Mwandishi:
Dkt. Sospeter B, MD
Mhariri:
Dkt. Adolf S, MD
Jumatano, 22 Septemba 2021
Maudhi ya kuacha vidonge vya majira
Mtumiaji wa muda mrefu wa njia za uzazi wa mpango zenye vichocheo anapoacha huweza patwa na hedhi nzito, yenye maumivu makali au isiyoeleweka, chunusi, kuota nywele zisizotakiwa, kutopata ujauzito kwa wakati n.k. Wasiliana na daktari kama dalili zitadumu zaidi ya miezi sita.
Kuacha matumizi ya majira
Kama una mpango wa kuacha matumizi ya vidonge vya majira au njia zingine zinazotumia vichochezi, baadhi ya dalili ulizokuwa nazo kabla ya kuanza matumizi ya njia hii zitarejea. Hata hivyo kama hukuwa na dalili pia, utapata dalili mpya zitakazodumu kwa kipindi fulani kabla ya kupotea. Makala hii imezungumzia madhara ya kuacha vidonge vya majira hata hivyo dalili hizi zinaweza kutokea pia kwa waliotumia njia za uazi wa mpango zenye vichochezi kama kitanzi, kipandikizi, bangiri, sindano pachi n.k.
Maudhi ya kuacha kuacha matumizi ya njia za uzazi wa mpango zenye
Maudhi ya kuacha vidonge vya majira baada ya kuvitumia kwa muda mrefu yanajumuisha;
Chunusi
Vichochezi vilivyo kwenye vidonge vya majira mbali na kufanya kazi ya kuzuia uzalishaji wa yai na manii kuingia kwenye mfuko wa kizazi, hupunguza pia kiwango cha homon za kiume kwenye damu yaani testosterone. Kupungua kwa testosterone hupelekea kuamka upya kwa chunusi. Kama unasumbuliwa na chunusi baada ya kuacha majira, wasiliana na daktari ili akupatie matibabu ya chunusi.
Kipanda uso cha hedhi
Baadhi ya watu wanaweza kupata kipanda uso cha hedhi karibia na siku ya 14 ya mzunguko wa hedhi, hii hutokea kutokana na mwitikio wa miili yao kwenye kiwango cha estrogen kilichopungua kwa kuacha matumizi ya vidonge vya majira.
Kubadilika kwa hali ya moyo
Mtumiaji wa vidonge vya majira huwa na mhemko wa na hasira au masikitiko na hii hutegemea mwitikio wa mtu na mtu. Kwa kuwa vidonge vya majira huwa na homoni zinazodhuru mfumo wa fahamu, baadhi ya watu wanaotumia vidonge vya majira hupata mihemko inayotulia baada ya kuacha matumizi ya dawa hizi. Hata hivyo baadhi ya watumiaji hupata mabadiliko makubwa ya hali ya moyo kiasi cha kupata mhemuko wa sonona kutokana na kuacha vidonge vya majira.
Mabadiliko ya uzito
Kuongezeka au kupungua uzito hutokea sana kwa wanaosimama kuchoma sindano Depo-Provera kwa kuwa kuacha matumizi hudhuru hamu ya kula. Mabadiliko ya uzito yanaweza kuathiri pia hedhi yako.
Mabadiliko ya hamu ya ngono
Vidonge vya majira hupunguza hamu ya kufanya ngono kwa baadhi ya wanawake, tegemea kurejea haraka kwa hamu ya tendo hili mara utakaposimama matumizi ya vidonge hivi.
Maumivu wakati wa hedhi
Kama ulikuwa na hedhi yenye damu nyingi na yenye maumivu na yakaisha baada ya kuwa unatumia vidonge vya majira, tegemea kurejea kwa dalili hizi.
Dalili zingine ni;
Kupoteza nywele hivi karibuni au kuota kwa nywele zisizotakiwa
Hedhi yenye damu nyingi au maumivu
Kutoona hedhi kwa muda wa miezi mitatu au zaida mara baada ya kuacha kutumia majira
Maumivu ya tumbo wakati wa yai kutolewa
Ugumba
Kubadilika kwa tabia ya tumbo
Hasira na sonona
Kiwango cha juu cha sukari
Haipothairoidizm
Sindromu ya hedhi
Dalili za hatari zinazohitaji uchunguzi
Mbali na kupata dalili hizo, zinapaswa kupungua kwa jinsi siku zinavyoenda, unapaswa kuwasiliana na daktari haraka endapo;
Dalili hazipungui makali
Dalili zinadumu zaidi ya miezi sita
Unapata homa au kupata hedhi yenye damu nyingi baada ya kutolewa kitanzi
Mambo ya kufanya kukabiliana na maudhi
Ili kukabiliana na maudhi yanayotokea baada ya kucha matumizi ya vidonge vya majira, unapaswa kuishi kiafya kwa kuzingatia chakula na mazoezi.
Chakula na mazoezi
Vyakula vya kuondoa sumu mwilini
Kwa vile ini lako lilikuwa linafanya kazi kila siku ya kuondoa vidonge vya majira kwenye damu, ukila vyakula vinavyotakasa mwili husaidia kuondoa sumu za oksijeni zilizotengenezwa.
Vyakula hivyo ni vile vyenye vitamin kwa wingi kama
Karoti
Kabeji
Vitunguu maji
Kale
Bruzeli
Brokoli
Vitunguu swaumu
Zabibu
Tangawizi
Majani ya mboga za majani
Chai ya ndizi, tangawizi na vitunguu swaumu
Matumizi pia ya nyama kutoka kwa wanyama waliofungwa kwa njia asili (wasiotumia dawa kukuzwa) kama;
Samaki
Kuku
Ngo’mbe Vyakula vingine
Unapaswa kuzingatia mlo wako kwa kula mlo kamili wa vitu asili wenye matunda kwa wingi na mboga za majani. Usisahau kutumia protini na mafuta ya kiafya kwa kiasi.
Mazoezi
Unapaswa kufanya mazoezi yenye mpangilio maalumu angalau mara tatu kwa wiki na kila zoezi lidumu angalau kwa muda wa dakika 30 na kuendelea. Tafiti zinaonyesha mazoezi husaidia kuondoa msongo na kupunguza maumivu ya hedhi. Soma zaidi kuhusu mazoezi kwenye linki ya chakula na mazoezi zilizo kwenye tovuti hii.
Tiba ya nyumbani
Tiba inayolenga dalili husika inaweza kufanyika pia, mfano kama una maumivu makali ya hedhi, tumia njia ya kuweka chupa ya maji moto juu ya tumbo lako ili kukabiliaa na maumivu au kutumia dawa jamii ya NSAIDs. Maelezo zaidi kuhusu njia za kukabiliana na maumivu yanapatikana kwenye makala husika ya maumivu ya hedhi.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
7 Oktoba 2021 04:36:06
Rejea za mada hii:
NCBI. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6736472/. Imechukuliwa 21/09/2021
Dietary guidelines for Americans, 2020-2025. https://www.dietaryguidelines.gov/sites/default/files/2021-03/Dietary_Guidelines_for_Americans-2020-2025.pdf. Imechukuliwa 21/09/2021
Girum T, et al. Return of fertility after discontinuation of contraception: A systematic review and meta-analysis. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6055351/. Imechukuliwa 21/09/2021
Hwang, J. H. Treatment of postpill amenorrhea with abdominal obesity by traditional Korean medicine treatment focused on pharmacopuncture and moxibustion.
https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6736472/. Imechukuliwa 21/09/2021
Johnson, B. A. Insertion and removal of intrauterine devices.
https://www.aafp.org/afp/2005/0101/p95.html. Imechukuliwa 21/09/2021
NHS. When will my periods come back after I stop taking the pill?. https://www.nhs.uk/conditions/contraception/when-periods-after-stopping-pill/. Imechukuliwa 21/09/2021
Planned parentohood. How does IUD removal work?. . https://www.plannedparenthood.org/learn/birth-control/iud/how-does-iud-removal-work. Imechukuliwa 21/09/2021