Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Helen L, M.D
2 Aprili 2026, 16:17:51

Lala muda wa kutosha, imarisha afya yako
Kulala muda wa kutosha huongeza ufanisi wa mwili na akili, pia ni kinga ya magonjwa sugu kama kisukari aina ya 2, magonjwa ya moyo, uzito mkubwa kupita kiasi na sonona. Jali afya yako, lala masaa yanayoshauriwa kiafya kulingana na umri wako.
Faida za kulala muda wa kutosha
Kuna faida nyingi za kulala muda wa kutosha unaoshauriwa kulingana na umri wako. Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba kulala muda wa kutosha wakati wa usiku;
Huamsha chembe za ulinzi wa mwili na 'antibodies' zinazopambana na maradhi mbalimbali ndani ya mwili wako
Huamsha kemikali mbalimbali za ulinzi mwilini zenye jina la 'cytokine' ambazo huzuia uvimbe unaosababishwa na kuamka kwa kinga za mwili pia huimarisha usingizi na kupambana na maradhi
Hupunguza kiwango cha homoni ya 'cortisol' inayochangia kwa kiasi kukubwa ongezeko la uzito mkubwa kupita kiasi na msongo.
Hupunguza upinzani wa mwili dhidi ya homoni inayorekebisha kiwango cha sukari kwenye damu yenye jina la 'insulin'
Huamsha homoni ya ukuaji yenye jina la 'growth hormone' inayosaidia kuponya majeraha na kurejesha seli mbalimbali zilizokufa
Hutuliza mfumo wa neva wa 'sympathetic' ili kushusha shinikizo la damu wakati umelala
Hufanya ubongo uweze kuchakata taarifa mbalimbali ulizozipokea muda mfupi kabla ya kulala na hivyo kukusababisha uwe na kumbukumbu nzuri
Endapo utalala muda wa kutosha wakati wa usiku, utaweza kujikinga na:
Magonjwa ya moyo kama shinikizo la juu la damu, kiharusi, magonjwa ya mishipa ya moyo na mapigo ya moyo kwenda isivyo kawaida
Uzito mkubwa kupita kaisi (ugonjwa wa obeziti)
Sonona
Kisukari aina ya 2
Ni masaa mangapi unatakiwa kulala kwa siku?
Kwa watu wazima wanatakiwa kulala angalau masaa 7 hadi 8 mfululizo wakati wa usiku
Vijana wa miaka 13 hadi 19 wanatakiwa kulala angalau masaa 9 hadi 10 mfululizo wakati wa usiku
Watoto wadogo chini ya miaka 13 wanatakiwa kulala masaa 10 au zaidi wakati wa usiku.
Kumbuka
Kulala zaidi ya muda unaoshauriwa huweza kuambatana na tatizo la kukosa usingizi, kupata usingizi usio bora na kushindwa kuanza au kuendelea kulala.
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 16:17:51
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
​
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:
