Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Sospeter M, MD
Jumamosi, 24 Julai 2021
Uchanganyaji wa ORS
ORS hupunguza asilimia 93 ya vifo kwa watoto kutokana na tatizo la kuharisha. Kufahamu namna sahihi ya kuchanganya na kutumia ORS kutapunguza vifo vingi zaidi.
ORS ni nini?
ORS ni kifupi cha neno ‘Oral Rehydration Salt’ linalomaanisha chumvi ya kurejesha maji mwilini. Mchanganyiko huu licha ya kuitwa chumvi, umetengenezwa kwa chumvi za sodium chloride, potassium chloride na sodium citrate pamoja na sukari aina ya glukosi.
Kutumia ORS husaidia wagonjwa wanaoharisha au kutapika kurejesha sukari na madini chumvi yanayopotea wakati huo na hivyo kuzuia vifo kutokana na madhara ya kupoteza madini na sukari mwilini.
Walezi na wanawake wengi wenye watoto na wanaohudhuria kliniki wanafahamu sana kuhusu ORS licha ya kutofahamu namna ya kutengeneza na kutumia mchanganyiko mzuri.
Namna ya kuchanganya ORS
Fuata hatua zifuatazo ili kutengeneza mchanganyiko mzuri wa ORS
Pima lita moja ya maji safi na salama ya kunywa,sawa na chupa nne za soda, kisha yaweke kwenye chombo safi
Fungua ORS kisha miminia kweye maji uliyoandaa
Koroga mchanganyiko wako wa ORS na maji kuhakikisha dawa yote imeyeyuka kwenye maji na hakuna chembe inayoonekana kwa macho
Weka mchanganyiko wako katika chupa kisha funika kwa kifuniko tayari kwa matumizi
Mchanganyiko wa ORS ni salama baada ya muda gani?
Machanganyiko wa ORS unapaswa kutumika ndani ya masaa 24 tu. Endapo muda umepita na dawa imebaki, unatakiwa kumwaga dawa hiyo kwa kuwa hupoteza usalama wake. Dawa iliyochanganywa na kukaa muda mrefu huchafuliwa na vimelea wa bakteria na hivyo huweza kuleta matatizo zaidi endapo itatumika.
Kiasi gani cha ORS unapaswa kutumia kwa tatizo la kuharisha?
Dawa ya ORS inapaswa kutumika mara nyingi iwezekanavyo kwa mgonjwa anayeharisha. Matumizi ya ORS yanatakiwa kwendana na hali ya kuhalisha pamoja na dalili za upungufu wa maji. Kwa kila gramu moja ya kinyesi anachopoteza mgonjwa anapswa kurejesha kwa kunywa mililita moja ya maji ya ORS.
Kwa dalili za wastani za kuishiwa maji
Kiasi cha maji ya kunywa katika mililita utakipata kwa kuzidisha uzito mara 10, kiasi hiki anywe kila mgonjwa anapoharisha
Au
Kupata kiasi cha maji ya kunywa ndani ya masaa 3 hadi 4 zidisha uzito wa mgonjwa mara 100. Kiasi hiki unachopata tumie ndani ya masaa 3 hadi 4 tu
Kwa wagonjwa wenye ugonjwa mkali wa kuharisha kama kipindupindu
Kama mgonjwa anaharisha sana na unahisi ana kipindupindu, mpeleke hospitali haraka huku ukizingatia kanuni za kujikinga na kipindupindu. Wakati unamsafirisha kwenda hospitai fanya mambo yafuatayo;
Kama ni mtoto mkubwa au mtu mzima, mpe mililita 100 za ORS kila baada ya dakika 5 mpaka pale atakapoacha kuharisha au kutoonyesha dalili za kuishiwa maji.
AU
Kwa mtu mzima anayeharisha sana, mpatie lita moja ya ORS kwa kila saa mpaka pale atakapokuwa vema( kuacha kuharisha na kupotea kwa dalili za kuharisha)
Kumbuka kama mgonjwa anataka kiasi zaidi yaani anapata kiu, mpe kiasi kingi kama anavyohitaji.
