top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Madaktari wa ULY CLINIC

Dkt. Lugonda S, MD

26 Juni 2026, 12:47:27

Sekunde chache za kushika kipimo: Je, Quantum Analyzer Inaona Magonjwa Mengi au ni Madai Tu?

Je, Mashine za "Quantum Analyzer" zinazoshikwa kwa mkono zinaweza kugundua mamia ya magonjwa? Ukweli wa kisayansi

Utangulizi

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mashine zinazodai kupima afya kwa kumshikiza mtu kifaa mkononi kwa dakika chache tu. Mashine hizi hujulikana kwa majina kama Quantum Analyzer, Quantum Resonance Magnetic Analyzer (QRMA), Bioresonance Scanner, na majina mengine yanayofanana.


Watengenezaji wake hudai kuwa zinaweza kugundua mamia ya magonjwa ndani ya dakika 1 hadi 5 bila kuchukua damu, mkojo au kufanya vipimo vingine vya hospitali.


Lakini je, madai haya yanaungwa mkono na ushahidi wa kisayansi?

Kwa sasa, hakuna ushahidi wa kisayansi wa kiwango cha juu unaothibitisha kuwa mashine hizi zinaweza kugundua mamia ya magonjwa kwa usahihi kwa kumshikiza mtu sensa mkononi kwa dakika chache tu.


Mashine hizi hudai kugundua nini?

Kwa kawaida matangazo ya mashine hizi hudai zinaweza kugundua:

  • Magonjwa ya moyo

  • Magonjwa ya ini

  • Magonjwa ya figo

  • Kisukari

  • Saratani

  • Matatizo ya homoni

  • Upungufu wa vitamini

  • Upungufu wa madini mwilini

  • Aleji

  • Kutovumilia vyakula fulani

  • Sumu za metali nzito

  • Magonjwa ya kinga ya mwili

  • Magonjwa ya mifupa

  • Magonjwa ya mfumo wa chakula

  • Na hata mamia ya magonjwa mengine


Baadhi ya matangazo hudai mashine hizi zina usahihi wa asilimia 90 hadi 95. Hata hivyo, madai hayo hayajaungwa mkono na tafiti kubwa za kisayansi zilizofanywa kwa kujitegemea.


Vipimo vya hospitali kinakubalika vipi kisayansi?

Kabla kipimo chochote hakijaanza kutumika hospitalini, lazima kifanyiwe tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa kinaaminika.

Kwa kawaida watafiti huangalia kama kipimo:

  • Kinaeleweka kisayansi jinsi kinavyofanya kazi.

  • Kikifanywa mara nyingi kinatoa matokeo yanayofanana.

  • Kinaweza kugundua wagonjwa kweli.

  • Kinaweza kutambua watu wasiokuwa na ugonjwa.

  • Kimelinganishwa na vipimo vinavyoaminika tayari.

  • Kimehakikiwa na watafiti wengine tofauti.

  • Kinaweza kusaidia madaktari kufanya maamuzi sahihi.


Vipimo kama:

  • CBC

  • HbA1c

  • ECG

  • Ultrasound

  • CT Scan

  • MRI

  • Biopsy

vimepitia hatua zote hizi kwa miaka mingi kabla ya kutumika kwa wagonjwa. Kwa upande mwingine, mashine nyingi za Quantum Analyzer hazina ushahidi wa kiwango hiki unaothibitisha madai yake makubwa.


Tafiti za kisayansi zinasema nini kuhusu vipimo vya aina hii?

Kwanza ni muhimu kuelewa kuwa Quantum Analyzer (QA) siyo kifaa cha Kipimo cha Mchakato wa Umeme kwenye Ngozi (Electrodermal Activity - EDA). Hizi ni teknolojia tofauti.


EDA ni kipimo halisi kinachotumiwa na watafiti na baadhi ya wataalamu wa afya kupima mabadiliko madogo ya umeme kwenye ngozi. Mabadiliko haya hutokana hasa na kutokwa na jasho na kazi ya mfumo wa neva unaojiendesha wenyewe (autonomic nervous system). Kwa sababu hiyo, EDA hutumika katika tafiti za msongo wa mawazo, usingizi, hisia za binadamu, uchovu na baadhi ya tafiti za mfumo wa neva.

