Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Salamo A, MD
18 Julai 2026, 05:58:37

Kifafa kwa Watoto Wadogo: Mwongozo wa Kina
Kifafa ni hali ya neva inayosababisha mshtuko wa ghafla wa misuli na mabadiliko ya fahamu au tabia kutokana na shughuli isiyo ya kawaida ya umeme katika ubongo. Kifafa ni mojawapo ya magonjwa ya neva yanayoathiri watoto, na linaweza kuanza mapema katika maisha. Uelewa wa kifafa, dalili zake, sababu, na jinsi ya kumhudumia mtoto ni muhimu kwa familia na walezi.
Dalili za kifafa
Dalili zinatofautiana kulingana na aina ya kifafa. Dalili kuu ni pamoja na:
Mshtuko wa misuli
Mtoto anaanza kutikisika ghafla, mikono na miguu inachezacheza au kushambuliwa bila yeye mwenyewe kuweza kudhibiti.
Wakati mwingine mwili mzima hutetemeka, au ni sehemu ndogo tu kama mkono au mguu unaotikisika.
Kutowajibika au kutokuwa makini
Mtoto anakaa kimya na kuangalia tu kwa sekunde chache kana kwamba ameghafilika au amepotea mawazoni.
Anaweza kuacha kabisa kufanya anachofanya, mfano: anakula ghafla anasimama, au anaongea ghafla anakaa kimya.
Baada ya sekunde chache anarudi kawaida bila kujua kilichotokea.
Tabia zisizo za kawaida wakati wa kifafa
Mtoto anaweza kucheka bila sababu, kusogea mara kwa mara sehemu ileile, au kufanya harakati ndogo zisizo na maana mara kwa mara.
Wengine huonekana kama wanasogea midomo kana kwamba wanatafuna, au wanatikisa kichwa kwa kurudia rudia.
Dalili zinazoambatana na kifafa
Kutapika au kichefuchefu kabla ya kifafa.
Kutokuwepo kwa pumzi kwa muda mfupi.
Uchovu au usingizi mkubwa baada ya kifafa.
Visababishi vya kifafa kwa watoto
Sababu zinaweza kuwa nyingi na mara nyingi zinahusiana na maendeleo ya ubongo na historia ya familia. Kimsingi, zinajumuisha:
Visababishi vya kurithi
Vinasaba vinaweza kuongeza hatari ya kifafa.
Historia ya kifafa katika familia.
Uharibifu wa ubongo wa Awali
Ajali au jeraha la kichwa.
Ukosefu wa oksijeni wakati wa kuzaliwa.
Maambukizi na magonjwa ya ubongo
Meninjaitis, encephalaitis, au maambukizi mengine ya ubongo.
Mazingatio ya kemikali au Madhaifu ya umetaboli
Upungufu wa sukari mwilini (hypoglaisemia).
Upungufu wa madini muhimu kama kalsiamu na magnesium.
Sababu zisizojulikana
Kati ya watoto wenye kifafa, baadhi hawana sababu inayojulikana.
Vipimo na Uchunguzi
Uchunguzi wa kifafa unalenga kubaini aina ya kifafa na sababu yake. Vipimo vya kawaida ni:
Historia na Uchunguzi wa Kimatibabu
Historia ya kifafa na mambo yanayochochea.
Uchunguzi wa kuona dalili za mwili na maendeleo ya mtoto.
Electroencephalogram (EEG)
Kupima shughuli za umeme katika ubongo na kubaini aina ya kifafa.
Vipimo vya Imaging (CT/MRI)
Kubaini uharibifu wa ubongo au matatizo ya kimuundo.
Vipimo vya Damu
Kupima sukari, madini, na vipengele vya metabolism vinavyoweza kusababisha kifafa.
Matibabu
Matibabu yanayopendekezwa na madaktari ni pamoja na:
Dawa za Kifafa
Dawa kama carbamazepine, valproate, levetiracetam, au phenytoin.
Zinawekwa kulingana na aina ya kifafa na umri wa mtoto.
Upunguzaji wa sababu zinazoweza kubadilika
Kutibu maambukizi ya ubongo, upungufu wa madini, au matatizo ya metabolic.
Upasuaji wa ubongo
Kwa watoto wenye kifafa kisichoweza kudhibika kwa dawa na tatizo la kimuundo kwenye ubongo.
