Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Sospeter M, MD
Alhamisi, 22 Julai 2021
Ubora wa dawa
Matumizi ya dawa zenye bora huleta matokeo mazuri ya kitiba. Dawa zisizo na ubora si kwamba hazitibu tu, bali hudhuru afya au kupelekea kupoteza maisha na fedha nyingi. Ubora wa dawa hufahamika kwa kuangalia tarehe ya mwisho wa matumizi, lebo, rangi, harufu na umbile la dawa.
Ubora wa dawa ni nini?
Matumizi ya dawa zenye bora huwa na matokeo mazuri katika matiababu, hata hivyo dawa zisizo na ubora si tu hazitibu, bali huwa zinadhuru afya ya mtu hata kupelekea kupoteza maisha na fedha.
Mgonjwa hupoteza muda mwingi akihangaika na ugonjwa na hivyo kushindwa kufanya kazi na kuathiri uchumi.
Ni wajibu wa mtengenezaji, msambazaji na muuzaji kuhakikisha kuwa dawa zote zinazotolewa kwa jamii zinazokidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi wa kitaifa na kimataifa.
Makala hii imezungumzia kuhusu, sifa za dawa zenye ubora, sababu za dawa kupoteza ubora na namna ya kuhakiki ubora wa dawa.
Sifa za dawa yenye ubora
Baadhi ya mambo muhimu unayotakiwa kuangalia wakati wa kuhakiki ubora wa dawa ni pamoja na:
Tarehe ya kuisha muda wa matumizi
Lebo
Kifungashio asilia
Rangi
Harufu
Umbile la dawa
Dawa huweza kuharibika hata kabla ya kufikia tarehe ya mwisho wa matumizi hivyo watoaji na watumiaji wa dawa wanapaswa kuwa waangalifu kabla ya kutoa au kutumia dawa
Dawa isitolewe au kutumika pale inapobainika kuwa na mojawapo ya mambo yafuatayo;
Kubadilika kwa harufu
Kubadilika kwa rangi ya kawaida
Dawa za vidonge kuvunjika kwa urahisi
Kuota ukungu na fangasi juu ya uso wa dawa mbalimbali.
Kugandamana kwa dawa aina ya vidonge, tembe na dawa za unga
Kukatika kwa dawa za emalsheni
Kutengana kwa ”suspension” kunaashiria upungufu wa ubora wadawa na hasa pale ambapo juhudi za kutikisa hazirejeshi dawa hiyo katika hali yake ya kawaida
Dawa bandia, hazikidhi vigezo vya ubora kama dawa zilizotengenezwa na mtengenezaji halisi zinaweza kutambuliwa kwa kufananisha lebo na maandishi ya dawa halisi pamoja na mwonekano wa kidonge
Utunzaji mzuri wa dawa ili kuhifadhi ubora wake
Ubora wa dawa unaweza kupotea endapo dawa imehifadhiwa katika mazingira yasiyo salama. Mazingira yanayoweza kuathiri dawa mazingira ya;
Joto kali
Mwanga wa jua
Unyevunyevu
Uchafu
Bakteria na fangasi
Unyevu
Kama vifaa vya kuwekea dawa havitafunikwa vizuri, unyevunyevu unaweza kuingia ndani na kuharibu dawa.
Vidonge vinaweza kupata maji maji na hivyo kupondeka, wakati dawa za tembe zinaweza kugandamana. Dawa nyingine kama aspirin zinaweza kuharibika inapochanganyika na unyevu.
Ni muhimu kuzingatia yafuatayo ili kuzuia dawa kupata unyevu
Mambo ya kufanya mtumiaji wa dawa
Weka dawa sehemu kavu
Acha dawa katika chombo chake asili kwa muda wote
Funika vizuri chombo cha kuhifadhia dawa wakati wote. Chombo cha kuhifadhia dawa baada ya kufungua.
Hifadhi makasha ya dawa kwenye kabati ya mbao au kioo
Mambo unatakiwa kuepuka
Kuhifadhi dawa kwenye sakafu
Kutoa pakiti ya kunyonya unyevu iliyo ndani ya kashala dawa
Mambo ya kufanya mtunzaji au mtoa dawa
Hakikisha kwamba sehemu zote za jengo hazivuji
Weka madirisha kwenye chumba cha kutunzia dawa ili kuhakikisha hewa inapita vema
Usihifadhi dawa kwenye sakafu kuepusha kufyonza unyevu kutoka kwenye sakafu
Hifadhi makasha ya dawa kwenye chaga au kwenye kreti la dawa
Wakati wa kupiga deki kwenye duka au chumba cha kutunzia dawa fungua madirisha yote ili kuongeza mzunguko wa hewa na kukausha sakafu haraka
Mambo ya kuepuka
Kuhifadhi dawa kwenye sakafu
Kutoa pakiti ya kunyonya unyevu iliyo ndani ya kashala dawa
Mwanga wa jua
Baadhi ya dawa hasa zile za maji huharibika kama zikiachwa mahali penye mwanga wa jua.
