Mwandishi:
Dkt. Sospeter B, MD
Mhariri:
Dkt. Charles W, MD
Ijumaa, 8 Oktoba 2021
Utambuzi wa jinsi ya mtoto kwenye ujauzito
Wajawazito wengi wana shauku ya kufahamu jinsia ya mtoto ili kufanya maandalizi mbalimbali kabla ya mtoto kuzaliwa. Licha ya kuwepo kwa vipimo tambuzi vya aina kadhaa, kipimo cha DNA-PCR hutambua jinsia kuanzia wiki 5 na kuendelea.
Faida za kufahamu jinsia ya mtoto akiwa tumboni
Baadhi ya faida zilizoripotiwa kwenye tafiti mbalimbali kuhusu kufahamu jinsia ya mtoto ni;
Kupata muda mzuri wa kufanya maandalizi kabla mtoto hajazaliwa kama vile kununua nguo gani na vifaa vinavyoendana na jinsia ya mtoto
Kuimarisha uhusiano wa mama na mtoto tumboni
Kuondoa msongo wa kufahamu jinsia
Kupata muda mrefu wa kutafuta jina la mtoto
Sababu za kutaka kufahamu jinsia ya mtoto
Kuna sababu mbalimbali zinazotolewa na mama mjamzito au wapenzi za kwanini wanataka kufahamu jinsia ya mtoto, miongoni mwa sababu hizo ni;
Kutaka kufahamu tu
Shauku ya kufahamu ni mtoto gani yupo tumboni
Kutoweza vumilia maswali ya jinsia ya mtoto
Uchaguzi wa jinsia pendwa
Kufanya maandalizi ya kichanga kabla ya kuzaliwa
Kumfanyia maandalizi kaka/dada zake
Kutohitaji butwaa
Kwa sababu inawezekana
Kuna raha kufahamu jinsia
Njia za kutambua jinsia ya mtoto tumboni
DNA-PCR
DNA ya mtoto hutengwa kutoka kwenye damu ya mama mjamzito kisha kupimwa uwepo wa kromosomu Y (DYS14) katika wiki ya 5 hadi 7 ya ujauzito. Baada ya kutambua uwepo wa kromosomu DYS14, majibu huthibitishwa mtoto anapozaliwa kama ni ya kweli. Uthibitisho baada ya kuzaliwa kwa mtoto umeonyesha kuwa kipimo cha DNA_PCR huwa na uwezo tambuzi wa asilimia 95 kwa ujauzito una wiki 5 na asilimia 100 kwa ujauzito wa wiki 7 na kuendelea.
Picha ya mawimbi sauti
Kipimo hiki hutumia kifaa kinachotengeneza mawimbi ya sauti na kutengeneza picha kwenye kioo. Kipimo cha picha ya mawimbi sauti huweza kuonyesha jinsia ya mtoto kuanzia wiki ya 11 ya ujauzito na kuendelea ( Usahihi wa majibu huongezeka zaidi jinsi mimba inavyokuwa kubwa). Licha ya kuwa ni kipimo kisicho jeruhi mwili wa mama na mtoto, ufanisi wa majibu hutegemea uzoefu wa mpimaji na umri wa ujauzito.
Tafiti moja (2018) iliyofanyika kuangalia uwezo tambuzi na usahihi wa kipimo hiki kwa wajawazito 150, imeonyesha kuwa na uwezo wa kutambua jinsia kwa asilimia 64.6 (watoto 97 tu). Usahihi wa majibu kwa watoto waliotambuliwa ulikuwa kama ifuatavyo;
Watoto 57 walitambuliwa kwa usahihi kuwa wanaume na 8 walitambuliwa kimakosa kuwa ni wanaume wakati ni wanawake
Watoto 31 walitambuliwa kwa usahihi kuwa na 1 alitambuliwa kimakosa kuwa ni mwanaume
Kutoka kwenye tafiti hii inaonyesha kuwa usahihi wa kipimo hiki kutambua jinsia ni asilimia 87.6 kwa jinsia ya kiume na 96.8 kwa jinsia ya kike kati ya watoto walioweza kutambuliwa jinsia. Usahihi wa majibu katika tafiti hii hata hivyo unaonekana kuwa juu zaidi kuliko tafiti zilizowahi fanyika nyuma ambazo zilionyesha ufanisi wa asilimia 75.