Huduza ya nyumbani
Huduma ya nyumbanihusaidia kudhibiti kifafa na kuzuia shambulio zaidi:
Jedwali 1: Matibabu ya Nyumbani kwa Mtoto Mwenye Kifafa
Hatua ya matibabu ya nyumbani | Maelezo ya kina | Namna ya kutekeleza kwa mtoto |
1. Kufuata dawa kila siku | Dawa za kifafa ni muhimu sana kudhibiti mashambulizi. Ikiwa mtoto hatapewa dawa kwa usahihi, kifafa kinaweza kurudi mara nyingi au kuwa kibaya zaidi. | - Mpe dawa kwa muda uliopangwa na usikose dozi. - Weka kumbukumbu ya kila dozi kwenye daftari au simu. - Usimpe dawa zaidi au pungufu bila ushauri wa daktari. |
2. Kuepuka vichocheo | Vichocheo kama kukosa usingizi, msongo wa mawazo, mwanga mkali unaorudia (mfano taa zinazowaka na kuzimika haraka), na kelele kubwa vinaweza kuamsha kifafa. | - Hakikisha mtoto analala masaa ya kutosha (8–10 kwa watoto wadogo). - Mpe mazingira tulivu ya kucheza na kujifunza. - Epuka michezo ya video yenye mwanga unaowaka haraka. - Mlee kwa utulivu bila kumkasirikia kupita kiasi. |
3. Lishe bora | Lishe sahihi husaidia ubongo kufanya kazi vizuri na kupunguza mashambulizi ya kifafa. Madini na vitamini fulani (calcium, magnesium, vitamini B6) ni muhimu. | - Mpe chakula chenye mboga za majani, matunda, samaki, maziwa, maharagwe, na mayai. - Epuka kumpa vyakula vya sukari nyingi kupita kiasi au vyakula vya mafuta yasiyo na afya. - Kwa baadhi ya watoto, daktari anaweza kupendekeza lishe maalum (kama ketogenic diet). |
4. Kutunza historia ya kifafa | Kumbukumbu sahihi husaidia daktari kufuatilia maendeleo na kubadilisha dawa au matibabu inapohitajika. | - Andika tarehe na saa ya kila kifafa. - Eleza dalili zilizoonekana (mfano: kutetemeka, kuangalia tu, au kucheka bila sababu). - Andika muda kifafa kilichodumu na hali ya mtoto baada ya kifafa. |
Hudumia mtoto wakati wa Kifafa
Jedwali 2: Namna ya Kumhudumia Mtoto Wakati wa Kifafa
Hatua ya huduma | Maelezo rahisi | Jinsi ya Kutekeleza |
1. Usiogope | Kifafa mara nyingi hakidumu muda mrefu (dakika chache tu). Hofu inaweza kufanya mzazi ashindwe kumsaidia mtoto. | Tulia, pumua kwa kina, na zingatia hatua zinazofuata. |
2. Usimshike au kumkandamiza | Kushikilia kwa nguvu au kumkandamiza mtoto wakati anatetemeka kunaweza kumuumiza zaidi. | Acha mwili wake utembee wenyewe, usishikilie mikono au miguu. |
3. Mweke sehemu salama | Mtoto anaweza kujeruhiwa akipiga vitu vya karibu. | Ondoa viti, meza, au vyombo vyenye ncha kali vilivyo karibu. |
4. Mweke chini | Ni salama mtoto akiwa chini kuliko akiwa amesimama au kukaa juu. | Mweke kitandani, kwenye mkeka au sakafuni taratibu. |
5. Laza kichwa upande | Hii huzuia mate au chakula kuingia kwenye koo na kusaidia kupumua. | Geuza kichwa chake upande mmoja kwa upole. |
6. Usimweke kulala chali (mgongo) | Mtoto akilala chali, kuna hatari ya kukosa pumzi endapo atatapika. | Hakikisha kichwa kiko upande mmoja. |
7. Usimpe kitu mdomoni | Kumpa dawa, chakula au kuingiza kitu mdomoni kunaweza kuziba njia ya hewa au kujeruhi meno. | Subiri kifafa kipite ndipo utakapompa maji au dawa. |
8. Usiache mtoto peke yake | Mtoto anahitaji uangalizi mpaka kifafa kimalizike. | Kaa karibu naye hadi atakapopata nafuu. |
9. Rekodi muda wa kifafa | Daktari anahitaji kujua muda wa kifafa. Kifafa kikiendelea zaidi ya dakika 5–10 ni hatari. | Angalia saa au simu kuhesabu muda. Ikiwa kinaendelea zaidi ya dakika 5, mwite daktari au peleka hospitali haraka. |
Baada ya kifafa kupita
Acha mtoto apumzike – Kawaida watoto huishiwa nguvu na wanahitaji usingizi.
