top of page

Mwandishi:

Dkt. Mangwella S, MD

Mhariri:

Dkt. Adolf S, M.D

Jumapili, 17 Oktoba 2021

Maziwa ya ng'ombe kwa mtoto mdogo

Maziwa ya ng'ombe kwa mtoto mdogo

Matumizi ya maziwa ya ngombe yanaweza kuambatana na upotevu mdogo wa damu kwenye kinyesi kwa vichanga na watoto chini ya umri wa mwaka mmoja. Hii imeonekana kwenye tafiti mbalimbali ambapo moja yake iliyofanyika kwa watoto 52, waliotumia maziwa ya ng’ombe au maziwa ya fomula kwa muda wa siku 168 ilionyesha matokeo yafuatayo;


 • Kuongezeka uwiano wa damu kwenye kinyesi kutoka asilimia 3 mpaka asilimia 30.3 ndani ya siku 28 za awali kwa watoto waliotumia maziwa ya ng’ombe

 • Kuongezeka uwiano wa damu kwenye kinyesi kutoka asilimia 3 hadi 5 kwa maziwa ya fomula

 • Ongezeko la kiasi cha hemoglobin kwenye kinyesi ndani ya siku 28 za kwanza

 • Ongezeko lisilo na mashiko la himoglobin(Hb) kwenye kinyesi cha mtoto kwa wale waliotumia maziwa ya fomula


Upotevu wa damu kwenye kinyesi kutokana na matumizi ya maziwa ya ng’ombe hutokea kwa watoto chini ya mwaka mmoja tu na baada ya hapo hupotea kwa jinsi umri unavyoongezeka.


Je, ni kawaida watoto kupoteza damu kwenye kinyesi?


Ndio ni kawaida

Licha ya kuwa ni jambo la kawaida kwa watoto chini ya mwaka mmoja kupoteza kiasi fulani cha damu kwenye kinyesi wakati wote, kumpatia mtoto maziwa ya ng’ombe kwenye umri huu huongeza kwa kiasi kikubwa upotevu wa damu kama ilivyoonekana kwenye tafiti mbalimbali.


Vihatarishi vya upungufu wa madini chuma

Vihatarishi vingine vya upuungufu wa damu kutokana na upunfugu wa madini chuma ni;


 • Kuchelewa anza chakula kingine mbali na maziwa ya mama baada ya kufikisha umri wa miezi sita

 • Matumizi ya vyakula visivyo na madini chuma ya nyongeza baada ya kufikisha umri wa miezi sita

 • Mtoto kuchagua chakula

 • Kunywa maziwa ya ng’ombe au matumizi makubwa ya maziwa ya ng’ombe ya zaidi ya mililita 700 kwa siku

 • Kutopata madini chuma ya ngongeza kwa watoto waliozaliwa na uzito mdogo


Vilivyomo kwenye maziwa ya ng’ombe

Maziwa ya ngombe huwa na kiasi kikubwa cha;


Viamsha mzio vikuu kwa mtoto

 • Immunoglobulini

 • β-lactoglobulin(β-LG)

 • α-lactalbumin(α-LA)

 • Caseins


Viamsha mzio vidogo kama;

 • Bovine serum albumin (BSA)

 • Lactoferrin


Madini yaliyomo kwenye maziwa ya ngombe ni;

 • Maadini chuma

 • Sodium

 • Potassium

 • Chloride

 • Fosporasi


Je, ni nini kilichomo kwenye maziwa kinachosababisha upotevu wa damu?

Kwa sababu watoto chini ya umri wa mwaka mmoja wakinywa maziwa ya ng’ombe yaliyochakatwa kwa joto kiwandani huwa hawapotezi damu nyingi, inadhaniwa kuwa maziwa ya ng’ombe huwa na kiasi kikubwa cha protini bovine albumin (BSA) inayosababisha upotevu wa damu. Kiasi cha bovine albumin hupungua au kupotea kama maziwa yatachemshwa kwenye nyuzi joto za sentigredi 120 kwa muda wa dakika 15.


