Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
24 Agosti 2026, 03:43:15

Kisababishi kikuu cha vidonda vya tumbo?
Mambo ambayo sayansi ya tiba iliaminisha watu lakini baadaye yakathibitika kuwa si sahihi au hayakuwa kamili
Utangulizi
Katika historia ya tiba, kumekuwa na nyakati nyingi ambapo wataalamu wa afya, taasisi za udhibiti wa dawa, vyuo vya tiba na jumuiya za kisayansi walitoa mapendekezo yaliyokuwa yakiaminika kuwa sahihi kulingana na ushahidi uliokuwepo wakati huo. Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, tafiti kubwa na zenye ubora wa juu zilionyesha kuwa baadhi ya mapendekezo hayo hayakuwa sahihi, hayakuwa kamili au katika baadhi ya mazingira yalikuwa na madhara kuliko manufaa.
Mabadiliko hayo yamesababisha baadhi ya watu kuamini kuwa "sayansi ya tiba ilidanganya." Lakini je, kauli hiyo ni sahihi?
Kwa kiasi kikubwa, jibu ni hapana, katika mazingira mengi, wataalamu wa afya hawakuwa wanatoa taarifa za uongo kwa makusudi. Badala yake walikuwa wakitoa ushauri uliotegemea ushahidi bora uliokuwepo wakati huo. Kadiri tafiti zilivyoendelea kufanyika, mbinu za utafiti zikaboreshwa na idadi ya wagonjwa walioshirikishwa ikaongezeka, ilionekana kuwa baadhi ya hitimisho la awali lilikuwa na mapungufu.
Ndiyo maana katika tiba kuna msemo unaosema:
"Nusu ya yale tunayofundisha wanafunzi wa tiba leo yanaweza kuonekana si sahihi baada ya miaka ishirini. Changamoto ni kwamba hatujui ni nusu ipi."
Makala hii haikusudii kupunguza imani kwa tiba ya kisasa. Badala yake, inalenga kuonyesha namna sayansi inavyojirekebisha kila ushahidi mpya unapopatikana. Huo ndiyo msingi wa tiba inayotegemea ushahidi (Tiba kutokana na ushahidi).
Kwa nini wataalamu wa afya waliamini mambo ambayo baadaye yalionekana kuwa si sahihi?
Swali hili ni muhimu sana.
Mtu anaweza kujiuliza, ikiwa jambo lilikuwa si sahihi, kwa nini karibu madaktari wote duniani walikuwa wakilifundisha?
Sababu ni kwamba si ushahidi wote una uzito unaofanana. Kwa mfano, daktari anaweza kuona wagonjwa 100 wanaotumia dawa fulani na wengi wao wakapata nafuu. Kutokana na uzoefu huo anaweza kuamini dawa hiyo ni nzuri.
Lakini kuna tatizo, huenda wagonjwa hao wangepata nafuu hata bila kutumia dawa hiyo. Huenda walikuwa na ugonjwa usio mkali. Huenda walikuwa vijana wenye afya nzuri. Huenda pia walikuwa wanatumia matibabu mengine yaliyowasaidia.
Hivyo uzoefu wa kitabibu peke yake hauwezi kuthibitisha kuwa dawa ndiyo iliyosababisha matokeo hayo.
Ndiyo maana sayansi ya tiba hutumia mbinu mbalimbali za kutafuta ushahidi.
Kwa ujumla, ushahidi wa kitabibu hupangwa kuanzia wenye nguvu ndogo hadi wenye nguvu kubwa kama ifuatavyo:
Maoni ya wataalamu;
Taarifa za wagonjwa wachache (Case reports);
Tafiti za uchunguzi (Observational studies);
Majaribio yaliyodhibitiwa kwa nasibu (Randomized Controlled Trials - RCTs);
Mapitio ya kimfumo (Systematic Reviews);
Uchambuzi wa pamoja wa tafiti nyingi (Meta-analysis).
Kadiri ushahidi unavyokuwa juu katika ngazi hii, ndivyo uwezekano wa kupata hitimisho sahihi unavyoongezeka. Ndiyo maana historia ya tiba imejaa mifano ambapo tafiti ndogo zilionyesha dawa ina manufaa, lakini baada ya kufanyika majaribio makubwa ilionekana kuwa dawa hiyo haina manufaa au hata inaongeza vifo.