Uangalizi wa kawaida- Angalia kama kuna jeraha, kichefuchefu, au hali nyingine isiyo ya kawaida.
Himiza mtoto Kunywa maji – Ili kusaidia kuimarisha mwili.
Eleza kwa mtoto (Ikiwa anaelewa) – Kumsaidia kuelewa ni nini kilitokea na kuondoa hofu.
Rekodi tukio – Muda, tabia, na dalili baada ya kifafa ili kumsaidia daktari kuboresha matibabu.
Hitimisho
Kifafa kwa watoto wadogo ni hali ya kawaida inayohitaji uangalizi wa kitaalamu na nyumbani. Uelewa wa dalili, visababishi, vipimo, na matibabu (kawaida na nyumbani) ni muhimu. Kumhudumia mtoto kwa usahihi wakati wa kifafa na baada yake husaidia kupunguza hatari na kuongeza ustawi wa mtoto.
Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)
1. Je, mtoto akipata kifafa mara moja tu ina maana ana ugonjwa wa kifafa?
Hapana. Mtoto kupata kifafa mara moja hakumaanishi moja kwa moja kuwa ana ugonjwa wa kifafa. Baadhi ya watoto hupata mshtuko unaosababishwa na homa kali (febrile seizure), upungufu wa sukari mwilini, maambukizi, au sababu nyingine zinazoweza kutibika. Katika hali hizi, mtoto anaweza asipate tena kifafa baada ya sababu hiyo kuondolewa.
Madaktari husema mtoto ana ugonjwa wa kifafa pale anapopata mashambulizi ya kifafa yanayojirudia bila sababu ya muda mfupi inayoweza kueleza tukio hilo. Ili kuthibitisha hali hiyo, mtoto anaweza kuhitaji vipimo kama EEG, CT scan au MRI kulingana na ushauri wa daktari.
Ikiwa mtoto amepata kifafa kwa mara ya kwanza, ni muhimu kufika hospitalini kwa uchunguzi ili kubaini chanzo na kuamua kama anahitaji matibabu au ufuatiliaji zaidi.
2. Kifafa kwa watoto kinaweza kupona kabisa?
Watoto wengi wenye kifafa wanaweza kuishi maisha ya kawaida ikiwa watapata matibabu sahihi na kufuatiliwa vizuri. Kwa baadhi ya watoto, kifafa hupungua kadiri wanavyokua, na baada ya miaka kadhaa bila mashambulizi, daktari anaweza kuamua kupunguza au kusitisha dawa taratibu.
Kwa watoto wengine, kifafa kinaweza kuendelea kwa muda mrefu na kuhitaji matumizi ya dawa kwa miaka kadhaa au maisha yote. Hii hutegemea aina ya kifafa, sababu yake, na jinsi mtoto anavyoitikia matibabu.
Ni muhimu kutokukatisha dawa bila ushauri wa daktari hata kama mtoto hajapata kifafa kwa muda mrefu, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kusababisha mashambulizi kurudi.
3. Je, kifafa kinaweza kuathiri maendeleo ya mtoto?
Watoto wengi wenye kifafa hukua na kuendelea vizuri, hasa ikiwa mashambulizi yanadhibitiwa mapema na matibabu yanafuatwa ipasavyo. Hata hivyo, mashambulizi ya mara kwa mara au yanayodumu kwa muda mrefu yanaweza kuathiri uwezo wa mtoto kujifunza, kuzungumza au kuzingatia masomo.
Baadhi ya watoto pia wanaweza kupata changamoto za kitabia, kumbukumbu au maendeleo ya lugha kulingana na sehemu ya ubongo iliyoathirika. Hii ndiyo sababu ufuatiliaji wa maendeleo ya mtoto ni muhimu.
Ikiwa mzazi ataona mtoto anachelewa kukaa, kutambaa, kutembea au kuzungumza ikilinganishwa na watoto wa umri wake, anapaswa kumjulisha daktari ili afanyiwe tathmini mapema.
