top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

5 Julai 2026, 11:31:25

Je, sehemu ya katikati ya nanasi ni salama wakati wa ujauzito?

Uchambuzi wa ushahidi wa kisayansi kuhusu bromelain, kizazi na uchungu

Utangulizi

Kwa miaka mingi kumekuwa na imani katika jamii mbalimbali duniani kwamba kula nanasi, hasa sehemu ya katikati ya tunda (shina la tunda), kunaweza kuanzisha uchungu wa kujifungua au hata kusababisha mimba kutoka. Imani hii imeonekana katika baadhi ya tamaduni za Asia, Afrika na Amerika Kusini, ambako nanasi limetumika katika tiba za asili kwa madhumuni mbalimbali yanayohusiana na afya ya uzazi.


Katika miaka ya hivi karibuni, mada hii imevutia watafiti kutokana na uwepo wa bromelain, kundi la vimeng'enya vinavyopatikana kwenye mmea wa nanasi-(Ananas comosus). Tafiti za maabara zimeonyesha kuwa baadhi ya viambato vya nanasi vinaweza kuathiri misuli ya kizazi na michakato ya kibaolojia inayohusika katika kuiva kwa mlango wa kizazi kutanuka kwa mlango wa kizazi). Hata hivyo, tafiti za binadamu bado ni chache, na ushahidi uliopo haujathibitisha kuwa kula nanasi kwa kiwango cha kawaida husababisha kuharibika kwa mimba.


Makala hii inachambua ushahidi wa kisayansi kutoka tafiti za maabara, tafiti za wanyama na tafiti za binadamu ili kueleza kile kinachojulikana kwa sasa kuhusu matumizi ya nanasi wakati wa ujauzito.


Nanasi lina viambato gani vinavyovutia watafiti?

Nanasi lina virutubisho vingi vinavyofaa kwa afya, ikiwemo vitamini C, manganizi, nyuzinyuzi, pamoja na misombo mbalimbali ya mimea. Miongoni mwa viambato vilivyochunguzwa zaidi ni bromelain, kundi la vimeng'enya vinavyovunja protini.


Bromelain hupatikana katika sehemu mbalimbali za mmea wa nanasi, lakini kiwango chake hutofautiana. Kwa ujumla, bromelain inayotolewa kutoka kwenye shina la mmea (bromelain ya shina) huwa na mkusanyiko mkubwa kuliko ile inayopatikana kwenye tunda linaloliwa. Hii ndiyo sababu bromelain ya matumizi ya dawa hutengenezwa kutoka kwenye shina la mmea badala ya tunda.


Mbali na bromelain, nanasi pia lina misombo mingine ya kibaolojia kama polyphenols, vitamini C na kiasi kidogo cha serotonin (5-hydroxytryptamine), ambacho kimekuwa kikichunguzwa kutokana na uwezo wake wa kuathiri misuli ya kizazi katika tafiti za maabara.


Kwa nini kuna imani kwamba nanasi linaweza kuathiri ujauzito?

Sababu kubwa ni matumizi yake katika tiba za asili kwa muda mrefu. Katika baadhi ya maeneo ya India, Bangladesh na nchi nyingine, nanasi limekuwa likitajwa katika maandiko ya ethnomedicine kama mmea uliotumiwa kwa madhumuni yanayohusiana na ujauzito na kujifungua.


Kutokana na matumizi hayo ya kitamaduni, watafiti waliamua kuchunguza kama kuna msingi wa kisayansi unaoweza kueleza imani hizi. Hapo ndipo zilipoanza tafiti za maabara zilizolenga kuchunguza athari za viambato vya nanasi kwenye misuli ya kizazi na tishu zinazohusika katika ujauzito.


Ni muhimu kutambua kuwa matumizi ya kitamaduni peke yake hayawezi kuthibitisha kuwa tiba fulani inafanya kazi. Ndiyo maana tafiti za maabara, tafiti za wanyama na tafiti za binadamu zinahitajika ili kuthibitisha au kukanusha madai hayo.


Tafiti za maabara zinasema nini?

Moja ya tafiti zilizochunguzwa sana ilichapishwa mwaka 2016 katika Journal of Ethnopharmacology. Watafiti walichunguza athari za sehemu inayoliwa ya nanasi kwenye misuli ya kizazi ya panya wajawazito pamoja na vipande vya misuli ya uterasi ya binadamu vilivyochunguzwa maabara.


Katika utafiti huo, baadhi ya sehemu za extract ya nanasi zilisababisha kuongezeka kwa nguvu za mikazo ya kizazi. Athari hiyo ilionekana kupungua baada ya kutumia dawa inayozuia vipokezi vya serotonin (5-HTâ‚‚A), jambo lililoashiria kuwa njia za serotonin zinaweza kushiriki katika athari hiyo.


Matokeo haya yanaonyesha kuwa baadhi ya viambato vya nanasi vina uwezo wa kuchochea misuli ya kizazi katika mazingira ya maabara. Hata hivyo, matokeo ya maabara hayawezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa mtu anayekula nanasi atapata athari sawa, kwa sababu kiwango cha viambato kinachofika mwilini baada ya kula chakula hutofautiana na kiwango kinachotumika kwenye majaribio ya maabara.


Je, bromelain ndiyo inayohusika?

Bromelain imekuwa ikichunguzwa kwa sababu ina uwezo wa kuvunja protini na kuathiri baadhi ya michakato ya uchochezi (inflamesheni). Watafiti wamependekeza kuwa uwezo huu unaweza kuwa na mchango katika mabadiliko ya tishu za mlango wa kizazi yanayotokea mwishoni mwa ujauzito.


Hata hivyo, bromelain si kiambato pekee kinachopatikana kwenye nanasi. Utafiti wa mwaka 2016 ulipendekeza kuwa misombo inayofanana na serotonin pia inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuchochea mikazo ya misuli ya kizazi. Hivyo, bado haijafahamika kwa uhakika ni kiambato gani kina mchango mkubwa zaidi katika athari zilizozingatiwa kwenye maabara.


Kwa sasa, watafiti wanaendelea kuchunguza iwapo bromelain, serotonin au mchanganyiko wa viambato mbalimbali vya nanasi ndiyo unaohusika zaidi na athari hizi.


Tafiti za wanyama zinaonyesha nini?

Baada ya tafiti za awali za ethnomedicine kuonyesha kuwa nanasi limekuwa likitumika katika baadhi ya jamii kwa madhumuni yanayohusiana na ujauzito, watafiti walifanya majaribio kwa wanyama ili kuchunguza kama kuna msingi wa kibaolojia wa madai hayo.


Baadhi ya tafiti za zamani zilionyesha kuwa viambato vilivyotolewa kutoka kwenye mmea wa nanasi vilipunguza idadi ya maeneo ya upandikizaji wa kijusi katika panya na panya-maabara. Tafiti nyingine pia zilionyesha kuwa extract za nanasi ziliweza kuathiri ukuaji wa viinitete katika mifano ya maabara kama zebrafish. Hata hivyo, matokeo haya hayakuwa ya aina moja; tafiti nyingine hazikuweza kurudia athari hizo, jambo linaloonyesha kuwa ushahidi bado haujakubaliana kikamilifu.


Ni muhimu kutambua kuwa matokeo ya tafiti za wanyama hayawezi kutafsiriwa moja kwa moja kwa binadamu. Dozi zinazotumika maabara mara nyingi huwa kubwa zaidi kuliko kiasi kinachopatikana kwa kula chakula cha kawaida, na pia kuna tofauti za kibaolojia kati ya spishi.