Mgonjwa anapaswa kufanyiwa uchunguzi kila baada ya saa 1 au 2 mpaka kiwango cha maji kitakaporejea kawaida.
Dalili kali za kuishiwa maji
Mgonjwa atakuwa na dalili moja au zaidi kati ya zifuatazo;
Uchovu mkali au kulegea mwili
Kupotea kwa mapigo ya mishipa wa damu au mapigo dhaifu
Kupumua kwa shida
Au dalili mbili zifuatazo;
Kuzama kwa macho
Kushindwa kunywa maji au kunywa kwa shida
Mfinyo wa ngozi kurejea taratibu
Mgonjwa mwenye dalili kali za kuishiwa maji anapaswa kutibiwa kwa kuongezewa maji kwenye mishipa. Usikae nyumbani na mgonjwa wa aina hii.
Dalili za wastani za kuishiwa maji
Kutokuwepo kwa dalili za hatari, na angalau dalili mbili zifuatazo;
Kutotulia au kulialia
Kuzama ndani kwa macho
Mapigo ya mishipa ya damu kwenda kasi
Kiu kali ya maji
Mfinyo wa ngozi kurejea taratibu sana
Dalili za kutoishiwa maji
Kuwa macho na kujielewa
Mapigo ya mishipa ya damu kuwa kawaida
Kiu ya kawaida
Kutozama kwa macho
Mfinyo wa ngozi kurejea kiurahisi
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
7 Oktoba 2021 04:56:33
Rejea za mada hii:
1. Melinda K. Munos, et al. The effect of oral rehydration solution and recommended home fluids on diarrhoea mortality. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2845864/. Imechukuliwa 23.07.2021
2. Bryce J, et al. WHO estimates of the causes of death in children. Lancet. 2005;365:1147–52
3. Cash RA, et al. A clinical trial of oral therapy in a rural cholera-treatment center. Am J Trop Med Hyg. 1970;19:653–56.
4. Mahalanabis D, et al. Oral fluid therapy of cholera among Bangladesh refugees. Johns Hopkins Med J. 1973;132:197–205
5. Mahalanabis D, Wallace CK, Kallen RJ, et al. Water and electrolyte losses due to cholera in infants and small children: a recovery balance study. Pediatrics. 1970;45:374–85
6. Nalin DR, et al. Oral or nasogastric maintenance therapy in pediatric cholera patients. J Pediatr. 1971;78:355–58
7. Nalin DR, et al. Oral maintenance therapy for cholera in adults. Lancet. 1968;2:370–73
8. World Health Organization. . Oral Rehydration Therapy for Treatment of Diarrhoea in the Home (Report No.: WHO/CDD/SER/86.9) Geneva: WHO1986; 2006.
9. Thane T, et al. Oral rehydration therapy in the home by village mothers in Burma. Trans R Soc Trop Med Hyg. 1984;78:581–89
10. Aksit S, et al. Carob bean juice: a powerful adjunct to oral rehydration solution treatment in diarrhoea. Paediatr Perinat Epidemiol. 1998;12:176–81
11. Umana MA, et al. Rehydration by the oral route in newborn infants dehydrated by acute diarrheal disease. Bol Med Hosp Infant Mex. 1984;41:460–63. [PubMed] [Google Scholar]
12. Uzel N, et al. Outcome of rehydration of diarrhea cases by oral route. Acta Paediatr Scand. 1991;80:545–56
13. CDC. Rehydration Therapy.https://www.cdc.gov/cholera/treatment/rehydration-therapy.html. Imechukuliwa 23.07.2021
14. Fluid and Electrolyte Therapy. https://www.utmb.edu/Pedi_Ed/CoreV2/Fluids/Fluids13.html#. Imechukuliwa 23.07.2021
15. Oral Rehydration Solutions: Made at Home. https://rehydrate.org/solutions/homemade.htm. Imechukuliwa 23.07.2021
16. Oral rehydration. https://www.ghsupplychain.org/sites/default/files/2019-02/MNCH%20Commodities-OralRehydration.pdf. Imechukuliwa 23.07.2021