Kwa upande mwingine, QA ni kifaa cha kibiashara kinachodai kugundua mamia ya magonjwa kwa kumshikiza mtu sensor mkononi kwa dakika chache. Watengenezaji wake hutaja maneno kama "quantum", "bioresonance" au wakati mwingine ishara za umeme wa mwili, lakini madai hayo hayajathibitishwa na ushahidi wa kutosha wa kisayansi.


Hadi sasa, hakuna tafiti kubwa, huru na zenye ubora wa juu zilizolinganisha QA na vipimo vinavyokubalika hospitalini (gold standards) na kuonyesha kuwa inaweza kugundua magonjwa kwa usahihi unaoweza kutegemewa. Ndiyo maana haijakubalika kama mbadala wa vipimo vya kawaida vya hospitali.

Baadhi ya tafiti ndogo zimechunguza teknolojia zinazohusiana na upimaji wa umeme wa ngozi au bioresonance. Hata hivyo, tafiti hizo hazijathibitisha kuwa teknolojia hizo zinaweza kugundua mamia ya magonjwa kama inavyodaiwa na baadhi ya mashine za QA. Kwa mfano, tafiti za EDA zinaonyesha kuwa teknolojia hiyo inaweza kutumika kupima msongo wa mawazo, hisia, uchovu na shughuli za mfumo wa neva, lakini haijathibitishwa kutambua saratani, kisukari, magonjwa ya figo, magonjwa ya ini, upungufu wa vitamini au magonjwa mengine mengi.


Kwa sababu hiyo, mashirika ya afya na miongozo ya matibabu bado hayajaikubali QA kama kifaa cha kutambua magonjwa au kuchukua nafasi ya vipimo vinavyotumika hospitalini.


Kwa nini mashine hizi za QA hutiliwa shaka?

Tatizo kubwa si kwamba zinatumia teknolojia ya kupima umeme wa ngozi. Tatizo ni kwamba zinadai kutoa taarifa ambazo hazijathibitishwa kisayansi.

Kwa mfano, mtu akishika sensa mkononi kwa dakika chache, mashine inaweza kutoa taarifa kuwa ana:

  • upungufu wa vitamini

  • ugonjwa wa ini

  • matatizo ya homoni

  • aleji

  • matatizo ya figo

  • saratani

  • U.T.I

  • P.I.D

  • vidonda vya tumbo

lakini hakuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa taarifa hizo zinaweza kupatikana kwa usahihi kupitia umeme wa ngozi pekee.


Kwa nini haiwezekani kugundua kila ugonjwa kwa kushika sensa?

Kila ugonjwa una njia tofauti ya kugunduliwa. Kwa mfano:


Saratani

Mara nyingi huhitaji:

  • Bayopsi

  • Vipimo vya maabara

  • CT Scan

  • MRI

  • Vipimo vya vinasaba (molecular tests)


Kisukari

Hugunduliwa kwa:

  • Kipimo cha sukari kwenye damu

  • HbA1c


Magonjwa ya figo

Huhitaji:

  • Creatinine

  • eGFR

  • Kipimo cha mkojo


Magonjwa ya ini

Huhitaji:

  • Kipimo cha damu cha utendaji kazi wa Ini

  • Bilirubin

  • Ultrasound au CT Scan


Upungufu wa vitamini

Huthibitishwa kwa vipimo vya damu.


Kwa sasa hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa taarifa zote hizi zinaweza kupatikana kwa kupima umeme wa ngozi kwa dakika chache.


Je, zipo mashine zisizochoma sindano zinazofanya kazi kweli?

Ndiyo lakini kila moja imeundwa kwa kazi maalumu. Mfano:

  • ECG hupima matatizo ya mpigo wa moyo.

  • Ultrasound huonyesha viungo vya ndani ya mwili.

  • Pulse Oximeter hupima kiwango cha oksijeni kwenye damu.

  • Retinal skana hutumika kuchunguza baadhi ya matatizo ya macho kwa wagonjwa wa kisukari.

  • Kichakataji cha pumzi bado inafanyiwa tafiti kwa magonjwa maalumu.

Hakuna kati ya vifaa hivi kinachodai kugundua mamia ya magonjwa kwa wakati mmoja.


Je, tafiti zote zinakataa kabisa teknolojia hii ya QA?

La. Baadhi ya tafiti ndogo zimeonyesha matokeo mazuri katika matumizi maalumu ya EDA.

Lakini tafiti hizo:

  • zilikuwa na washiriki wachache

  • zilichunguza magonjwa maalumu

  • hazijarudiwa na watafiti wengi kwa matokeo yanayofanana

  • hazijabadilisha miongozo ya matibabu duniani

Katika tiba, tafiti chache zenye matokeo mazuri hazitoshi kuthibitisha kipimo kipya.

Madaktari hutegemea ushahidi unaotokana na tafiti nyingi zilizofanywa katika mazingira tofauti.


Hatari za kutegemea mashine hizi za QA

Kutegemea mashine ambayo haijathibitishwa kunaweza kusababisha:

  • Kuambiwa uko salama wakati una ugonjwa mkubwa.

  • Kuambiwa una ugonjwa ambao huna.

  • Hofu isiyo ya lazima.

  • Kuchelewa kupata matibabu sahihi.

  • Kupoteza fedha kwa kununua dawa au virutubisho usivyohitaji.

  • Kukosa nafasi ya kugundua ugonjwa mapema kwa kutumia vipimo vinavyoaminika.


Mlinganisho wa vipimo vya hospitali na QA

Kipengele

Vipimo vya hospitali

Vipimo vya Quantum Analyzer

Vimehakikiwa kisayansi

Ndiyo

Mara nyingi hapana

Hutumika hospitalini

Ndiyo

Kwa ujumla hapana

Vinatambuliwa kwenye miongozo ya matibabu ya kisasa

Ndiyo

Hapana

Vina ushahidi kutoka tafiti nyingi

Ndiyo

Ushahidi ni mdogo au haupo

Vinategemea vipimo halisi vya mwili

Ndiyo

Mara nyingi hapana

Vinagundua mamia ya magonjwa kwa wakati mmoja

Hapana

Hivyo ndivyo vinavyodai, lakini haijathibitishwa kisayansi


Mlinganisho wa Quantum Analyzer na vipimo vinavyokubalika hospitalini

Ugonjwa/Hali

Kipimo kinachokubalika hospitalini

Je, Quantum Analyzer imethibitishwa kisayansi kugundua ugonjwa huo?

Kisukari

Sukari ya damu, HbA1c

Hapana. Hakuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi unaothibitisha uwezo wake wa kugundua kisukari kwa usahihi.

Magonjwa ya ini

Kipimo cha utendaji kazi wa INi (ALT, AST), Bilirubin, Ultrasound

Hapana. Hakuna tafiti kubwa zinazothibitisha kuwa inaweza kuchukua nafasi ya vipimo hivi.

Magonjwa ya figo

Creatinine, eGFR, kipimo cha mkojo

Hapana. Hakuna ushahidi unaokubalika wa uwezo wake wa kugundua magonjwa ya figo.

Saratani

Biopsy, CT Scan, MRI, Ultrasound na vipimo vingine maalumu

Hapana. Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa inaweza kugundua au kuthibitisha saratani.

Upungufu wa vitamini

Vipimo vya damu vya vitamini husika

Hapana. Vipimo vya damu ndiyo njia inayokubalika kuthibitisha upungufu wa vitamini.

Upungufu wa madini mwilini

Vipimo vya damu

Hapana. Hakuna ushahidi wa kutosha unaounga mkono madai hayo.

Aleji

Skin Prick Test, IgE Maalumu Kipimo cha Damu

Hapana. Mashine hizi hazijathibitishwa kuwa mbadala wa vipimo vya aleji.

Magonjwa ya moyo

ECG, Echocardiografia Troponin na vipimo vingine

Hapana. Hakuna ushahidi kuwa zinaweza kugundua matatizo ya moyo kwa usahihi unaokubalika.

Maambukizi

Vipimo vya damu, mkojo, uoteshaji wa vimelea (culture), PCR na vingine

Hapana. Hakuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha uwezo huo.

Magonjwa ya mifupa

X-ray, CT Scan, MRI, Uchunguzi wa ujazo wa mifupa

Hapana. Hakuna ushahidi kuwa Quantum Analyzer inaweza kugundua magonjwa ya mifupa kwa usahihi.