Ushahidi kuhusu kukaza kwa misuli ya kizazi

Utafiti uliochapishwa mwaka 2016 katika Journal of Ethnopharmacology uliweka msingi muhimu katika eneo hili. Watafiti walitengeneza extract kutoka sehemu inayoliwa ya nanasi na kuipima kwenye misuli ya kizazi ya panya wajawazito pamoja na myometrium ya binadamu katika mazingira ya maabara.


Waligundua kuwa sehemu ya maji ( F4) ilisababisha mikazo ya kizazi kwa namna inayoongezeka kadiri dozi ilivyoongezeka. Walipozuia vipokezi vya serotonin (5-HTâ‚‚A), nguvu ya mikazo ilipungua kwa kiasi kikubwa, jambo lililoonyesha kuwa mfumo wa serotonini unaweza kuwa sehemu muhimu ya utaratibu huo.


Matokeo haya yanaonyesha kuwa baadhi ya viambato vya nanasi vina uwezo wa kuchochea misuli ya kizazi katika maabara. Hata hivyo, haya ni matokeo ya maabara na hayatoshi peke yake kuthibitisha athari sawa kwa wanawake wanaokula nanasi wakati wa ujauzito.


Utafiti wa baadaye uliimarisha hoja hii

Mwaka 2018, kundi hilohilo la watafiti liliendelea kuchunguza utaratibu wa kibaolojia wa mikazo ya misuli ya kizazi ya nanasi-Ananas comosus. Walionyesha tena kuwa njia ya serotonini ina mchango mkubwa katika kuchochea mikazo ya kizazi, na walipanua ushahidi kwa kutumia majaribio ya maabara na baadhi ya mifano ya wanyama.


Kwa pamoja, tafiti hizi zinaongeza ushahidi kwamba nanasi lina viambato vinavyoweza kuathiri fiziolojia ya kizazi. Hata hivyo, bado hazijibu swali muhimu la kitabibu: je, kula nanasi kwa kiwango cha kawaida kuna athari sawa kwa mwanamke mjamzito?


Ushahidi wa binadamu kuhusu cervical ripening

Katika utafiti wa hivi karibuni wa kundi kubwa la wanawake nchini Nigeria, watafiti walichunguza uhusiano kati ya matumizi ya nanasi katika kipindi cha tatu cha ujauzito na matokeo ya kujifungua. Wanawake waliokuwa wakitumia nanasi mara kwa mara walikuwa na alama bora za alama za Bishop, walipata muda mfupi wa uchungu na walikuwa na uwezekano mkubwa wa kujifungua kwa njia ya kawaida kuliko wale ambao hawakutumia nanasi. Aidha, hakukuwa na tofauti kubwa katika afya ya watoto waliozaliwa kati ya makundi hayo.


Ingawa matokeo haya yanavutia, utafiti huu ulihusisha wanawake waliokuwa karibu kujifungua, si wanawake waliokuwa katika trimester ya kwanza ya ujauzito. Kwa hiyo, hauwezi kutumiwa kuthibitisha athari katika hatua za mwanzo za ujauzito.


Tafsiri ya ushahidi wa sasa

Kwa kuzingatia tafiti zote zilizopo, kuna ushahidi unaoongezeka kwamba baadhi ya viambato vya (nanasi) Ananas comosus vinaweza kuwa na shughuli za mikazo ya misuli ya kizazi katika maabara na vinaweza kuhusika katika michakato ya kutanuka kwa shingo ya kizazi. Ushahidi huu unatokana na tafiti za seli, tishu, wanyama na baadhi ya tafiti za uchunguzi kwa binadamu.


Hata hivyo, bado kuna pengo muhimu la ushahidi kuhusu athari za matumizi ya kawaida ya nanasi katika hatua za mwanzo za ujauzito. Tafiti za ubora wa juu kwa binadamu bado zinahitajika ili kubaini kama kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ulaji wa nanasi na matokeo ya ujauzito katika mazingira halisi ya kitabibu.


Wajawazito wanapaswa kufanya nini?

Kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi uliopo sasa, hakuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kwamba kula nanasi kwa kiasi cha kawaida husababisha kuharibika kwa mimba kwa binadamu. Hata hivyo, tafiti za maabara zimeonyesha kuwa baadhi ya viambato vya nanasi- Ananas comosus vina uwezo wa kuchochea misuli ya kizazi katika mazingira ya maabara na vinaweza kushiriki katika michakato ya kutanuka kwa shingo ya kizazi.


Kutokana na hali hiyo, ni busara kwa wanawake wajawazito kuepuka kutumia bidhaa zenye viwango vikubwa vya bromelain au kutumia nanasi kwa makusudi wakiamini kwamba linaweza kuanzisha uchungu au kubadilisha mwelekeo wa ujauzito. Badala yake, maamuzi yoyote yanayohusu ujauzito yanapaswa kufanywa kwa ushauri wa daktari au mtaalamu wa afya.


Ikiwa mjamzito atapata maumivu ya tumbo, kutokwa na damu ukeni, kupungua kwa harakati za mtoto au dalili nyingine zisizo za kawaida, anapaswa kufika kituo cha afya mara moja badala ya kutumia tiba za nyumbani.


Mapungufu ya ushahidi uliopo

Licha ya maendeleo ya tafiti kuhusu nanasi-Ananas comosus, bado kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa.

Kwanza, tafiti nyingi zimefanyika kwenye seli, tishu au wanyama, na matokeo hayo hayawezi kutafsiriwa moja kwa moja kwa binadamu. Pili, tafiti nyingi hazijapima kiasi halisi cha nanasi kinacholiwa, tofauti za aina za nanasi, au mkusanyiko wa bromelain na viambato vingine.


Aidha, bado hakuna tafiti kubwa za muda mrefu zinazoweza kueleza kwa uhakika kama kuna uhusiano wa kisababishi kati ya ulaji wa nanasi na matokeo ya ujauzito katika hatua za mwanzo. Hili linaonyesha umuhimu wa tafiti zaidi katika eneo hili.


Hitimisho

Ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa nanasi-Ananas comosus lina viambato vinavyoweza kuathiri misuli ya kizazi katika tafiti za maabara, na tafiti za hivi karibuni zimeonyesha uhusiano kati ya matumizi ya nanasi katika kipindi cha tatu cha ujauzito na kutanuka kwa mlango wa kizazi pamoja na muda mfupi wa uchungu wa kujifungua kwa binadamu. Hata hivyo, ushahidi wa moja kwa moja kwa binadamu kuhusu kuharibika kwa mimba(kutoa mimba) katika kipindi cha kwanza cha ujauzito kutokana na ulaji wa nanasi bado haujathibitishwa.


Kwa hiyo, wajawazito wanapaswa kutegemea ushauri wa wataalamu wa afya na kuepuka kufanya maamuzi kuhusu ujauzito kwa kuzingatia taarifa zisizothibitishwa.


Wakati huo huo, mwandishi anashauri kuwa kutokana na ushahidi mdogo uliopo, utumiaji wa nanasi hasa sehemu ya katikati kwa wingi unapaswa kuchukuliwa kwa umakini ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokana na kuwa na viambato vingi vinavyoweza kuanzisha/kuongeza mikazo ya misuli ya kizazi hasa katika kipindi cha mwanzo wa ujauzito.


Pia mwandishi anaita wanasayansi kufanya tafiti zenye ubora kwenye eneo hili ili kutatua kitendawili cha muda mrefu na kujibu maswali yaliyobakia.


Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara kuhusu nanasi(FAQ)

1. Je, mjamzito anaweza kula nanasi?

Ndiyo, kwa ujumla ulaji wa nanasi kama sehemu ya mlo wa kawaida haujaonyeshwa kusababisha madhara kwa ujauzito katika tafiti za binadamu. Kama ilivyo kwa vyakula vingine, ni vyema kula kwa kiasi na kuwa na mlo wenye uwiano wa virutubisho mbalimbali.

