njia ya mkojo pamoja na kukufanya uingie gharama zaidi katika kutibu madhara yaliyojitokeza.


Je kama sijiwezi kifedha na nahitaji tiba ya usaha sehemu za siri nawezaje kupata matibabu?

Unaweza tumia huduma ya ushauri na tiba mtandaoni kwa gharama nafuu kutoka kwa watoa huduma na huduma zilizosajiliwa kama hutoweza fika hospitali hutokana sababu mbalimbali ikiwa pamoja na kukosa fedha. Watoa huduma hao watakupa huduma kamili na salama kwa kuzingatia miongozo ya matibabu, sera ya usiri wa taarifa za wagonjwa na kiapo walichokula kutoa huduma ya matibabu.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

1 Agosti 2024 18:39:54

Rejea za mada hii:

1. NCBI. Guidelines for the management of symptomatic sexually transmitted infections [Internet].https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK572662/#. Imechukuliwa 23.07.2023

2. CDC. Diseases Characterized by Urethritis and Cervicitis. https://www.cdc.gov/std/treatment-guidelines/urethritis-and-cervicitis.htm#. Imechukuliwa 23.07.2023.

3. ULY CLINIC. gono. https://www.ulyclinic.com/magonjwa-na-saratani/Gono. Imechukuliwa 23.07.2023.

4. Tanzania standard treatment guideline @2021

bottom of page