4. Je, mtoto mwenye kifafa anaweza kucheza na kwenda shule kama watoto wengine?
Ndiyo. Watoto wengi wenye kifafa wanaweza kucheza, kujifunza na kushiriki shughuli mbalimbali kama watoto wengine, mradi kifafa kinadhibitiwa vizuri. Michezo na shughuli za kawaida husaidia ukuaji wa mtoto na kuimarisha afya yake.
Hata hivyo, ni muhimu kuchukua tahadhari katika shughuli zinazoweza kuwa hatari ikiwa kifafa kitatokea ghafla, kama kuogelea peke yake, kupanda sehemu za juu au kucheza karibu na moto.
Walimu na walezi wanapaswa kufahamu hali ya mtoto na kujua namna ya kumsaidia endapo atapata kifafa akiwa shuleni.
5. Je, homa inaweza kusababisha degedege kwa watoto?
Ndiyo. Watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miaka 5 wanaweza kupata degedege la homa wakati joto la mwili linapopanda haraka kutokana na maambukizi. Hii ni hali inayowapata baadhi ya watoto na mara nyingi si dalili ya ugonjwa wa kifafa wa kudumu.
Kifafa cha homa kwa kawaida hudumu kwa dakika chache na mtoto hurudi katika hali yake ya kawaida baada ya muda mfupi. Hata hivyo, mtoto anapaswa kupelekwa hospitalini ili kubaini chanzo cha homa na kuhakikisha hakuna tatizo jingine.
Ikiwa kifafa kinadumu zaidi ya dakika tano, kinajirudia ndani ya saa 24, au mtoto ana umri chini ya miezi sita, anahitaji huduma ya haraka ya kitabibu.
6. Je, mtoto mwenye kifafa anatakiwa kutumia dawa kwa muda gani?
Muda wa matumizi ya dawa hutegemea aina ya kifafa, umri wa mtoto, na jinsi anavyoitikia matibabu. Baadhi ya watoto hutumia dawa kwa miaka miwili hadi mitano kabla ya daktari kutathmini kama zinaweza kusimamishwa.
Wakati wa matibabu, ni muhimu mtoto kutumia dawa kila siku kama alivyoelekezwa. Kukosa dozi kunaweza kuongeza hatari ya kupata mashambulizi mengine.
Usiache dawa kwa hiari hata kama mtoto ameonekana kupona. Uamuzi wa kusitisha dawa unapaswa kufanywa na daktari baada ya tathmini ya kina.
7. Ni lini mtoto mwenye kifafa anatakiwa kupelekwa hospitali haraka?
Mtoto anatakiwa kupelekwa hospitali haraka ikiwa kifafa kinadumu zaidi ya dakika tano, anapata kifafa kingine kabla hajapata fahamu, anapata shida ya kupumua, au amejeruhiwa wakati wa kifafa.
Pia mtoto anahitaji huduma ya haraka ikiwa ni mara yake ya kwanza kupata kifafa, kifafa kimetokea baada ya kuanguka au kupata jeraha la kichwa, au ana homa kali inayoshukiwa kutokana na maambukizi makubwa.
Kupata matibabu mapema kunaweza kuzuia madhara makubwa na kusaidia kubaini chanzo cha kifafa.
8. Je, mtoto mwenye kifafa anaweza kupata chanjo zote?
Ndiyo. Watoto wengi wenye kifafa wanapaswa kuendelea kupata chanjo zote za kawaida kulingana na ratiba ya taifa. Chanjo husaidia kuzuia magonjwa ambayo yanaweza kusababisha homa kali na kuongeza hatari ya kifafa.
Kwa watoto wachache wenye matatizo maalumu ya mfumo wa kinga au magonjwa mengine ya neva, daktari anaweza kutoa ushauri wa ziada kuhusu chanjo fulani.
Mzazi hapaswi kuacha chanjo kwa sababu tu mtoto ana kifafa bila kushauriana na daktari.
9. Je, kifafa kinaweza kurithiwa kutoka kwa wazazi?
Ndiyo. Baadhi ya aina za kifafa zina uhusiano na vinasaba, hivyo historia ya kifafa katika familia inaweza kuongeza hatari ya mtoto kupata hali hiyo.
Hata hivyo, watoto wengi wenye kifafa hawana ndugu wala wazazi wenye ugonjwa huo. Vivyo hivyo, kuwa na mzazi mwenye kifafa hakumaanishi lazima mtoto atapata kifafa.