Kuchemsha maziwa ya ngombe

Kuchemsha maziwa ya ngombe kwa muda wa dakika 15 katika nyuzi joto 120 za sentigredi husababisha upotevu wa protini katika mlolongo ufuatao;


 • Immunoglobulin (Ig)

 • Bovine serum albumin (BSA)

 • β-LG

 • α-LA

 • Casein


Casein ni protini ngumu kupotea haraka kwa kuchemsha maziwa na huondolewa kirahisi kiwandani.


Kuna madini na virutubisho vingine muhimu ambavyo huharibiwa na joto kali, hii ndio maana maziwa haya yanapaswa kuongezewa virutubisho vya ziada kwa afya ya mtoto.


Maziwa ya ng’ombe yaliyotengenezwa kiwandani huwa yameongezewa virutubisho muhimu kama vitamin A, B, D, madini chuma n.k


Mambo mengine ya kufahamu kuhusu maziwa ya ngombe na upungufu wa damu

Kiasi cha madini chuma kwenye maziwa ya mama na ng’ombe huwa kidogo chini ya 0.3mg/L hadi 1mg/L.


Licha ya kuwa na kiasi kidogo cha mdini chuma kwenye maziwa ya mama na ng’ombe, asilimia 50 ya madini chuma kwenye maziwa ya mama hufyonzwa na kuingia kwenye damu, wakati ni asilimia 10 ya madini chuma kwenye maziwa ya ng’ombe hufyonzwa. Sababu kuu ya ufyonzwaji mzuri wa madini chuma kutoka kwenye maziwa ya mama inadhaniwa kutokana na kuwa na kiasi kidogo cha kalisiamu na fosforasi na pia kutokana na kuwa na lactoferrin.


Protini za maziwa ya ngombe huzuia ufyonzwaji wa madini chuma kwenye utumbo na hivyo kuweza kupelekea mtoto kutopata kiasi kinachotakiwa kwa ajili ya kutengeneza chembe nyekundu za damu. Madini chuma ni muhimu sana kwenye utengenezaji wa damu, watoto wenye upungufu wa madini chuma hupata upungufu wa damu unaotokana na upungufu wa madini chuma.


Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, kumlisha mtoto maziwa ya ng’ombe kwenye umri wa miezi sita badala ya maziwa ya ng’ombe yaliyotiwa virutubisho nyongeza kulipelekea ongezeko la upungufu wa madini chuma watoto walipofikisha umri wa mwaka mmoja.


Kumpa mtoto vyakula vyenye madini chuma kuna saidia kuepuka upungufu wa madini hayo?

Kumpa mtoto vyakula vyenye madini chuma huweza kufanya kazi ya kuzuia upungufu wa madini chuma lakini si wakati wote unaweza kumpatia mtoto madini chuma ya kutosha mahitaji haswa katika kipindi cha pili cha miezi sita kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.


Mbadala wa maziwa ya ng’ombe kwa mtoto

 • Maziwa ya ng’ombe ya fomula

 • Maziwa ya soya ya fomula


Vyakula vyenye madini chuma kwa wingi

Vyakula vyenye madini chuma kwa wingi ni;


 • Nyama ( ngombe, mbuzi, nguruwe na ndege kama kuku n.k)

 • Vyakula vya baharini au ziwani ( samaki, dagaa n.k)

 • Maharagwe

 • Mboga za kijani iliyokolea kama spinachi

 • Matunda yaliyokaushwa kama aprikoti, choya n.k

 • Vyakula vya mbegu vilivyoongezewa virutubisho

 • Peasi


Vyakula vinavyoongeza ufyonzaji wa madini chuma

Vyakula vinavyoongeza ufyonzwaji wa madini chuma ni vile vyenye vitamin C kwa wingi kama;


 • Brokoli

 • Zabibu

 • Kiwi

 • Mboga za kijani

 • Tikiti maji

 • Machungwa

 • Pilipili

 • Stroberi

 • Nyanya

 • Chenza


Madhara ya upungufu wa damu kutokana na upungufu wa madini chuma

Upungufu wa damu kutokana na upungufu wa madini chuma kwa watoto chini ya umri wa mwaka mmoja husababisha madhara mbalimbali kwenye ubongo wa mtoto kiasi cha kuchelewa kwa maendeleo ya ukuaji wake au kutopata maendeleo mazuri ya kitabia na ki saikomota.


