Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
2 Aprili 2026, 16:17:51

Njia za dawa kuingia mwilini
Ili kufanikiwa kwa tiba, unapaswa kutumia dawa kwa njia sahihi uliyoelekezwa na daktari au mtoa dawa. Kwa ufanisi wa dawa, tumia kama ulivyoelekezwa na daktari wako.
Njia ya mdomo
Njia ya kuweka mdomoni
Matumizi ya dawa kwa njia ya mdomo ni njia salama na inayofaa, dawa huingia mwilini kupitia kinywa na inaweza kutumiwa kwa njia kuu tatu ambazo ni 1. Kumeza 2. Kuweka chini ya ulimi au 3. Kusukutua kisha kutema
Faida ya matumizi ya dawa kwa njia ya mdomo
Ni rahisi kutumia
Inakubalika kwa watu wengi
Mara nyingi haihitaji uangalizi wa kitaalamu
Mapungufu ya matumizi ya dawa kwa njia ya mdomo
Uchokozi wa tumbo kwa baadhi ya dawa
Kufyonzwa kwa dawa kwenda mwilini kunategemea na hali ya tumboni (hakuna au kuna chakula)
Dawa inaweza kuharibika kikemikali kabla haijafyonzwa kutokana na vimeng’enyo vilivyomo tumboni
Siyo dawa zote zinaweza kupitia mdomoni
Ufyonzaji unaweza usiwe kamilifu
Njia ya matone
Njia hutumika kutibu magonjwa ya macho, pua na masikio au mdomoni.
Faida ya matumizi ya dawa kwa njia ya matone
Rahisi kutumia
Huwekwa na kutumika katika sehemu iliyoathirika
Mapungufu ya matumizi ya dawa kwa njia ya matone
Upungufu wa njia hii ni kuwa ni vigumu kwa watumiaji wengi kukadiria kipimo (dozi) sahihi na hivyo huweza kusababisha kifo.
Inaweza kusababisha muwasho
Njia ya sindano
Kuna aina nyingi za matumizi ya dawa kwa njia ya kuchoma sindano ambazo ni;
Kuchomwa chini ya ngozi
Kuchoma kwenye ngozi
Kuchoma ndani ya msuli/mnofu
Kuchoma ndani ya mshipa wa damu
Faida ya matumizi ya dawa kwa njia y sindano
Hufanya kazi haraka hasa katika kuokoa maisha
Inatumika kwa wanaotapika sana
Hutumika kwa wagonjwa waliopoteza fahamu
Mapungufu ya matumizi ya dawa kwa njia ya sindano
Inahitaji mtaalamu anayejua kuchoma sindano
Inaumiza/inauma
Kama haikuchomwa inavyotakiwa inaweza kusababisha madhara makubwa kama vile kupooza.
Inaogopesha kwa watoto na baadhi ya wakubwa
Kama sindano iliyotumika si salama yaweza kuambukiza magonjwa mfano virusi vya UKIMWI
Njia ya haja kubwa
Hufahamika kwa jina jingine la 'njia ya puru' huhusisha kuingizwa dawa ndani ya njia ya haja kubwa ili baadaye zifyonzwe na damu na kupelekwa sehemu nyingine ya mwili au kutibu magonjwa ya sehemu hiyo ilipowekwa. Dawa hizo hutengenezwa kwa umbo la sapozitori au katika hali ya maji maji
Faida ya kutumia dawa kwa njia ya haja kubwa
Inafaa kwa dawa ambazo zinaweza kuleta usumbufu tumboni, kwa mfano aspirini, Aminophylline, indomethacin
Inafaa kwa mgonjwa anayetapika
Inafaa kama unataka kutibu baadhi ya magonjwa ya sehemu ya haja kubwa
Inafaa kwa mgonjwa mwenye matatizo katika kumeza (swallowing) au hajitambui.
Watoto wanaokataa kunywa dawa
Mapungufu ya kutumia dawa kwa njia ya haja kubwa
Mgonjwa kuona aibu wakati wa kupewa maelekezo ya jinsi ya kutumia
Kama mgonjwa anatumia njia hii mara kwa mara, kuna uwezekano wa kusababisha maumivu na uvimbe katika sehemu hiyo.
Kufyonzwa kwa dawa kwenda sehemu nyingine za mwili kunaweza kuathiriwa na kinyesikilichoko kwenye sehemu hiyo.
Njia ya ukeni
Matumizi ya dawa kwa kuweka ukeni, hutumika kutibu magonjwa yaliyo katika mfumo wa uzazi wa kike mfano Clotrimazole na nystatin katika kutibu fangasi ukeni.
Faida ya matumizi ya dawa kwa kuweka ukeni
Ni rahisi kutumia
Huwekwa na kutumika katika sehemu iliyoathirika
Mapungufu ya matumizi ya dawa kwa kuweka ukeni
Mgonjwa kuona aibu wakati wa kupewa maelekezo ya jinsi ya kutumia
Kama mgonjwa anatumia njia hii mara kwa mara, kuna uwezekano wa kusababisha maumivu
Njia ya kuvuta pumzi
Njia hii hutumika kwa kuvuta dawa kwenye pumzi na hutumika zaidi kwa wagonjwa wenye matatizo ya pumu yakifua na matatizo ya dharura ya mfumo wa hewa kutokana na kuziba kwa njia za hewa yanayoweza kutibiwa kwa kutumia njia hii.
Dawa zinazotumiwa kwa njia hii, hufanya kazi ya kutanua njia zinazopitisha hewa kupeleka kwenye mapafu zenye jina la bronkodaileta kama vile dawa ya salbutamol.
Faida ya matumizi ya dawa kwa kuvuta pumzi
Dawa hufanya kazi kwa haraka
Mapungufu ya matumizi ya dawa kwa kuvuta pumzi
Ni vigumu kwa watumiaji wengi kukadiria kipimo (Dose) sahihi na hivyo huweza
kuzidisha au kupunguza kipimo.
Kiwango cha dawa kikizidi sana mgonjwa anaweza kupata madhara yanayoweza kusababisha kifo.
Njia ya kupakaa
Mara nyingi njia hii hutumika kutibu magonjwa ya ngozi. Aidha, inaweza kutumika kutibu magonjwa yaliyoko ndani ya mwili. Dawa hizo huweza kupenya ngozi hadi mfumo wa damu na kusambazwa sehemu mbali mbali za mwili.
Faida ya matumizi ya dawa kwa njia ya kupaka
Rahisi kutumika – mgonjwa anaweza kujipakaa mwenyewe.
Dawa hupakwa moja kwa moja kwenye sehemu yenye ugonjwa
Kupakwa kwa sehemu kubwa hurahisisha ufyonzaji wa dawa
Mapungufu ya matumizi ya dawa kwa njia ya kupaka
Baadhi ya dawa zinaweza kusababisha usumbufu au mzio wa ngozi
Baadhi ya dawa zinaweza kufyonzwa kwenda ndani ya mwili na kuleta madhara
Kutokuwa na uhakika wa kufyonzwa kikamilifu kwa dawa
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 16:17:51
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
​
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:
