top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Helen L, M.D

Jumamosi, 16 Januari 2021

Shinikizo la juu la damu ni muuaji wa siri

Shinikizo la juu la damu ni muuaji wa siri

Shinikizo la juu la damu, watu wengi hufahamu kama presha, ni tatizo linaloua kwa siri watu zaidi ya milioni saba kila mwaka duniani. Hii ni kwa sababu tatizo hili huwa halionyeshi dalili yoyote ile linapotokea. Weka mikakati ya kujikinga, anza kwa kupima kila baada ya miezi miwili.


Umuhimu wa kufahamu shinikizo la damu


Shinikizo la damu ni muuaji wa siri wa mamilioni ya watu duniani, kutokana na taarifa za tafiti za shirika la afya duniani(WHO) zinaonyesha kwamba watu bilioni 1.13 duniani wana shinikizo la juu la damu. Idadi ya wagonjwa licha ya kuwa kubwa bado inaendelea kuongezeka. Hata hivyo tafiti zingine zinaonyesha kuwa kila mwaka watu milioni 7.6 hufa kwa magonjwa yanayotokana na shinikizo la juu la damu duniani.


Unaweza kuepuka kupata shinikizo la juu la damu kwa kiasi kikubwa endapo utafuata ushauri wa wataalamu wa afya. Kipimo cha shinikizo la damu hupimwa bure katika vituo vingi vya afya, hivyo unatakiwa kupima kila baada ya miezi miwili ili kuwa na rekodi ya shinikizo lako na kutambua mabadiliko mapema endapo yatatokea.


Endapo shinikizo la juu la damu halijatambulika mapema na kutibiwa, shinikizo hilo linaweza kupelekea kuharibu viungo mbalimbali ndani ya mwili kama moyo, ubongo, figo, macho au kusababisha magonjwa mengine.


Matokeo ya uharibifu wa viungo vya mwili


Baadhi ya matokeo ya uharibifu wa viungo vya mwili kutokana na shinikizo la juu la damu ni;


  • Ubongo- Kupelekea kiharusi

  • Moyo- Kupelekea moyo kufeli, magonjwa ya mishipa ya moyo na mshituko wa moyo

  • Figo- kupelekea kufeli kwa figo

  • Macho- Hupelekea presha ya jicho (glaukoma) ambayo huleta upofu wa macho


Fahamu shinikizo lako kwa kupima kila baada ya miezi miwili, chukua tahadhari za kuzuia shinikizo la juu la damu kwa kufanya mazoezi, kutumia chumvi kidogo na kufuata ushauri ulioandikwa kwenye kipengele kinachofuata chini.


Namna ya kujikinga na shinikizo la juu la damu


  • Punguza kiasi cha chumvu unachokula kutoka kwenye chakula. Inashauriwa kula chini ya gramu 5 kwa siku

  • Kula matunda mengi zaidi na mboga za majani kuliko vitu vingine

  • Ushughulishe mwili wako angalau mara tatu kwa wiki kwa kufanya mazoezi au kufanya kazi zinazokutoa jasho

  • Acha kuvuta sigara

  • Punguza matumizi ya kilevi

  • Punguza kutumia vyakula vyenye mafuta kwa wingi kama chipsi, nyama za kukaangwa, mayai ya kukaangwa n.k

  • Acha au punguza matumizi ya mafuta yenye rehamu (kolestro) nyingi

  • Punguza na pata tiba ya tatizo la msongo wa mawazo

  • Kuwa na uzito unaotakiwa kiafya (uwe na BMI kati ya BMI 18.6 hadi 24.9)

  • Pima na fahamu shinikizo lako la damu kila miezi miwili


Kumbuka


Mchango wa chakula asilia kuzuia na kutibu shinikizo la juu la damu. Endelea kusoma zaidi namna ya kupima, kushusha na kujikinga na shinikizo la juu la damu kwa kutumia chakula sehemu nyingine ndani ya tovuti hii.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

19 Julai 2023 20:41:55

Rejea za mada hii:

1.Hisatomi Arima etal. Mortality patterns in hypertension. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22157565/#. Imechukuliwa 15.01.2020

2.Minoru Lida etal. Impact of elevated blood pressure on mortality from all causes, cardiovascular diseases, heart disease and stroke among Japanese: 14 year follow-up of randomly selected population from Japanese -- Nippon data 80. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/14704729/. Imechukuliwa 15.01.2020

3.WHO. Hypertension. https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/hypertension. Imechukuliwa 15.01.2020

4.Facts About Hypertension. https://www.cdc.gov/bloodpressure/facts.htm. Imechukuliwa 15.01.2020

5.Global Burden of Hypertension and Systolic Blood Pressure of at Least 110 to 115 mm Hg, 1990-2015. https://jamanetwork.com/journals/jama/fullarticle/2596292. Imechukuliwa 15.01.2020

6.Suada Brankovic etal. Frequency of Blood Pressure Measuring According to the Degree of Working Population Education in Canton Sarajevo. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3804429/. Imechukuliwa 15.01.2020

bottom of page