top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Helen L, M.D

Alhamisi, 4 Februari 2021

Soma tarehe ya mwisho wa matumizi kwa kila dawa unayonunua

Soma tarehe ya mwisho wa matumizi kwa kila dawa unayonunua

Kufahamu tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa ni njia mojawapo ya kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza pamoja na usugu wa vimelea vya maradhi dhidi ya dawa hiyo. Jenga tabia ya kusoma mwisho wa matumizi wa kila dawa unayonunua.


Utambuzi wa tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa


Tarehe ya mwisho wa matumizi huandikwa na kiwanda kinachozalisha dawa au mtaalamu wa dawa. Alama ya tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa huandikwa kwa majina mbalimbali kama;


  • Exp

  • Exp date

  • Expires

  • Expiry

  • Expiry date

  • Use before

  • Use by

  • Isitumike baada ya

  • Tarehe ya kuisha muda wa matumizi

  • Tumia kwa siku baada ya kufungua


Maelezo ya ziada kuhusu tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa


Endapo dawa yako imeandikwa, 'tumia kabla' au 'tumia mpaka' au 'tarehe ya mwisho wa matumizi', hii humaanisha dawa hiyo haipaswi kutumika baada ya muda huo kuisha. Dawa pia huweza kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza kwa kutumia maneno ambayo yameorodheshwa hapo juu.


Mfano 1

Endapo dawa imeandikwa, 'tumia mpaka Julai 2021', kwa lugha ya kiingereza ‘Use by July 2021’, hii inamaanisha, usitumie dawa hii kuanzia tarehe 31/7/2021 na kuendelea.


Mfano 2

Baadhi ya dawa za kimiminika zinazofunguliwa huandikwa, 'Tumia kwa siku 7 tu baada ya kufungua chupa ya dawa au kwa lugha ya kiingereza "discard 7 days after opening". Hii inamaanisha usitumie dawa hiyo siku 7 baada ya kufungua dawa hiyo, hata kama hujaimaliza na tarehe ya mwisho wa matumizi haijafika.


Muda wa dawa kuishi


Baadhi ya dawa zina muda mfupi wa matumizi, hivyo kuwa makini kusoma tarehe zinazoandikwa kwenye dawa hizo. Dawa za kimiminika kama dawa za kuweka machoni, masikioni, kunywa, n.k huwa na muda mfupi sana wa matumizi, takribani kuanzia siku saba hadi wiki nne tu tangu zimefunguliwa.


Dawa zenye asili ya vidonge vigumu au tembe huishi kwa muda mrefu na tarehe ya mwisho wa matumizi huweza kuwa takribani mwaka mmoja na kuendelea.


Kumbuka


  • Usitumie dawa za kwenye kopo ambazo hazionyeshi tarehe ya mwisho wa matumizi

  • Usitumie dawa zilizo kwenye karatasi ambazo hazina tarehe za kutengenezwa na tarehe ya kuisha muda wake

  • Usinunue dawa kwa wingi ambayo inakaribia kuisha muda wake

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

19 Julai 2023 20:41:55

Rejea za mada hii:

1.Why do medicines have expiry dates. https://www.nhs.uk/common-health-questions/medicines/why-do-medicines-have-expiry-dates/#. Imechukuliwa 04.02.2021

2.https://www.health.harvard.edu/staying-healthy/drug-expiration-dates-do-they-mean-anything. Imechukuliwa 04.02.2021

3.Dan Gikonyo, et al. Drug expiry debate: the myth and the reality. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC7040264/#R2. Imechukuliwa 04.02.2021

bottom of page