top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Jumatatu, 23 Agosti 2021

Tumbo kubwa kuzunguka kiuno kwa mwanamke

Tumbo kubwa kuzunguka kiuno kwa mwanamke

Tumbo kubwa kuzunguka juu ya kiuno kwa mwanamke huchangiwa na ulaji wa nishati nyingi, kufanya kazi za kutumia nishati kidogo na kuwa na umri mkubwa. Licha ya kuambatana na magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, kisukari na upumuaji, tumbo kubwa huepukwa kwa kula nishati kidogo na mazoezi.


Ni nini huchangia kupata tumbo kubwa ni nini?


Tumbo kubwa kuzunguka juu ya kiuno huchangiwa na ulaji wa nishati nyingi kutoka kwenye chakula, kufanya kazi zisozotumia nishati nyingi, kuwa na umri mkubwana kwa kiasi kidogo sababu za kijeni.


Vyakula vyenye nishati nyingi ni vipi?


Vyakula vyenye nishati nyingi ni kama;


 • Vinywaji vya kusindikwa kama Soda, Juisi, bia n.k

 • Vyakula visivyokobolewa kama vile wali, ugali na vingine

 • Vyakula vyenye mafuta kwa wingi kama vile chipsi na nyama za kukaangwa


Maelezo kuhusu visababishi vya tumbo kubwa


Umri unachangiaje kuwa na tumbo kubwa?


Jinsi unavyozeeka, ujazo wa misuli hupungua taratibu na wakati huo kiwango cha mafuta huongezeka. Kupungua kwa ujazo wa misuli husababisha mwili kutumia nishati kidogo kiasi cha kufanya kuwa vigumu kuwa na uzito wa kiafya. Mwanamke pia anapozeeka kiasi cha homon estrogen kwenye damu hupungua, homon hii hufanya kazi ya kuamuru mafuta yakae sehemu nyingine za mwili mbali na maeneo ya kuzunguka kiuno.Kula nishati nyingi kunachangiaje kuwa na tumbo kubwa?


Mwili una kiasi cha nishati unachoweza kutumia kwa siku kwa ajili ya kukupa nguuvu ya kutembea, kufikiria na kufanya moyo ufanye kazi. Endapo nutakula nishati nyingi zaidi, nishati ya ziada hubadilishwa na ini kuwa mafuta na hivyo huhifadhiwa maeneo mbalimbali ya mwili ikiwa pamoja na ndani ya tumbo au chini ya ngozi kama ilivyo maeneo ya juu ya kiuno, makalio na juu ya tumbo kwa baadhi ya wanawake.


Kufanya kazi kidogo huchangiaje kuwa na tumbo kubwa?


Jinsi unavyofanya kazi mfano, kulima, kutembea, kuendesha baiskeli, kukimbia n.k, mwili hutumia nishati nyingi kuipa misuli yako nguvu ili iweze kufanikisha lengo. Mtu anayekula chakula bila kufanya kazi, au kufanya kazi kidogo, kiasi cha nishati anayotumia pia huwa kidogo na hivyo kiasi cha nishati kinachobaki huhifadhiwa kama mafuta chini ya ngozi na kupelekea kuwa na tumbo kubwa.


Kwanini kuwa na tumbo kubwa kuzunguka kiuno ni hatari?


Tafiti zinaonyesha, kuwa na tumbo kubwa huambatana na magonjwa yafuatayo;


 • Shinikizo la juu la damu

 • Kisukari aina ya pili

 • Magonjwa ya moyo

 • magonjwa ya mishipa ya damu

 • Matatizo ya upumuaji


Kuwa na tumbo kubwa bila kujali uzito au uwiano wa uzito kwa urefu ulionao huambatana na kufa kabla ya wakati kutokana na magonjwa ya mishipa ya damu na moyo.


Namna ya kupunguza tumbo kubwa kuzunguka kiuno


Unaweza punguza tumbo kwa kufanya mazoezi ya tumbo, hata hivyo mafuta ndani ya tumbo hayawezi pungua kwa mazoezi tu bali kwa kupunguza kiasi cha nishati unachotumia. Kufanya mambo yafuatayo hupunguza tumbo kubwa kuzunguka maeneo ya kiuno;


 • Kula mlo wa kiafya. Kula vyakula asili kutoka kwenye mimea kama vile matunda, mboga za majani na wanga wa vyakula visivyokobolewa. Unapokula nyama, kula ile isiyo na mafuta, unapokunywa maziwa pia, kunywa yale yaliyopunguzwa mafuta.

 • Punguza au acha kula vyakula na vinywaji vya kusindikwa kama soda, nyama ice creem na vinginevyo.

 • Pia unaweza chagua kula nyama kutoka kwenye viumbe wenye nyama nyeupe kama samaki na kuku badala ya nyama ya ngombe, mbuzi na zinazofanana na hizo

 • Acha au punguza kula au kunywa vyakula vyenye wanga au nishati kwa wingi wakati wa usiku. mfano kula ugali, kunywa soda au vinjwaji vingine vya kutia nguvu)

 • Badala ya kunywa vinywaji vyenye sukari, kunywa maji au vinywaji visivyo na sukari au nishati kwa wingi isipokuwa ni lazima sana

 • Kula mlo wenye wanga kidogo, lakini ongeza matunda na mboga za majani kwa wingi

 • Fanya mazoezi yenye mpangilio maalumu, mazoezi ya viungo vya mwili, mazoezi ya misuli ya tumbo na yale ya moyo( mfano kukimbia, kutembea haraka, kuogelea n.k)

 • Unashauriwa kufanya mazoezi kwa muda wa nusu saa angalau mara tatu kwa wiki

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

7 Oktoba 2021 04:54:12

Rejea za mada hii:

1. L. Perreault, et al. Obesity in adults: Prevalence, screening, and evaluation. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 23.08.2021

2. National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Disorders. Understanding adult overweight and obesity.. https://www.niddk.nih.gov/health-information/weight-management/adult-overweight-obesity/all-content. Imechukuliwa 23.08.2021

3. Hoffman BL, et al. Menopausal transition. In: Williams Gynecology. 3rd ed. New York, N.Y.: McGraw-Hill Education; 2016. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 23.08.2021

4. Physical Activity Guidelines for Americans, 2nd ed. U.S. Department of Health and Human Services. https://health.gov/paguidelines/second-edition. Imechukuliwa 23.08.2021

5. ULY CLINIC. Chakula na mazoezi. https://www.ulyclinic.com/program-ya-mazoezi. Imechukuliwa 23.08.2021

bottom of page