2. Bromelain ni nini?

Bromelain ni kundi la vimeng'enya vinavyopatikana kwenye mmea wa nanasi. Viwango vya juu zaidi hupatikana kwenye shina la mmea kuliko kwenye tunda. Bromelain imekuwa ikichunguzwa kwa matumizi mbalimbali ya kitabibu kutokana na uwezo wake wa kuvunja protini na kuathiri baadhi ya michakato ya uchochezi.

3. Kwa nini nanasi huhusishwa na uchungu wa kujifungua?

Imani hii imetokana na matumizi ya kitamaduni katika baadhi ya jamii na pia tafiti za maabara zilizoonyesha kuwa baadhi ya viambato vya nanasi vinaweza kuchochea misuli ya kizazi. Hata hivyo, ushahidi wa binadamu bado ni mdogo na haujathibitisha uhusiano wa moja kwa moja.

4. Je, kula nanasi kunaweza kuanzisha uchungu kwa mwanamke aliye karibu kujifungua?

Baadhi ya tafiti za uchunguzi zimeonyesha uhusiano kati ya matumizi ya nanasi katika trimester ya tatu na cervical ripening pamoja na muda mfupi wa uchungu. Hata hivyo, tafiti hizo hazijathibitisha kuwa nanasi ndilo lilisababisha mabadiliko hayo, hivyo utafiti zaidi bado unahitajika.

5. Je, bromelain ya virutubisho (supplements) ni sawa na bromelain ya kwenye tunda?

Hapana. Virutubisho vya bromelain huwa na mkusanyiko mkubwa zaidi wa kimeng'enya kuliko kiasi kinachopatikana kwenye tunda linaloliwa. Hii ndiyo sababu matumizi ya virutubisho hivyo yanapaswa kufanywa kwa ushauri wa mtaalamu wa afya.

6. Je, kuna tofauti kati ya sehemu ya katikati ya nanasi na sehemu nyingine za tunda?

Sehemu ya katikati huwa na nyuzinyuzi nyingi na inaweza kuwa na viwango tofauti vya baadhi ya viambato ikilinganishwa na nyama ya tunda, lakini bado ushahidi haujathibitisha kuwa ulaji wa sehemu hiyo una matokeo tofauti ya kitabibu kwa ujauzito.

7. Kwa nini tafiti za wanyama haziwezi kutumika moja kwa moja kwa binadamu?

Mwili wa binadamu na wa wanyama hutofautiana katika jinsi unavyomeng'enya na kutumia dawa au viambato vya mimea. Pia dozi zinazotumika maabara mara nyingi ni kubwa zaidi kuliko zile zinazopatikana kupitia chakula.

8. Je, ni lini mjamzito anapaswa kuwahi hospitali?

Mjamzito anapaswa kupata huduma za haraka endapo atapata kutokwa na damu ukeni, maumivu makali ya tumbo, kutoka kwa maji mengi ukeni, kupungua kwa harakati za mtoto au dalili nyingine zozote zinazomtia wasiwasi.

9. Je, kuna tafiti zaidi zinahitajika?

Ndiyo. Watafiti bado wanahitaji kufanya tafiti kubwa za ubora wa juu kwa binadamu ili kufafanua athari za viambato vya nanasi katika hatua mbalimbali za ujauzito na kubaini kama kuna uhusiano wa kisababishi.

10. Ujumbe muhimu kwa wajawazito ni upi?

Usifanye maamuzi kuhusu ujauzito kwa kutegemea taarifa za mitandao, simulizi au imani za kitamaduni pekee. Ikiwa una swali kuhusu chakula, dawa au kirutubisho wakati wa ujauzito, zungumza na daktari, mkunga au mtaalamu mwingine wa afya ili upate ushauri unaozingatia hali yako binafsi.


Imeandikwa:

4 Julai 2026, 14:43:53

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

​

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

bottom of page