Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Jumanne, 20 Julai 2021
Matumizi ya dawa yasiyo sahihi
Ili tiba ifanikiwe, itawezekana pale tu mtoa dawa atakapotoa maelezo ya matumizi sahihi ya dawa na mtumiaji akafuata maelekezo hayo. Epuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa kuzuia madhara.
Matumizi ya dawa yasiyo sahihi
Ili tiba ifanikiwe, itawezekana pale tu mtoa dawa atakapotoa maelezo ya matumizi sahihi ya dawa na mtumiaji akafuata maelekezo hayo. Epuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa kuzuia madhara.
Aina za matumizi yasiyo sahihi ya dawa
Matumizi yasiyo sahihi ya dawa hujumuisha;
Kutumia dozi isiyo sahihi
Kushindwa kumaliza kozi
Kutumia dawa isiyo sahihi katika kutibu ugonjwa
Kutumia dawa kwa njia isiyo sahihi
Kununua na kutumia dawa kiholela bila kufanyiwa uchunguzi
Kutumia dawa yenye viwango vya chini vya ubora
Kutumia dawa ambayo ni ghali bila sababu ya msingi
Kutumia dawa zinazoingiliana kiutendaji kwa pamoja, mfano tetracycline na magnesium trisilicate
Kutumia viuavija sumu kutibu magonjwa yanayotokana na virusi
Kutumia dawa na pombe
Kutumia dawa zisizoruhusiwa wakati wa ujauzito mfano albendazole, doxycycline, phenytoin n.k
Sababu zinazochangia matumizi yasiyo sahihi ya dawa
Kuna sababu mbalimbali zinazochangia matumizi yasiyo sahihi ya dawa kama ifuatavyo;
Kutokugundua ugonjwa
Uandikaji wa dawa usio sahihi
Utoaji wa dawa usio sahihi
Mgonjwa kushindwa kumudu gharama ya dawa
Mgonjwa kutokutumia dawa kwa usahihi
Mgonjwa kujiamulia matumizi ya dawa bila kupata ushauri wa Mtaalamu wa afya
Maelezo zaidi;
Kutokugundua ugonjwa
Mtoa dawa au mtaalamu mwingine wa afya anaweza kushindwa kugundua ugonjwa, hii inaweza kuchangiwa na ukosefu wa vifaa muhimu vya kufanyia uchunguzi, mgonjwa kushindwa kujieleza au mtaalamu kukosa elimu na uzoefu wa kutosha.
Uandikaji wa dawa usio sahihi
Mapungufu yanayoweza kufanyika wakati wa uandikaji cheti ni pamoja na;
Kumshauri na kumuandikia mgonjwa dawa katika dozi kubwa na kutumia dawa kwa muda mrefu wakati haihitajiki
Kumuandikia au kumshauri mgonjwa kutumia dawa wakati haihitajiki.
Mfano kumshauri mgonjwa atumie viuwavijasumu kutibu mafua au kuharisha wakati haihitajiki
Kumuandikia au kumshauri mgonjwa atumie dawa ambayo siyo sahihi
kwa matatizo ya kiafya aliyonayo
Kumuandikia mgonjwa dawa nyingi bila sababu
Kushindwa kumuandikia au kumshauri mgonjwa kutumia dawa inayohitajika. Mfano kushindwa kumuandikia mtoto mdogo anayeharisha dawa ya maji ya chumvichumvi (ORS) na Zinki (Pedzink)
Kumuandikia mgonjwa dozi iliyo chini ya kiwango kinachohitajika au kumuuzia kiasi kidogo mgonjwa
Kumuandikia mgojwa dawa ghali ambayo atashindwa kumudu badala ya dawa mbadala yenye bei rahisi.
Kumuandikia mgonjwa sindano wakati angeweza kutumia dawa ya vidonge
Utoaji wa dawa usio sahihi
Ili Mtoa Dawa aweze kutekeleza kazi zake anatakiwa kuwa na uelewa juu ya magonjwa na dawa, kutumia miongozo ya kitaifa ya tiba, vitabu vya rejea na stadi za mawasiliano.
Mtoa Dawa anaweza kuchangia matumizi yasiyo sahihi ya dawa kama atafanya yafuatayo;
Kushindwa kuelewa cheti cha mganga na kuacha kuwasiliana naye ili
kupata ufafanuzi
Kutoa dawa isiyo sahihi
Kushindwa kukokotoa au kutoa kiasi sahihi cha dawa
Kuandika lebo kwa makosa au isiyosomeka vizuri
Kutoa maelekezo yasiyojitosheleza kuhusu matumizi ya dawa
Kushindwa kuhakikisha kuwa mgonjwa ameelewa maelekezo ya matumizi ya dawa
Kutoa dawa au maelezo ya dawa bila kuzingatia imani, mazingira au mila za mgonjwa
Kushindwa kuhimili shinikizo la mgonjwa la kutaka kuuziwa dawa ambayo kimsingi haiitajiki
Kutoa dawa kwa tamaa ya fedha bila kuzingatia ubora wa huduma
Mgonjwa kushindwa kumudu gharama ya Dawa
Endapo mgonjwa atashindwa kumudu gharama za kununua dawa aliyoandikiwa na Daktari, itapelekea mgonjwa kushindwa kumaliza kozi iliyokusudiwa na hivyo kuwa katika hatari ya kutokupona ugonjwa na pia hatari ya kujenga usugu wa dawa ambayo hajamaliza kozi kama alivyoandikiwa.