Hitimisho

Maziwa ya mama ni chakula kizuri kwa watoto chini ya umri wa mwaka mmoja, endapo maziwa haya hayapatikani, maziwa ya fomula yaliyoongezewa madini chuma yanaweza kutumika kama mbadala.


Makala hii imejibu pia kuhusu

Makala hii imejibu maswali mbalimbali yanayohusu:

 • Maziwa ya ng'ombe kwa mtoto wa miezi mitatu

 • Maziwa ya ngo'mbe kwa mtoto wa miezi sita

 • Maziwa ya ng'ombe kwa mtoto mchanga

 • Maziwa ya ng'ombe kwa vichanga


Maelezo zaidi

Unaweza kusoma makala zingine zaidi kuhusu

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

20 Julai 2023 06:44:23

Rejea za mada hii:

Ziegler EE, et al. Cow milk feeding in infancy: Further observations on blood loss from the gastrointestinal tract. J Pediatr. 1990;116:11–8

Wilson JF, Lahey ME, Heiner DC. Studies on iron metabolism. V. Further observations on cow’s milk-induced gastrointestinal bleeding in infants with iron-deficiency anemia. J Pediatr. 1974;84:335–44.

Bu, Guanhao et al. “Milk processing as a tool to reduce cow's milk allergenicity: a mini-review.” Dairy science & technology vol. 93,3 (2013): 211-223. doi:10.1007/s13594-013-0113-x

Leung AK, Chan KW.Iron deficiency anemia Adv Pediatr(In press)
Tunnessen WW, et al. Consequences of starting whole cow’s milk at 6 months of age. J Pediatr. 1987;111:813–6.

Penrod JC, et al. Impact of iron status of introducing cow’s milk in the second six months of life. J Pediatr Gastroenterol Nutr. 1990;10:462–7.

de Andraca I, et al. Psychomotor development and behavior in iron-deficiency anemic infants. Nutr Rev. 1997;55:125–32.

Ziegler EE. Consumption of cow's milk as a cause of iron deficiency in infants and toddlers. Nutr Rev. 2011 Nov;69 Suppl 1:S37-42. doi: 10.1111/j.1753-4887.2011.00431.x. PMID: 22043881.

Kaushansky K, et al. Iron deficiency and overload. In: Williams Hematology. 9th ed. New York, N.Y.: The McGraw-Hill Companies; 2016. http://accessmedicine.mhmedical.com/content.aspx?sectionid=94304160&bookid=1581&jumpsectionID=94304237&Resultclick=2#1121092571. Imechukuliwa 17/10/2021

Schrier SL, et al. Treatment of iron deficiency anemia in adults. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 17/10/2021

American Society of Hematology. Iron-deficiency anemia. http://www.hematology.org/Patients/Anemia/Iron-Deficiency.aspx. Imechukuliwa 17/10/2021

National Institutes of Health Office of Dietary Supplements. Vitamin C: Fact sheet for health professionals. https://ods.od.nhih.gov/factsheets/VitaminC-HealthProfessional/. Imechukuliwa 17/10/2021

National Heart, Lung, and Blood Institute. What is iron-deficiency anemia? http://www.nhlbi.nih.gov/health/health-topics/topics/ida/. Imechukuliwa 17/10/2021

Schrier SL, et al. Approach to the adult patient with anemia. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 17/10/2021

Mahoney DH, et al. Iron deficiency in infants and young children: Treatment. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 17/10/2021

bottom of page