top of page

Mwandishi:

Dkt. Hellen P, MD

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Jumapili, 12 Septemba 2021

Mfungo katika Afya

Mfungo katika Afya

Mfungo wa kiafya huimarisha mwili na akili, hudhibiti uzito na kuzuia magonjwa yatokanayo na uzito mkubwa kama kisukari. Usifanye mfungo tu, fanya mfungo wa kiafya.


Kwanini mfungo una faida kwenye afya?


Tafiti nyingi za wanyama na binadamu zinaunga mkono faida za mfungo katika afya kwa ujumla.


Mfungo kwa ujumla huwa na faida ya kuondoa sumu mwilini na kuamlisha chembe hai za mwili kufanya umetaboli ambao kwa kawaida haufanyiki wakati mwili una nguvu za kutosha.


Unapofunga mwili hukosa glukosi (inayotumika kutengeneza nishati) kutoka kwenye chakula na hivyo mwili hutafuta njia nyingine ya kutengeneza nishati. Kukosekana kwa glukosi kutoka kwenye chakula husababisha ini kutumia kemikali zisizo wanga kama lactate, amino acid na mafuta ili kuzalisha glukosi itakayotumika kuzalisha nishati.


Mbali na hivyo, wakati wa mfungo, mwili hutunza kiasi cha nishati ulichonacho na hivyo hupunguza mapigo ya moyo na shinikizo la damu.


Mfungo pia hutengeneza msongo wa wastani kwenye chembe hai na hivyo kuzifanya zitengeneze njia ya kukabiliana na hali hii na kuwa imara. Hii ni sawa na mtu anayefanya mazoezi ya misuli, jinsi anavyoipa misuli uzito mkubwa zaidi, chembe za misuli hutengeneza njia ya kukabiliana na uzito kwa kuongezeka umbile na hivyo kufanya misuli kuwa mikubwa na imara. Mfungo mfupi wa kiafya husaidia kuzifanya chembe hai kuwa iamra zaidi.


Aina za mfungo


Kuna aina tatu za mfungo wa kiafya ambazo zimeonyesha mafanikio chanya kwa afya na kuongeza umri wa kuishi, aina hizo ni;


  • Mfungo wa muda

  • Mfungo wa kukatisha na kudhibiti nishati

  • Mfungo wa mkali


Mfungo wa muda


Ni aina ya mfungo inayofanyika kwa kujizuia kutumia nishati kwa masaa kadhaa katika siku, mara nyingi kati ya masaa 8 hadi 12 kwa siku.


Mfungo wa kukatisha na kudhibiti nishati


Aina hii ya mfungo hufanyika kwa kupunguza kiasi cha nishati unachotumia kwa siku. Mfano kula nusu ya nishati uliyozoea kutumia kwa siku na kuacha kutumia wanga kwa muda wa siku mbili hadi tatu kwa wiki.


Aina hii ya mfungo huuweka mwili kwenye mfungo mkali na wa muda mfupi na huukumbusha mwili kutokuwa na mazoea ya kupata nishati ile ile kila siku. Unapotumia mfungo huu, chagua vema nini unachokula wakati unaendelea na mazoezi na chakula chenye nishati kidogo.


Mfungo mkali


Mfungo huu hufanyika kwa kujizuia kutumia nishati kwa kipindi cha muda wa siku 3 hadi 5. Mfungo huu husababisha mwili kumaliza nishati yote iliyokuwa imehifadhi na kufanya ijitengenezee nishati nyingine kutoka kwenye mafuta. Mfungo wa aina hii pia huambatana na kiwango kikubwa cha kemikali za ketone kwenye damu, hii humaanisha kuwa mwili unajitengenezea nguvu kwa kuvunja mafuta yaliyohifadhiwa sehemu mbalimbali za mwili.


Ingawa mfungo huu unaweza kufanyika kwa kuacha kula kabisa, kufanya hivyo ni hatari kiafya kwa kuwa huweza kuleta magonjwa mengine.


Ili kupata faida za mfungo huuu, unaweza tumia njia ya kudhibiti kiasi cha nishati mfano, tumia kalori 1000 tu kwa siku. Mfungo wa kipindi huufanya mwili wako ujisafishe na huwa mzuri kuliko mifungo iliyotangulia hapo juu.


Faida za kiafya za mfungo


Mfungo wa kiafya huwa na faida zifuatazo;


  • Huimarisha uwezo wa kiakili

  • Hukinga mwili dhidi ya uzito mkubwa kupita kiasi

  • Hukinga magonjwa sugu yanayoambatana na uzito mkubwa kupita kiasi kama kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu n.k

  • Hupunguza michomo kinga mwilini

  • Huimarisha afya kwa ujumla

  • Hudhibiti uzito

  • Hupunguza hatari ya magonjwa ya kimetaboli kama kisukari

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

30 Juni 2023 19:23:49

Rejea za mada hii:

Terrence Sanvictores, et al. Physiology, Fasting. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK534877/. Imechukuliwa 12/09/2021

Rynders CA, et al. Effectiveness of Intermittent Fasting and Time-Restricted Feeding Compared to Continuous Energy Restriction for Weight Loss. Nutrients. 2019;11(10):2442. Published 2019 Oct 14. doi:10.3390/nu11102442. Imechukuliwa 12/09/2021

Stockman, et al. “Intermittent Fasting: Is the Wait Worth the Weight?.” Current obesity reports vol. 7,2 (2018): 172-185. doi:10.1007/s13679-018-0308-9. Imechukuliwa 12/09/2021

Anton, Stephen D et al. “Flipping the Metabolic Switch: Understanding and Applying the Health Benefits of Fasting.” Obesity (Silver Spring, Md.) vol. 26,2 (2018): 254-268. doi:10.1002/oby.22065. Imechukuliwa 12/09/2021

Hopskins. Intermittent Fasting: What is it, and how does it work?. https://www.hopkinsmedicine.org/health/wellness-and-prevention/intermittent-fasting-what-is-it-and-how-does-it-work. Imechukuliwa 12/09/2021

bottom of page