Sababu zifuatazo zinaweza kupelekea mgonjwa kushindwa kumudu gharama za dawa
Bei ya dawa kuwa juu
Uwezo wa kiuchumi wa mgonjwa kumudu gharama za manunuzi ya dawa
Mgonjwa kutokutumia dawa kwa usahihi
Mgonjwa kusahau maelekezo ya mtoa dawa kwa Mfano; Ni muhimu kwa mtoa dawa kumuelezea mgonjwa kwa kina namna sahihi ya kuingiza dawa mwilini, Kwa mfano dawa za kuingia mwilini kwa njia ya puru au Ukeni mara nyingine zinaweza kufanana kabisa na zile zinazopitia njia ya mdomoni, Hivyo ni muhimu kumuelewesha mgonjwa namna sahihi ya kuingiza mwilini dawa husika.
Mgonjwa kujiamulia matumizi ya dawa bila kupata ushauri wa Mtaalamu wa afya
Kumekuwa na tabia kwenye jamii kwa baadhi ya watu kujiamulia kutumia dawa bila kumuona mtaalamu wa afya, hii inaweza kusababishwa na sababu zifuatazo:-
Kujitibu kupitia kwenye mitandao
Kufuata ushauri wa mtu ambaye sio mtaalamu wa dawa
Matumizi ya dawa zilizobaki ambazo zilikuwa za mtu mwingine au kuhifadhi dawa kwa matumizi ya baadae
Mgonjwa kushindwa kumudu gharama za kumuona mtaalamu wa Afya
Athari zitokanazo na matumizi yasiyo sahihi ya dawa
Mgonjwa asipotumia dawa kwa usahihi yafuatayo yanaweza kutokea:-
Mgonjwa hatapata tiba sahihi na hivyo kuendelea kuugua au kufa
Uwezekano wa kupata madhara ya dawa
Kuongezeka kwa usugu wa vimelea. Hii hutokea zaidi kwa dawa aina ya viuavija sumu na dawa za malaria
Kupoteza fedha nyingi katika matibabu
Mgonjwa kutegemea zaidi dawa hata kama haiitajiki
Mambo ya kufanya ili kufanikisha matumizi sahihi ya dawa
Ili kuhakikisha dawa zinatumika kwa usahihi, Mtoa Dawa na mgonjwa wanapaswa;
Kugundua kwa usahihi dalili za ugonjwa na kufanya uchunguzi kabla ya kutumia dawa
Kutoa rufaa kwa mgonjwa kwenda ngazi inayohusika kulingana na mahitaji ya kiafya
Kumpa na kutumia dawa sahihi kulingana na cheti cha daktari au maelezo ya mgonjwa (dawa inatakiwa kuandikwa na daktari kabla ya kutumia)
Kutoa na kupokea maelekezo juu ya matumizi na uhifadhi sahihi wa dawa.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
6 Oktoba 2021 19:06:58
Rejea za mada hii:
1. World Health Organisation. Rational use of Medicines. Available at http://www.who.int/medicines/areas/rational_use/en/index.html; 2010. Imechukuliwa 20.07.2021
2. Mnyika K.S, et al. Irrational drug use in Tanzania. Health Policy Plan. 1991;6(2):180–184.
3. Patel V, et al. Irrational drug use in India: a prescription survey from Goa. Jour Postgrad Med. 2005;51:9–12.
4. Kastury N, et al. An audit of prescription for rational use of fixed dose combinations. Indian J Pharmacol. 1999;31:367–369.
5. Calva J. Antibiotic use in a periurban community in Mexico: a household and drugstore survey. Soc Sci Med. 1996;42(8):1121–1128.
6. Arustiyono. Promoting Rational Use of Drugs at the Community Health Centers in Indonesia, [dissertation]. Department of international health, School of Public Health, Boston University; 1999.
7. Mathur AG. Outpatient prescription patterns in a tertiary level service hospital. Proceedings of the XVI Asia Pacific Military Medicine Conference; 1996 Mar; New Delhi.
8. Adebayo E.T , et al. Pattern of prescription drug use in Nigerian army hospitals. Ann Afr Med. 2010;9(3):152–158.
9. Mehta S, et al. From the pen to the patient: Minimising medication errors. J Postgrad Med. 2005;51:3–4.
10. Bhatt A.D. Drug promotion and doctor: a relationship under change? J Postgrad Med. 1993;39:120.