Hitimisho la Mwandishi

Kwa mujibu wa ushahidi wa kisayansi uliopo kwa sasa, hakuna uthibitisho wa kutosha unaoonyesha kuwa Quantum Analyzer inaweza kuchukua nafasi ya vipimo vinavyotumika hospitalini katika kutambua magonjwa. Ikiwa mashine hii itatoa matokeo yanayoonyesha una ugonjwa, ni muhimu kuyathibitisha hospitalini kwa uchunguzi wa daktari na vipimo vinavyokubalika kabla ya kuanza kutumia dawa au matibabu yoyote. Hii husaidia kuepuka matumizi ya dawa zisizo sahihi na kuchelewa kugundua ugonjwa halisi.


Hata hivyo, historia ya tiba inaonyesha kuwa teknolojia nyingi zilianza kama mawazo mapya na baadaye zikaboreshwa kupitia tafiti za kina. Endapo teknolojia za aina hii zitafanyiwa utafiti mkubwa wa kujitegemea, zikaboreshwa na kuthibitishwa kisayansi kuwa ni sahihi, zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho la uchunguzi wa magonjwa katika siku zijazo. Mpaka ushahidi huo utakapopatikana, matumizi yake yanapaswa kuwa ya tahadhari na yasichukue nafasi ya vipimo vya kawaida vya hospitali.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu mashine za quantum kupima magonjwa mengi

1. Kama matokeo ya mashine ya QA yalifanana na dalili zangu, je, hiyo inaonyesha kuwa mashine ni sahihi?

Si lazima. Ripoti nyingi zinazotolewa na mashine hizi huwa na maelezo ya jumla kama vile "upungufu wa vitamini", "kinga ya mwili imepungua", "matatizo ya mfumo wa chakula" au "mwili una sumu". Haya ni mambo ambayo yanaweza kuonekana kwa watu wengi, hivyo ni rahisi mtu kuhisi kuwa ripoti hiyo inamhusu.


Pia, kuna hali inayoitwa upendeleo wa uthibitisho, ambapo mtu hukumbuka taarifa zilizolingana na hali yake lakini husahau taarifa nyingi ambazo hazikuwa sahihi. Kwa mfano, mashine inaweza kutoa matokeo 40, lakini mtu akazingatia matokeo mawili yaliyofanana na dalili zake na kupuuza mengine yote.


Katika tiba, usahihi wa kipimo hauamuliwi na mfano mmoja wa mtu mmoja. Kipimo kinakubalika tu baada ya kufanyiwa tafiti kubwa zinazohusisha watu wengi na kulinganishwa na vipimo vinavyoaminika hospitalini. Hadi sasa, mashine nyingi za aina hii hazijathibitishwa kwa kiwango hicho.

2. Kwa nini baadhi ya watu wanasema mashine hizi za QA ziliwasaidia?

Watu wanaweza kuwa na uzoefu tofauti. Baadhi wanaweza kuhisi walisaidika kwa sababu baadaye waligunduliwa kweli kuwa na ugonjwa fulani. Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa mashine ndiyo iligundua ugonjwa huo kwa usahihi.


Pia kuna athari inayoitwa plasebo, ambapo mtu huhisi hali yake imeimarika kwa sababu anaamini amepata huduma nzuri au matibabu mazuri, hata kama huduma hiyo haikuwa sababu halisi ya kupona. Aidha, baadhi ya magonjwa hubadilika yenyewe au dalili hupungua bila kuhusiana na mashine iliyotumika.


Ndiyo maana sayansi haitumii ushuhuda wa mtu mmoja kuthibitisha kifaa cha tiba. Badala yake, hutegemea tafiti kubwa zinazofanywa kwa njia zinazopunguza upendeleo na makosa ili kujua kama kifaa kinafanya kazi kweli.

3. Je, mashine hizi za QA zimeidhinishwa kuchukua nafasi ya vipimo vya hospitali?

Kwa sasa, jibu ni hapana. Hakuna ushahidi wa kisayansi unaokubalika unaoonyesha kuwa mashine hizi zinaweza kuchukua nafasi ya vipimo vya damu, mkojo, picha za uchunguzi kama Ultrasound, CT Scan au MRI, pamoja na uchunguzi wa daktari.


Madaktari hutumia vipimo tofauti kwa sababu kila ugonjwa una njia yake ya kuthibitishwa. Kwa mfano, kisukari hupimwa kwa sukari ya damu na HbA1c, wakati saratani mara nyingi huhitaji biopsy na vipimo vya maabara.