Daktari anaweza kuhitaji kujua historia ya kifafa katika familia ili kusaidia kubaini aina ya kifafa na kupanga matibabu yanayofaa.
10. Je, mtoto akipata kifafa akiwa amelala nifanye nini?
Ikiwa mtoto anapata kifafa akiwa amelala, jambo la kwanza ni kuhakikisha njia yake ya hewa iko wazi na kumgeuza upande mmoja ili mate au matapishi yasimzibe koo.
Usimtikise, usimshike kwa nguvu, wala usiweke kitu chochote mdomoni. Angalia muda kifafa kinachukua na hakikisha hakuna vitu vinavyoweza kumuumiza karibu naye.
Baada ya kifafa kuisha, mwache apumzike na mpeleke hospitali ikiwa kifafa kimedumu zaidi ya dakika tano, kimerudia, au kuna dalili nyingine zisizo za kawaida.
11. Mtoto wangu ana miezi miwili. Juzi ghafla mwili ulikakamaa na kujikunja kwa dakika kadhaa, halafu hali hiyo ikamuachia. Shida inaweza kuwa ni nini?
Kwa mtoto mwenye umri wa miezi miwili, mwili kukakamaa na kujikunja ghafla si jambo la kawaida na kunahitaji uchunguzi wa haraka wa daktari. Hali hii inaweza kusababishwa na kifafa, lakini pia inaweza kutokana na matatizo mengine kama upungufu wa sukari mwilini, upungufu wa madini kama kalsiamu, maambukizi makubwa, matatizo ya ubongo, au aina fulani za mshtuko wa watoto wachanga. Kwa sababu mtoto bado ni mdogo sana, ni muhimu kutofanya hitimisho bila uchunguzi wa kitaalamu.
Ikiwa tukio lilidumu kwa dakika kadhaa, lilihusisha mwili kukakamaa au kujikunja, macho kubadilika, mtoto kushindwa kuitikia, au kupumua kwa shida, anapaswa kufikishwa hospitalini haraka hata kama sasa anaonekana kuwa mzima. Daktari anaweza kupendekeza vipimo kama EEG, vipimo vya damu vya sukari na madini, pamoja na uchunguzi wa ubongo ikiwa utahitajika.
Usisubiri tukio lijirudie kabla ya kutafuta matibabu. Watoto walio chini ya miezi mitatu wanaopata mshtuko au mwili kukakamaa wanahitaji kutathminiwa mapema ili kubaini chanzo na kuanza matibabu yanayofaa. Uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kuzuia madhara ya muda mrefu na kuboresha afya ya mtoto.
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 16:07:21
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:
Berg AT, Berkovic SF, Brodie MJ, Buchhalter J, Cross JH, van Emde Boas W, et al. Revised terminology and concepts for organization of seizures and epilepsies: Report of the ILAE Commission on Classification and Terminology, 2005–2009. Epilepsia. 2010;51(4):676–85.
World Health Organization. Epilepsy. Geneva: WHO; 2019. Available from: https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/epilepsy
Camfield P, Camfield C. Epidemiology of epilepsy in children. Epileptic Disord. 2015;17(2):110–8.
Shinnar S, Pellock JM. Update on the epidemiology and prognosis of pediatric epilepsy. J Child Neurol. 2002;17(Suppl 1):S4–S17.
National Institute for Health and Care Excellence (NICE). Epilepsies: diagnosis and management. London: NICE; 2022. Available from: https://www.nice.org.uk/guidance/ng217
Fisher RS, Acevedo C, Arzimanoglou A, Bogacz A, Cross JH, Elger CE, et al. ILAE official report: a practical clinical definition of epilepsy. Epilepsia. 2014;55(4):475–82.
Vining EP, Freeman JM, Pillas DJ, Pyzik PL, Casey JC, Kelly LM. Clinical efficacy of the ketogenic diet. Neurology. 1998;50(4):1072–6.
Pellock JM, Nordli DR, Bourgeois B. Pediatric epilepsy: diagnosis and therapy. Pediatr Clin North Am. 2002;49(4):799–823.
Negrão AB, Sander JW, Shorvon SD. Epilepsy in childhood: clinical aspects and management. Lancet. 1992;339(8796):785–9.
Fisher RS, Cross JH, French JA, Higurashi N, Hirsch E, Jansen FE, et al. Operational classification of seizure types by the International League Against Epilepsy: Position paper of the ILAE. Epilepsia. 2017;58(4):522–30.
