top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Helen L, M.D

Jumapili, 31 Januari 2021

Utambuzi wa VVU ndani ya masaa 24 hadi siku 90

Utambuzi wa VVU ndani ya masaa 24 hadi siku 90

Unaweza kutambuliwa kwa vipimo endapo umepata maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) ndani ya masaa 24 hadi siku 90 baada ya kupata maambukizi. Pima maambukizi ya VVU na anza PEP endapo unahofu kuwa umepata maambukizi.


Vipimo vya Mambukizi ya VVU


Maambukizi ya VVU yanaweza kutambuliwa kwa vipimo kuanzia siku 9 hadi 90 toka umepata maambukizi. Baadhi ya vipimo vinavyotumika sana havina uwezo wa kutambua maambukizi ya VVU ndani ya siku chache mpaka virusi vizalishwe kwa wingi na kutambuliwa na kinga za mwili zenye jina la kitiba 'antibody'.


Kipindi hiki ambacho vipimo huwa havina uwezo wa kutambua maambukizi licha ya kuwa mtu ana maambukizi huitwa 'window period'


Endapo unahisi umepata maambukizi na upo kipindi cha 'window period', inashauriwa ukaanza dawa za 'PEP' ndani ya masaa 24 toka umehisi kupata maambukizi. Hii itazuia kuzaliana kwa virusi vya ukimwi na kuendelea kwa maambukizi endapo umeyapata wakati unasubiria kuhakikisha kwamba huna maambukizi baada ya kipindi cha 'window period' kuisha.


Kipimo cha HIV DNA PCR


Kipimo cha HIV DNA PCR hutambua uwepo wa maambukizi kuanzia siku 9 hadi 33. Kipimo hiki hupima nakala ya vinasaba vya kirusi (DNA) kwenye damu na huwa na uwezo wa kutambua uwepo wa virusi kwa asilimia 99 hadi 100. Kipimo cha HIV DNA PCR ni nadra kufanyika kwa sababu ya gharama.


Kipimo cha HIV antibodi/antigeni


Kipimo cha HIV antibodi/antigen hufanyika maabara. Kipimo hiki hupima kiwango cha kemikali za ulinzi zinazozalishwa na mwili kuitikia maambukizi ya VVU zenye jina la 'antibodi' au protini za virusi zenye jina la 'antigeni'. Endapo damu ya kidole itatumika , maambukizi yanaweza kugunduliwa kuanzia siku 19 hadi 90 ya kupata maambukizi, na endapo damu ya mishipa mkubwa itatumika, maambukizi yatagunduliwa kuanzia siku 19 hadi 45 ya kupata maambukizi. Kipimo hiki huwa na uwezo wa kutambua maambukizi kwa asilimia 95 hadi 99.


Kipimo cha HIV antibodi (HIV SD bioline )


Kipimo cha HIV 'antbodi' , hutumia kifaa cha HIV SD bioline. Kipimo hiki hutambua kemikali za kinga mwilini zenye jina la 'antibodi', ambazo huzalishwa na mwili ili kupambana na virusi vya UKIMWI. Kipimo hiki hufanyika kwenye vituo vya ushauri nasaha na hospitali au nyumbani. Huwa na uwezo wa kutambua maambukizi ya VVU kuanzia siku 23 hadi 90 baada ya kupata maambukizi. Kipimo hiki huwa na uwezo wa kutambua maambukizi kwa asilimia 95 hadi 99.


Kipimo cha HIV Unigold


Kipimo cha HIV unigold hutumiwa kuthibitisha majibu ya kipimo cha HIV SD bioline endapo kitaonyesha kuwa mtu ana maambukizi. Kipimo hiki kina uwezo wa kutambua maambukizi kwa asilimia 99.8. Kuna baadhi ya wataalamu wa afya hutumia kipimo cha Unigold moja kwa moja kupima maambukizi ya VVU.


Je kama ninawezaje kutambua maambukizi ndain ya masaa 24?


Mpaka sasa bado hakijagunduliwa kipimo kinachoweza kutambua maambukizi ya VVU ndani ya masaa 24. Kwa sababu ya ukuaji w atekinolojia, huenda hivi karibuni kipimo cha kutambua maambukizi ndani masaa machache kitagunduliwa.


Nini cha kufanya kama nahisi nimepata maambukizi ndani ya masaa 24?


Kama unahisi umepata maambukizi ndani ya masaa 24, licha ya kuwa huwezi kuthibitisha kwa kipimo, unapaswa kufika kituo cha kutolea huduma za afya au huduma kwa wtu wenye VVU kwa ushauri zaidi. Katika kituo unaweza kupewa dawa za kuzuia maambukizi zenye jina la PEP. Dawa za PEP hutolewa kwa watu waliojihatarisha ndani ya masaa 72. Ufanisi wa dawa huwa unapungua kwa jinsi muda unavyoongezeka, baada ya muda wa masaa 72 kupita huwa hakuna faida za kutumia daw ahiyo.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

19 Julai 2023, 20:41:55

Rejea za mada hii:

1. Estelle Piwowar-Manning, et al. Validation of Rapid HIV Antibody Tests in Five African Countries
.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2989535/. Imechukuliwa 30.01.2021

2.Eligius F Lyamuya et al. Evaluation of simple rapid HIV assays and development of national rapid HIV test algorithms in Dar es Salaam, Tanzania. https://bmcinfectdis.biomedcentral.com/articles/10.1186/1471-2334-9-19. Imechukuliwa 30.01.2021

3. Katie Huynh et al. HIV Testing. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK482145/. Imechukuliwa 30.01.2021

4. Margaret Fearon, MD FRCPC. The laboratory diagnosis of HIV infections. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2095005/. Imechukuliwa 30.01.2021

5. Bharat S. Parekh et al. Diagnosis of Human Immunodeficiency Virus Infection. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6302353/. Imechukuliwa 30.01.2021

6. WHO Recommendations on the Diagnosis of HIV Infection in Infants and Children. 5LABORATORY METHODS FOR DIAGNOSIS OF HIV INFECTION IN INFANTS AND CHILDREN. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK138552/. Imechukuliwa 30.01.2021

7. WHO Rapid HIV tests. https://www.who.int/hiv/pub/vct/en/Rapid%20Test%20Guide%20-%20FINAL.pdf. Imechukuliwa 30.01.2021

8. HIV ASSAYS - WHO . https://www.who.int/diagnostics_laboratory/publications/Report16_final.pdf. Imechukuliwa 30.01.2021

bottom of page