Ikiwa mashine ya aina hii itatoa matokeo yanayoonyesha una ugonjwa mkubwa, matokeo hayo yanapaswa kuthibitishwa kwa vipimo vinavyotumika hospitalini kabla ya kuanza matibabu yoyote.

4. Je, mashine hizi za QA zinaweza kugundua saratani mapema?

Kwa sasa hakuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa mashine zinazoshikwa mkononi zinaweza kugundua saratani kwa usahihi. Saratani ni kundi la magonjwa yenye aina nyingi, na kila aina inaweza kuhitaji vipimo tofauti ili kuthibitishwa.


Madaktari hutumia vipimo kama CT Scan, MRI, Ultrasound, Mammogram, Endoscopy, pamoja na biopsy ili kuthibitisha uwepo wa saratani. Mara nyingi kipande kidogo cha tishu huchukuliwa na kuchunguzwa maabara ili kupata jibu sahihi.


Kumtegemea mtu mashine ambayo haijathibitishwa kunaweza kuchelewesha uchunguzi na matibabu ya saratani. Ugonjwa huu unapogunduliwa mapema kwa njia sahihi, nafasi ya matibabu kuwa na mafanikio huwa kubwa zaidi.

5. Kama mashine ya QA ilisema sina ugonjwa, je, ninaweza kuamini matokeo hayo?

Hapana. Hakuna mashine isiyothibitishwa inayoweza kuhakikisha kuwa mtu hana ugonjwa. Magonjwa mengi yanaweza kuwepo hata kama hayajasababisha dalili au kama hayajaonekana kwenye ripoti ya mashine hiyo.


Kwa mfano, mtu anaweza kuwa na shinikizo la damu, kisukari au hata saratani katika hatua za mwanzo bila dalili zozote. Ndiyo maana uchunguzi wa kitabibu na vipimo vinavyokubalika bado ni muhimu.


Ikiwa una dalili zinazoendelea au una historia ya ugonjwa katika familia, usipuuzie dalili hizo kwa sababu tu mashine ilisema uko sawa.

6. Kwa nini madaktari wengi hawatumii mashine hizi za QA?

Madaktari hutakiwa kutumia njia ambazo zimeonyesha usahihi kupitia tafiti nyingi za kisayansi. Kabla ya kifaa chochote kutumika kwa wagonjwa, lazima kiwe kimeonyesha kuwa kinaweza kutoa matokeo sahihi kwa watu wengi na katika mazingira tofauti.


Kwa sasa, mashine nyingi zinazodai kupima mamia ya magonjwa kwa kushika sensor mkononi hazijafikia kiwango hicho cha ushahidi. Ndiyo sababu hazijaingizwa katika miongozo mingi ya kimataifa ya uchunguzi wa magonjwa.


Hii haimaanishi kuwa madaktari wanapinga teknolojia mpya. Badala yake, wanahitaji ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa teknolojia hiyo ni salama na ina manufaa kwa wagonjwa.

7. Je, mashine hizi za QA zinaweza kutumika kama uchunguzi wa awali?

Baadhi ya watu hudhani kuwa hata kama mashine si sahihi kabisa, inaweza kutumika kama uchunguzi wa awali. Hata hivyo, hata vipimo vya uchunguzi wa awali vinahitaji kuthibitishwa kisayansi kabla ya kutumika kwa watu wengi.


Kipimo cha uchunguzi kinapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kugundua watu wenye ugonjwa bila kutoa matokeo mengi ya uongo. Vinginevyo kinaweza kuwafanya watu wengi wapate hofu isiyo ya lazima au kupuuzwa wakati wana ugonjwa.


Kwa sasa, hakuna ushahidi wa kutosha unaounga mkono matumizi ya mashine hizi kama vipimo rasmi vya uchunguzi wa awali wa magonjwa mengi.

8. Je, ni salama kutumia mashine hizi za QA?

Kwa ujumla, kushika sensor mkononi mara nyingi hakusababishi madhara ya moja kwa moja kwa mwili. Hata hivyo, hatari kubwa ipo kwenye maamuzi yanayofanywa kutokana na matokeo yake.


Mtu anaweza kuanza kutumia dawa, virutubisho au bidhaa mbalimbali bila sababu za msingi. Vilevile anaweza kuacha kwenda hospitalini kwa sababu ameambiwa hana tatizo lolote.