1. Vidonda vya tumbo havikusababishwa na msongo wa mawazo pekee
Imani iliyokuwa ikifundishwa
Kwa zaidi ya miaka 70, wanafunzi wa tiba walifundishwa kuwa vidonda vya tumbo (PUD) vilisababishwa na:
Msongo wa mawazo;
Kula vyakula vyenye pilipili;
Uzalishaji mkubwa wa tindikali tumboni;
Maisha yenye wasiwasi.
Wagonjwa waliambiwa waepuke pilipili, kahawa, mawazo mengi na kula chakula laini. Katika kipindi hicho, matibabu yaliyotolewa yalikuwa hasa:
Magnesiamu haidroksaidi
Aluminiamu haidroksaidi
Cimetidine
Ranitidine
baadaye Omeprazole.
Dawa hizi zilipunguza tindikali tumboni na wagonjwa wengi walipata nafuu kwa muda. Hivyo ilionekana kana kwamba nadharia ilikuwa sahihi.
Kwa nini ilionekana kuwa kweli?
Kwa sababu dalili zilikuwa zinapungua. Mgonjwa alipokunywa dawa za kupunguza tindikali, maumivu yalipungua.
Lakini kupungua kwa maumivu hakukumaanisha kuwa chanzo cha ugonjwa kilikuwa kimetibiwa.
Vidonda vilikuwa vinarudi tena baada ya miezi kadhaa. Madaktari walidhani mgonjwa amerudia kula pilipili au anaendelea kuwa na msongo wa mawazo.
Ugunduzi uliobadilisha historia ya tiba
Mwaka 1982, watafiti wawili kutoka Australia:
Dk. Barry Marshall
Dk. Robin Warren
Waligundua bakteria aliyekuwa akiishi kwenye utando wa tumbo aitwaye Helicobacter pylori. Wazo hili lilikataliwa sana.
Kwanini?
Kwa miaka mingi iliaminika kuwa hakuna bakteria anayeweza kuishi kwenye tindikali kali ya tumbo.
Ili kuthibitisha nadharia yake, Barry Marshall alifanya jambo ambalo leo lingeonekana kuwa gumu kuruhusiwa na kamati za maadili ya utafiti. Alimeza makusudi bakteria huyo, baada ya siku chache alipata gastraitisi (uvimbe kinga wa utando dani ya tumbo), na vipimo vikathibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa bakteria huyo.
Baadaye alitibiwa kwa antibiotiki na kupona, hatimaye tafiti nyingi duniani zilithibitisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vidonda vya sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo (Duodenamu) na sehemu kubwa ya vidonda vya tumbo (tumbo) vilihusishwa na maambukizi ya Helicobacter pylori au matumizi ya dawa za kutuliza maumivu zisizo za steroidi (Non-Steroidal Anti-inflammatory Drugs - NSAIDs) kama:
Aspirini
Diclofenac
Ibuprofen
Naproxen
Ketoprofen.
Mwongozo wa sasa unasemaje?
Leo hii mgonjwa mwenye vidonda vya tumbo hufanyiwa uchunguzi wa kutafuta Helicobacter pylori. Iwapo bakteria huyo atapatikana, hutibiwa kwa mchanganyiko wa dawa kadhaa kama:
Omeprazole au Pantoprazole (dawa za kupunguza uzalishaji wa tindikali tumbonikwa kuzuia ripeta H);
Amoxicillin;
Clarithromycin;
au mchanganyiko mwingine kulingana na usugu wa bakteria katika eneo husika. Badala ya kutibu maumivu pekee, matibabu hulenga kuondoa chanzo cha ugonjwa. Ugunduzi huu uliwapatia Barry Marshall na Robin Warren Tuzo ya Nobel mwaka 2005.
Somo muhimu
Kutoweka kwa dalili si ushahidi kwamba chanzo cha ugonjwa kimetibiwa. Pia, jambo linaloonekana kuwa haliwezekani kisayansi linaweza kuwa kweli pale ushahidi mzuri unapopatikana.
Historia ya Helicobacter pylori imekuwa mojawapo ya mifano bora kabisa ya jinsi sayansi ya tiba inavyojirekebisha.
2. Tiba homoni ya komahedhi zilidhaniwa kulinda moyo
Imani iliyokuwa ikifundishwa
Kuanzia miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, wanawake wengi waliomaliza hedhi walipewa tiba ya homoni inayofahamika kama Homoni ya komahedhi-HRT, si tu kupunguza dalili za kukoma hedhi, bali pia kuzuia:
Mshtuko wa moyo;
Kiharusi;
Kudhoofika kwa mifupa;
Kuzeeka kwa mishipa ya damu.
Dawa zilizotumika sana zilikuwa:
Premarin® (Conjugated equine estrogens)
Prempro® (Conjugated estrogens + Medroxyprogesterone acetate).
Madaktari wengi waliamini kuwa estrojeni hulinda mishipa ya damu kwa kuongeza lehemu(kolestro) nzuri (lehemu HDL) na kupunguza lehemu mbaya (Lehemu LDL). Kwa msingi huo, ilionekana kuwa matumizi ya homoni yangepunguza magonjwa ya moyo.
Kwa nini ilionekana kuwa kweli?
Ushahidi uliokuwepo wakati huo ulitokana hasa na tafiti za uchunguzi (Observational studies). Katika tafiti hizo ilionekana kuwa wanawake waliokuwa wanatumia HRT walikuwa na kiwango kidogo cha ugonjwa wa moyo.
Lakini kulikuwa na tatizo kubwa lililoitwa Upendeleo wa kiafya kwa mtumiaji.
Wanawake waliokuwa wanatumia HRT mara nyingi walikuwa:
Wenye kipato kikubwa;
Wenye elimu zaidi;
Wanaofanya mazoezi;
Wasiovuta sigara;
Wanaopata huduma bora za afya.
Kwa hiyo afya yao nzuri haikutokana na homoni pekee.
Utafiti uliobadilisha historia
Mwaka 2002 ulianza kuchapishwa matokeo ya utafiti mkubwa wa Women's Health Initiative (WHI).
Tofauti na tafiti zilizopita, huu ulikuwa ni utafiti wa majaribio yaliyodhibitiwa kwa nasibu (Randomized Controlled Trial). Zaidi ya wanawake 16,000 walishiriki.
Matokeo yalikuwa ya kushangaza.
Badala ya kupunguza ugonjwa wa moyo, matumizi ya estrojeni pamoja na projestini yaliongeza hatari ya:
Kuganda kwa damu kwenye vena;
Kiharusi (Stroku);
Saratani ya matiti;
Mshtuko wa moyo kwa baadhi ya wanawake.
Kutokana na matokeo hayo, sehemu ya utafiti ilisimamishwa mapema kwa sababu ya masuala ya usalama wa washiriki. Mwongozo wa tiba duniani ukabadilika ndani ya muda mfupi.
Mwongozo wa sasa unasemaje?
HRT bado hutumika, hata hivyo matumizi yake sasa ni kwa:
Kupunguza dalili kali za kukoma hedhi;
Kwa muda mfupi iwezekanavyo;
Baada ya kutathmini faida na hatari kwa kila mwanamke mmoja mmoja.
Haipendekezwi tena kuitumia kwa lengo la kuzuia ugonjwa wa moyo kwa wanawake wenye afya.
Somo muhimu
Tafiti za uchunguzi zinaweza kuonyesha uhusiano, lakini haziwezi kuthibitisha sababu. Ni baada ya kufanyika majaribio yaliyodhibitiwa kwa nasibu ndipo ilionekana kuwa hitimisho la awali lilikuwa limeathiriwa na upendeleo wa washiriki.
Huu ni mojawapo ya mifano maarufu zaidi inayofundishwa katika tiba kuhusu umuhimu wa kutofautisha uhusiano na uhusiano wa kisababishi.
3. Thalidomide: Dawa iliyobadilisha historia ya usalama wa dawa duniani
Imani iliyokuwa ikifundishwa
Mwishoni mwa miaka ya 1950, kampuni ya Chemie Grünenthal nchini Ujerumani ilitengeneza dawa iliyoitwa Thalidomide. Dawa hii ilitangazwa kuwa salama sana kiasi kwamba ilidaiwa kuwa hata mtu akimeza vidonge vingi hangeweza kupata madhara makubwa.
Kutokana na sifa hiyo, Thalidomide ilianza kutumika kutibu:
Kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito (Homa ya asubuhi);
Kukosa usingizi (Insomnia);
Wasiwasi.
Katika nchi nyingi za Ulaya, Australia na sehemu nyingine za dunia, wanawake wajawazito walipewa dawa hii kwa imani kuwa ilikuwa salama kwa mama na mtoto.
Wakati huo, hakukuwa na sheria kali zinazotaka dawa zote mpya zipimwe kwa kina kwa wanawake wajawazito au kuthibitisha usalama wake kwa mtoto aliyeko tumboni.
Kwa nini ilionekana kuwa salama?
Katika majaribio ya awali, Thalidomide ilionekana kuwa na sumu ndogo kwa watu wazima.
Haikusababisha:
Kushindwa kupumua;
Kupoteza fahamu kirahisi;
Madhara makubwa kwenye ini;
Madhara makubwa kwenye figo.
Kwa hiyo ilionekana kuwa dawa salama kuliko dawa nyingi za usingizi zilizokuwepo wakati huo kama Phenobarbital.
Tatizo kubwa ni kwamba tafiti za wakati huo hazikuwa zimechunguza kwa kina athari zake kwa mtoto anayekua tumboni.
Ukweli uliojitokeza baadaye
Miaka michache baadaye madaktari walianza kuona ongezeko lisilo la kawaida la watoto waliozaliwa wakiwa na:
Mikono mifupi sana;
Miguu mifupi;
Kutokuwa na mikono;
Kutokuwa na miguu;
Kasoro za moyo;
Kasoro za masikio;
Kasoro za figo.
Baada ya uchunguzi wa kina ilibainika kuwa karibu watoto wote hao walikuwa wamezaliwa na mama waliotumia Thalidomide katika wiki za mwanzo za ujauzito.
Athari hii ilijulikana kama ulemavu wa kuzaliwa unaosababishwa na dawa (Teratojeni).
Leo inajulikana kuwa Thalidomide huathiri ukuaji wa mishipa mipya ya damu (kizuia ukuaju wa mishopa ya damu). Bila mishipa ya damu ya kutosha, viungo vya mtoto haviwezi kukua kawaida. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto 10,000 duniani walizaliwa na ulemavu kutokana na dawa hii.
Matokeo kwa sayansi ya tiba
Tukio hili lilibadilisha kabisa sheria za maendeleo ya dawa.
Baada ya hapo nchi nyingi zilianza kuhitaji:
Majaribio ya kina kwa wanyama wajawazito;
Tathmini ya madhara kwa kijusi;
Ufuatiliaji wa usalama baada ya dawa kuingia sokoni (Pharmacovigilance);
Ushahidi wa kutosha kabla ya dawa kuidhinishwa.
Hadi leo, Thalidomide bado hutumika kutibu baadhi ya magonjwa kama:
Saratani ya seli za plasma (Myeloma Mchanganyiko);
Ugonjwa wa ngozi unaohusiana na ukoma (Erithima Nodosamu Leprosamu).
Lakini matumizi yake yanafuatana na sheria kali sana za kuhakikisha mwanamke hatumii dawa hiyo akiwa mjamzito.
Somo muhimu
Dawa inaweza kuwa salama kwa mtu mzima lakini isiwe salama kwa mtoto aliyeko tumboni.
Ndiyo maana dawa nyingi huandikwa kuwa "zitumike tu kama faida zinazidi hatari wakati wa ujauzito."
4. Rofecoxib (Vioxx): Dawa iliyokuwa bora kwa maumivu lakini ikaongeza hatari ya mshtuko wa moyo
Imani iliyokuwa ikifundishwa
Mwaka 1999 kampuni ya Merck ilianzisha dawa ya maumivu iliyoitwa Rofecoxib (Vioxx®), dawa hii ilikuwa katika kundi la Dawa za kupunguza maumivu zisizo za steroidi zinazochagua kimeng'enya COX-2 (Vizuia COX-2 chaguzi au Selective Cyclooxygenase-2 Inhibitors). Lengo lilikuwa kutengeneza dawa ambayo:
Inapunguza maumivu;
Inapunguza uvimbe;
Lakini isisababishe vidonda vya tumbo kama Aspirini au Diclofenac.
Mwanzoni ilionekana kuwa mafanikio makubwa. Madaktari duniani kote waliianza kuitumia kwa wagonjwa wenye:
Yabisi kavu(Osteoarthraitisi);
Baridi yabisi (Rheumatoid athraitisi);
Maumivu ya muda mrefu.
Zaidi ya wagonjwa milioni 80 waliitumia duniani.
Kwa nini ilionekana kuwa bora?
Kwa sababu ilikuwa kweli ina faida, ikilinganishwa na Diclofenac au Naproxen, wagonjwa waliotumia Vioxx walikuwa na;
Vidonda vichache vya tumbo;
Kuvia damu tumboni kwa kiwango kidogo.
Kwa hiyo ilionekana kuwa dawa bora kuliko NSAIDs nyingine, lakini kulikuwa na tatizo ambalo halikuonekana mapema.
Kilichogunduliwa baadaye
Baada ya wagonjwa wengi kuitumia kwa muda mrefu, tafiti zilianza kuonyesha kuwa Vioxx iliongeza hatari ya:
Mshtuko wa moyo (Myocardial infarction);
Kkiharusi (Stroke);
Vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo.
Hatari hiyo ilionekana hasa kwa matumizi ya muda mrefu. Mwaka 2004, kampuni ya Merck iliondoa Vioxx duniani kote kwa hiari yake. Tukio hili limekuwa mojawapo ya matukio makubwa zaidi katika historia ya usalama wa dawa.
Kwa nini madhara haya hayakuonekana mapema?
Majaribio ya awali yalihusisha maelfu ya wagonjwa, lakini madhara yaliyokuwa yanaongezeka yalikuwa nadra kiasi kwamba yalihitaji mamilioni ya watu kutumia dawa ndipo yaonekane vizuri. Hii ndiyo sababu dawa huendelea kufuatiliwa hata baada ya kuidhinishwa.
Somo muhimu
Kupewa kibali cha matumizi hakumaanishi kuwa kila athari ya dawa imegunduliwa, baadhi ya madhara huonekana baada ya dawa kutumiwa na watu wengi kwa miaka kadhaa. Ndiyo maana taarifa za madhara kutoka hospitali na vituo vya afya ni muhimu sana.
5. Aspirini haipaswi kutumiwa na kila mtu ili kuzuia mshtuko wa moyo
Imani iliyokuwa ikifundishwa
Kwa miaka mingi, watu wenye umri wa kati waliambiwa watumie:
Aspirini (Acetylsalicylic acid) 75–100 mg kila siku
ili kuzuia:
Mshtuko wa moyo;
Kiharusi.
Matumizi haya yaliitwa Kinga ya awali ya ugonjwa wa moyo. Kwa kuwa Aspirini hupunguza kuganda kwa damu kwa kuzuia kimeng'enya cha Cyclooxygenase-1 (COX-1) kwenye chembe sahani za damu (Pletileti), ilionekana kuwa ingepunguza kuziba kwa mishipa ya moyo.
Kwa nini ilionekana kuwa kweli?
Tafiti za mwanzo zilionyesha kuwa Aspirini hupunguza kuganda kwa damu. Kwa wagonjwa waliokwisha kupata:
Mshtuko wa moyo;
Kiharusi;
Kuziba kwa mishipa ya moyo,
faida zake zilikuwa kubwa sana. Tatizo lilikuwa ni kudhani kuwa faida hizo zingekuwa sawa hata kwa watu ambao hawajawahi kupata ugonjwa wa moyo.
Tafiti zilizobadilisha miongozo
Baada ya tafiti kubwa kama:
Jaribio la ARRIVE,
Jaribio la ASPREE,
Jaribio la ASCEND,
ilibainika kuwa kwa watu wengi wasiowahi kupata ugonjwa wa moyo, kupungua kwa hatari ya mshtuko wa moyo kulikuwa kidogo sana.
Lakini wakati huo huo kulikuwa na ongezeko la:
Kuvia damu tumboni;
Kuvia kwa damu kwenye ubongo;
Kuvia/kutokwa na damu sehemu nyingine za mwili.
Kwa watu wengi, madhara yalikuwa makubwa kuliko faida.
Mwongozo wa sasa
Aspirini bado ni dawa muhimu sana, lakini hutumika zaidi kwa kama Kinga ya pili, hii ina maana ya wagonjwa ambao tayari wamewahi kupata:
Mshtuko wa moyo;
Kiharusi;
Upasuaji wa mishipa ya moyo;
Kuziba kwa mishipa ya moyo.
Kwa watu wenye afya wasio na historia hiyo, matumizi yake yanahitaji tathmini ya hatari binafsi badala ya kupewa kila mtu.
Somo muhimu
Faida ya dawa kwa wagonjwa wenye ugonjwa si lazima iwe faida kwa watu wenye afya.
Katika tiba, kundi la wagonjwa linaweza kubadilisha kabisa uwiano wa faida na madhara.
Hitimisho-Sayansi ya tiba hubadilika kwa sababu inajifunza
Sayansi ya tiba huboresha maarifa yake kila ushahidi mpya na wenye nguvu unapopatikana, ndiyo maana baadhi ya mapendekezo ya zamani hubadilishwa ili kuboresha usalama na ufanisi wa matibabu. Hivyo, mabadiliko ya miongozo ya tiba hayaonyeshi udhaifu wa sayansi, bali yanaonyesha uwezo wake wa kujirekebisha na kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa.
Imeandikwa:
27 Julai 2026, 16:43:31
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:
Vandenbroucke JP. Thalidomide: an unanticipated adverse event. J Clin Epidemiol. 2003;56(6):527-529.
Stephens T, Brynner R. Dark Remedy: The Impact of Thalidomide and Its Revival as a Vital Medicine. Cambridge: Perseus Publishing; 2001.
Mellin GW, Katzenstein M. The saga of thalidomide: neuropathy to embryopathy, with case reports of congenital anomalies. N Engl J Med. 1962;267:1184-1192.
Krumholz HM, Ross JS, Presler AH, Egilman DS. What have we learnt from Vioxx? BMJ. 2007;334(7585):120-123.
Bresalier RS, Sandler RS, Quan H, Bolognese JA, Oxenius B, Horgan K, et al. Cardiovascular events associated with rofecoxib in a colorectal adenoma chemoprevention trial. N Engl J Med. 2005;352(11):1092-1102.
Bombardier C, Laine L, Reicin A, Shapiro D, Burgos-Vargas R, Davis B, et al. Comparison of upper gastrointestinal toxicity of rofecoxib and naproxen in patients with rheumatoid arthritis. N Engl J Med. 2000;343(21):1520-1528.
Echt DS, Liebson PR, Mitchell LB, Peters RW, Obias-Manno D, Barker AH, et al. Mortality and morbidity in patients receiving encainide, flecainide, or placebo: the Cardiac Arrhythmia Suppression Trial. N Engl J Med. 1991;324(12):781-788.
Roberts I, Yates D, Sandercock P, Farrell B, Wasserberg J, Lomas G, et al. Effect of intravenous corticosteroids on death within 14 days in 10008 adults with clinically significant head injury (MRC CRASH trial). Lancet. 2004;364(9442):1321-1328.
Finfer S, Chittock DR, Su SY, Blair D, Foster D, Dhingra V, et al. Intensive versus conventional glucose control in critically ill patients. N Engl J Med. 2009;360(13):1283-1297.
Writing Group for the Women’s Health Initiative Investigators. Risks and benefits of estrogen plus progestin in healthy postmenopausal women: principal results from the Women’s Health Initiative randomized controlled trial. JAMA. 2002;288(3):321-333.
Anderson GL, Limacher M, Assaf AR, Bassford T, Beresford SA, Black H, et al. Effects of conjugated equine estrogen in postmenopausal women with hysterectomy: the Women's Health Initiative randomized controlled trial. JAMA. 2004;291(14):1701-1712.
Rossouw JE, Anderson GL, Prentice RL, LaCroix AZ, Kooperberg C, Stefanick ML, et al. Risks and benefits of estrogen plus progestin in healthy postmenopausal women. JAMA. 2002;288(3):321-333.
Herbst AL, Ulfelder H, Poskanzer DC. Adenocarcinoma of the vagina: association of maternal stilbestrol therapy with tumor appearance in young women. N Engl J Med. 1971;284(15):878-881.
Lenz W. A short history of thalidomide embryopathy. Teratology. 1988;38(3):203-215.
Nissen SE, Wolski K. Effect of rosiglitazone on the risk of myocardial infarction and death from cardiovascular causes. N Engl J Med. 2007;356(24):2457-2471.
Cohen D. Rosiglitazone: what went wrong? BMJ. 2010;341:c4848.
Lipscombe LL, Gomes T, Levesque LE, Hux JE, Juurlink DN, Alter DA. Thiazolidinediones and cardiovascular outcomes in older patients with diabetes. JAMA. 2007;298(22):2634-2643.
Furberg CD, Pitt B. Withdrawal of cerivastatin from the world market. Curr Control Trials Cardiovasc Med. 2001;2(5):205-207.
Shepherd J, Blauw GJ, Murphy MB, Bollen EL, Buckley BM, Cobbe SM, et al. Pravastatin in elderly individuals at risk of vascular disease (PROSPER). Lancet. 2002;360(9346):1623-1630.
Omenn GS, Goodman GE, Thornquist MD, Balmes J, Cullen MR, Glass A, et al. Effects of a combination of beta carotene and vitamin A on lung cancer and cardiovascular disease. N Engl J Med. 1996;334(18):1150-1155.
Yusuf S, Dagenais G, Pogue J, Bosch J, Sleight P. Vitamin E supplementation and cardiovascular events in high-risk patients. N Engl J Med. 2000;342(3):154-160.
Moseley JB, O’Malley K, Petersen NJ, Menke TJ, Brody BA, Kuykendall DH, et al. A controlled trial of arthroscopic surgery for osteoarthritis of the knee. N Engl J Med. 2002;347(2):81-88.
Thorlund JB, Juhl CB, Roos EM, Lohmander LS. Arthroscopic surgery for degenerative knee: systematic review and meta-analysis. BMJ. 2015;350:h2747.
Sackett DL, Rosenberg WMC, Gray JAM, Haynes RB, Richardson WS. Evidence based medicine: what it is and what it isn't. BMJ. 1996;312(7023):71-72.
Guyatt GH, Sackett DL, Sinclair JC, Hayward R, Cook DJ, Cook RJ. Users' guides to the medical literature: IX. A method for grading health care recommendations. JAMA. 1995;274(22):1800-1804.
Ioannidis JPA. Why most published research findings are false. PLoS Med. 2005;2(8):e124.
Sterne JAC, Egger M, Moher D. Addressing reporting biases. In: Higgins JPT, Green S, editors. Cochrane Handbook for Systematic Reviews of Interventions. Chichester: Wiley; 2008.
Chou R, Gordon DB, de Leon-Casasola OA, Rosenberg JM, Bickler S, Brennan T, et al. Management of postoperative pain: a clinical practice guideline. J Pain. 2016;17(2):131-157.
Kolodny A, Courtwright DT, Hwang CS, Kreiner P, Eadie JL, Clark TW, Alexander GC. The prescription opioid and heroin crisis: a public health approach to an epidemic of addiction. Annu Rev Public Health. 2015;36:559-574.
Porter J, Jick H. Addiction rare in patients treated with narcotics. N Engl J Med. 1980;302(2):123.
Finucane TE, Christmas C, Travis K. Tube feeding in patients with advanced dementia: a review of the evidence. JAMA. 1999;282(14):1365-1370.
Carson JL, Stanworth SJ, Dennis JA, Trivella M, Roubinian N, Fergusson DA, et al. Transfusion thresholds for guiding red blood cell transfusion. Cochrane Database Syst Rev. 2021;12(12):CD002042.
Villanueva C, Colomo A, Bosch A, Concepción M, Hernandez-Gea V, Aracil C, et al. Transfusion strategies for acute upper gastrointestinal bleeding. N Engl J Med. 2013;368(1):11-21.
Therapeutics and Technology Assessment Subcommittee of the American Academy of Neurology. Practice advisory: the use of corticosteroids in traumatic brain injury. Neurology. 2000;55(11):1680-1685.
Sackett DL. The arrogance of preventive medicine. CMAJ. 2002;167(4):363-364.
Guyatt G, Cairns J, Churchill D, Cook D, Haynes B, Hirsh J, et al. Evidence-based medicine: a new approach to teaching the practice of medicine. JAMA. 1992;268(17):2420-2425.