Mfano: adrenaline na ergometrine. Dawa hizi huharibika kiini chake hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari zifuatazo kuzuia uharibifu huu:
Mambo ya kufanya mtoa au mhifadhi wa dawa
Hifadhi dawa zote zinazoathirika na mwanga mkali kwenye kabati isiyoingiza mwanga wa jua
Weka mapazia kuzuia mwanga mkali
Kufunga dawa vizuri na zisiwekwe kwenye dirisha linalopitisha mwanga moja kwa moja
Dawa zilizo kwenye chupa ya kahawia zihifadhiwe kwenye giza
Tunza dawa za chupa( ampuli) kwenye chombo kilichofunikwa
Joto kali
Joto kali huharibu aina nyingi za dawa. Kwa mfano dawa aina ya krimu au losheni huweza kuyeyuka na kuharibika kama zikiachwa kwenye joto kali. Ni vema kuhifadhi dawa sehemu isiyo na joto kali na kuzingatia maelezo ya utunzaji kama yalivyoanishwa kwenye lebo ya dawa.
Mambo ya kufanya mtoaji wa dawa
Fanya mambo yafuatayo ili kukinga dawa na joto kali;
Hakikisha stoo na sehemu ya kutolea dawa ina dari nzuri na imara
Funga feni, uweke tundu la hewa au weka madirisha mapana kwenye stoo
Hakikisha kuta za jengo ni ndefu vya kutosha ili kuruhusu mzunguko wa hewa
Kuta na dari zipakwe rangi nyeupe ili kuakisi mwanga na hivyo kupunguza joto
Fungua madirisha wakati wa mchana ili kuwezesha hewa kuzunguka bila kipingamizi na kupitisha hewa safi kwenye stoo
Tumia jokofu kuhifadhi dawa ambazo zinahitaji kutunzwa kwenye joto la nyuzi kati ya 2 na 8 za selishiazi.
Usiruhusu dawa kuganda kwani ukifanya hivyo unaweza kupunguza nguvu ya dawa
Uchafu
Uchafu huweza kusababisha dawa kuingiliwa na vimelea vya maradhi. Hii huweza kuchangia mgonjwa kupata maradhi mengine ambayo huhitajika kutibiwa na dawa nyingine na hivyo kumuongezea mgonjwa gharama. Ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo;
Weka duka lako katika hali ya usafi siku zote
Hakikisha hakuna wadudu waharibifu kama panya, mende, mchwa, na kunguni
Safisha sakafu mara tu baada ya dawa kumwagika
Ondoa maboksi, chupa na vifungashio vya dawa visivyo na kazi
Kama duka lina jokofu, weka ratiba ya kuihakiki, kuisafisha na kuyeyusha barafu
Bakteria na Fangasi
Dawa zinaweza kuharibiwa na bakteria au fangasi, kwa hiyo kuna umuhimu wa kuzihifadhi katika usafi wa hali ya juu. Unaweza kufanya yafuatayo, ili kuzuia uharibifu wa namna hiyo kutokea;
Hakikisha vyombo vya kuhifadhia dawa vimefunikwa wakati wote kuzuia uchafuzi kutokana na bakteria, fangasi na vumbi.
Hakikisha eneo la kutolea dawa ni safi wakati wote
Safisha kijiko cha kutolea dawa kila mara unapotoa dawa na mikono iwe safi wakati wote
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
7 Oktoba 2021 04:55:46
Rejea za mada hii:
1. SándorGörög, et al. Drug safety, drug quality, drug analysis
https://www.sciencedirect.com/science/article/abs/pii/S0731708507006590#. Imechukuliwa 22.07.2021
2. Drug quality and storage. https://medicalguidelines.msf.org/viewport/EssDr/english/drug-quality-and-storage-16688167.html. Imechukuliwa 22.07.2021
3. Storage of medications. . http://file.cop.ufl.edu/ce/consultwb/2015Workbook/CHAPTER%2021.pdf. Imechukuliwa 22.07.2021
4. WHO. Guide to good storage practices for
pharmaceuticals1. https://www.who.int/medicines/areas/quality_safety/quality_assurance/GuideGoodStoragePracticesTRS908Annex9.pdf?ua=1. Imechukuliwa 22.07.2021
5. Storing your medicines. https://medlineplus.gov/ency/patientinstructions/000534.htm. Imechukuliwa 22.07.2021