top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Helen L, M.D

2 Aprili 2026, 16:17:51

Mazoezi ni dawa ya msongo

Mazoezi hupunguza kiwango cha homoni zinazozalishwa wakati una msongo, na kuongeza homoni zinazoboresha hali ya moyo wako, kuondoa maumivu na kukupa usingizi. Tumia mazoezi kama dawa ya msongo.


Msongo ni nini , na kwa nini mazoezi hutibu msongo?


Msongo ni mwitikio wa mwili dhidi ya mabadiliko yoyote ambayo yanahitaji marekebisho au majibu. Kuna aina mbalimbali za msongo kama vile msongo wa mwili, msongo wa mawazo na msongo wa mhemko(hisia) .


Mwili wa binadamu huzalisha kwa wingi homoni ili kukabiliana na msongo wowote ule, homoni hizo ni cortisol, adrenaline na norepinephrine. Homoni kuu ya msongo huitwa kwa jina la cortisol.


KICHOCHEZI CHA UZALISHAJI WA HOMON ZA MSONGO


Homoni za msongo huzalishwa kwa wingi endapo;


  • Kuwa na mawazo mengi (ya kupata pesa, kukosa pesa, kukosa ajira, kudaiwa na bank n.k)

  • Kuwa na shauku kuu ya kusubiria kitu ambacho bado hakijatokea

  • Kuwa na hofu ya kupatwa na jambo baya, au kufanya vibaya

  • Kuwa na sononeko baada ya kupoteza ndugu au mtu wako wa karibu, kufutwa kazi, kuachika n.k


Kiwango hicho cha homoni za msongo huishi kwenye damu muda wote kisababishi kinapokuwepo.


Endapo mtu ataondokana na kisababishi, kiwango cha homoni za msongo hupungua kwenye damu.


Njia za kupunguza homoni za msongo


Njia nzuri na rahisi ya kupunguza kiwango cha homoni za msongo ni kufanya mazoezi. Tafiti zinaonyesha mazoezi huwa na faida kuu tatu;


  • Hupunguza kiwango cha homoni ya cortisol

  • Huongeza uzalishaji wa homoni ya kutuliza mwili, kuondoa maumivu, kuleta usingizi na kuboresha hali ya moyo yenye jina la endorphins

  • Huimarisha afya ya mwili wako kwa kuongeza kinga mwilini dhidi ya maradhi na hivyo kukufanya uwe imara.


Mazoezi gani ya kufanya?


Jaribu kufanya mazoezi ambayo yanakufanya ufurahie na kutumia akili yako kama;


  • Kutembea

  • Kucheza mziki

  • Kupanda mlima

  • Kuogelea

  • Kuendesha baiskeli

  • Yoga

  • Kupalilia bustani

  • Kukimbia

  • N.k


Madhara


madhara ya kukaa na homoni za msongo kwa muda mrefu ni;


  • Kupata shinikizo la juu la damu (presha ya kupanda)

  • Kupata mshituko wa moyo unaoweza pelekea kifo cha ghafla

  • Kufeli kwa moyo

  • Kufeli kwa figo

  • Kuongezeka kwa kiwango cha lehamu (kolestro) kwenye damu


Njia zingine za kuondoa msongo zimeorodheshwa sehemu nyingine katika tovuti hii.

Imeandikwa:

2 Aprili 2026, 16:17:51

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

​

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

bottom of page