Hatari nyingine ni kuchelewa kugundua ugonjwa halisi. Hivyo, hata kama kifaa chenyewe hakidhuru mwili, matokeo yake yanaweza kusababisha maamuzi yasiyo sahihi kuhusu afya.

9. Je, kuna teknolojia zinazofanana na QA ambazo zimekubalika kisayansi?

Ndiyo. Teknolojia nyingi zisizochoma sindano zimetengenezwa na kuthibitishwa kwa matumizi maalumu. Mfano ni ECG kwa matatizo ya moyo, Ultrasound kwa viungo vya ndani, Kipima oksijeni kwa kiwango cha oksijeni na baadhi ya vifaa vya kupima kazi ya mfumo wa neva.


Tofauti kubwa ni kwamba vifaa hivyo havidai kugundua kila ugonjwa. Kila kifaa kimeundwa kwa kazi maalumu na kimefanyiwa tafiti nyingi kabla ya kuanza kutumika hospitalini.


Hii inaonyesha kuwa teknolojia mpya inaweza kukubalika ikiwa itaungwa mkono na ushahidi wa kutosha wa kisayansi. Tatizo si teknolojia yenyewe, bali madai yanayozidi ushahidi uliopo.

10. Nifanye nini kama nimeshapata ripoti kutoka kwenye mashine hizi za QA?

Usiogope wala usianze matibabu mara moja kwa kutegemea ripoti hiyo pekee. Kwanza, soma matokeo kwa utulivu na uyachukulie kama taarifa inayohitaji kuthibitishwa, si utambuzi wa mwisho wa ugonjwa.


Ikiwa ripoti inaonyesha una ugonjwa mkubwa au una dalili zinazoendelea, nenda hospitalini au kituo cha afya ili ufanyiwe uchunguzi na vipimo vinavyokubalika. Daktari ataamua vipimo vinavyofaa kulingana na historia yako ya afya na dalili ulizonazo.


Kumbuka kuwa lengo la afya bora si kupata ripoti nyingi, bali kupata majibu sahihi. Uamuzi wa matibabu unapaswa kufanywa kwa kutumia ushahidi wa kisayansi, uchunguzi wa daktari na vipimo vinavyoaminika.



Rejea za mada hii

  1. Posada-Quintero HF, Chon KH. Innovations in Electrodermal Activity Data Collection and Signal Processing: A Systematic Review. Sensors (Basel). 2020;20(2):479. doi:10.3390/s20020479.

  2. Sánchez-Reolid R, López de la Rosa F, Sánchez-Reolid D, López MT, Fernández-Caballero A. Machine Learning Techniques for Arousal Classification from Electrodermal Activity: A Systematic Review. Sensors (Basel). 2022;22(22):8886. doi:10.3390/s22228886.

  3. Novak P. Electrochemical Skin Conductance: A Systematic Review. Clin Auton Res. 2019;29(1):17-29.

  4. Farraia MV, Cavaco AM, Paciência I, Delgado L, Moreira A. The Electronic Nose Technology in Clinical Diagnosis: A Systematic Review. Porto Biomed J. 2019;4(4):e42.

  5. Bossuyt PM, Reitsma JB, Bruns DE, Gatsonis CA, Glasziou PP, Irwig L, et al. STARD 2015: An Updated List of Essential Items for Reporting Diagnostic Accuracy Studies. BMJ. 2015;351:h5527.

  6. Bossuyt PM, Reitsma JB, Linnet K, Moons KGM. Beyond Diagnostic Accuracy: The Clinical Utility of Diagnostic Tests. Clin Chem. 2012;58(12):1636-43.

  7. Deeks JJ, Altman DG. Diagnostic Tests 4: Likelihood Ratios. BMJ. 2004;329(7458):168-9.

  8. Akobeng AK. Understanding Diagnostic Tests 1: Sensitivity, Specificity and Predictive Values. Acta Paediatr. 2007;96(3):338-41.

  9. Akobeng AK. Understanding Diagnostic Tests 2: Likelihood Ratios, Pre-test and Post-test Probability. Acta Paediatr. 2007;96(4):487-91.

  10. Whiting PF, Rutjes AWS, Westwood ME, Mallett S, Deeks JJ, Reitsma JB, et al. QUADAS-2: A Revised Tool for the Quality Assessment of Diagnostic Accuracy Studies. Ann Intern Med. 2011;155(8):529-36.

  11. Sackett DL, Haynes RB, Guyatt GH, Tugwell P. Clinical Epidemiology: A Basic Science for Clinical Medicine. 2nd ed. Boston: Little, Brown and Company; 1991.

  12. Guyatt G, Rennie D, Meade MO, Cook DJ, editors. Users' Guides to the Medical Literature: A Manual for Evidence-Based Clinical Practice. 3rd ed. New York: McGraw-Hill Education; 2015.

  13. Horvers A, Tombeng N, Bosse T, Lazonder AW, Molenaar I. Detecting Emotions through Electrodermal Activity in Learning Contexts: A Systematic Review. Sensors (Basel). 2021;21(23):7869.

  14. Posada-Quintero HF, Florian JP, Orjuela-Cañón AD, Aljama-Corrales T, Charleston-Villalobos S, Chon KH. Power Spectral Density Analysis of Electrodermal Activity for Sympathetic Function Assessment. Ann Biomed Eng. 2016;44(10):3124-35.


Imeandikwa:

26 Juni 2026, 12:18:18

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

Rejea za mada hii:

  1. Posada-Quintero HF, Chon KH. Innovations in Electrodermal Activity Data Collection and Signal Processing: A Systematic Review. Sensors (Basel). 2020;20(2):479. doi:10.3390/s20020479.

  2. Sánchez-Reolid R, López de la Rosa F, Sánchez-Reolid D, López MT, Fernández-Caballero A. Machine Learning Techniques for Arousal Classification from Electrodermal Activity: A Systematic Review. Sensors (Basel). 2022;22(22):8886. doi:10.3390/s22228886.

  3. Novak P. Electrochemical Skin Conductance: A Systematic Review. Clin Auton Res. 2019;29(1):17-29.

  4. Farraia MV, Cavaco AM, Paciência I, Delgado L, Moreira A. The Electronic Nose Technology in Clinical Diagnosis: A Systematic Review. Porto Biomed J. 2019;4(4):e42.

  5. Bossuyt PM, Reitsma JB, Bruns DE, Gatsonis CA, Glasziou PP, Irwig L, et al. STARD 2015: An Updated List of Essential Items for Reporting Diagnostic Accuracy Studies. BMJ. 2015;351:h5527.

  6. Bossuyt PM, Reitsma JB, Linnet K, Moons KGM. Beyond Diagnostic Accuracy: The Clinical Utility of Diagnostic Tests. Clin Chem. 2012;58(12):1636-43.

  7. Deeks JJ, Altman DG. Diagnostic Tests 4: Likelihood Ratios. BMJ. 2004;329(7458):168-9.

  8. Akobeng AK. Understanding Diagnostic Tests 1: Sensitivity, Specificity and Predictive Values. Acta Paediatr. 2007;96(3):338-41.

  9. Akobeng AK. Understanding Diagnostic Tests 2: Likelihood Ratios, Pre-test and Post-test Probability. Acta Paediatr. 2007;96(4):487-91.

  10. Whiting PF, Rutjes AWS, Westwood ME, Mallett S, Deeks JJ, Reitsma JB, et al. QUADAS-2: A Revised Tool for the Quality Assessment of Diagnostic Accuracy Studies. Ann Intern Med. 2011;155(8):529-36.

  11. Sackett DL, Haynes RB, Guyatt GH, Tugwell P. Clinical Epidemiology: A Basic Science for Clinical Medicine. 2nd ed. Boston: Little, Brown and Company; 1991.

  12. Guyatt G, Rennie D, Meade MO, Cook DJ, editors. Users' Guides to the Medical Literature: A Manual for Evidence-Based Clinical Practice. 3rd ed. New York: McGraw-Hill Education; 2015.

  13. Horvers A, Tombeng N, Bosse T, Lazonder AW, Molenaar I. Detecting Emotions through Electrodermal Activity in Learning Contexts: A Systematic Review. Sensors (Basel). 2021;21(23):7869.

  14. Posada-Quintero HF, Florian JP, Orjuela-Cañón AD, Aljama-Corrales T, Charleston-Villalobos S, Chon KH. Power Spectral Density Analysis of Electrodermal Activity for Sympathetic Function Assessment. Ann Biomed Eng. 2016;44(10):3124-35.

bottom of page