Picha ya mawimbi sauti huangalia nini kutambua jinsia?
Picha ya mawimbi sauti hutambua jinsia kwa kuangalia uelekeo wa nundu ya mkia wa mtoto na ishara ya sagittal na hamburger. Maelezo zaidi yanafuata kwenye aya hapa chini.
Ishara ya sagittal
Mwishoni mwa mstari wa kufikirika unaogawa mwili vipande viwili (mstari sagittal) kushoto na kulia kuna nundu ndogo inayoitwa notchi ya kaudo. nundu hii kama ikiangaliwa kutoka kwenye mstari wa sagittal na kuonekana kwenye nyuzi 10 kutoka mstari huu, mtoto huyu huwa na jinsia ya kike. Kama mwelekeo wa nundu unatengeneza nyuzi 30 kwenda juu kutoka kwenye mstari wa sagittal, mtoto huwa na jinsia ya kiume.
Ishara ya Hamburger
Ishara ya Hamburger ni jina la utani linaloelezea mwonekano wa mashavu ya uke na kinembe kwenye picha ya mawimbi sauti. Uke unapoangaliwa kwa karibu, mashavu yake huonekana kama vipande viwili vya mkate wakati kinembe huonekana kama nyama iliyowekwa katikati ya vipande hivyo na kutengeneza mwonekano wa baga au hamburger.
Amniocentesis au kipimo cha sampuli ya chorionic villus (CVS)
Kipimo hiki hufanyika kwa kuchukua majimaji kutoka kwenye chupa ya uzazi kwa kutumia sindano ndogo ili kupima uwepo wa chembe za mtoto zinazotambua jinsia. Licha ya kuwa na hatari katika ujauzito, njia hii huwa na uwezo mkubwa wa kutambua jinsia ya mtoto ukifananisha na njia ya picha ya mawimbi sauti.
Hasara za njia hii;
Huongeza hatari ya mimba kutoka na kujifungua kabla ya wakati
Huongeza hatari ya maambukizi kwenye mfuko wa kizazi
Haina ufanisi mkubwa wa kutambua jinsia ya mtoto kwenye ujauzito chini ya wiki 12
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
8 Oktoba 2021 16:50:59
Rejea za mada hii:
1. Honda H, et al. Fetal gender determination in early pregnancy through qualitative and quantitative analysis of fetal DNA in maternal serum. Hum Genet. 2002 Jan;110(1):75-9. doi: 10.1007/s00439-001-0649-3. Epub 2001 Nov 23. PMID: 11810300.
2. Martinhago CD, et al. Accuracy of fetal gender determination in maternal plasma at 5 and 6 weeks of pregnancy. Prenat Diagn. 2006 Dec;26(13):1219-23. doi: 10.1002/pd.1592. PMID: 17089442.
3. Gharekhanloo, et al. “The ultrasound identification of fetal gender at the gestational age of 11-12 weeks.” Journal of family medicine and primary care vol. 7,1 (2018): 210-212. doi:10.4103/jfmpc.jfmpc_180_17
4. Kooper AJ, et al. Why do parents prefer to know the fetal sex as part of invasive prenatal testing?. ISRN Obstet Gynecol. 2012;2012:524537. doi:10.5402/2012/524537
5. PAPP, Z. et al. MD Prenatal Sex Determination by Amniocentesis, Obstetrics & Gynecology: September 1970 - Volume 36 - Issue 3 - p 429-432
6. Abunadi N, , et al. Reported benefits of early fetal sex determination. Int J Pregn & Chi Birth. 2020;6(3):63-65. DOI: 10.15406/ipcb.2020.06.00199